Wakati kila mmoja akiwa na hamu kubwa ya kuutazama mchezo mkubwa kabisa wa ligi kuu Tanzania Bara ambao unazikutanisha timu kutoka katika jiji la Dar Es Salaam lakini mchezo ukipigwa mbali kabisa na nje ambapo unapigwa katika jiji la miamba yaani Mwanza katika uwanja wa CCM Kirumba.
Tunafahamu kuwa mechi kama hizi tumezoea kuziona katika uwanja wa Benjamin Mkapa lakini safari hii haitachezwa kutokana na kuwa uwanja huu umefungiwa na serikali na upo katika matengenezo ili kuhakikisha kuwa unaendelea kukaa sawa lakini taarifa zikidai kuwa utatumika katika zile mechi za kimataifa pekee kwa timu za Simba na Yanga.
Baada ya danadana nyingi ilitangazwa kuwa mchezo huu utapigwa katika dimba la CCM Kirumba mkoani Mwanza tofauti na wengi ambao walitegemea labda mchezo huu ungepigwa mkoa wa karibu na Dar Es Salaam na kamwe siwezi kupinga uamuzi waliochukua klabu ya Simba kupeleka mchezo huu wa ligi kuu CCM Kirumba Mwanza kwani ni hatua kubwa katika kukuza michezo mikoani.
Tunafahamu kuwa kwa sasa hakuna timu ya ligi kuu kutoka Mwanza hivyo ni wazi mashabiki wa soka wa eneo hilo watapata fursa ya kushuhudia moja ya mechi kubwa kubwa ya ligi kuu jambo ambalo litaendelea kuongeza hamasa na upendo kwa mchezo.
Mara nyingi timu ambayo inakua nyumbani huwa wanafaidika na mapato ambayo huwa yanaingia katika mchezo husika jambo ambalo klabu ya Simba watafaidika pakubwa sana kutokana na kuwa mkoa wa Mwanza wameikosa burudani hii kwa muda mrefu na watu watakua tayari kuhakikisha kuwa wanalipia viingilio ili kushuhudia mtanange huu.
Lakini pia utajiuliza kuwa kuupeleka mchezo huu Mwanza wamefata alama 3 za mchezo huu au mapato? Jibu ni kwamba wamefata vyote na hii ni kutokana na upinzani mkubwa ambao Azam ameuonesha msimu huu na namna ambavyo msimamo wa ligi kuu ulivyo huku Simba wakiwa nafasi ya 3 lakini na mchezo mmoja mkononi.
Mchezo wa Simba dhidi ya Azam CCM Kirumba Mwanza tunategemea utakua na burudani kubwa lakini pia ni fursa kwa jamii na uchumi wa eneo la uwanja huo kuimarika.
1 Comment
Pingback: Niliyoyategemea Sijayaona Kabisa Simba vs Azam - Kijiweni