Vigogo wa Azam Hawajamaliza! Saa chache baada ya kumalizana na Yanga na kumbeba, kiungo Feisal Salum ‘Fei Toto’ iliyompa mkataba wa miaka mitatu, klabu ya Azam imehamia Msimbazi ikianza mazungumzo ya kumnyakua winga, Peter Banda.

Azam imeanza mazungumzo na wawakilishi wa nyota huyo wa kimataifa kutoka Malawi mwenye miaka 22 na kwa hatua waliyofikia kuna uwezekano mkubwa, Banda akavaa uzi wa Azam msimu ujao kutokana na Simba kuwa tayari kumuuza au kumtoa kwa mkopo kipindi hiki akiwa amebakiza mkataba wa  mwaka mmoja.

Nyota huyo tegemeo wa timu ya taifa ya Malawi, hayupo kwenye mipango ya kocha mkuu, Roberto Oliveira ‘Robertinho’ aliyowapa mabosi wa chama hilo na Azam inatumia mwanya huo ili kumshawishi atue viunga vya Chamazi yalipo maskani ya klabu hiyo.

Moja ya Vigogo Azam FC, aliyeomba jina lake kuhifadhiwa amethibitisha kuwa wanamhitaji Banda kutokana na uwezo na umri alionao.

“Pale Simba tutang’oa mtu, kama tulivyowapa wao wachezaji miaka ya nyuma na sisi watatupa mastaa wao, mmoja wao ni yule winga Banda, kama wanaona hawafai, sisi atatufaa na tunajua tutamtumiaje.” alisema mtu huyo na kuongeza;

“Kuna mazungumzo tumefanya na wawakilishi wa mchezaji lakini pia tunajiandaa kwenda mezani kwa Simba kumuomba Banda, baada ya hapo tutakachojibiwa tutakifanyia kazi.”

Banda alijiunga na Simba mwanzoni mwa msimu uliopita kwa mkataba wa miaka mitatu akitokea Nyassa Big Bullets ya kwao Malawi, lakini tangu ametua kwa Wanamsimbazi hao, hakuwa na muendelezo  mzuri wa kiwango chake huku Majeraha ya mara kwa mara yakitajwa kuwa sababu.

Leave A Reply


Exit mobile version