Michuano ya 34 ya Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) itaanza Januari 13, nchini Ivory Coast na kumalizika Februari 11 jijini Abidjan. Timu kadhaa za Ligi Kuu ya Uingereza zitawakosa nyota wake. Mshambuliaji wa Liverpool, Mohamed Salah atakuwa na hamu ya kuchukua kombe la Afrika baada ya kupita miaka 14.

Mohamed Salah (Misri)

Mwaka 2022, Misri ilipata kipigo mara mbili kutoka kwa Senegal. Kupoteza fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika kisha kukosa nafasi ya kwenye Kombe la Dunia huko Qatar.

Mechi zote mbili ziliisha kwa mikwaju ya penalti – na Salah hakupata hata nafasi ya kupiga penalti kwenye fainali ya Afcon, kwani ilibidi asipige tena penalti ya tano.

Taji la mwisho la Misri kati ya mataji yake saba lilikuwa mwaka 2010 na Salah anatazamiwa kufanya vyema zaidi kuliko Gabon mwaka 2017 na Cameroon mwaka jana.

Salah ameshinda medali nyingi akiwa na Liverpool, lakini mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 31 atakuwa na nia ya kuongeza mabao katika mechi za Kombe la Mataifa ya Afrika ili kujaribu kuwaongoza Mafarao hao kutwaa kombe.

Akiwa bado na ushawishi mkubwa Anfield msimu huu, “Mfalme wa Misri” atakuwa nahodha wa timu yake dhidi ya Ghana, Cape Verde na Msumbiji katika Kundi B.

Victor Osimhen (Nigeria)

Baada ya kutokuwepo katika kikosi cha 2021 kutokana na kuugua Uviko-19 na majeraha. Je, Mchezaji Bora wa Mwaka wa Afrika ataweza kuisaidia Nigeria kushinda taji lao la kwanza tangu 2013?

Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 24 amejidhihirisha kuwa mmoja wa washambuliaji bora zaidi barani Ulaya, akimaliza msimu uliopita kama mfungaji bora wa Serie A na kuisaidia Napoli kutwaa taji lao la kwanza la ligi ya Italia tangu 1990.

Nigeria, bila Osimhen, iliweza tu kutoa sare katika mechi ya kufuzu Kombe la Dunia 2026 dhidi ya Lesotho na Zimbabwe mwezi Novemba. Lakini sasa ana fursa ya kuichezea nchi yake kwenye Afcon.

Mchezaji huyo wa zamani wa Lille alikuwa sehemu ya kikosi cha Super Eagles kwenye fainali za 2019 lakini akatolewa baada ya mapumziko – Nigeria iliposhinda mchujo wa kuwania nafasi ya tatu.

Wenyeji hao wa Afrika Magharibi wanachuana na Ivory Coast, Equatorial Guinea na Guinea-Bissau katika Kundi A. Kuna tetesi mchezaji huyo atahamia Ligi Kuu ya Uingereza. Je, huu ndio wakati wa Osimhen kujitangaza kwenye anga za kimataifa?

Serhou Guirassy (Guinea)

Mshambulizi huyu amekuwa na mwanzo mzuri katika msimu huu akiwa na klabu yake ya Stuttgart, amefunga mabao 15 katika mechi 10 za kwanza kwenye Bundesliga ya Ujerumani.

Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 27 atashiriki Afcon kwa mara ya kwanza baada ya kucheza mechi yake ya kwanza nchini Guinea Machi 2022.

Katika Kundi C, Senegal, bingwa mtetezi, na Cameroon, watampa Guirassy wakati mgumu. Nayo Gambia, iliyofuzu kwa mara ya pili, nayo itaonyesha ubabe wake.

Guinea itamtumia Guirassy wakati timu hiyo ya Afrika Magharibi itakapo tafuta nafasi ya kufuzu hatua ya makundi.

Mohammed Kudus (Ghana)

Mohammed Kudus alifunga mabao mawili kwa Ghana ilipoilaza Korea Kusini kwenye Kombe la Dunia la 2022 nchini Qatar.

Ghana itasafiri hadi Ivory Coast na itapambana ili isiondolewe katika hatua ya makundi kama ilivyotokea katika Kombe la Mataifa ya Afrika 2021. Ilimaliza kwa kufungwa (3-2) na Comoro.

Black Stars wamekosa ushindi katika mechi zao mbili za kwanza za kufuzu Kombe la Dunia la 2026. Katika moja ya mechi hizo ilipoteza tena dhidi ya Comoro.

Kudus alikuwa mfungaji bora wa Ghana wakati wa mechi za kufuzu Kombe la Mataifa ya Afrika, akiwa na mabao matatu. Na uwezo wake katika klabu ya West Ham United umeendelea kukua tangu ajiunge na klabu hiyo ya Ligi Kuu ya Uingereza mwezi Agosti.

Alifunga mabao mawili kwenye Kombe la Dunia la 2022. Je, mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 23 anaweza kuisaidia Ghana kurejea kileleni mwa soka la Afrika, ikikabiliwa na mechi ya kwanza ngumu dhidi ya Misri?

Issa Kaboré (Burkina Faso)

Beki huyo wa kulia anayeshambulia alichaguliwa kuwa mchezaji bora chipukizi mwaka 2021 na alivutia macho ya wengi pale Burkina Faso ilipoingia nusu fainali, kabla ya kushindwa na mabingwa Senegal.

Kabore alijiunga na Manchester City akitokea klabu ya Ubelgiji, Mechelen mwaka 2020, lakini bado anasubiri mechi yake ya kwanza akiwa na mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu ya Uingereza na Ulaya.

Baada ya kuwa kwa mkopo nchini Ufaransa katika klabu za Troyes na Marseille, mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 22 sasa anapata ladha ya kucheza Ligi Kuu ya Uingereza akiwa na Luton Town kwa mkopo, ambayo inapambana isishuke daraja.

Burkina Faso itakapo kabiliana na Algeria, Mauritania na Angola katika Kundi D, Kabore, ambaye tayari amecheza mechi nyingi za kimataifa, ana nafasi ya kuonyesha uwezo wake ili kujinyakulia nafasi katika timu ya City ya Pep Guardiola msimu ujao.

Azzedine Ounahi (Morocco)

Uchezaji mzuri wa kiungo huyo wakati Morocco ikicheza Kombe la Dunia la 2022 – ulichangia pakubwa uhamisho wake kwenda Olympique Marseille baada ya mashindano hayo.

Hata hivyo, alipata majeraha mwezi Machi akiwa na Morocco. Ounahi hakushiriki katika mechi za kufuzu Kombe la Dunia mwezi Novemba.

Ingawa Kocha Walid Regragui anaweza kumleta mchezaji huyo ambaye alifanya kazi kubwa hadi nusu fainali ya Kombe la Dunia – wakati Morocco itakapomenyana na DR Congo, Zambia na Tanzania katika Kundi F.

Endelea kusoma zaidi kuhusu AFCON kwa kugusa hapa.

 

1 Comment

  1. Pingback: Klabu Zilizotoa Wachezaji Wengi AFCON 2023 - Kijiweni

Leave A Reply


Exit mobile version