Ilipoishia “Yaani Mama kisa tu ana hela basi umechanganikiwa kiasi  hicho, kweli umasikini mbaya sana Mama, ila usijali siku siyo  nyingi nitaanza kazi nitakufanyia kila kitu, sawa Mama?” 

“Mmh! Sawa” Mama alisema kisha aliondoka zake ila aliniacha  na jambo la kufikiria ndani ya akili yangu, nilikumbuka  kitendo chake cha kuondoka pale wodini baada ya Mosses  kuingia, ila ni yeye ndiye aliyempigia simu Mosses baada ya  kuchukua namba kwenye simu yangu.  Endelea

SEHEMU YA TATU

Sikutaka sana kuanza kufikiria hilo jambo, niliona ni bora  niwasiliane na Mosses maana baada ya kuachana naye kule  Hospitali sikuongea naye kabisa, simu ya Mosses ilikuwa  imezimwa, ilinipa maumivu makali sana ndani ya moyo wangu,  nilijigeuza geuza kisha Usingizi ulinichukua. 

Kulipopambazuka nilianza kuhisi hali ya tofauti, mwili  ulianza kuchoka hadi nilijishangaa, Mama aliendelea  kunihudumia huku akiendelea kutafuta uwezekano wa kupata  Figo, alienda kwa daktari ambaye aliunganishwa na Osman,  upatikanaji wa Figo ulikuwa mgumu sana huku hali yangu  ikizidi kudhohofu, nilikuwa napewa dawa tu nimeze, maumivu  niliyokuwa nikiyasikia kwenye tumbo langu yalikuwa makali  sana nilitamani hata kufa kabisa, kwa siku zote hizo  sikumuona wala kumpata Mosses kwenye simu, ilizidi kunifanya  niwe mgonjwa zaidi. 

“Mama Mosses hapatikani leo siku ya kumi na mbili”  Nilimueleza Mama 

“Usijali pengine amepatwa na tatizo kama hapa anapajuwa basi  atakuja siku moja” Alisema Mama, angalau alinipa moyo na  tumaini, lakini nilimuuliza

“Haya maumivu makali yanatokana na nini Mama? Mwili wangu  hauna nguvu kabisa nazidi kudhohofu” Nilipomuuliza niliona  macho ya Mama yaliyojaa maumivu, alitamani kulia lakini  hakusema shida iliyokuwa ikinisumbua 

“Utapona Mwanangu! Mungu ni mwingi wa huruma, atakujalia afya  njema Binti yangu” Alisema Mama kisha alininywesha uji 

“Hivi umewasiliana na Osman Mama?” Nilimuuliza Mama 

“Ndiyo usiwe na wasiwasi ukipona tu utaanza kazi, pumzika kwa  sasa” Mama alikuwa ameshamaliza kuninywesha uji, alinifuta na  kuondoka zake, alipofika chumbani kwake alilia sana sababu  tumaini la Mimi kupona lilikuwa hafifu sana, siku zilisogea. 

Mama pamoja na daktari walijitahidi kutafuta Mtu wa kunitolea  Figo, walitangaza dau kubwa kadili siku zilivyokuwa zikienda  ila waliojitokeza walikuwa ni Watu wenye Afya zisizoridhisha,  figo zao pia zilionekana kuwa na Hitilafu, hazikufaa.  Ilipofika siku ya 20 nilipekwa Hospitalini nikiwa katika hali  mbaya sana, nilikuwa sijitambui kabisa. Mama yangu alikuwa  Mtu wa kulia kila wakati, pesa ilipatikana kwa ajili ya Figo  lakini mtoaji wa figo hakupatikana, daktari alimwambia Mama 

“Hakuna namna tunaweza kufanya, nahisi kukata tamaa Mama  Jacklin” Alisema Daktari wakiwa ofisini kwa Daktari huyo  aliyeitwa Dokta Simon 

“Unaposema hivyo daktari unanipa wakati mgumu wa kuangalia  mbele, sitaki kuamini kama siku za kuishi za Jacklin zimefika  mwisho, Huyu ndiye Binti yangu wa pekee, sisi ni masikini  sana, basi toa figo yangu kwa ajili ya Binti yangu” Alisema  Mama, ilifika wakati ambao Mama alishindwa kuhimili maumivu  aliyokuwa akiyasikia katika kifua chake 

“Mama Jacklin, umri wako na hilo jambo haviwezi kwenda  sambamba. Najuwa tumaini ni dogo sana katika jambo hili,  lakini…” 

“Dokta, kama kufa Mimi kutamsaidia Binti yangu hilo siyo  tatizo, hajawahi kuishi Maisha ya furaha katika Maisha yake,  ndiyo kwanza alikuwa amepata kazi….leo afe aaaah hapana”  Alisema Mama akiwa analia, alionesha uchungu wake kwangu 

“Sawa Mama! Ngoja tuiangalie kama itafaa” Alisema Dokta  Simon, kisha waliongozana hadi chumba cha Uchunguzi. Mama  alitakiwa kufanyiwa uchunguzi wa figo yake ili niwekewe Mimi  nipate kunusuru Maisha yangu ambayo yalikuwa hatua za mwisho  sana.

Huu ndiyo upendo ambao Mama huwa nao kwa Mtoto wake,  watakukimbia wote katika Maisha lakini Mama yako atasimama  kwa ajili yako kila siku za Maisha yako, Mama alianza  kufanyiwa uchunguzi. Bahati mbaya figo ya Mama ilikuwa na  Mawe hivyo isingeliweza kunifaa, Mama alilia sana 

“Dokta weka hiyo hiyo ili Jacklin aamke, tumaini langu ni  yeye pekee” Mama alilia hadi Dokta Simon alidondosha Chozi  lake 

“Mama usilie, tuna siku 10 zilizobakia, Mungu atafanya wepesi  wa hili jambo, kwasasa Jacklin anahitaji Maombi” Alisema  Dokta Simon, Mama alifikiria afanye nini, alichukua namba ya  Mosses kisha aliipiga akiwa Hospitalini 

Bahati nzuri siku hiyo simu ya Mosses iliita aliipokea, Mama  alimueleza Mosses hali ya afya yangu kwa wakati huo, Mosses  alimwambia Mama kuwa alipata tatizo ndiyo maana alishindwa  kuja akaahdi kuwa atakuja Hospitalini. Kweli, Mchana Mosses  alifika Hospitalini, aliishuhudia hali ya Afya yangu ambayo  alisimuliwa kama hadithi za Amza Stories, alikubali kuwa Mimi  nilikuwa mgonjwa sana kwa jinsi nilivyodhohofu, pumua yangu  ilikuwa ya shida mno 

“Hali ndiyo hiyo, leo siku ya tatu haongei wala hafumbui  Macho. Kama unampenda Jacklin jitolee Mosses Mungu atakulipa  kwa wema wako” Mama alisema, walikuwa wodini wakiwa na yule  Daktari Simon 

“Mama Mimi nitajitoa kwenye nini tena ikiwa mmetangaza dau  kubwa na bado figo haijapatikana, tumuombee Jacklin pengine  Mungu atampa nafuu” Alisema Mosses 

“Kuomba tunaomba lakini hatuwezi kukaa kimya bila kufanya  jitihada zozote Baba, mimi leo siku ya tatu sijala chochote,  nione sina raha kwasababu ya Jacklin” Alisema Mama huku  akibubujika Mchozi, Dokta Simon aliingilia kati akamwambia  Mosses 

“Ndugu najuwa inaweza kuwa ngumu kwako lakini kama huyu Mtu  ana umuhimu kwako jitolee figo moja kwa ajili ya kumuamsha”  Alisema Dokta, Mosses alishtuka akauliza 

“Nitoe nini?” 

“Figo kwa ajili ya Mpenzi wako” Alijibu Dokta Simon huku Mama  akiwa analia pembeni,

“Nitoe figo? Hiyo ni hatari sana Dokta nitafanya vyote lakini  siyo kutoa figo yangu, ingekuwa wote wanaopendana wanatoleana  viungo basi hii Dunia ingejaa walemavu kila kona” Alisema  Mosses, Maneno yake yalimchukiza sana Mama alinyanyuka na  kumpiga kofi Mosses 

“Mama hupaswi kufanya hivyo hapa ni Hospitalini istoshe ni  wodini ambako panahitaji utulivu sana” Alisema Dokta Simon 

“Dokta huyu ni mshenzi anawezaje kusema maneno ya kikatili  namna hiyo hakuona neno lingine la kusema? Huyu si ndiye  ambaye alikuwa akikupa furaha, leo amelala hujali tena si  ndiyo?” Alihoji Mama huku akiwa anahema juu juu 

“Unathubutu vipi kunipiga Mimi? Unanijuwa Mimi? Kama Maisha  yake ni muhimu kwangu basi hata kwako ni Muhimu kwanini wewe  usitoe hiyo figo? Siwezi kutoa kiungo kisa Mapenzi tena kwa  kiumbe anayeitwa Mwanamke, Jacklin akipona Mimi nipo akifa  Maisha yataendelea” Alisema Mosses kisha aliondoka Wodini,  Mama alilia sana, kauli ya Mosses ilizidi kumfanya akate  tamaa, Dokta Simon alimwambia Mama 

“Siku bado zipo tuzidi kufanya jitihada na Maombi” Alisema  kisha aliondoka zake, Mama aliendelea kulia kwa kukata tamaa  alinisogelea akasema 

“Jacklin nimekuzaa kwa shida sana, nimekulea kwa tabu mno,  leo nakupoteza Mama kwa shida sana, Nisamehe Mama yako  nimefanya jitihada zote lakini nimeshindwa Mimi sababu hata  Mungu hayupo upande wangu tena” Maneno ya Mama niliyasikia,  Chozi lilinivuja, sikuwa na nguvu ya kufanya chochote kile 

••••••••••••••••••••••••••••••••• 

Ndani ya Dubai, Kilichompeleka Osman Dubai kilikuwa ni  kumtafuta Zahra, achana na kiasi kikubwa cha pesa ambacho  Mwanamke huyo aliondoka nacho na kwenda huko kuishi na  Mwanaume mwingine, Osman alikuwa akimpenda sana Mwanamke  huyo, jitihada za kumpata Zahra ziligonga mwamba. Alirudi  Nchini, aliitafuta Familia ya Zahra lakini wazazi wa Zahra  walionekana kufurahia ambacho Bitni yao alikifianya. 

Hawakuwa na huruma, Osman alijitoa sana kuhakikisha Maisha ya  Wazazi wa Zahra yanakuwa bora, aliwajengea jumba la kifahari,  aliwanunulia magari ya kutembelea, alibadilisha Maisha yao  kwa kiasi kikubwa sana, Osman aliondoka na kwenda kwenye  gari, alikumbuka jinsi ambavyo aliishi kwa furaha na amani na  Zahra, alilia sana, Maumivu yalijaa ndani ya kifua chake  alipoikumbuka meseji ya mwisho ambayo Zahra aliituma, meseji  hiyo ilisema

“Osman! Najua ujumbe wangu utakupa maumivu makali sana lakini  inabidi uupokee sababu ndiyo maamuzi yangu, asante kwa  kubadilisha Maisha ya Wazazi wangu kwa kiasi kikubwa lakini  hukuwa chaguo la Moyo wangu japo ulinipenda sana, kwasasa  mimi nipo Dubai na Mwanaume ambaye ninampenda. Usiwazumbue  wazazi wangu wala usinitafute, pesa zote zilizo kwenye  akaunti yako ya Benki nimezichukua, unaweza kujiona Mjinga  lakini hiyo ndiyo nguvu ya Mapenzi ambayo ninayo, nilikufanya  ukawa dhahifu kwangu! Nakutakia Maisha Mema, ni Mimi Zahra” 

Ulikuwa ndiyo ujumbe wa Zahra baada ya hapo simu yake  haikupatikana tena,, alipoupata ujunbe huo Osman alipoteza  fahamu akaenda kuzinduka kwenye Hospitali ya Dokta Simon,  aliishi Maisha yaliyojaa maumivu na aliapa kuwa hatokuja  kupenda tena. 

Basi, alifuta chozi akiwa ndani ya gari yake ya kifahari,  alipotoka kwa Wazazi wa Zahra alikuja moja kwa moja  Hospitalini maana aliwasiliana na Mama na akaambiwa kuwa hali  yangu siyo nzuri na haina tumaini. 

Alimkuta Mama akiwa analia nje, Osman alimuuliza Mama “Hali yake kwasasa ipoje Mama?” Alimuuliza baada ya salam 

“Kama nilivyokueleza Baba, hali ya Jacklin ni mbaya sana,  ninahofu juu ya uhai wake” Alisema Mama akiwa anaendelea  kumwaga chozi 

“Pole Mama, wakati mwingine Dunia inakuwa katili sana, naomba  nikamuone” Alisema Osman, walirudi wodini, Osman aliponiona  hakuamini kama ni Mimi ndiye niliyemchachafya siku kadhaa  zilizopita, nilikuwa nimekonda sana, nilikuwa nikipumua kwa  shida sana, alidondosha chozi akamuuliza Mama 

“Upatikanaji wa figo?” Mama alitikisa kichwa kuashiria kuwa  hakukuwa na uwezekano wa kupatikana figo kabisa japo  zilisalia siku 10 

“Nitarudi Mama” Osman alitoka haraka akaelekea ofisini kwa  Dokta Simon. 

“Bilonea Kijana karibu sana” Alisema Dokta Simon sababu  alikuwa akimfahamu sana Kwa ukaribu Osman 

“Dokta Simon, Mama Jacklin amesema uwezekano wa kupatikana  Figo ni mdogo sana, nataka kusikia kutoka kwako!” 

“Huo ndiyo ukweli Osman, kilichobakia ni kudra za Mwenyezi  Mungu pekee, tumepima Watu wengi lakini hakuna hata mmoja mwenye figo yenye afadhali alafu kibaya zaidi Mpenzi wa huyo  Jacklin amegoma kufanya hivyo” Alisema Dokta Simon 

“Nitatoa Figo yangu” Alisema Osman, kauli hii ilimshtua sana  Dokta Simon 

“Unatoa figo yako? Umefikiria mara mbili Osman? Hii familia  inakuhusu nini wewe ikiwa mpenzi wa Jacklin amekataa, ufanye  hivyo wewe kama Nani? Umesahau kilichokutokea Osman?”  Aliuliza Dokta Simon 

“Natoa kama Binadamu niliyeguswa na hili Dokta Simon, Maisha  ya yule Msichana ni tunu Kwa Mama yake, ni furaha kwenye  macho ya Mama yake ambaye muda wote analia. Umewahi kufikiria  jinsi Mama yule anavyokosa raha kwasbabu ya Binti yake?  Unajuwa ni furaha kiasi gani ataisikia endapo Binti yake  atasimama tena?” Aliuliza Osman kwa hisia kali sana 

“Fikiria mara mbili sikushauri kufanya hivyo Osman, wewe ni  Bilionea Mkubwa hupaswi kuishi Maisha yenye kasoro kiasi  hicho!” 

“Mkamilifu ni Mungu pekee, nitatoa Figo yangu kuokoa Maisha  yake” Alisema Osman kisha aliondoka akarudi Wodini, Dokta  Simon hakukubaliana na uamuzi wa Osman alinyanyua simu na  kuwapigia Wazazi wa Osman, aliwapata taarifa hiyo ambayo  iliwakasirisha sana Wazazi wa Osman 

Basi, Osman aliporudi alimwambia Mama kuwa nitapona na kuanza  kazi mara moja, japo Mama alikuwa katika hali ya huzuni sana  ila maneno ya Osman yalimjaza tumaini. 

Alipotoka Hospitalini Osman alikuwa mwenye mawazo na maumivu  makali sana, alipigiwa simu na Wazazi wake na kumtaka aachane  na mpango wa kutaka kutoa figo kwani haitokuwa na faida  yoyote kwake, Wazazi wa Osman waliamini kuwa Osman alikuwa  akitaka kutoa figo kwa ajili ya Mapenzi, walinuonya sana kwa  kile kilichomtokea kwa Zahra ila Osman aliwaambia Wazazi wake  kuwa hana mahusiano ya kimapenzi na Mimi bali ni ubinadamu tu  wa kutaka kuhakikisha afya yangu inaimarika. 

Osman aliwasiliana na Hospitali nyingine ambayo ingefanya  operesheni ya kupandikiza figo kwenye mwili wangu, kutokana  na utajiri alionao aliweza kupata Hospitali Nchini India,  tulisafiri kwenda huko. Osman alishauriwa na kuambiwa kila  kitu kiafya kuhusu uamuzi wake. 

Nini Kitaendelea? Osman atatoa FIGO? Usikose Sehemu Ya NNE Ya PUMZI YA MWISHO

Mpe Nguvu ADMIN Kwa ajili ya bando Kwa kumtumia Chochote aendelee kupost RIWAYA Mpya Hapa Kijiweni

Lipa Namba: 57900454
Jina: LIPA KIJIWENI TIPS
Mtandao: VODACOM  

SOMA RIWAYA YA KOTI JEUSI KWA KUBONYEZA HAPA 

SOMA RIWAYA YA FUNGATE KWA KUBONYEZA HAPA 

SOMA RIWAYA YA NILIPANGA NYUMBA MOJA NA MAJINI 

SOMA RIWAYA YA GORYANAH HAPA 

SOMA KISASI CHANGU HAPA  

SOMA RIWAYA YA MSALA HAPA

JIUNGE NIPO KIJIWENI Kwa Kubonyeza Hapa

 

Pumzi Ya Mwisho xx Pumzi Ya Mwisho xx  Pumzi Ya Mwisho xx Pumzi Ya Mwisho xx Pumzi Ya Mwisho xx Pumzi Ya Mwisho xx Pumzi Ya Mwisho xx Pumzi Ya Mwisho xx 

14 Comments

    • Ila sas ili ujue binadamu jau😄😄😄 au ngoja …. nisiharibu uhondo siku ikifikia ntakwambiaa…hii tamthiliya inaweza kuliza watu huko mbele 🥲🥲🥲 me siyo mtabiri akin

Leave A Reply


Exit mobile version