Klabu ya Singida FG imepokea hundi ya Sh50 milioni ambayo ni bonasi kutoka kwa wadhamini wao Sportpesa.

Sportpesa imetoa pesa hiyo baada ya klabu ya Singida Fountain Gate kumaliza nafasi ya nne katika Ligi Kuu.

Akizungumza na Waandishi wa Habari, Mwenyekiti wa Bodi ya Sportpesa, Abassi Tarimba amesema kitendo cha timu hiyo kufanya vizuri kinawapa faraja wao wadhamini.

“Inatupa faraja sisi SportPesa tujisikie fahari kwani licha ya kutoka Championship wamemaliza ndani ya tano bora, kwa hatua ambayo wamefika tunawapa bonasi ya Sh50 milioni;

“Tangu tumeingia 2017 kwenye udhamini wa mpira wa miguu umefanya wengine waje kwenye hizi timu.”

Tarimba amesema wana timu tatu ambazo wana zidhamini ikiwemo Yanga ambao ndio mabingwa, Singida Fountain Gate ambayo ni ya nne na Namungo ya tano zote zinafanya vizuri.

“Hii Fedha msiione ndogo bali ni motisha kwamba msimu ujao timu zikija kucheza na nyie zisichukue pointi kirahisi,” amesema Tarimba.

Upande wa Makamu wa Rais, Singida FG, John Kadutu amesema leo ni siku maalum kwao kupata bonasi hiyo.

Kadutu amesema haikuwa rahisi kwanza kuaminiwa kwani walikuwa wageni na Sportpesa wamechangia kwa kiasi kikubwa kwao kufanya vizuri.

“Mtaani watu wanaulizana wapi ambapo tunatoa nguvu kubwa lakini wanasahau kwamba nyuma yetu kuna watu kama SportPesa ambao wanatushika mkono;

“Kuendesha hizi timu ni jambo kubwa, inatumika gharama kubwa sana lakini uwepo wa wadhamini unatusaidia.”

Sportpesa na Singida Fountain Gate zina mkataba wa miaka minne na sasa umetumika mwaka tu.

Kwa taarifa zaidi za kimichezo ulimwenguni, tufuatilie hapa.

Leave A Reply


Exit mobile version