Mvua ilikuwa ikinyesha, moyo wangu ulijawa na tabasamu kubwa  sana, nilijinyoosha ili kuianza siku mpya ambayo ilianza kwa  hali ya hewa kuwa nzuri yenye ubaridi. Niliposhika simu yangu  niliona picha ya Mwanaume niliyempenda sana. Niliiweka kwenye  kioo cha simu yangu, alikuwa akiitwa Mosses, alikuwa ni  mwanaume aliyeuteka moyo wangu sana, nilimpenda kwa nguvu  zangu zote, hisia zangu ziliniambia Mosses ndiye Mume wangu. 

Tabasamu lilikuwa limejaa usoni pangu, nilimpigia Mosses ili  niweze kusikia sauti yake, sauti ambayo ilikuwa ndiyo tulizo  pekee la nafsi yangu! 

“Hello My love” Nilisikia sauti ya Mosses ikisema, basi moyo  wangu ulifurahi sana, wewe msomaji unaweza kuwa shahidi wa  hili ile furaha unayoipata unapoongea na mpenzi wako nyakati  za asubuhi basi ndiyo iliyonivaa wakati huo. Kwanza nilihema  kidogo ili niweze kumjibu Mosses 

“Mambo Mpenzi, bado haujaamka?” Nilimuuliza Mosses kwa sauti  iliyojaa bashasha. Mosses alinijibu 

“Ndiyo naamka Mpenzi, yaani huwezi amini nimetoka kukuwaza  muda huu nawe ndiyo unanipigia, hakika tunaishi katika Dunia  yetu iliyojaa Huba zito Jacklin” Alisema Mosses, mara zote  alikuwa na maneno matamu sana kwangu kitu ambacho kilinifanya  nizidi kuvutiwa nawe, mara mlango wa chumba changu uligongwa,  nilisikia sauti ya Mama ikiwa inaniita. 

“Samahani Mosses, Mama ananiita” nilisema 

“Haya ukimaliza niambie” Alisema Mosses 

“Sawa Mume wangu mtarajiwa” Nilisema kisha nilimwambia kuwa  nampenda sana na kamwe sitoweza kumsaliti. Mara moja nilikata  simu, nilinyanyuka kitandani na kwenda kuitika wito wa Mama 

“Shikamoo Mama” Nilimsalimia baada ya kuwa nimeshafungua  mlango, nilikuwa nafikicha macho yangu kutokana na Mwanga  uliokuwa ukimulika macho yangu.

“Marhaba!! Ndiyo unaamka sasa hivi Jacklin? Umesahau kama leo  unatakiwa kwenda kwenye Interview?” Alisema Mama 

“Oooh Mungu wangu nilishasahau ngoja nijiandae Mama” Nilisema  kisha nilikimbilia Bafuni kuoga, siku hiyo ilikuwa ni siku ya  Jumatatu nilipaswa kwenda kwenye interview ya kazi katika  kampuni moja ambayo niliomba nafasi miezi michache iliyopita,  Mama alinitazama hadi nazama Bafuni kisha aliingia chumbani  kwangu na kuanza kukagua vitu vyangu. 

Aliona kadi za mapenzi ambazo Mosses alikuwa akinitumia,  alitikisa kichwa chake kisha aliondoka chumbani kwangu. 

Asubuhi hiyo hiyo, kwenye moja ya jumba la kifahari alikuwepo  Mtoto wa kitajiri aliyeitwa Osman, alikuwa mweupe mwenye  asili ya uarabu, ndiye mmiliki wa kampuni ambayo Mimi  nilitakiwa kwenda kufanyiwa usaili kwa ajili ya kazi, huyu  Osman ni Mwanaume mwenye maumivu makali ndani ya moyo wake  kwani miezi miwili iliyopita aliachwa na Mwanamke  aliyetarajia kumuowa, Mwanamke huyo aliitwa Zahra, huyo Zahra  alitoroka na kiasi kikubwa cha pesa kisha kwenda nje ya Nchi,  alimtumia ujumbe Osman kuwa hamuhitaji tena katika Maisha  yake, tokea siku hiyo Osman amekuwa ni Mwanaume mwenye  kuutafuta upendo wa kweli. 

Asubuhi hiyo Osman aliondoka kwenye jumba hilo na kuelekea  kwenye kampuni ambayo mimi nilikuwa naenda kufanya usaili,  kutokana na mvua kubwa kunyesha kulisababisha foleni kubwa  iliyoniweka kwa zaidi ya dakika hamsini, nilikuwa tayari  nimechelewa kwenye Usahili, pembezoni mwangu kulikuwa na gari  aina ya Benzi nyeusi, alionekana huyo Osman akiwa anaangalia  sana saa yake, ilikuwa ndiyo mara ya kwanza namuona, jinsi  alivyokuwa akihangaika kuangalia saa yake ilinipa moyo kuwa  siyo mimi tu niliyechelewa kwenye jambo bali tupo wengi  pasipo kujuwa huyo Mtu ndiye mmiliki wa hiyo kampuni. 

Nikiwa kwenye daladala, Mosses alinipigia akaniuliza niko  wapi, kiukweli jinsi nilivyokurupuka nyumbani sikuweza hata  kumuaga kuwa naenda kwenye Usahili, ilinibidi nimueleze kuwa  nipo kwenye daladala naelekea kwenye Usahili ila nimechelewa. 

“Kama ni hivyo basi chukua pikipiki nitakutumia pesa kidogo  ulipe maana hapo utazidi kuchelewa” Alisema Mosses,  alinifanya nitabasamu, niliona ndiye Mwanaume anayenijali  kuliko Wanaume wote Duniani. Basi nilishuka, nilimuona pia  Osman naye akishuka kwenye gari, sote tulitazama upande mmoja  tukaita pikipiki moja iliyokuwa karibu, ilitushangaza kuona  sote tunamuita Bodaboda huyo, Osman alinitazama nami  nilimtazama kwa sekunde kadhaa kisha alinisogelea sababu yule Bodaboda alikuwa akija kwangu, si unajuwa tena Mwanamke  ananguvu kubwa sana kwa Mwanaume? Basi ndivyo ilivyokuwa kwa  Bodaboda huyo 

“Samahani Dada yangu naomba usubirie Pikipiki nyingine mimi  nina dharura kuna Watu wananisubiria!” Alisema Osman, maneno  yake yalinifanya nimuulize 

“Ina maana wewe ndiye mwenye haraka peke yako? Hata Mimi  nasubiriwa huko ninakoenda hivyo wewe ndiye unayepaswa  kusubiria nyingine” Nilisema kwa haiba ya kike, ilikuwa ndiyo  mara ya kwanza namuona Osman, sikujuwa kama ndiye mmiliki wa  hiyo kampuni niliyokuwa naenda kwenye Usahili. Bodaboda  aliingilia kati 

“Kwani wewe Bro unaenda wapi na wewe Sistaa unaenda wapi?”  Aliuliza Bodaboda huyo 

“JM Motors” Nilisema 

“JM Motors” Alisema Osman, sote tulijikuta tukiitaja sehemu  moja ambayo ndiyo hiyo kampuni ya Uuzaji wa Magari kutoka  Dubai 

“Sasa si unaona mlitaka kunikosesha pesa za vichwa viwili,  panda sistaa huyo jamaa aje kwa nyuma” Alisema Bodaboda huku  manyunyu yakianza tena 

“Siwezi kuanza, apande yeye mimi nitakaa nyuma” Nilisema,  Osman alicheka tu kisha alisema 

“Naitwa Osman Dhabi” alinipatia Mkono kwa lengo la kutaka  kunifahamu pia lakini sikutaka mazoea naye kabisa, sikumpa  mkono wangu, Osman alitabasamu tu kisha alipanda kwenye  pikipiki kisha nami nilifuatia. Safari ilianza kuelekea JM  Motors, Osman alionekana kuwa muongeaji kiasi, niliwasikia  wakiongea kuhusu Wanawake ili sikutaka kujali sana, mwendo wa  dakika kama 30 hivi tulifika JM Motors huku mvua ikianza  kuchanganya, Niliposhuka tu nilikimbilia kujihifadhi kwenye  maegesho ya Magari nikiwa natetema baridi, Osman alilipa pesa  ya Pikipiki kisha yule Bodaboda aliondoka, niliangalia simu  yangu kuona kama Mosses alikuwa amenitumia pesa ya Pikipiki  lakini alikuwa bado hajatuma. 

Osman alisogea akaniambia 

“Nimeshalipa usijali” Alisema kisha alitabasamu tu, kwangu  niliona kama amenidharau hivi, nilifungua pochi yangu nikatoa  elfu tano ambayo ndiyo ilibakia hiyo hiyo ya kurudia  nyumbani, nilimpa Osman

“Huwa sipendi vitu vya Bure” Nilisema kwa hasira 

“Samahani sikujuwa kama ungechukia, upo hapa kwa ajili ya  Usahili?” Aliniuliza 

“Ukijuwa itakusaidia nini? Sihitaji mazoea ya kijinga”  Nilisema kisha niliekea ambako Watu walikuwa wakiingia, Osman  alitabasamu tu akiwa ndani ya Shati jeupe ambalo lilikuwa  limeloa na suruali nyeusi iliyomkaa vizuri, moyo wangu  uliniambia kuwa Mwanaume huyo alikuwa na mvuto sana ila  alikuwa na dharau. 

Nilipofika ndani nilielekea mapokezi, niliambiwa kuwa Bosi  anayepaswa kutufanyia Usahili bado hajafika hivyo nilioneshwa  chumba ambacho Watu wanaotakiwa kusahiliwa walikuwepo, wakati  natembea nilihisi kupoteza kitu. Ndiyo, nilisahau Bahasha  yenye vyeti vyangu ndani ya ile Daladala. 

Roho iliniuma sana na sikuuona umuhimu wa Usahili tena,  nilitamani kuondoka lakini yule Mdada alisema 

“Ingia chumba hicho Bosi huyo anakuja” Alikuwa kama  amenishtua hivi, haraka niliekelea kwenye chumba hicho bila  kugeuka nyuma. 

Nilijaribu kumtumia ujumbe Mosses lakini hakujibu, nilimpigia  lakini hakupokea simu yangu, nilijiona nina mzigo ndani ya  moyo wangu, nilimpigia Mama kumueleza hali halisi, aliniambia  kuwa alibakiwa na pesa ile aliyonipa hivyo labda baadaye  anaweza akapata kisha akanitumia. 

Osman alielekea ofisini kwake, alibadilisha nguo zake huko,  alikuwa ni Kijana wa kisasa na mwenye pesa sana, alikuwa  akisimamia miradi mingi ya Baba yake Mzee Dhabi aliyeko  Dubai. 

Tulipaswa kusubiria kwa zaidi ya saa nzima, njaa ilikuwa  ikizidi kuniuma, Mdada mmoja aliye jirani yangu aliniambia 

“Jinsi ulivyolowa na unasema umesahau vyeti jiandae kwa  maneno ya shombo, huyo Bosi ni kijana tu, msafi sana, alafu  mzuri, huoni zimetangazwa nafasi wanawake wengi ndiyo  waliojitokeza tena wakiwa wamevalia vizuri zaidi yako!”  Alisema kwa sauti ya Chini, nilimjibu 

“Sikuja kwenye mashindao ya urembo nimekuja kutafuta kazi,  kama sitopata nitatafuta kwingine, siwezi kuwa Mtumwa wa  umasikini wangu” Nilimjibu, nilimkata kauli hakusema tena, ni  kweli alichokuwa amekisema Wasichana walikuwa wakijipodoa sana ili wakiingia huko wakamshawishi huyo Bosi ambaye mimi  nimetoka kuzozana naye bila kujuwa. 

Jina langu lilikuwa la kwanza kuitwa, niliomba niwe wa mwisho  sababu nguo zangu zilikuwa zinavuja maji, bahati nzuri Mdada  aliyekuja kuniita alinielewa, Basi walianza kwenda huko  pasipo kurudi hadi pale nilipobakia peke yangu ndani ya  Chumba hicho. Maneno ya yule Mdada yalizidi kujirudia kwenye  ufahamu wangu, kwa kiasi kikubwa yalianza kunitisha sana.  Basi, zamu yangu ilipofika nilivuta pumzi kwa nguvu ndani  kisha nilizitoa ili kuondoa hali ya woga ambayo niliona  inaanza kuniandama, nilikuwa kama kichaa hivi sababu nguo  bado zilikuwa mbichi, sikuwa na vyeti vya elimu yangu ya  Biashara. 

Nilipiga hatua ndogo ndogo kuelekea kwenye ofisi kwa ajili ya  Usahili, nilipoingia nilipigwa na butwaa, nilimuona Osman  akiwa ameinama anaandika jambo, yule Mdada alimwambia Osman 

“Bosi, huyu wa mwisho anaitwa Jacklin, alitakiwa kuwa wa  kwanza ili hakuwa tayari” Alisema, Osman hakunyanyua macho  yake, alisema 

“Sawa anaweza akaketi” Alisema bila kuniangalia usoni,  nilitamani kuondoka maana kwa jinsi nilivyomjibu vibaya  kuanzia kule barabarani hadi tunafika ofisini kwake  sikufikiria kama atanisikiliza, basi niliketi hivyo hivyo  kama Mtu aliyeyavulia maji nguo, Sharti ayaoge. Nilisubiria  kwa sekunde kadhaa, yule Mdada aliondoka, baadaye Osman  alinyanyua kichwa chake, aliponiona alinitazama kwa  kunishangaa kama vile alikuwa hajawahi kuniona. 

“Karibu” Alisema Osman, jicho lake niliona lilikuwa na ujumbe  fulani kwenye hisia zangu, alinitazama kama vile alikuwa  akitengeneza kitu alafu akawa anakiangalia kama kipo sawa,  nilihisi pengine kwasababu nilikuwa nimeloa na pia nilimsemea  vibaya. 

“Asante!” Nilisema kwa sauti iliyojaa aibu 

“Naitwa Osman Dhabi, ni Mmiliki wa kampuni hii, Unaitwa  nani?” Aliniuliza kama vile hakuna kilichotokea baina yetu,  ilinifanya niwe na maswali mengi kichwani kwangu 

“Naitwa Jacklin Sembu, nimekuja kwa ajili ya Usahili wa kazi”  Nilisema nikiwa nimeinamia chini, Osman aliniambia 

“Sina haja ya kukufanyia Usahili sababu nimeshakufanyia  tukiwa njiani, sitaki kuingilia Maisha yako Jacklin lakini kuna wakati unapaswa kuacha jeuri yako” Alisema kisha  alichukua barua akaniambia 

“Hii uje nayo baada ya siku saba, nilihitaji nafasi ya Mtu  mmoja pekee, nimechagua kufanya kazi na wewe” Alisema Osman,  nilijikuta nikitabasamu kwa shida sana, ni kweli nilikuwa  nahitaji hiyo kazi kwa udi na uvumba lakini niliishiwa maneno  ya kuyasema mbele ya Osman, nilijiona nimeelemewa kabisa,  nafsi ilinisuta nikasema 

“Nashukuru na Mungu akubariki” 

“Usijali Jacklin, ubaya haulipwi kwa ubaya katu, ubaya  hulipwa kwa mazuri yasiyosahaulika” Alisema tena kisha  alinipa mkono ambao niliukataa kule barabarani, ilinibidi  niupokee, aliuchezea kidogo mkono wangu kwa kunisabahi 

“Nakutakia siku njema” Alisema Osman kisha aliendelea na kazi  zake, nilinyanyuka kisha niliangalia kiti nilichokalia  niliona kimeloa maji ambayo yalikuwa yakinichuruzika,  niliondoka ofisini kwa Osman nikiwa mwenye furaha sana.  Mosses hakunipigia kabisa wakati alisema angenipa pesa ya  kulipia usafiri, basi nililazimika kumpigia Mama 

“Jacklin Mwanangu sijapata pesa kama unaweza kusubiria hadi  jioni sawa” Alisema Mama 

“Usijali Mama nitarudi tu” Nilisema, sikuwa na pesa ya nauli  ya kurudia nyumbani alafu mvua ilikuwa ikinyesha sana,  kulikuwa na hali ya radi pia, nilifikiria kama Osman  angelinikuta pale nje ingeleta picha mbaya zaidi, nilifikiria  pia ile pesa niliyompa kwa hasira, nilijilaumu sana kwa  kiburi changu. Basi niliingia kwenye mvua, nilivua viatu  vyangu. Nini Kitaendelea? Usikose Sehemu Ya Pili Ya PUMZI YA MWISHO

Mpe Nguvu ADMIN Kwa ajili ya bando Kwa kumtumia Chochote aendelee kupost RIWAYA Mpya Hapa Kijiweni

Lipa Namba: 57900454
Jina: LIPA KIJIWENI TIPS
Mtandao: VODACOM  

SOMA RIWAYA YA KOTI JEUSI KWA KUBONYEZA HAPA 

SOMA RIWAYA YA FUNGATE KWA KUBONYEZA HAPA 

SOMA RIWAYA YA NILIPANGA NYUMBA MOJA NA MAJINI 

SOMA RIWAYA YA GORYANAH HAPA 

SOMA KISASI CHANGU HAPA  

SOMA RIWAYA YA MSALA HAPA

JIUNGE NIPO KIJIWENI Kwa Kubonyeza Hapa

 

Pumzi Ya Mwisho xx Pumzi Ya Mwisho xx  Pumzi Ya Mwisho xx Pumzi Ya Mwisho xx Pumzi Ya Mwisho xx Pumzi Ya Mwisho xx Pumzi Ya Mwisho xx Pumzi Ya Mwisho xx 

 

17 Comments

Leave A Reply


Exit mobile version