Klabu ya Singida BS imeuza hisa zake kwa mmiliiki wa Fountain Gate huku moja ya masharti ya mkataba ambao wameingia ikiwa ni pamoja na kutobadili jina na maskani ya timu hiyo.

Viongozi wa taasisi hizo mbili walikutana leo, Jumatano Juni 14 kwenye jijini Dar es Salaam na kuutangazia umma kupitia mkutano na waandishi wa habari juu ya hatua hiyo.

Aliyekuwa Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Singida BS, John Peter alisema katika mkutano huo; “Kwa mwaka mmoja tumekuwa kwenye Ligi Kuu, baada ya kupanda Ligi tulibadili jina na kuitwa Singida Big Stars, malengo yetu yalikuwa ni makubwa, ilikuwa kuingia kwenye nne bora,”

“Wenzetu wa Tukuyu waliingia Ligi Kuu na kuchukua ubingwa tofauti na sasa ambapo Ligi ni tofauti na zamani, Ligi hii imekuwa na uwekezaji mkubwa, hivyo hata ushindani nao umekuwa mkubwa,”

“Msimu ujao tutashiriki michuano ya Kimataifa, lazima tujipange na kuona tutafanikiwa kwa namna gani, tumekuwa navikao vingi, kazi kubwa sana imefanyika kufika hapa,”

“Tunawashukuru wadhamini wote, wametusaidia kuwa hapa, wametusaidia kusafiri bila matatizo na kuweka kambi bila tatizo, tumeshiriki mapinduzi na kushika nafasi ya pili yote haya mafanikio ni kwa sababu ya uwepo wao,”

Hakuishia hapo aliendelea kwa kusema; “Siku hizi gharama za uendeshaji wa klabu ni kubwa sana, tumetafakari hili pamoja na changamoto tulizonazo, tukatafuta na kuona nani wa kumtua mzigo, tukaona tuungane na hawa ndugu zetu wa Fountain, tulizungunza nao hawa wenzetu ambao wanajua kuhusu mpira kwa sababu wamekuwa na timu ya daraja la kwanza na hata Ligi Kuu kwa upande wa Wanawake,”

“Tumewasogelea ili kufanya nao biashara ili kuendeleza furaha ya mpira, tumekaa nao mezani na kukubaliana vipengele vya kuchukua timu na kununua, moja na sharti kubwa ni timu kubaki Singida na lazima neno Singida libakie kwenye timu ili kuenzi.”

Kwa upande wake, aliyekuwa Mkurugenzi wa Akademi ya Fountain Gate, Japhet Makau ambaye kwa sasa ni Rais wa klabu hiyo kwenye muundo mpya, alisema; “Tumeona fursa ambayo imetokea Singida BS, baada ya kuona watafute mtu wa kutake-over,”

“Singida BS, kwetu tumeona ni sehemu nzuri na kuona kuichukua Singida BS, timu kubaki Singida kwetu hiyo sio changamoto kabisa na Fountain inaweza kuwa Tanzania nzima,” alisema.

Makau alitangaza kwenye mkutano huo kuanzia sasa timu ya Fountain Gate Princess itafahamika kama Singida Fountain Gate Princess ili kukidhi matakwa ya CAF kushiriki michuano ya Kimataifa msimu ujao.

Miongoni mwa watu ambao watakuwa sehemu ya Bodi ya watu tisa ya Singida Fountain Gate FC, ni Festo Sanga na Mbunge wa Singida Mjini, Mussa Sima.

Leave A Reply


Exit mobile version