Katika hatua inayotia moyo kwa mashabiki wa soka nchini Tanzania ni Taifa Stars kumteua kaimu kocha mkuu mpya Hemed Morocco ambaye ni Mtanzania akisaidiana na Juma Mgunda kukaimu nafasi ya ukocha baada ya alikua kocha mkuu Adel Amrouche kufungiwa na CAF mechi 8 baada ya kutoa kauli ambazo sio za kweli kuhusu timu ya Taifa ya Morocco.

Uteuzi huu ni dalili ya kujiamini na imani katika vipaji vya ndani lakini pia unaweka matumaini mapya kwa Taifa Stars kuelekea mchezo wa 2 dhidi ya Zambia katika michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON).

Yapo mengi ambayo yalikua yanazungumzwa katika mitandao ya kijamii na vijiweni kuhusu aliekua kocha mkuu wa Taifa Stars ambaye ni raia wa Algeria lakini hapa tutazame kwanini mabadiliko ya benchi la ufundi yanavyoweza kuwa muhimu sana kwa Stars na jinsi wanavyoweza kupata alama muhimu kwenye mchezo dhidi ya Zambia.

Uteuzi wa Hemed Morocco na Juma Mgunda ambao ni Watanzania unafungua mlango wa fursa mpya kwa wachezaji wa Taifa Stars. Kocha wa ndani anaelewa vyema utamaduni wa soka nchini, anafahamu vizuri wachezaji, na anaunganisha moyo wa taifa. Hii inaweza kuwa na athari kubwa kwa morali ya wachezaji na kujenga umoja wa kipekee katika kikosi.

Nadhani pia mabadiliko ya benchi la ufundi linaweza kuwa na athari ya kuongeza kujiamini kwa wachezaji. Kwa kufanya kazi na kocha ambaye anaelewa changamoto na mafanikio ya wachezaji wa Kitanzania, wachezaji wanaweza kuwa na motisha zaidi ya kujituma na kufanya vizuri uwanjani.

Taifa Stars wanaingia katika mchezo huu muhimu dhidi ya Zambia wakirejesha upya matumaini kwa Watanzania kutokana na uwepo wa makocha wenye uzoefu na wanaopendwa na kuaminiwa kwa mbinu zao Uwanjani kuwa zitaleta matokeo chanya uwanjani.

Tunaingia katika mchezo huu dhidi ya Zambia ambapo bila shaka makocha wao washafanya marekebisho ya changamoto ambazo wamekwisha ziona katika mchezo wa kwanza hivyo ni muhimu kwa wachezaji kuingia na mbinu ambazo wamepewa makocha hawa ili kupata alama katika mchezo dhidi ya Zambia.

Ni wajibu kwa wachezaji sasa kuwasaidia makocha hawa wazawa na kuufanya uongozi wa shirikisho la soka Tanzania (TFF) kuamini kuwa ni kitu ambacho kinawezekana kabisa endapo tutaamua kuwaamini wazawa na kuongoza timu zetu za taifa kama ambavyo tumewaamini kuanzia timu za vijana na zile za wanawake.

Nadhani katika kipindi kama hiki tuendeee kuzidisha matumaini na uzalendo katika kambi ya Taifa Stars. Kupitia kujitolea na uzoefu wao,makocha hawa wana nafasi ya kubadilisha mwelekeo wa timu na kuleta mafanikio makubwa.

SOMA ZAIDI: Umri Wa Djigui Diarra Unaruhusu Kwenda Ulaya

1 Comment

  1. Pingback: Wachezaji Hawakuutaka Ushindi Licha Ya Zambia Kuwa Pungufu - Kijiweni

Leave A Reply


Exit mobile version