Ukiuzungumzia mpira wa miguu Tanzania basi huwezi kuacha kulitaja Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) chini ya Rais wake Wallace Karia ambaye anaingia katika orodha ya marais wa shirikisho hilo kwa mafanikio mengi makubwa ambayo ameyapata wakati wa uongozi wake akiwa na Katibu wake Wilfred Kidao ambao wamechukua hatua muhimu katika kuendeleza mchezo wa soka Tanzania.

Kwa sasa huwezi kuacha kutaja namna ambayo kumekua na ligi bora yenye ushindani lakini pia kukiwa na wadhamini wa kutosha wanaoendelea kuipa nguvu ligi yenyewe kuanzia ile ya Wanaume na ligi kuu ya wanawake ambayo pia imekua na ushindani mzuri tu.

Tumeona kile ambacho wamekifanya makocha wazawa Hemed Morocco akisaidiana na Juma Mgunda katika michuano ya mataifa barani Afrika kwa mechi 2 za mwisho ambazo walizikaimu baada ya kufungiwa kwa kocha mkuu Adel Amrouche. Nadhani ni wakati sahihi kuwa na njia hii ya kuwapa fursa makocha wazawa kujifunza zaidi nje ya nchi, hasa katika mataifa yaliyoendelea kwani hii ni hatua muhimu ambayo inaweza kuleta mabadiliko chanya katika maendeleo ya soka nchini.

TFF wanapaswa kufahamu kuwa kwa kuwapa fursa makocha wazawa kwenda kujifunza nje ya nchi kunawezesha upatikanaji wa maarifa mapya ya kufundisha soka kwani mataifa yaliyoendelea mara nyingi yanajulikana kwa mifumo bora ya mafunzo ya soka na teknolojia ya hali ya juu katika maendeleo ya wachezaji. Makocha wazawa wakipata fursa ya kujifunza katika mazingira haya, wanaweza kurudi na maarifa mapya na mbinu za kufundishia, hivyo kuboresha ubora wa mafunzo wanayotoa.

Makocha wetu wazawa wakishiriki katika programu za kimataifa kunawawezesha kujenga mtandao wa kimataifa na wenzao duniani kote. Hii inaweza kusaidia kuleta ushirikiano katika maendeleo ya soka, kubadilishana uzoefu, na hata kuanzisha mikataba ya ushirikiano na taasisi za kimataifa. Mtandao huu unaweza kuwa muhimu katika kuvutia rasilimali na fursa za maendeleo ya soka nchini.

Tufahamu kuwa maendeleo ya soka yanaweza kuvutia wadhamini na uwekezaji. Kwa kuboresha ubora wa mafunzo na kuongeza ushindani, Tanzania inaweza kuwa na soko lenye thamani kubwa kwa wadhamini na wawekezaji kuja kuwekeza katika ligi zetu lakini pia na miundombinu ya michezo na kupelekea kujenga msingi imara wa soka la kitaifa.

Kuwapa makocha wazawa nafasi ya kujifunza nje ya nchi ni uamuzi wa busara ambao unalenga kuleta mabadiliko chanya katika soka la Tanzania na matumaini yangu ni kuwa mkakati huu utachangia kukuza vipaji na kuleta mafanikio katika ngazi ya kitaifa na kimataifa.

SOMA ZAIDI: Yanga Walikua Sahihi Kumpiga Kitanzi Ibrahim Bacca

Leave A Reply


Exit mobile version