Ilipoishia “Kwahiyo umeanza kua na huruma si ndiyo? Basi hakuna sababu  ya kujificha, jitokeze hadharani ujitangaze kua Bilionea  mwenye Mtoto Mlemavu, si una shida sana ya Mtoto basi hakuna  sababu ya Mimi kubeba huu mzigo wakati una Mtoto unaye muonea  huruma” Alisema Neema kwa hasira zaidi, akanyanyuka ili  aondoke lakini James akamshika mkono kwa lengo la kumzuia  asiondoke 

“Mpenzi hupaswi kua na hasira sababu wewe ni Mama mtarajiwa,  natamani haya mambo yaishe kwa namna nzuri, basi nitaenda  Polisi kwa ajili ya kuzungumza na Matilda ili aondoke hapa  Mjini” Alisema James lakini Neema akatoa Mkono wa James  akaelekea chumbani.  Endelea

SEHEMU YA TANO

“Nifanye nini sasa?” Alijiuliza James akiwa ametulizana  kochini, moyoni alikaa kikao akakubali kua Patra ni Mtoto  wake lakini aibu ya kuonekana Bilionea ana Mtoto mlemavu  hakutaka kuipata kabisa ndiyo maana alitumia nguvu zote  kumkana Mtoto lakini upande wa pili moyo wake ulijawa na  maumivu makali sana, akanyanyua simu yake akampigia rafiki  yake

“Chilo naomba tuonane Muda huu, tuonane palepale” Alisema  James kisha akanyanyuka na kuvuta kitasa cha mlango akatoka,  akaingia kwenye gari yake ya kifahari kisha akaondoka  nyumbani hapo na kuelekea Sinza Vatcan, akaingiza gari  maegesho ya Pub moja yenye hadhi kisha akaelekea mahali  ambapo alipanga kuonana na rafiki yake anayeitwa Chilo. 

Alimkuta rafiki yake akiwa hapo anamsubiria, alipomwona  aligundua kuna jambo lililomsibu, licha ya kua rafiki yake  pia alikua mshauri wake wa mambo mengi binafsi, alijitupa  kwenye kiti 

“Niambie James” Alikaribishwa na neno hilo kabla ya salam “Mambo si shwari Chilo” Alisema James 

“Unamaanisha nini?” 

“Ni kuhusu Matilda” 

“Enhee….” 

“Neema ameenda kumfungulia kesi ya wizi lengo likiwa kumtisha  ili aondoke hapa Dar, lakini moyo wangu nahisi unaumia sana  kwa hili” Alisema James akiwa ameshika kichwa chake 

“Oooh imefikia huko Babuu…Kwanini unampa mamlaka makubwa  Neema kiasi hicho James….Huoni kama Mtoto atateseka?” 

“Nifanye nini Chilo na unajua nahitaji sana Mtoto kutoka kwa  Neema, sina sauti sababu ana mimba ya Miezi mitatu na  anatishia kuitoa endapo nitafanya makosa, nakiri Kuumia sana  kuhusu Matilda na ambacho Mtoto anapitia, unajua wakati  mwingine natamani hata Mtoto angekufa tu” 

“Unasema nini James, Mtoto afe kisa ulemavu alionao, bado  Patra ni Mtoto wako hata ufanye nini hakuna  

kitakachobadilika, zaidi hapo unamtesa tu, Bro kubali hali  halisi kua Patra ni Mtoto wako wa kwanza” Alisistiza Chilo 

“Bilionea nawezaje kukubali aibu ya kua na Mtoto Mlemavu  Chilo? nitaweka wapi sura yangu endapo Watu watajua….nakosa  amani kabisa, Mimi nataka kufanya jambo fulani ili niwe na  amani, nataka kumpatia pesa ya kutosha Matilda arudi Njombe  na Mtoto alafu baada ya hapo nitakubali rasmi kua Baba wa  Patra lakini kwa siri sana” Alisema James akiwa anatokwa na  jasho

“Katika vitu ambavyo utakuja kujuta mbele ya safari ni  kumtelekeza yule Mtoto, ya Mungu mengi alafu la mbele wewe  hulijui James, Hujui ni maumivu kiasi gani anayapata Matilda,  kumbuka amekupa heshima ya wewe kuitwa Baba, ametoroka kwao  kwa ajili yako bado huoni thamani na heshima aliyokupa  ikikufanya ujione ni Mwanaume uliye kamilika?” Maneno ya  Chilo yalimfanya James amimine Unywaji kwenye glasi kisha  akanywa, koo ikawa lahini sana huku akiugulia maumivu ya  kinywaji alichokunywa, alikunja sura kama anayehisi maumivu,  akapangusa mkono wake kinywani alafu akamwambia Chilo 

“Tatizo ni aibu nitakayokumbana nayo Chilo, najua Patra ni  Binti yangu lakini siwezi kulea Mtoto mlemavu” Alisema kisha  akanyanyuka kwa ajili ya kuondoka 

“Unasimamia hilo hadi mwisho?” Akauliza Chilo akiwa naye  ameinuka 

“Huwenda” Akajibu James huku akiingia kwenye gari yake, Macho  ya Chilo yakamsindikiza Bilionea Kijana akitokomea zake 

Usiku uliingia, Mchungaji George alisubiria hadi alichoka,  hakupewa nafasi ya kuingia na kujua maendeleo ya Matilda,  akainuka huku sauti fulani ikimsindikiza nyuma yake 

“Mtu wa Mungu unafanya nini hapa hadi muda huu?” Mchungaji  George akageuka, ilikua ni sauti ya mmoja wa polisi aliyekua  lindo, Mchungaji akajipangusa vumbi kisha akamjibu 

“Mungu aliye hai amenipa kibali cha kuondoka sasa hivi,  nasikitika naondoka bila kujua Binti anaendeleaje” Alisema  Mchungaji George kwa sauti iliyojaa upole na maumivu makubwa  sana, Polisi mwenye Buduki akasogea na kumwambia 

“Dunia uliyopo na Dunia tunayoishi sisi ni vitu viwili  tofauti kabisa, unafikiria utashinda?” 

“Mimi siwezi kua Mshindi sababu yupo anayejua namna ya  kushinda kwenye nyakati ngumu, Kijana nakutakia Usiku mwema”  Alisema kwa mafumbo mchungaji George kisha akaingia kwenye  gari ya kanisa akaondoka mahala hapo taratibu huku akiwa  mwingi wa kutafakari. 

“Mnataka nini kwangu?” aliuliza Matilda usiku huo akiwa  kwenye chumba maalum kilichoandaliwa kwa ajili ya mateso yake, kilikua ni chumba chenye kiza la kutosha, akamulikwa  tochi usoni, masikini alikua ameumia vibaya, alichanika mdomo  huku damu ikimvuja 

“Nimekueleza mara nyingi kua unapaswa kuondoka Hapa Mjini  vinginevyo utazidi kuteseka kisha utafungwa na kumkosa Binti  yako mazima” Alisema Polisi ambaye alikua akimpa mteso  Matilda, ilionesha polisi huyo alimtesa Matilda kwa muda  mrefu hadi alichoka, akawa anahema kwa uchovu 

“Kama mnaweza kuniuwa ni Bora mfanye hivyo lakini siko tayari  kubeba msalaba wa dhambi kwa Binti yangu, siwezi kuondoka  hapa” Alisema Matilda kwa ujasiri, sauti ya rungu kuanguka  ikasikika kisha geti likafungwa, polisi aliondoka na kumwacha  Matilda akiwa hoi sana. Muda huo Bilionea James alikua  akifika nyumbani kwake, jumba lilikua giza tofuati na  alivyotegemea, Mlinzi alipomfungulia geti ikabidi amuulize 

“Kwanini jumba lipo giza?” aliuliza akiwa ameshashuka kwenye  gari 

“Madam hayupo tokea jioni, hata hivyo wafanyakazi wengine  amewapa likizo isipokua Mimi tu” Alisema Mlinzi huyo, 

“Hayupo tokea jioni!?” 

“Ndiyo Bosi kwani hakukuaga maana alitoka na begi dogo hivi”  Alisema tena Mlinzi, James akaelewa, 

“Ok! endelea na kazi” Akasema James kisha akaelekea kufungua  mlango, akawasha taa, kisha akampigia simu Neema lakini simu  haikupokelewa usiku huo. 

Asubuhi ya siku iliyofuata, James hakutaka kufanya chochote  zaidi ya kutaka kujua Neema alikua ameenda wapi, akakumbuka  ile kauli kua anaweza akatoa Mimba, akazidi kuingiwa na  wasiwasi, akapiga simu mahali akiwa ameegemea gari yake 

“Hello Mama” Alisema James mara baada ya simu kupokelewa “Unasemaje James” Ikasikika sauti upande wa pili “Nakuja sasa hivi kuna jambo ambalo halipo sawa Mama” 

“Sawa…Karibu!” ukasikika tena simu upande wa pili kisha  simu ikakatwa, Alikua ameshajiandaa hivyo kilichobakia kwake  kilikua ni kutoka tu, akapanda kwenye gari yake kisha akatoka  kuelekea mahali alipopiga simu.

Haikuchukua muda mrefu sana kufika alipokusudia, alikua  tayari yupo mbele ya nyumba moja iliyo na hadhi kubwa,  akapiga Honi, mara geti likasukumwa na kumpa nafasi aingize  gari humo, akiwa anaingia maegesho ya Magari akaliona gari la  Neema likiwa limekwisha paki eneo hilo, ikampa ishara kua  Neema yupo hapo, 

Alionekana kua ni Mtu aliyesongwa na mawazo sana James,  akashuka kisha akaelekea ndani ya nyumba hiyo, akamkuta Neema  akiwa ameweka Miguu yake kwenye miguu ya Mwanaume mmoja  aliyekua akichezea simu, hakuna aliyeshtuka kati yao hata  baada ya kumwona James, mshangao ukawa mkubwa kwa James, Mara  Mama mmoja akafika hapo akitokea chumbani 

“James karibu!” Alisema Mama huyo ambaye naye aliketi kabla  ya James kuketi, James akaketi taratibu huku akimtazama  Mwanaume huyo 

“Oooh ni Masudi huyo, Kaka yake Neema ametokea Dodoma”  Alitambulisha Mama huyo ambaye alionekana kua ni Mama yake  Neema, angalau kidogo sura ya James ikaingia uchangamfu,  Neema alionekana kumkasirikia kabisa James, hakutaka kusema  naye chochote kile 

“Mama tunaweza kuongea?” alisema James 

“Hakuna shaka nakusikiliza James” Alisema Mama huyo, James  akanyanyuka na kumpa ishara kua alikua akihitaji kuzungumza  wakiwa wawili tu. Wakatoka ndani wakaelekea nje kuzungumza 

“Mama, Neema alilala hapa?” aliuliza James 

“Ndiyo alilala hapa” 

“Amekueleza chochote?” 

“Nilihitaji kwanza ufike James, hebu fikiria kwa akili yako,  Mwanamke ambaye anaenda kukupa heshima ya kuitwa Baba  unamtendea hivi, hujui kama Mjamzito anapaswa kupewa malezi  ya utofauti?” Alisema Mama huyo 

“Lakini Mama, lilikua ni jambo la Mimi na Yeye kuelewana tu  na hakua na sababu ya kuja huku” 

“Amekuja huku sababu ni kwao, hukumkuta shimoni, Neema ana  kwao na Mimi ni Mama yake, kila Mama katika Dunia hii  anapigania Mtoto wake aishi vizuri sasa Mtoto wa Neema atakua katika hali gani ikiwa tayari una Mtoto mwingine na hutaki  yeye afanye maamuzi?” 

“Siyo hivyo Mama yote nimezungumza na Neema, ilikua ni Mimi  kuanza kutekeleza, Mama nisingewanunulia hii nyumba kama  nisingekua na nia na Neema, nimefanya yote sababu ya upendo  wangu, najua Neema anaenda kua Mama miezi michache ijayo,  jukumu langu ni kuhakikisha natekeleza ahadi zangu…” 

“Ikiwemo na kumrudisha kwao Matilda si ndiyo?” alihoji Mama  Neema akionekana kuutambua vizuri mgogoro wa James na Neema,  kigugumizi kikamjaa James 

“Unaona unajiuma uma sababu bado una mapenzi na huyo  Mwanamke, hukua na sababu ya kuhitaji Mtoto kutoka kwa Neema  wakati tayari una Mtoto wako James…” 

“Mama, yote yanazungumzwa sababu naonekana Mimi kama vile  sitaki Matilda aondoke, kinachonipa wakati mgumu ni hali ya  Mtoto wake, laiti kama angelikua mzima basi angeondoka muda  mrefu. Kwasasa yupo kwenye matibabu, akipona ataondoka Mama” 

“Hivyo Eee? sasa akishaondoka ndipo utamchukua Neema, kwasasa  Mwache aishi Hapa” Alisema Mama Neema kisha haraka akaingia  na kufunga mlango, James akajaribu kufungua na kuita Lakini  hakuna aliyefungua mlango. 

“Mimi ni Mama Naomi” Alisema Mama Naomi, simu ikiwa sikioni  akiwa anamnyonyesha Naomi, alikua amekaa kwenye gogo chini ya  Mti nje kidogo ya eneo analoishi, Sauti ya Jack ikasikika 

“Oooh!! uko wapi?” alihoji Jack ambaye ni mfanyakazi katika  ofisi ya James 

“Nipo nyumbani hata hivyo najiandaa kuelekea Hospitalini”  Alisema Mama Naomi akiwa anaweka titi vizuri baada ya Naomi  kushiba 

“Tunaweza kuonana?” 

“Hakuna shida sijui tutaonana wapi?” 

“Nielekeze hiyo Hospitali, mchana nitakuja hapo” “Ni MJ Hospital, Magomeni Mapipa” 

“Sawa Naijua hiyo Hospitali, naomba ubaki hadi mchana”

“Haya sawa!” alisema Mama Naomi kisha alikata simu hiyo,  haraka akamweka Naomi mgongoni, akaelekea kituo cha Daladala  kwa ajili ya kuelekea Hospitali, lakini alihitaji kujua  kwanza kuhusu Matilda, akapiga tena simu kwa Mchungaji,  akaambiwa kua hadi kufikia muda huo hakukua na taarifa  nyingine kuhusu Matilda, alinyimwa hata haki ya kumwona.  Majibu hayo yalimfanya Mama Naomi amuonee huruma sana  Matilda, akaweka simu kwenye sidiria kisha akazidi kuelekea  kituo cha daladala. 

Mwendo wa masaa mawili, Mama Naomi alikua akiingia viunga vya  Hospitali ya JM, alikua amechoka kutokana na purukushani za  hapa na pale katika Daladala, moja kwa moja safari yake  ikaelekea hadi kwa Daktari ambaye alikua akimwangalia Patra. 

“Dokta…..Hali ya Mtoto inaendeleaje?” akauliza Mama Naomi  akiwa anafuta jasho lililokua likimtiririka, hakukua na hali  ya uchangamfu kwa daktari huyo kisha akasema 

“Ni Mungu pekee aliyeishikilia pumzi ya Mtoto, tumaini lipo  kwake. Ina maana hadi sasa hamjafanikisha chochote, vipi  kuhusu Mama wa Mtoto?” akahoji Daktari huku akiwa amemkazia  Macho Mama Naomi 

“Mama wa Mtoto yupo polisi, amekamatwa tokea jana mchana,  pesa zilikua zimekwisha patikana na kibaya zaidi amekamatiwa  hapa” Alisema Mama Naomi huku akiweka kituo 

“Amekamatwa na Polisi, kwa kosa gani?” 

“Kwa Madai ya polisi ni kua ametuhumiwa kwa wizi” “Ina maana Pesa ya matibabu ya Mtoto alienda kuiba Mahali?” 

“Hapana, pesa zilichangwa kanisani Mimi nikiwa shahidi wa  hilo hata Mchungaji wa kanisa akiwepo, lakini cha kushangaza  amekamatwa akipewa shutuma hizo za wizi kitu ambacho si  kweli, namjua vizuri Matilda si Mtu wa kuchukua kitu cha Mtu  hata mara moja” Alisema Mama Naomi 

“Unajua hali ya Mtoto inazidi kua mbaya pengine siku chache  zijazo tunaweza kumpoteza, kiasi cha pesa kinachohitajika ni  kingi mno, hakuna namna nyingine zaidi ya kupatikana ili  Mtoto atibiwe, vinginevyo mtamkosa kabisa” Akasema daktari  huyo 

“Eeeh Mungu sasa tunfanye nini waja wako, huu mtihani mzito  sana Jamani” Akasema Mama Naomi

“Nenda kahangaike, pesa ya Matibabu madogo madogo na dawa za  kupoza ugonjwa naendelea kuzilipa Mimi lakini haitosaidia  kwani matibabu makubwa yanahitajika” Alisema Daktari. 

“Sawa Dokta, sijui hata niingilie wapi….Eeeh na Mchungaji  huyo anapiga” Akasema Mama Naomi, akapokea simu aliyokua  ameishikilia mkononi, sauti ya Mchungaji ikasikika 

********* 

Masaa kadhaa baadaye yalimkuta Mama Naomi akiwa ameketi nje  ya Hospitali akisubiria simu ya Jack ambaye aliahdi angefika  hapo Hospitalini kwa lengo la kuzungumza naye, njaa ilikua  ikimtafuna Mama Naomi, alikua akinyonyesha hivyo ni kawaida  kwa Mama kama huyo kua na njaa muda wote, Naomi alikua tayari  amelala akiwa amemlaza mgongoni, Mara simu yake ikaita,  mpigaji alikua ni Jack 

“Eeh Mungu asante anapiga” Alisema Mama Naomi akiwa  anahangaika kuipokea 

“Habari” ilisikika sauti ya Jack mara baada ya simu  kupokelewa 

“Nzuri tu sijui wewe siku yako imeendaje?” 

“Namshukuru Mungu, nakuja hapo Hospitalini, si bado upo?” “Ndiyo nipo utanikuta” 

“Haya ndiyo natoka ofisini” Akasema Jack na kukata simu. 

“Mama huwenda James ameamua kukaa mbali na Mimi kwasababu ya  ulichomwonesha?” Ilikua ni sauti nyororo ya Neema akiwa  ameketi kwenye Bustani, alikua akizungumza Na Mama yake 

“Hivi unajua thamani ya Mtoto wewe kwa hawa matajiri, hawezi  kabisa sababu anajua unaenda kumpatia Mtoto siku chache  zijazo, Mtoto ambaye atarithi kila kitu chake. Najivunia  kukuzaa Neema, pasi na wewe ningekua naishi kule Uswahilini  nauza vitumbua lakini leo nipo hapa kwenye Bangaloo” Alisema  Mama yake Neema akiwa anatabasamu 

“Lakini Mama mimi nina hofu sana maana tokea asubuhi hadi  muda huu James hajapiga simu, au amekasirika?

“Wasiwasi wako unatokana na nini kwani James ndiye Baba wa  Mtoto?” 

“Hata kama Mimba siyo yake lakini ameniahidi vingi ambavyo  sitaki kuvikosa ndiyo maana nimehonga pesa kwa askari ili  matilda akubali kurudi kwao” 

“Basi Mimi Mama yako nakuhakikishia kua James hana ujanja  mbele yako sababu ni Mama mtarajiwa!! ila tu punguza ukaribu  na Masudi pale unapokua karibu na James vinginevyo utaharibu  mambo, bado hatujafaidika na utajiri wake, ndiyo kwanza  tunaanza kula” Alisema Mama huyo kisha akapeana mikono na  Neema 

Ulikua ni Mpango wa Mama huyo ili wapate pesa kutoka kwa  James ambaye alikua na shida sana ya kupata Mtoto  atakayerithi mali zake zote siku zijazo. 

Matilda alionekana kua kikwazo sababu alikua na Mtoto wa  James japo Mtoto huyo alikataliwa na James kisa ulemavu. 

Ndani ya kituo cha polisi, Matilda akiwa amekaa sakafuni  ndani ya Mahabusu aliyohifdhiwa baada ya kupigwa usiku kucha,  alikua hoi sana akiwa anataja jina la Binti yake Patra, Chozi  lilikua likimbubujika, alikua amechoka hawezi hata  kunyanyuka. Mchungaji George alikua amekaa nje ya kituo  hicho, Mara gari nyeusi iliyoonesha kua haikua gari ya  thamani ndogo iliingia ndani ya Uzio wa kituo cha polisi. 

Akashuka James akiwa amevalia Miwani nyeusi, akaongoza moja  kwa moja hadi mapokezi, hakuhitaji kujitambulisha sana sababu  mwonekano wake pekee ulionesha yeye ni Mtu wa Namna gani 

“Nahitaji kumwona Matilda” Alisema James akiwa ameegemea meza  ya mapokezi, mbele yake kulikua na polisi wa kike ambaye  alikua akimsikiliza 

“Zunguka” Akasema Polisi huyo huyo akiuangalia utanashati wa  James, Haraka James alizunguka akamfuata Polisi huyo ambaye  alimpeleka James hadi Mahabusu aliyohifadhiwa Matilda 

“Wewe Hebu nyanyuka” Akasema Polisi huyo akiwa anagonga nondo  za Mahabusu kwa kutumia kiatu chake, Matilda akaamka na  kugeuka, akamwona James akiwa hapo, taratibu akajikokota hadi  karibu na James, katika hali isiyo ya kawaida kutokana na  hasira akapeleka mkono na kumshika shingoni James,  akaing’ang’ania shingo ya James kwa nguvu na kumfanya James  akose pumzi, yule polisi akasogea haraka na kupiga Mikono ya  Matilda.

James akawa anakohoa baada ya Matilda kumwacha James,  kilichowatengenisha kilikua ni geti la Mahabusu hiyo 

“Uko sawa?” akauliza polisi huyo 

“Aaah Usijali nipo sawa” Akasema James akiwa anajifuta uso  kwa kutumia kitambaa, wakati hayo yote yanatokea kulikua na  polisi mmoja ambaye alikua amekula pesa ya Neema kwa ajili ya  kumshikilia Matilda kwa kesi bandia, akawa anafwatilia kujua  kitakachoendelea hapo 

“Matilda huna haja ya kunionesha chuki kiasi hiki, Mimi siye  niliyesababisha ukawa hapo leo hii” Alisema James 

“Kama si wewe Mwanamke wako anapata wapi ujasiri wa kuyafanya  yote haya?, sijui wewe ni Binadamu katili kiasi gani, Uko  tayari Mtoto afe kwa kukosa pesa ambayo ingeweza kumtibia,  James Mtoto yupo Hospitali alafu unashiriki kunichezea Mchezo  mchafu namna hii?” Alisema kwa hasira Matilda, moyo wa James  uliumia sana kwa jinsi ambavyo Matilda alikua ameumizwa vya  kutosha 

“Matilda huwezi nielewa lakini kwasasa kubali tu kurudi  nyumbani, nakuhakikishia nitamtunza Mtoto wako, nitahakikisha  unaishi Maisha mazuri lakini kwasasa nenda ili kuepusha  shari” Alisema James 

“James!! kama unafikiria nitamsaliti Mtoto wangu hilo litoe  katika akili yako, nitapambana hadi tone la mwisho, siku  Mtoto wangu anaingia Kaburini ndiyo siku ambayo nitakata  tamaa, nitawaambia nini Wazazi wangu,….( Anacheka kidogo)  au niwaambie Baba yake alikufa?” Chozi la maumivu lilikua  linavuja kwenye macho ya Matilda 

“Natamani ufumbue macho yako uone ni jinsi gani nipo katika  wakati Mgumu Matilda, nenda tu nyumbani yasije kutokea mambo  mengine, ukikubali nitamtibu Patra” 

“James! kumtibu Mtoto wako siyo jambo la hiyari hilo ni jambo  la lazima, ni lazima umtibie patra, na laiti kama hutofanya  hivyo nitahakikisha unafirisika” Alisema kwa hasira Matilda  hadi James akashtuka, mara polisi akamwambia James 

“Muda umekwisha” Alisema akiwa anamtoa James ambaye alikua  akitafakari kauli ya Matilda kua atahakikisha ana firisika

“Matilda kubali kuondoka hapa Mjini nakuomba, rudi Njombe”  Alisema James akiwa anaondolewa hapo, yule polisi akampigia  simu Neema akamwambia kua James alikua hapo kuzungumza na  Matilda. 

“Nipo kwenye maegesho ya Magari” Ilikua ni sauti ya Jack  ambaye alikua ameshafika kwenye Hospitali aliyolazwa Patra,  Mara moja Mama Naomi akaelekea Maegesho kuonana Na Jack,  alijisikia faraja sana kumwona Jack ambaye pengine angekua  Msaada 

“Poleni kwa matatizo, Mtoto yupo wapi?” akauliza Jack “Wodini” 

“Ooh naomba nimwone” 

“Haya twende kwakua wamesharuhusu kwa leo” Akasema Mama Naomi  kisha akaongoza kuelekea wodini kwa ajili ya kunwona Mtoto  Patra, wakapewa mavazi maalum kwa ajili ya kuingia kwenye  wodi hiyo ambayo ilikua chini ya Uangalizi maalum, Patra  alikua amelala juu ya kitanda, alikua hawezi kula mwenyewe  bali kulishwa kwa mipira, alikua mdhaifu mno, macho yalimtoka  Jack, ilikua ni jambo ambalo lilimshangaza sana kwa Bilionea  kama James amtelekeze Mtoto ambaye anateseka kiasi hicho,  akasogea na kumtazama vizuri Patra 

Chozi lilimbubujika Jack huku akiishiwa hata aseme nini,  mshangao mkubwa ulimjaa Jack, akamtazama Mama Naomi 

“Hiyo ndiyo hali halisi Dada, Mtoto anateseka Mno, hakuna  tumaini” Alisema Mama Naomi akitoa tabasamu la maumivu, japo  hakua Mtoto wake lakini Maisha ya Patra na Mama yake Matilda  yalimgusa mno. 

“Masikini….hebu tuzungumze vizuri nje” Akasema Jack  akionekana wazi hawezi kuvumilia kuangalia namna Patra  alivyokua akiteseka na homa ya Mapafu. 

“Jamani roho imeniuma sana, siamini kama Bosi wangu anaweza  kufanya hivi, unajua huu ni zaidi ya Unyama?” akasema Jack  akiwa ameketi, Mama Naomi akiwa amesimama 

“Hatuwezi kumsingizia, Patra ni Binti yake wa kumzaa, ni damu  yake lakini kwakua ni Mlemavu ameamua kumkataa kabisa”  Akasema Mama Naomi lakini moyo na akili ya Jack haikutaka  kuamini kabisa kwa namna ambavyo Bosi wake alikua akiishi  naye ofisini

 “Yupo kituo gani Mama yake?” akauliza 

“Ukihitaji nitakupeleka hata sasa hivi” 

“Basi twende huko” akasema Jack kisha wakaelekea kwenye gari,  safari ya kutoka Hospitali kuelekea kituo cha polisi ilianza 

Masaa kadhaa baadaye walifika Kituo cha Polisi, ilikua ni  majira ya jioni, jua likiwa linaangaza Ulimwengu dakika za  mwisho. Waliposhuka walikutana na Mchungaji George ambaye  alishinda hapo kituoni kutwa nzima hadi mida hiyo ya Jioni 

“Shikamoo Baba” Akasalimia Jack 

“Marhaba….Vipi hali ya Mtoto?” akauliza Mchungaji 

“Hakuna tumaini Mchungaji, tumehangaika mno huku na kule bado  ngoma ngumu, bahati nzuri yule Daktari analipia gharama za  matibabu ya Patra japo kidogo kidogo ili kusogeza hizi siku  maana bila hivyo tungekua na simulizi nyingine kabisa”  Akasema Mama Naomi 

“Hata hapa ngoma bado ngumu, sijamwona Matilda tokea asubuhi  nimefika hapa hadi muda huu. Umeongozana na Nani?” 

“Huyu ni Mfanyakazi kwenye ofisi ya James Mwanaume aliyezaa  na Matilda” 

“Ooh karibu Sana” 

“Asante Baba, sijui wataniruhusu kumwona Huyo Matilda?” 

“Mh! sina hakika labda ukajaribu bahati yako tu” Akasema  Mchungaji, Jack akakitazama kituo cha polisi kisha akaelekea  huko huku Mchunagaji akiendelea kupewa maelezo kuhusu Jack 

Kiatu kirefu cha Jack kikagusa ngazi na kuanza kupandisha  kuelekea mapokezi yalipo, alipofika akamkuta askari aliyekua  zamu hapo. 

“Nikusaidie nini?” aliuliza 

“Naitwa Jack! nimekuja kumwona Matilda” Alisema, yule polisi  akamtazama kwa sekunde chache kisha akashusha pumzi na  kumweleza kua

“Ni dakika mbili tu, huyu Mtu hapaswi kuonwa na yeyote,  nafanya hivi sababu wewe ni Mwanamke mwenzangu” Alisema kisha  akaongezea 

“Fanya haraka” Akaelekezwa mahali ambapo angemwona Matilda,  japo dakika mbili zisingetoshea kuzungumza naye ila alihitaji  kumwona na kupata uhakika kua ana Mtoto na Bosi wake,  akapelekwa chumba kimoja ambacho kilikua rasmi kwa ajili ya  kuonana na Mahabusu, akasubiria hapo Matilda aletwe, sekunde  chache Matilda akafika hapo akiwa ameongozana na yule Polisi 

Hakumkumbuka Jack sababu alimwona kwa Mara ya kwanza pale  ofisini kwa James hivyo ilikua rahisi kwake kukubali kuonana  na Jack, akaketi huku akiwa anamtazama sana Jack 

“Samahani na pole Matilda, Naitwa Jack” Alijitambulisha Jack 

“Unanifahamu Mimi?” akauliza Matilda akionekana alikua  ameteswa sana, uso ulikua na majeraha kadhaa 

“Ndiyo nakufahamu japo si sana”  

Nini Kitaendelea? Usikose Sehemu Ya TANO Ya PIGO TAKATIFU Msisahau COMMENTS Ziwe Nyingi

Mpe Nguvu ADMIN Kwa ajili ya bando Kwa kumtumia Chochote aendelee kupost RIWAYA Hapa Kijiweni

Lipa Namba: 57900454
Jina: LIPA KIJIWENI TIPS
Mtandao: VODACOM  

SOMA RIWAYA YA KOTI JEUSI KWA KUBONYEZA HAPA 

SOMA RIWAYA YA FUNGATE KWA KUBONYEZA HAPA 

SOMA RIWAYA YA NILIPANGA NYUMBA MOJA NA MAJINI 

SOMA RIWAYA YA GORYANAH HAPA 

SOMA KISASI CHANGU HAPA  

SOMA RIWAYA YA MSALA HAPA

JIUNGE NIPO KIJIWENI Kwa Kubonyeza Hapa

Pigo Takatifu xx Pigo Takatifu xx Pigo Takatifu xx Pigo Takatifu xx Pigo Takatifu xx Pigo Takatifu xx Pigo Takatifu xx Pigo Takatifu xx Pigo Takatifu xx Pigo Takatifu xx Pigo Takatifu xx Pigo Takatifu xx Pigo Takatifu xx Pigo Takatifu xx Pigo Takatifu xx Pigo Takatifu xx

9 Comments

Leave A Reply


Exit mobile version