Simba SC ipo sokoni kuangalia silaha za kuondoa aibu kwa msimu ujao na unyonge wa mashabiki wanaoupitia kwa msimu huu, ikidondosha mataji yote, tayari imetua nchini Ivory Coast ikiwinda winga la ASEC Mimoses, huku mastaa wakilimwa barua.
Winga ambaye Simba ipo naye kwenye mazungumzo mazito kuhakikisha inaipata saini yake kuja kuongeza nguvu zaidi kikosini anatajwa kwa jina la Kramo Aubin.
Huyo jamaa ni hatari kwa mikimbio na Simba ilishaonja joto la jiwe la mchezaji huyo aliwahi kuwafunga mwaka 2022 walipocheza Kombe la Shirikisho la Afrika, wakichapwa mabao 3-0 ugenini lakini pia msimu huu amekuwa bora kwenye michezo yote.
Wakati winga huyo akitajwa kuna asilimia kubwa ya kujiunga na Wanamsimbazi, dili hilo likitiki atapishana na Augustine Okra, Nelson Okwa, Ismael Sawadogo na Gadiel Michael ambao tayari wamepewa barua za kwaheri klabuni hapo.
Mastaa hao tayari wamepewa barua za kuachana na timu hiyo baada ya kushindwa kuonyesha uwezo ambao walikuwa wanautarajia kutoka kwao Okrah, Okwa walisajiliwa dirisha kubwa la usajili msimu huu wakati Sawadogo akisajiliwa dirisha dogo huku Gadiel alijiunga na Simba akitokea Yanga msimu wa 2019.
Chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya Simba kilieleza kuwa uongozi upo kwenye hatua nzuri za mazungumzo kwa ajili ya kumalizana na staa huyo wa Asec ambaye wanaamini ataweza kuongeza kitu ndani ya timu.
Kramo Aubin amecheza mechi nane za Kombe la Shirikisho Afrika na kuifungia timu yake mabao manne kwenye michezo hiyo moja alilifunga uwanja wa nyumbani na matatu kwenye michezo ya ugenini.
Staa huyo amecheza timu tatu tu hadi sasa zote zikiwa za nchini kwao Ivory Coast amekuzwa na ASEC Mimosas ambayo alianza kuitumikia mwaka 2015 akicheza kwa misimu miwili baadae akatimkia Africa Sports alicheza msimu mmoja, 2019 alitimkia FC San Penro na 2021 akaamua kurudi tena ASEC Mimosas ambayo anaitumikia hadi sasa.