Ni rahisi kusema Simba wamezidiwa tena ujanja baada ya kipa wanaodaiwa kumtaka Washington Arubi kutoka Marumo Gallants kusaini timu nyingine.

Arubi alionyesha kiwango cha juu wakati Marumo walipovaana na Yanga kwenye hatua ya nusu fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika na kuelezwa kuwa Simba walionyesha nia ya kumsajili.
Chanzo cha uhakika kutoka ndani ya Simba kimeeleza kuwa, jina la kipa huyo lilikuwa mezani kwa kocha Olvier Robert Robertinho likijadiliwa lakini jana wakapata taarifa kuwa ameshasaini sehemu nyingine.

Taarifa iliyoripotiwa na magazeti ya Afrika Kusini inasema kuwa kipa huyo ambaye pia alikuwa akiwindwa na Simba ameshasaini mkataba wa mwaka mmoja kwenye kikosi cha Sekhukhune United.

Arubi ameondoka Marumo bure kwa kuwa mkataba wake umeshamalizika na sasa ataitumikia timu hiyo inayoshiriki Ligi Kuu ya Afrika Kusini kwenye michuano ya Shirikisho Afrika msimu ujao.

Washington Arubi alikuwa na kipindi kizuri na Marumo na mwishoni mwa msimu alikuwa mmoja kati ya wachezaji waliopewa tuzo kutokana na mchango wao mkubwa kwenye timu hiyo ambayo imeshuka daraja.

Habari zinasema Simba walikuwa wanamhitaji kipa huyo raia wa Zimbabwe ili awe msaidizi wa Aishi Manula ambaye kwa sasa yupo Afrika Kusini akisubiri kufanyiwa upasuaji wa nyama za paja.

Kwa taarifa zaidi za usajili, tufatilie hapa.

Leave A Reply


Exit mobile version