Kama mashabiki wa Simba walikuwa wakijiandaa kumuona Kiungo fundi wa kupiga mashuti makali, Sospeter Bajana kutoka Azam FC, basi pole yao kwani, mabosi wa Chamazi wameamua kumzuia jumla kwa kumuongezea mkataba wa miaka miwili hadi mwaka 2025.

Simba ilikuwa kwenye mipango ya kumnasa Bajana na kumpa mkataba wa awali ili avae uzi wa klabu hiyo kwa msimu ujao baada ya kubaini mkataba wake na Azam ulikuwa ukingoni mwishoni mwa msimu huu, lakini ghafla upepo umebadilika.

Mabosi wa Azam baada ya kugundua Simba ilikuwa ikimnyemelea nahodha huyo na kuamua kumpa mkataba mpya, hivyo kuipa kazi Simba kuhaha kusaka kiungo mwingine sehemu nyingine.

Azam imeamua kumbakiza kikosini hapo kiungo huyo aliyekulia kwenye akademi ya timu hiyo kabla ya kujiunga na timu kubwa, baada ya kumaliza mkataba na kuonekana kuwindwa na klabu ya Simba.

Moja ya kiongozi wa juu wa Azam (jina tunalo), amethibitisha kumpa mkataba mpya Bajana na sasa kinachosubiliwa ni kutangazwa tu ambapo zoezi hilo litafanyika baada ya fainali ya Kombe la TFF (ASFC), itakayopigwa Juni 12, mwaka huu, Mkwakwani Tanga.

“Bajana haendi popote, tayari amesaini mkataba mpya wa miaka miwili hivyo kama kuna timu zilikuwa zinammendea ndio imeshakula kwao.

Ni kweli alikuwa anamaliza mkataba msimu huu lakini tumemuongezea na tunatarajia kutangaza baada ya kumaliza fainali ya ASFC. Sio  yeye tu, bali na wachezaji wengine wengi tu tumewaongezea mikataba.”

Leave A Reply


Exit mobile version