Michuano ya Kombe la mataifa ya Afrika 2023 (AFCON) inatarajiwa kuanza kutimua vumbi Januari 13 nchini Ivory Coast huku mataifa 24 yamefuzu katika michuano hiyo ya 34 inabaki kuwa michuano mikubwa kwa ngazi ya mataifa Afrika, ikionyesha vipaji vya juu kutoka kwa wachezaji mbalimbali  na ushindani mkubwa kutoka kwao.

Katika historia ya michuano ya mataifa barani Afrika majina kama Samuel Eto’o na Didier Drogba yanaongoza kwa kufanya makubwa katika michuano hiyo, hasa kwa umahiri wao wa kupachika mabao lakini kwa kizazi cha sasa huwezi kuacha majina kama  kama Mnigeria Victor Osimgen na Mcameroon Vincent Aboubakar wakilenga kufikia mafanikio ya watangulizi hao.

Leo hii tunakusogezea wafungaji bora zaidi wa mashindano haya makubwa zaidi barani Afrika kwa ngazi ya timu za taifa:

SAMUEL ETO’O – MABAO 18

Kwa sasa ni rais wa Shirikisho la soka la Cameroon ambapo aliwahi kuwa mchezaji bora wa Afrika akichukua mara nne.Etoo anashikilia rekodi ya kufunga mabao mengi zaidi katika historia ya mashindano haya makubwa barani Afrika baada ya kuzifumania nyavu mara 18.

Usichokifahamu ni kuwa Etoo aliitwa kujiunga na timu ya taifa ya Cameroon mwaka wa 1996 akiwa na umri mdogo tu wa miaka 16 ambapo akiwa na timu hiyo alishinda AFCON mwaka 2000 na 2002. Katika michuano ya Mwaka 2006 na 2008 aliibuka mfungaji bora mara mbili ambapo alipachika nyavuni mabao Matano.

LAURENT POKOU – MABAO 14

Kabla ya uwepo wa kizazi kipya cha kina Didier Drogba, Ivory Coast walikuwa na mshambuliaji mwingine maarufu Laurent Pokou ambaye katika michuano hii wamempa heshima kubwa ya kuupa jina lake mpira utakaotumika katika michuano hii. Pokou alifunga mabao 14 katika michezo 13 pekee ya AFCON akiwa na wastani wa mabao 1.17 kwa kila mchezo. Mwaka 1968 alifunga bao lake la kwanza huku akihitimisha michuano hiyo kwa mabao 6 katika mechi 5.
Mwaka uliofuata kimashindano yaani AFCON ya 1970, mshambuliaji huyo alifunga mabao manane katika michezo mitano, likiwemo la ushindi wa mabao matano dhidi ya Ethiopia, rekodi ambayo haijavunjwa hadi sasa.

RASHID YEKINI – MABAO 13

Wakati Nigeria ikielekea AFCON 2023 huku Victor Osimhen akitazamiwa kuwa ndiye mchezaji hatari zaidi timu katika timu hiyo, usisahau kwamba Super Eagles walikuwa na mshambuliaji hatari Rashid Yekini.

Mchezaji huyo wa zamani wa kimataifa wa Nigeria mwenye kumbukumbu nzuri anashika nafasi ya tatu kati ya wafungaji bora wa michuano hiyo, akiwa na mabao 13 katika mechi 24 katika matoleo manne ambayo ameshiriki. Mwaka 1992 aliibuka kuwa mfungaji bora akiwa na mabao manne huku mwaka 1994 akifunga mabao Matano. 

HASSAN EL-SHAZLY – MABAO 12

Licha ya uwepo wa wachezaji hatari kwenye kikosi cha Misri kama vile Mohamed Salah na wengine waliowahi kucheza kama Ahmed Mido aliyewahi kupita klabu kadhaa EPL ikiwemo Wigan, Tottenham na Middlesbrough, lakini Hassan El-Shazlyb alikuwa hatari.

El-Shazly alionekana kwa mara ya kwanza kwenye michuano hiyo mwaka 1963. Alifunga mabao sita na kuishia kuwa mfungaji bora wa michuano hiyo, na kuiongoza Misri kumaliza katika nafasi ya tatu. Mnamo 1970, alifunga mabao matano wakati Misri ikimaliza nafasi ya tatu.

PATRICK MBOMA – MABAO 11

Mmoja wa wanasoka mahiri wa Cameroon, Patrick Mboma alijihakikishia nafasi kati ya ufungaji bora wa michunao ya Afrika katika mashindano ya kwanza.

Mnamo mwaka 2000, Mboma sio tu alishinda Kombe la Mataifa ya Afrika lakini pia alijishindia medali ya dhahabu ya Olimpiki akiwa na ‘Indomitable Lions’.

HOSSAM HASSAN – MABAO 11

Hossam Hassan aliiwakilisha Misri kwenye michuano saba tofauti ya AFCON huku akijipatia mabao 11 katika mechi 21.

Akiwa na umri wa miaka 40, Hassan aliwahi kuwa nahodha wa Mafarao wa Misri wakati wa Kombe la Mataifa ya Afrika la 2006. Huu ulikuwa ushindi wake wa tatu wa bara na hitimisho la kuonekana kwake katika mashindano haya.

DIDIER DROGBA – MABAO 11

Drogba alicheza mechi yake ya kwanza ya Kombe la Mataifa ya Afrika mwaka 2006 na kufunga mabao matatu ingawa Cote d’Ivoire ilishindwa katika fainali na Misri kwa mikwaju ya penalti.
Mshambulizi huyo aliongeza mabao matatu mwaka 2008, huku Ivory Coast ikishika nafasi ya nne.

Wakati wa michuano ya mataifa ya Afrika ya mwaka 2010 alifunga bao moja pekee lakini mwaka 2012, Drogba alifunga mara tatu ambapo Ivory Coast walipomaliza michuano hiyo kwa kuwa washindi wa pili na alihitimisha mwaka 2013 ikiwa michuano yake ya mwisho ambapo alifunga bao moja pekee.

Wachezaji wengine Ndaye Mulamba wa DR Congo, Francileudo Santos wa Tunisia, Joel Tiéhi wa Ivory Coast, Mengistu Worku raia wa Ethiopia, Kalusha Bwalya wa Zambia na Andre Ayew hawa wote walihitimisha safari yao ya kuzitumikia timu zao za Taifa kwenye michuano hii wakiwa na mabao 10.

Endelea kufuatilia zaidi kuhusu taarifa mbalimbali za michuano ya mataifa barani Afrika kwa kugusa hapa.

 

Leave A Reply


Exit mobile version