Kutokana na mtifuano ulivyo baina ya Kitayosce na Pamba katika vita ya kupanda ligi kuu, huenda mikoa ya timu hizo ikakata kiu ya kuziona tena Simba na Yanga msimu ujao, huku Mashujaa FC nao wakichomoza.

Pamba ya jijini Mwanza iliyowahi kutwaa ubingwa wa Kombe la Muungano mwaka 1999, kisha kushuka daraja mwaka 2000, haijarejea tena ligi kuu na sasa inajipapatua kufuta mzimu msimu ujao.

Kitayosce ya mkoani Tabora wao ni msimu wa pili kushiriki Championship na imeonyesha nia ya kupanda ligi kuu baada ya mkoa huo kukosa burudani hiyo kwa zaidi ya misimu saba tangu Rhino Rangers waliposhuka msimu wa 2013/14. Kitayosce ipo nafasi ya pili kwa pointi 49 huku Pamba akifuata kwa 47 na Jumamosi hii wapinzani hao watakutana Uwanja wa Nyamagana.

Kama haitoshi, nao Mashujaa wameonyesha uhitaji wa kucheza ligi kuu baada ya Kigoma kukosa uhondo huo na kufanya vita kuendelea kuwa nzito kupanda daraja baada ya kukusanya pointi 41, nafasi ya nne.

Hadi sasa JKT Tanzania ndio wameingiza mguu mmoja ligi kuu baada ya kuwa na pointi 56, wakisaka alama sita tu kati ya michezo mitano iliyobaki.

Pamba imebakiza michezo sita ikiwa ni dhidi ya Kitayosce, Mbuni, African Sports, JKT Tanzania na Fountain Gate, huku Kitayosce ikiwa na mechi tano dhidi ya wapinzani hao, JKT Tanzania, Fountain Gate, Mbuni na African Sports.

Mashujaa wao wana michezo mitano wakianza dhidi ya Pamba, Fountain Gate, JKT Tanzania, African Sports na Mbuni FC ambazo zitaamua hatma ya timu hiyo kupanda au kubaki.

Leave A Reply


Exit mobile version