Simba SC imerejea mazoezini kuanza kujifua kwa ajili ya mechi ya mwisho ya makundi Ligi ya Mabingwa Afrika ugenini Morocco dhidi ya Raja Casablanca, itakayopigwa April Mosi jijini Casablanca, huku wana Msimbazi hao wakiwa na mpango wa kuwalipa kisasi waarabu hao nyumbani kwao.

Raja ndio kinara kwenye Kundi C ikiwa na pointi 13, huku Simba ikiwa nafasi ya pili ikikusanya pointi tisa na zote zikiwa zimeshafuzu robo fainali ya michuano hiyo na mechi hiyo ya mwisho ya kufungia hesabu itakuwa ni ya kutafuta heshima ikizingatiwa mchezo wa awali Simba SC walipoteza kwa goli 3-0.

Kwa kuitambua umuhimu na mechi yenye heshima na ya kulipa kisasi kutokana na kipigo hicho kikubwa ilichopewa timu yake nyumbani, Kocha Mkuu wa Simba Roberto Oliveira ‘Robertinho’ alieleza kuwa ameandaa mkakati tofauti wa kucheza mechi na Raja Casablanca kutokana na wachezaji wake wengi wa kikosi cha kwanza kuwa kwenye majukumu ya timu zao za taifa kwa sasa.

Wachezaji hao walio katika majukumu ya Timu ya taifa ni Makipa Aishi Manula na Beno Kakolanya, kiungo Mzamiru Yassin (Tanzania), Clatous Chota Chama (Zambia), Henock Inonga (DR Congo), Peter Banda (Malawi), Pape Sakho (Senegal) na Saido Ntibazonkiza (Burundi).

Robertinho aliongeza na kusema kuwa mechi ya marudiano itakuwa tofauti kidogo, watacheza kimkakati na kuhakikisha wanapata matokeo mazuri licha ya ugumu uliopo na pia kutakuwa na mabadiliko kwenye kikosi, na kuwa timu ina wachezaji wengi na watapata nafasi ya kufanya vizuri kwenye mchezo huo.

Robertinho alisema moja ya sapraizi aliyowaandalia Raja ni kuwatumia zaidi wachezaji ambao hawatumiki mara kwa mara, huku akiwataja Kennedy Juma, Erasto Nyoni kuwatumia katika pambano hilo la kukamilisha ratiba ya makundi ya michuano hiyo ya CAF.

Kurejea kwa Hassan Dilunga ni faraja kwa Kocha Robertinho, na kusema kuwa anaendelea kumuangalia zaidi mchezaji huyo licha ya kutokuwepo kwenye usajili na kuongeza kuwa anahitaji muda zaidi ili kufanya tathmini iliyo bora na mwisho wa siku kukamilisha ripoti yote ya kikosi na mahitaji katika uongozi wa Simba SC kwa ajili ya msimu ujao.

Leave A Reply


Exit mobile version