Kuna watu walizungumza mengi baada ya Nasredine Nabi kuachana na Yanga na kwenda kutafuta malisho mema zaidi. Kuna watu walijua mwisho wa Yanga kutamba umefika.

Ni kweli Nabi alifanya makubwa na Yanga. Alitwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara mara mbili. Alitwaa Kombe la Shirikisho la Azam. Aliwafikisha fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika. Alifanya makubwa sana.

Kwa kifupi, baadhi ya watu waliamini ingekuwa anguko la Yanga kama Nabi angeondoka. Ila ndio maisha ya soka. Kila mtu anatamani kufika sehemu nzuri zaidi. Ndicho alichofanya Nabi na kwenda katika Ligi kubwa zaidi Afrika. Kwenda kwenye klabu kubwa zaidi.

Ubaya ni kwamba siku chache baada ya Nabi kuondoka, kukatokea pigo jingine Jangwani. Akaondoka aliyekuwa mfungaji bora wa timu na Ligi Kuu, Fiston Mayele kwenda Pyramids ya Misri. Ikaonekana kama Yanga sasa itakwenda shimoni zaidi.

Ungewaza nini tofauti? Mayele alikuwa mfungaji bora wa Yanga kwa misimu miwili mfululizo. Alikuwa mfungaji bora wa Yanga katika Kombe la Shirikisho Afrika. Alifanya makubwa sana pale Jangwani. Ila ndio maisha ya soka, wachezaji wazuri huja na kuondoka.

Ni kama walivyoondoka Clatous Chama na Luis Miquissone pale Simba wakati ule. Waliata sehemu bora zaidi. Ungejiuliza kama Miquissone angekataa ofa ya Al Ahly angetaka kwenda wapi?

Miquissone amewahi kupata nafasi ya kucheza Mamelodi Sundowns, lakini hakufanya vizuri sana. Akarudi kwao Msumbiji kisha Simba. Ukipata ofa kama ya kwenda Al Ahly unawezaje kukataa? Ni ngumu.

Hivyo kwa fedha waliyowekewa mezani na Pyramids ilikuwa ngumu kuikataa. Ofa aliyopewa Mayele na Pyramids ilikuwa ngumu kukataa. Kila mtu anafanya kazi kwa ufanisi ili apate zaidi. Ndivyo ilivyo kwa wanasoka wote duniani.

Ndiyo sababu Neymar aliondoka Barcelona akaenda PSG. Walimwekea mezani ofa bora zaidi. Walimpa fedha ambayo hata angekaa Barcelona kwa miaka kadhaa asingeweza kuipata.

Hivyo baada ya Nabi na Mayele kuondoka, watu waliamini katika anguko la Yanga. Waliamini kuwa Nabi ndio alibeba maono ya Wananchi. Ndio aliwarudisha katika reli. Waliamini Mayele ndio aliwapa Yanga kitu bora zaidi katika ushambuliaji. Nani angefunga tena?

Hata hivyo, ukweli ni kwamba mambo yako tofauti kwani uongozi wa wananchi wakaifanya kazi yao vizuri kumleta Miguel Gamondi. Kocha mwenye uzoefu na soka la Afrika kwa zaidi ya miaka 20. Chaguo bora.

Kilichotokea baada ya hapo, Yanga wamekuwa bora zaidi ya msimu uliopita. Kwa sasa Yanga inacheza vizuri zaidi. Inapiga pasi zaidi. Inagawa vipigo vikubwa zaidi ya msimu uliopita. Inashangaza na kushtua kwa wakati mmoja.

Nani aliwaza watoto wa jangwani wangeweza kuwa hatari zaidi msimu huu. Nani aliwaza ingeweza kufika robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika na kutolewa kwa mbinde na Mamelodi Sundowns. Hakuna.

Nimeona sifa nyingi kwa Gamondi kwa namna ambavyo ameifanya Yanga kuwa tishio msimu huu. Ametawala katika Ligi Kuu. Anafanya kila anachojisikia. Kwa mara ya kwanza baada ya miongo kadhaa, Yanga imezifunga timu nyingi mabao matano ikiwemo watani wao Simba.

Ni kweli Gamondi amebadili vitu vingi kwa namna Yanga inacheza sasa. Mbinu zake bora katika Ligi ya Mabingwa Afrika nusura ziiondoshe Mamelodi Sundowns tena kwenye ardhi ya kwao. Ni mwamba kabisa.

Yote kwa yote, narudi kwenye hoja ya msingi. Tulimuona Nabi kuwa kocha mzuri sana akiwa na Yanga. Tunamuona Gamondi sasa kuwa kocha tishio Afrika akiwa na Yanga. Ila ukweli, hawa wawili ni sehemu tu ya kazi nzuri inayofanywa na viongozi wa Yanga.

Chini ya Rais Injinia Hersi Said, Yanga imefanya mradi wao kwa ufasaha sana. Imesajili wachezaji wengi wa maana. Fikiria kuhusu Pacome Zouzoua, Yao Kouassi, Khalid Aucho, Maxi Nzengele, Stephane Aziz Ki, Kennedy Musonda, Mudathir Yahya na wengineo. Yanga imejenga kikosi imara chenye mchanganyiko wa wachezaji wenye uzoefu mkubwa na chipukizi. Ndio hawa kina Clement Mzize, Nickson Kibabage, Kibwana Shomari, Abutwalib Mshery na wengine.

Wamekuwa makini sana katika eneo la usajili. Wachezaji wengi wanaosajiliwa Yanga sasa ni mahiri mno. Ni wazuri kuliko wa timu nyingine za Ligi Kuu. Ndio sababu licha ya kuwakosa wachezaji watatu tegemeo, G amondi bado aliweza kuwasimamisha Mamelodi Sundowns. Kwa nini? Kwa sababu ana kikosi kipana.

Hivyo bado naamini, huyu Gamondi anaweza kuondoka kama alivyofanya Nabi na bado timu hii ikawa imara zaidi. Ni kwa sababu wana wachezaji mahiri. Kocha anayekuja kazi yake inakuwa nyepesi.

Sio kama Simba Imejaa wazee na wachezaji wengi wa kawaida. Wamechukua mmoja wa makocha bora Afrika, Abdelhak Benchikha lakini bado ina wakati mgumu. Benchikha anafanya kila kitu lakini mwisho wa siku anawafundisha kina nani? Ndio hawa kina Kibu Denis, Ladack Chasambi, Babacar Sarr, Pa Omary Jobe na wengineo. Ni kama kupoteza muda tu.

Twende mbele, turudi nyumba ukweli Yanga imefanikiwa sana katika usajili. Kama itaendelea hivi, tutaendelea kuwaona makocha wake wanafanya maajabu. Ila ukweli ni kwamba wanafundisha timu yenye wachezaji wakomavu na wenye uwezo mkubwa.

5 Comments

Leave A Reply


Exit mobile version