IlipoishiaKwanza pole sana Jacklin, Dunia yako imekugeuka lakini  ndivyo ilivyo sababu siyo Watu wote wanakuwa na simulizi tamu  za Maisha yao, yako chungu sana. Osman alikutafuta sana,  ilisadikika kuwa Mlikuwa mmeuza kila kitu na kuondoka”  Alisema Dokta Simon, stori yake ilikuwa ngeni masikioni  mwangu 

“Tuliuza kila kitu?” Nilimuuliza 

“Ndiyo! Mzee Dhabi pia alihangaika kuwatafuta bila mafanikio,  mwisho alikata tamaa baada ya kupata taarifa kuwa mliuza  nyumba na kuondoka wewe na Mama yako!” 

Haraka niligundua kuwa Mzee Dhabi alifanya yote pasipo Osman  kujuwa. Endelea

Sehemu Ya Kumi Na Tatu

“Hapana Baba yake Osman alitumia hasira zake kutuondosha  kwenye ile nyumba na kuchukua kila kitu tulichonunuliwa na  Osman, hatukuuza nyumba wala mali yoyote ile vyote  vilichukuliwa na Mzee Dhabi, tuliishi Maisha ya mateso sana  Mimi na Mama yangu” nilisema, nilishindwa kuzuia uchungu ulio  ndani ya moyo wangu, nililia sana tena kwa kwikwi 

“Usilie Jacklin, kwasasa unaishi wapi?” Alihoji Dokta Simon,  nilifuta chozi langu nilitulia kwa sekunde kadhaa kisha  nilimjibu 

“Uswahilini, tulikuwa tunaishi kwa kuuza Mboga mboga mtaani.  Na hii hali yangu nitaweza vipi kuendesha Maisha yangu  Dokta!” Chozi liliendelea kunibubujika 

“Usijali nitakuchukua utaishi kwangu Jacklin wakati tunafanya  utaratibu mwingine” Alisema Dokta 

“Samahani hivi Osman yupo wapi?” Niliuliza 

“Osman anaishi Marekani..” Alijibu Dokta Simon huku akionesha  kutaka kusema kitu kingine ambacho alijizuia asikiseme 

“Anaishi na Zahra?” Nilimuuliza 

Alishusha pumzi zake kisha alinitazama akanijibu 

“Ndio, wanatarajia kufunga ndoa miezi mitatu ijayo hapa  Nchini” Alisema Dokta Simon 

“Natamani kumuona Osman ili nimwambie kuwa sikukataa kuokoa  Maisha yake ila nilikuwa nimechelewa” Nilisema kwa kilio  kikubwa 

“Jacklin, hayo yameshapita, kwasasa tuangalie Afya yako  kwanza ndiyo jambo lenye umuhimu zaidi kuliko chochote kile”  Alisema Dokta Simon, nilimkubalia. Hakuchelewa sana aliondoka  wodini 

Hakuna aliyekuja kuniona kwa siku nilizokuwa Hospitalini,  moyo ulijaa upweke na maumivu makali, nilimkumbuka Mama yangu  jinsi alivyonilea na kunipigani katika nyakati zote.  Nilitokwa na machozi kila wakati, Mama yangu aliondoka bila  hata kuniaga, ilinipa shida sana hadi kuwa sawa. Dokta Simon  alijitahidi sana kila alipopata muda alikuja kuniangalia na  kunipa faraja kwa kuniambia maneno yaliyojaa matumaini  makubwa sana japo nilishajuwa kuwa thamani ya Maisha yangu  ilikuwa imeshaondoka.

Bili za Hospitali alizilipa mwenyewe Dokta Simon,  nilimshukuru sana kwa ubindamu aliouonyesha kwangu.  Alinichukua na kunipeleka nyumbani kwake baada ya mwezi mmoja  kupita, alikuwa akiishi na Mke wake aliyeitwa Lidia. Niliishi  kwa upendo na amani ya hali ya juu sana, Mke wa Dokta Simon  alikuwa na moyo kama wa Mume wake ndio maana ndege hawa  wawili waliruka pamoja sababu walifanana kwa kila kitu 

“Usijali Jacklin Mungu atakupa ufalme mwingine kupitia  maumivu yako” Alisema Mke wa Dokta Simon wakati nilipokuwa  najifunza kutembea kwa kutumia Magongo 

“Nashukuru kwa ukarimu wenu Lidia, mmenionesha thamani kubwa  iliyo ndani yangu ambayo niliona imeondoka, nilihisi  sitotabasamu tena. Mwisho ninekubali hali halisi kuwa siwezi  kutembea hivyo nashukuru kwa kila kitu Lidia” Nilisema tukiwa  tumesimama kando ya Barabara. 

“Dokta Simon alinieleza kuhusu wewe na Osman, alikutolea figo  na kuokoa Maisha yako” 

“Ni kweli, katika vitu ambavyo ninajuta katika Maisha yangu  ni kutomshukuru Osman kwa wema wake alionitendea na kumuomba  Msamaha sababu sikuweza kuokoa uhai wake, nilishindwa kulipa  fadhila za Ubinadamu wake” Nilisema, nilihisi chozi  likinilenga taratibu 

“Usijali Jacklin, hayo yameshapita. Haina haja tena kuingia  kwenye Maisha ya Mtu nwingine na kumkumbusha yaliyopita.  Sahau tu na Maisha yaendelee ” Alisema Lidia, tuliendelea na  mazoezi 

“Pamoja na yote ila uzuri wako Jacklin upo pale pale, wewe ni  mzuri sana” Alisema Lidia,, alinifanya nitabasamu 

“Unanichokoza?” Nilisema kwa utani kisha tulicheka, tulikuwa  marafiki wakubwa sana kwa kipindi kifupi ambacho niliishi  nyumbani kwao, walijitahidi kuniondoa upweke, walinisaidia  sana sikuwa na mawazo kama Mwanzo. 

Usiku mmoja nikiwa nimelala, kutokana na dawa kali nilizokuwa  nameza kwa ajili ya kupunguza maumivu nilijikuta nikizama  ndotoni. Ndoto ilianza kwa furaha sana, Niliota Tukiwa  tunacheka na Osman, ghafla alikuja Mwanamke akiwa ameshikilia  Bastola, Mwanamke huyo sikuiyona sura yake ila alisema 

“Jacklin una muda mchache sana wa kuendelea kupumua, siwezi  kukubali furaha yangu ukaiharibu kirahisi, Pumzi yako ya  Mwisho sema neno moja kabla sijakumaliza” Alisema Mwanamke huyo, nilimtazama Osman ambaye alikuwa akishangaa tukio hilo,  nilisema 

“Nakupenda Osman” Lilikuwa ndiyo neneo langu la Mwisho katika  pumzi yangu ya Mwisho, alinipiga risasi. Ghafla nilishtuka  kutoka Usingizini, nilihema sana, Jasho lilikuwa  likinibubujika, niliamka na kwenda kuwasha taa. Jumba la  kifahari la Dokta Simon lilikuwa kimya sana, sikutaka  kuwasunbua ila ndoto niliyoiota ilinishtua mno. 

Nilijiuliza ndoto hiyo ilikuwa na maana gani, nilisali ili  Mungu aniweke mbali na hatari hiyo kabisa. Nilikesha  nikimuomba Mungu, Usingizi ulinichukua Alfajiri, Asubuhi  nilimsimulia Lidia kuhusu ndoto yangu, alicheka tuu kisha  alisema 

“Tatizo rafiki yangu unawaza sana kiasi kwamba unatengeneza  hadi picha ya Uwongo kwenye akili yako, kumbuka kila  unachokifikiria hutokea hivyo acha kutengeneza Maisha mabaya  ya Baadaye” Alisema akiwa ananiandalia chai, alikuwa  akinichukulia kama Mtoto mdogo yani kwa jinsi alivyokuwa  akinidekeza 

“Nimekuelewa Lidia” Nilisema. 

  • ••••••••••••••••••••••••••••••••• 

Osman aliwasili Nchini kwa ndege ya shirika la Fly Emirate  akitokea Marekani. Alirudi Nchini kwa ajili ya kufunga ndoa  na Zahra, tangu alipoondoka kwa ajili ya matibabu miezi kdhaa  iliyopita hakurudi tena. Aliwasiliana na Rafiki yake Dokta  Simon, ilikuwa ni furaha kwa marafiki hao kukutana tena Osman  akiwa mwenye Afya, katika Maongezi yao Osman aliniulizia  lakini Dokta Simon hakutaka kumwambia Osman kuwa Mimi nipo  nyumbani kwake, sina Mguu. Alifanya hivyo ili kuruhusu kila  kilichopita kasirudi tena. 

Nilishangaa siku hiyo Lidia aliniambia kuwa twende Shamba  tukakague, sikuwa na pingamizi sababu nilikuwa sina kazi  yoyote ile kumbe ndiyo siku ambayo Osman alikuwa anakuja  kutembelea nyumbani kwa Dokta Simon, hawakutaka nionane na  Osman, hawakutaka nijisikie vibaya. Basi tulipoondoka nyuma  Osman alienda nyumbani kwa Dokta Simon kwa ajili ya kupata  chakula cha Mchana na mazungumzo mengine ya kirafiki. 

Tukiwa njiani tunaenda Shamba nilihisi kama kuna kitu hakipo  sawa kwangu, sikuwa na furaha ya kwenda huko shamba,  nilimwambia Lidia kuwa sijisikii vizuri kuendelea na safari  hivyo turudi nyumbani.

“Unaumwa?” Aliniuliza Lidia 

“Hapana, sihisi kama natakiwa kuwa sehemu ya safari hii,  samahani Lidia” nilisema ili kama nitakuwa nitakuwa  nimemkwaza anisamehe, Lidia alisema 

“Mbona tumekaribia Jacklin jamani, ni hapo tu wala siyo mbali  hata hivyo hatuchelewi” Alisema Lidia, nilizungumza sasa kama  Binadamu ambaye sijatumia viungo vya mwili, si unajuwa vilema  jinsi ambavyo wanapenda kujiongelea madhaifu yao 

“Turudi Bwana au sababu unajuwa siwezi kutembea ndiyo  uniringie hivyo? Sijisikii na safari” Nilisema kisha  niliuchuna, niliegemea kwenye kioo huku moyo ukiniambia  niwahi kurudi nyumbani, hata mwenyewe sikujuwa ni kwanini  nilikuwa nataka kurudi nyumbani wakati tulikubaliana kuwa  twende Shambani. 

“Usiseme hivyo Jacklin, Usimkufuru Mungu kiasi hicho, haya  turudi” alisema Lidia kisha aligeuza gari, moyo ulianza  kuchanua 

Sasa kingine nilichokigundua ni kuwa Lidia alikuwa bize  kupiga simu mahali alafu simu ilikuwa haiiti, nilijaribu  kuchungulia niliona alikuwa akimpigia Mume wake, nilijuliza  alikuwa anataka kumwambia nini? 

Sikuwa na kifua cha kuweza kukaa na dukuduku, nilimuuliza 

“Unampigia nani?” Niliuliza makusudi tu wakati nilishaona  alikuwa akimpigia Mume wake Dokta Simon 

“Nampigia Dada atuandalie chakula” Alisema kwa tabasamu  ambalo hata yeye mwenyewe aligundua kuwa alikuwa akiongopa,  niliguna 

“Mh! Haya” Wala sikutaka eti kumuuliza zaidi wakati niliona  alikuwa akimpigia Mume wake, hali ile iliendelea kwa muda  mrefu, sijui sasa simu ilikuwa inaita alafu haipokelewi au  vipi, sikutaka kuhoji zaidi bali nilihisi jambo ambalo sikuwa  na uhakika nalo. Tulipofika Mjini kulikuwa na foleni kiasi  hivyo angalau nilimuona akitabasamu hadi nilishangaa yaani  Watu wanakasirika kisa foleni yeye anafurahia 

Nilicheka chini chini baada ya kugundua alikuwa amepagawa,  Basi haikutukuchukuwa muda mrefu kufika nyumbani. Niliiyona  gari ya kifahari ikiwa imeegeshwa karibu na Bustani ya Mauwa,  ilikuwa ya kifahari sana.

“Ile gari ni ya Nani?” Niliuliza maana sikuwahi kuiyona pale  nyumbani 

“Aaah ile?” Aliuliza Lidia kama vile hakuwa na jibu la  kunipa, nilimkazia 

“Ndiyo! Ile nyeusi sijapata kuiyona hapa nyumbani, inaonekana  ni ya kifahari sana.” Nilisema huku Lidia akiwa anasogeza  gari eneo la maegesho. 

Kumbe Dokta Simon alikuwa tayari amewasiliana na Mke wake kwa  njia ya ujumbe mfupi, lengo lao lilikuwa ni kutotaka Mimi na  Osman tuonane pale. Huko ndani sasa ambako Osman na Dokta  Simon walikuwepo walikuwa wakizungumza mambo yao ila  waliposikia ngurumo ya gari, Osman alitaka kuchungulia huku  akimuuliza Dokta Simon 

“Shemeji Lidia huyo?” Simon alipoulizwa hivi alibakia akiwa  anajiuma meno asijuwe ajibu vipi, ni kweli tulikuwa Mimi na  Lidia sasa angemjibi vipi ikiwa hataki Mimi na Osman tuonane? 

“Ndi…ndi…oo” 

“Mh! Mbona unajibu kama hauna uhakika, ni bora ukaangalie  kama ni yeye maana muda wangu umeisha hapa ingawa nilihitaji  sana kumuona” Alisema Osman 

“Sawa ngoja nikaangalie, jisikie huru rafiki yangu” alisema  Dokta Simon kisha alikuja kwenye Maegesho akatukuta mimi na  Lidia tukizozana maana alikuwa hataki nishuke kwenye gari 

“Bora hata Shemu umefika yaani Mkeo simuelewi kabisa, huwezi  amini ananizuia kushuka kwenye gari” nilisema 

“Aaah Mke wangu kwanini unafanya hivyo?” Aliuliza Dokta Simon 

“Jacklin hajanielewa, nilikuwa nimemwambia asubirie wewe  ufike ili ukamuoneshe sapraizi yake” Alisema Lidia,  nilijikuta nikitabasamu kusikia kuna Sapraiz 

“Sapraiz gani hiyo?” Niliuliza, mkononi Dokta Simon alikuwa  na kitambaa cheusi akaniambia anifunge machoni 

“Jamani jamani Sapraizi gani hiyo mbona mnanitisha” Nilisema 

“Hebu kwanza nikufunge ili ukaiangalie Sapraiz itakayo  kufanya upagawe” Alisema Dokta Simon, Basi nilikubali  kufungwa kitambaa kumbe lengo lao lilikuwa Nisimuone Osman,  Walinipeleka nyuma ya nyumba

“Jamani nna hamu ya kuona hiyo Sapraiz” Nilisema 

“Haya hebu nikufungue” Alisema Dokta Simon, moyo wangu  ulijawa na furaha sana nilipomuona Kasuku akiwa kwenye kizizi  chake, nilikuwa napenda sana Kasuku, sikuwaza chochote tena.  Nilivuta Magongo yangu na kulisogelea Zizi la Kasuku, Dokta  Simon alimpa Ishara Mke wake kuwa anatoka, muda huo akili  yangu wala haikuwa hapo, walinipeleka sehemu ambayo hata  nisingeliweza kusikia sauti ya gari 

Osman alikuwa akimsubiria Dokta Simon ndani, alipofika  alimdaka kwa swali 

“Ni yeye?” 

“Mke wangu?” 

“Ndiyo!” 

“Aah hapana, ni Kijana wangu wa kazi alikuwa akileta gari” 

“Oooh! Sawa Basi ngoja Mimi niende” Osman aliaga, alielekea  lilipo gari lake kisha aliondoka pale nyumbani bila kuhisi  wala kujuwa kuwa nilikuwa pale. 

Nilikuwa nacheza na kasuku wangu mzuri niliyepewa kama  zawadi, nilisahau kila kitu. Lidia na Mume wake waliingia  ndani 

“Hajashtuka chochote” aliuliza Lidia 

“Hapana sijui Jacklin!” 

“Hapana japo alikuwa na wasiwasi kama nilivyokutumia meseji  kuwa hatukufika shambami aligaili njiani” Alisema Lidia 

“Mmmh kuna namna hawa Watu wawili wanawasiliana kifikra,  sitaki waonane, sitaki turudi tulipotoka. Osman ameamua  kuendelea na Maisha yake, nataka Jacklin naye aendelee na  Maisha yake, atapata Mtu atakaye mpenda kwa jinsi alivyo”  Alisema Dokta Simon, alikuwa ni Mtu safi sana, roho yake  ilikuwa nzuri iliyojaa huruma 

“Cha Msingi ni kuendelea kuhakikisha hajisikii mpweke”  Alimalizia Dokta Simon. 

Hayo ndiyo yalikuwa Maisha yangu, mipango ya Harusi ya Osman  iliendelea kufanyika, kumbe katika kipindi hicho chote Osman  alikuwa hajakata tamaa ya kunitafuta japo Baba yake alimuongopea kuwa tuliuza nyumba na kuhama mji, alinitafuta  bila mafanikio lakini alijipa tumaini kuwa ipo siku ataniona, 

Masikini hakujuwa kama Mimi ni kilema wa Mguu, hakujuwa kuwa  Mama yangu ambaye alikuwa akihangaika naye kunitafutia figo  alikuwa amefariki siku nyingi. Hakujuwa kama nilikuwa  nikiishi kwa rafiki yake. 

Wazazi wa Osman walikuja kutoka Dubai, Harusi ilipangwa kwa  kuzingatia heshima aliyonayo Mzee Dhabi, umaarufu na utajiri  wake. Moyo wa Mzee Dhabi ulificha unyama ambao alitutendea  Mimi na Mama yangu. 

Lidia na Osman walikuwa ni miongoni Mwa Watu wa karibu wa  Familia ya Mzee Dhabi, walishiriki maandalizi kisiri sana  bila Mimi kujuwa kwa kipindi chote, walikuwa wakiingia na  kutoka alafu hakukuwa na stori zozote kuhusu Ndoa ya Osman,  nakumbuka siku moja nilimuuliza Dokta Simon kama ndoa ya  Osman ilikuwa imepita 

“Imeshapita, walitaka kufanyia huku lakini walighaili,  imefanyika huko Dubai ambako anaishi kwasasa” Ndicho  alichonijibu Dokta Simon, nilikuwa mnyonge baada ya kusikia  hivyo 

“Usijali Jacklin, haikuwa ridhki yako ndiyo maana yalitokea  yaliyotokea, sahau kila kitu Maisha yaendelee sawa?” Alisema  tena Dokta Simon 

“Sawa” Nilijibu huku moyo wangu ukiwa na maumivu makali sana,  Osman kuowa haikuwa shida kwangu ila kilichoniuma zaidi  ilikuwa ni kushindwa kumshukuru na kumwambia kuwa nipo Hai  anisamehe kwa kila kitu. 

Nilikaa na picha ya Osman kwa muda mrefu, siku moja  niliichoma moto, nilifungua ukurasa mpya wa Maisha yangu,  niliyapotezea maumivu kwa kucheza na Kasuku wangu, sikutaka  kabisa kumfikiria Osman wala kukumbuka kilichomfika Mama  yangu maana mambo hayo mawili yalikuwa yakinifanya nakuwa  mnyonge sana. Niliamua kujisahaulisha hata alichonifanyia  Mosses.. 

Siku moja ilikuwa Mchana nilimpigia simu Lidia nikamwambia  kuwa nina hamu ya kula Ice Cream, alikuwa kazini hivyo  alinitaka nivumilie kidogo, baadaye alimtuma dereva taxi aje  kunichukua anipeleke mahali ambapo Lidia alikuwepo ili  tukanunue Ice Cream. Nilipofika niliingia kwenye gari ya  Lidia, tulielekea kwenye Ice Cream huku tukipiga stori za  hapa na pale ambazo zilituburudisha kwa kiasi fulani.

Kutoka nilipomkuta Lidia hadi sehemu ambayo Ice cream  zilikuwa zinauzwa hapakuwa mbali sana, mwendo mfupi tu  tulikuwa tumefika. Kutokana na hali ya Mguu wangu Lidia  aliniomba nisishuke kwenye gari badala yake nimsubirie! Basi  Lidia alishuka na kuingia zinapouzwa Ice cream ambazo  nilikuwa nikizipenda sana, alichelewa sana hadi nilianza  kujiona mpweke ndani ya gari 

Nilitamani kushuka lakini kabla wazo la kushuka halijaniingia  sawa sawa, simu ya Lidia iliita, iliita kwa muda mrefu sana  hadi nilitamani kuangalia ni nani alikuwa akipiga ila  nilihisi uvivu fulani, sasa katika angalia angalia niliona  kitu kama kadi hivi. Nilipata shahuku ya kuiangalia,  nilinyoosha mkono na kuichukua. 

Nilianza kuisoma, ilikuwa ni kadi ya harusi ya Osman na  Zahra, moyo uliniripuka paa! Nikaangalia mlango ambao Lidia  aliingia hakukuwa na Mtu aliyekuwa akitoka nikaendelea  kuisoma. Cha ajabu kadi ile ilikuwa haijatumika kabisa yaani  tarehe iliyoandikwa ilikuwa ni siku mbili mbele, zilikuwa  kadi kama tano hivi zenye majina ila hiyo moja ilikuwa haina  jina basi niliiweka kwenye mkoba wangu haraka ili nikitulia  niisome vizuri, nilijikuta nikianza kuwa na huzuni sana. 

Punde Lidia alirejea ndani ya gari akiwa na Ice Cream,  nilimtazama sana hadi aliniuliza 

“Vipi kuna tatizo?” Aliniuliza akiwa ananipatia Ice Cream,  nilitabasamu tu baada ya kugundua kuwa nilikuwa nikifichwa  jambo maana Dokta Simon alisema Harusi imeshapita ila cha  ajabu kadi zile zilisema kuwa ni siku mbili baadaye 

“Hakuna shida” nilimjibu 

“Nimepata hiyo ile nyingine unayoipenda haipo” Alisema Lidia 

“Hata hii siyo mbaya kikubwa ni Ice Cream” nilimjibu kisha  nilianza kufakamia Ice Cream, nilikula kwa hasira sana baada  ya kugundua Lidia na Mume wake hawakuwa wakweli 

“Tunarudi nyumbani au kuna mahali unataka twende” aliuliza  Lidia akiwa anawasha gari 

“Nafikiri turudi nyumbani tu” Basi Tulirudi nyumbani. 

Tulipofika nilielekea chumbani kwangu nilihakikisha nimefunga  mlango vizuri ili niweze kuisoma ile kadi kwa utulivu,  nilikaa kitandani, niliitoa na kuanza kuisoma tena. Kibaya  zaidi ni kuwa waliokuwa wakizisambaza zile kadi walikuwa ni  Dokta Simon na Mke wake Lidia.

Nilitamani kulia kwa uchungu ambao nilikuwa nikiusikia kwenye  moyo wangu, mara nyingi nilikuwa nikiwauliza kuhusu Osman  lakini walikuwa wakinipa majibu ya Hatuna mawasiliano naye  sana kwa sasa 

Nililia sana, niliona nimenyimwa haki ya kumuomba msamaha na  kumshukuru Osman, niliihifadhi ile kadi kwenye Begi langu la  nguo. Sikutaka kuwauliza chochote kile, siku hiyo Usiku Lidia  alikuja chumbani kwangu na kuniambia kuwa anasafiri na Mume  wake kwenda Nje ya Jiji watarudi baada ya wiki moja 

“Nitawamiss sana jamani” nilisema 

“Usijali Jacklin hata sisi tutakumiss mno, ubaki salama na  kwa chochote usisite kutupigia simu” Alisema Lidia 

Alipoondoka nilitafakari nifanye nini maana nilijuwa tu  walitengeneza safri feki ili kunizuga kuhusu Ndoa ya Osman.  Kweli siku iliyofuata asubuhi mapema waliniaga rasmi,  waliingia kwenye gari niliwapungia mkono wa kuwaaga,  waliniacha na Mdada wa kazi na Mlinzi. 

Walipoondoka nilimfuata Mdada wa Kazi aliyekuwa anaitwa Scola  nikamuuliza 

“Unakunbuka siku ambayo Mimi na Lidia tulienda Shambani? Ile  siku ya mwisho?..” nilimuuliza alionekana kutafakari sana 

“Ndio nakumbuka” alinijibu baada ya kuwa tayari amemaliza  kutafakari 

“Kuna mgeni alikuja hapa si ndiyo?” Scola alinitolea macho  yake Makubwa 

“Scola nijibu alikuja Mgeni si ndiyo?” Nilimuuliza tena baada  ya kuona alikuwa hanipi jibu 

“Lakini Dada..” alisema Scola, nikahisi kuna jambo 

“Sitaki cha lakini nataka uniambie ukweli ni nani alikuja  hapa?” Nilimkazia sauti na jicho 

“Baba alisema nisiseme unanipa wakati mgumu Dada Jacklin”  Nilimshika mkono Scola nikamuingiza chumbani kwangu  nikamwambia 

“Tupo Mimi na wewe naomba unieleze ukweli ni nani alikuja  hapa” 

Nini Kitaendelea? Usikose Sehemu Ya KUMI NA NNE Ya PUMZI YA MWISHO

Mpe Nguvu ADMIN Kwa ajili ya bando Kwa kumtumia Chochote aendelee kupost RIWAYA Mpya Hapa Kijiweni

Lipa Namba: 57900454
Jina: LIPA KIJIWENI TIPS
Mtandao: VODACOM  

SOMA RIWAYA YA KOTI JEUSI KWA KUBONYEZA HAPA 

SOMA RIWAYA YA FUNGATE KWA KUBONYEZA HAPA 

SOMA RIWAYA YA NILIPANGA NYUMBA MOJA NA MAJINI 

SOMA RIWAYA YA GORYANAH HAPA 

SOMA KISASI CHANGU HAPA  

SOMA RIWAYA YA MSALA HAPA

JIUNGE NIPO KIJIWENI Kwa Kubonyeza Hapa

 

Pumzi Ya Mwisho xx Pumzi Ya Mwisho xx  Pumzi Ya Mwisho xx Pumzi Ya Mwisho xx Pumzi Ya Mwisho xx Pumzi Ya Mwisho xx Pumzi Ya Mwisho xx Pumzi Ya Mwisho xx Pumzi Ya Mwisho

  

4 Comments

Leave A Reply


Exit mobile version