Ligi Kuu ya Wanawake Tanzania Bara imeanza rasmi  huku mabingwa watetezi, JKT Queens na washindani wao wa karibu, Simba Queens wakianza kwa kugawa dozi nzito.

Timu hizo msimu uliopita zilipelekana mbio kwenye ubingwa wa Ligi Kuu ya Wanawake hadi pale michezo ya mwisho ilipoamua JKT kuwa mabingwa.

Pia katika maandalizi ya msimu huu, timu hizo zimepimana ubavu baada ya kucheza fainali ya michuano ya Ngao ya Jamii huku Simba ikiibuka bingwa kwa mikwaju ya penalti 5-4.

Mabingwa watetezi, JKT ilianza vyema kwa ushindi wa mkubwa wa mabao 4-0 dhidi ya Bunda Queens, mchezo uliopigwa leo kuanzia saa 10 jioni katika Uwanja wa Karume, mjini Musoma.

Mabao ya JKT yalifungwa na nyota mpya waliyemnasa kutoka Fountain Gate Princess, Winfrida Gerald aliyetupia mabao mawili, staa wa timu hiyo, Stumai Abdallah alifunga bao la tatu huku Donisia Minja akipigilia msumari wa nne na kuzamisha jahazi la Bunda ambao ni wageni kwenye Ligi Kuu.

Kwa upande wao, Simba iliyowahi kubeba taji hilo misimu mitatu mfululizo, imeibuka na ushindi mnono wa mabao 5-0 dhidi ya Ceassia Queens ya Iringa kwenye Uwanja wa Azam, Chamazi.

Simba imepata mabao yake kupitia kwa Aisha Mnunka aliyetupia mabao matatu (hattrick) na kuweka rekodi ya kuwa mchezaji wa kwanza msimu huu kufunga mabao matatu katika mchezo wa ufunguzi.

Mabao mengine ya Mnyama, yametupiwa kambani na mkongwe, Mwanahamisi Omary pamoja na nyota, Asha Djafari raia wa Burundi ambaye msimu wa mwaka 2021/2022 aliibuka mfungaji bora wa ligi hiyo akifunga mabao 27.

Ligi hiyo inashirikisha timu 10 za Simba Queens, JKT Queens, Fountain Gate Princess, Yanga Princess, Baobab, Bunda Queens, Alliance Girls, Geita Gold, Amani Queens na Ceassia Queens na bingwa ataiwakilisha Tanzania kwenye Ligi ya Mabingwa ukanda wa Afrika Mashariki, huku timu mbili zitazoshika nafasi za mwisho zikishuka daraja.

Endelea kufuatilia zaidi kuhusu taarifa za ligi kuu kwa kusoma hapa.

 

Leave A Reply


Exit mobile version