“Ahsante Mama Naomi” Ilikuwa ni sauti yenye upole, Matilda  alikuwa akimwambia Mama Naomi huku chozi likimlenga 

“Usijali Mdogo wangu Maisha ndivyo yalivyo, ni wajibu wangu  kukusaidia” Alisema Mama Naomi akiwa amesimama Mlangoni,  alikuwa amempatia Matilda kiasi cha shilingi Elfu tano 

“Nashukuru sana, Mungu azidi kukupa Mama Naomi, unaweza ona  hili ni dogo kwangu lakini Ulichonifanyia ni kikubwa mno”  Alisema Matilda akiwa analia, chozi lilimlenga Mama Naomi  akamwambia Matilda 

“Mpeleke Mtoto Hospitalini Matilda, utanijulisha  kitakachoendelea” Alisema Mama Naomi 

“Ahsante sana ngoja niwahi” Akasema Matilda kisha akakimbia  haraka kurudi anakoishi. Usiku huo ambao ulijawa na giza nene  Matilda alikatiza Uchochoro ili awahi kufika 

Bahati mbaya akakutana na vibaka wakampora pesa na kumpiga 

“Jamani pesa ya Mwanangu hiyo nawaombaa, Nisaidieni Jamani”  Aligumia Matilda lakini vibaka hao walikimbia, Masikini  alilia sana Matilda, alikuwa Msichana wa Miaka 26 tu, akarudi  anakoishi akiwa mnyonge mno, akaingia hadi nyumbani kwake,  akamtazama Mtoto wake aliyeitwa Patra, alikuwa mgonjwa kwa  zaidi ya miezi mitano akiwa ni Mtu wa kulala na kulishwa,  Mtoto huyo alikuwa na miaka mitatu 

Chozi likamvuja Matrida, alimtazama Patra akashindwa  kuvumilia akakimbilia nje na kuanza kulia. 

Asubuhi Mapema, Mama Naomi alikuwa wa kwanza kwenda nyumbani  kwa Matilda, akamkuta akiwa amevimba macho kwa kulia

“Mbona unalia Matilda?” aliuliza, alikuwa kama ameongeza  kilio kwa Matilda, alizidi kulia kwa uchungu sana 

“Usilie Matilda, Mitihani ndiyo nguzo muhimu kwenye Maisha  yetu sisi wanadamu, vipi ulifanikiwa kwenda Hospitali?”  aliuliza Mama Naomi akiwa amebeba deli la kuuzia vitumbua 

“Usiku ule nilikabwa na kuibiwa pesa Mama Naomi, hicho ndicho  kinachoniumiza, laiti kama ningelijua kuwa pesa ile ingeibiwa  ni bora ningekuachia ikusaidie mwenyewe” Alisema kwa Uchungu  sana Matilda 

“Masikini pole Mdogo wangu, Eeeh Dunia yako ina mitihani  mingi lakini Usijali Mdogo wangu sawa?” 

“Sawa Dada, leo sina pesa ya kula ila Mungu ndiyo anajua  nitaishi vipi na huyu Mtoto, afadhali ningekuwa mwenyewe Mama  Naomi yaani kila nikimtazama Patra nazidi kuumia” Alisema  Matilda akiwa analia, Chozi lilikuwa likimvuja 

“Usijali, Basi chukua hii hapa itakusaidia, nikirudi tutaona  jinsi ya kumpeleka Hospitali Patra” Alisema Mama Naomi, japo  naye alikuwa masikini lakini aliguswa mno na Maisha ya  Matilda 

“Sitaki kuwa mzigo kwako Dada, sipokei pesa yako sababu hata  wewe kula yako ya shida, acha Mungu anipiganie Mama Naomi” 

“Usiseme hivyo, Mtoto anatakiwa kula ili ameze dawa Mtilda,  sifanyi kwa ajili yako bali kwa ajili ya Mtoto wako Patra”  Alisema Mama Naomi, akampatia elfu mbili Matilda kisha  akaondoka. Alipofika nje aligeuka na kuitazama nyumba  anayoishi Matilda 

Alikuwa akiishi kwenye nyumba nzuri sana ambayo laiti kama  ungeambiwa kuwa anakosa hata shilingi Mia ya kununua panadol  huwezi amini 

“Eeeh Mungu mpunguzie Mitihani Matilda, anateseka sana”  Akajisemea kisha akaondoka zake 

Mara honi ya gari ikasikika, Matilda akajiuliza ni Nani  aliyekuja, akaenda getini kuangalia, alishangaa kidogo kisha  akafungua geti, likaingia gari la Kifahari sana, baada ya  kuegesha akashuka Mwanaume mmoja akiwa na Mwanamke  

“James afadhali hata nimekuona, Mtoto hali yake si nzuri siku  ya tatu sasa kula ni shida, anahitaji matibabu” Alisema  Matrida 

“Sasa unaniambia Mimi kama Nani?” aliuliza huyo James “Wewe ni Baba wa Mtoto wangu James” Alisema Matilda 

“Oooh kumbe…sikujua kama ni Baba, eti nina Mtoto mwenzio”  Alisema kwa utani kisha akacheka na Mwanamke aliyekuja naye,  akampiga busu 

“Sikia Matilda, nilikwambia unizalie Mtoto na siyo Mfu, yule  siyo Mtoto niliyekuwa namtaka, unawezaje kuwa na ujasiri wa  kuniita Baba wa Mtoto ambaye ni zezeta? hivi unanionaje kwa  mfano, nilivyo naweza kuwa na kitoto kama kile?” alisema  James kisha akashika tumbo la huyo Mwanamke aliyekuja naye 

“Mtoto wangu yupo humu Matilda, tafuta Baba haraka sana wa  hiyo maiti iliyo ndani, hautokuwa na muda mrefu wa kuendelea  kuishi hapa kwani Neema akijifungua atakuja kuishi hapa na  Mtoto wangu. Ila usijali sababu mimba bado changa hivyo una  miezi tisa ya kulea maiti yako” Alisema James, chozi lilizidi  kumvuja Matilda, maneno ya kikatili yalimuumiza sana 

“Baby hii ndiyo nyumba yako, utaishi hapa baada ya kujifungua  sawa?” alisema James 

“Asante Baby….sitaitwa Neema tena bali Mama fulani….”  Alisema huyo Mwanamke wakiwa wanacheka 

“ila Baby mpe hata pesa kiduchu apate kula maana anaonekana  mdhaifu sana” Alisema Neema 

“Kwakuwa umesema wewe Baby basi nitampatia” Alisema James  kisha akatoa noti ya elfu kumi akamtupia Matilda, James  alikuwa ni Mwanaume mtanashati sana, akaingia kwenye gari na  Mwanamke wake wakaondoka hapo.  

Matilda akainama na kuokota noti hiyo japo ilitolewa kwa  masimango lakini ilikuwa ni pesa muhimu sana kuendesha Maisha  yake, akafunga geti kisha akarejea ndani, akatulia kochini  akiwa anakumbuka jinsi alivyokutana na James 

Njombe Tanzania, Baba yake Matilda alikuwa ameketi na Mama  yake Matilda nje ya nyumba yao, Baba Matilda akamuuliza Mama  Matilda 

“Hatuna sababu ya kuendelea kuamini kuwa Matilda yupo hai  sababu ni muda mrefu tangu alipotoweka, hatuna taarifa zake  na hatujui huko aliko kama yupo hai au amekufa, kwanini  tusiweke Msiba?” alihoji akiwa ameketi, Mama Matilda  akajaribu kumsihi 

“Hatuwezi kufanya hivyo hadi pale tutakapo pata uhakika kuwa  Matilda amekufa, hisia zangu zinaniambia kuwa Matilda  anaishi” Alisema Mama Matilda kwa Uchungu sana 

“Bado unaamini hivyo hadi leo?” 

“Ndiyo Baba Matilda, tumuombee Binti yetu popote alipo Mungu  anyooshe mkono wake arejee nyumbani” Alisema Mama yake  Matilda, ilikuwa ni familia yenye majonzi baada ya Matilda  kutoroka hapo, hakuna aliyejua kuwa Matilda alikuwa hai na  alikuwa akiishi Dar tena kwa mateso makubwa sana. 

“Nimesikia Maimuna anaelekea Mjini kesho, naenda kumweleza  kuwa kwa upande wake ajitahidi kumtafuta Matilda huwenda  alitorokea Mjini” Alisema Mama Matilda ambaye alionesha kuwa  hayuko tayari kuamini kuwa Binti yake amekufa 

“Sawa! siku ukikata tamaa utanieleza tuweke Msiba” Alisema  Baba Yake Matilda, Basi Mama Matilda akaelekea kwa Maimuna. 

Familia ilimkumbuka sana Matilda ambaye alitoroka kwao Njombe  na kwenda kuishi Dar, yote aliyokuwa anayapitia hakuna  aliyekuwa akiyajua kabisa, Maimuna alipewa kazi ya kumtafuta  Matilda Njombe Mjini bila kujua kuwa Matilda alikuwa Dar. 

Usiku ulipoingia, Matilda alisali ili Mungu ampe unafuu wa  Maisha, alipomaliza aliketi kisha akamwambia Binti yake  aliyekuwa kitandani akiwa hawezi kutingisha japo kidole 

“Patra Mwanangu muda siyo mrefu utakuwa sawa, Mungu hawezi  kutuacha kirahisi tukaangamia” Alisema Huku chozi  likimbubujika. Maisha ya Matilda yalijaa maumivu makali sana,  Mara geti liligongwa 

Akaenda kufungua akakutana na Mama Naomi ambaye alikuwa  amebeba chakula kwenye Hotpot 

“Jitahidi ule na Mtoto” Alisema Mama Naomi

“Nashukuru sana Mama Naomi na Mungu akubariki” Alisema  Matilda kisha alipokea chakula kutoka kwa Mama Naomi 

“Msalimie shoga yangu Patra Mie hata siingii, nimemuacha  Naomi anakula” Alisema 

“Haya Lakini Ahsante sana” 

“Usijali Matilda, nakutakia Usiku mwema” Alisema Mama Naomi,  Matilda alishukuru tena kabla ya Mama Naomi kuondoka. 

Aliporudi sebleni aliketi kisha akawakumbuka wazazi wake  aliowaacha Njombe 

“Siwezi kurudi Njombe, Baba na Mama mimi nipo hai napigania  Maisha yangu” Akasema maana naye alijua ni jinsi gani wazazi  wake walikuwa wakihangaika kumtafuta 

Siku iliyofuata hali ya Patra ilibadilika akawa anahema kwa  shida sana, Matilda akakimbilia kwa Mama Naomi akamueleza,  wakarudi pamoja na kumchukua Patra hadi Hospitalini 

Baada ya vipimo dokta akawaambia kuwa Mtoto anatakiwa  kufanyiwa upasuaji kwa ajili ya kusafisha mapafu yake,  kuanzia muda huo Patra akawekwa kwenye chumba maalum huku  akisaidiwa na Mashine ya kupumulia 

“Upasuaji ni gharama Dokta, Nami sina uwezo wa kugharamia!”  Alisema Matilda 

“Itabidi uhangaike Dada yangu sababu bila hivyo utampoteza  Mtoto, fanya uwezavyo hakikisha unapata kiasi cha shilingi  milioni 8 ili kunusuru Maisha ya Mtoto” Alisema 

“Dokta kama alivyosema hali ya Maisha imezidi kuwa ngumu,  hakuna namna Hospitali inaweza ikatusaidia ili kuokoa Maisha  ya Patra?” Alidakia Mama Naomi 

“Yote hayo yameangaliwa kwa mapama na marefu yake, Hospitali  inaweza kukusaidia ila mzunguko wake ni mrefu mno kiasi  kwamba itahatarisha hata Maisha ya Mtoto, wewe hangaika  utakapofikia utasema” alieleza Dokta 

Mama Naomi na Matilda wakatoka hapo, Mama Naomi akiwa na  Mtoto Mgongoni akamueleza Matilda

“Itabidi uwende kwa James akakusaidie maana hicho kiasi ni  kidogo kwake” 

“Mama Naomi, James amemkataa Mtoto mara baada ya kuzaliwa tu,  hawezi kugharamia chochote licha ya kuwa Mimi najua Mtoto ni  wake” Alisema Matilda 

“Damu ni nzito kuliko Maji, hebu piga moyo konde twende  tukajaribu” Alisema Mama Naomi 

“Haya twende Mama Naomi japo Moyo wangu unasita kwenda kwa  James, unajua James wakati ananitongoza aliniambia anahitaji  Mtoto, kama nitamzalia atanipa nusu ya Mali zake lakini  alibadilika baada tu ya kujifungua” 

“Yaliyopita si ndwele Matilda hebu twende kwa James,  alivyolala jana sivyo alivyoamka leo” Mama Naomi alizidi  kumpa tumaini Matilda hadi akakubali kwenda kwa James  kumweleza kuhusu Mtoto 

Mishale ya saa tano wakapanda Daladala kuelekea Sinza mori  kutokea Hospitali ya JM iliyopo Magomeni mapipa, Kwenye  daladala Matilda alikuwa kimya sana akitafakari ni jinsi gani  atamueleza James, Mwanaume ambaye alionesha chuki na hasira  dhidi yake pindi tu alipojifungua Mtoto mlemavu, lakini  ilikuwa ni lazima akaonane na James ili asaidiwe pesa ya  matibabu ya Mtoto. Alikua amekaa siti ya mbele karibu na  dereva huku akipikicha macho yake kuzuia chozi kuvuja maana  moyo wake ulijaa maumivu makali mno kila alipofikiria kuhusu  Mtoto wake.

Haikuchukua muda mrefu wakafika Sinza ambako ofisi ya James  ilikuwepo, alikuwa hapafahamu mahali ambapo James alikuwa  akiishi isipokua ni kazini kwake, akasali kidogo kabla ya  kugonga mlango. 

Mlango ukafunguliwa na Mdada mmoja, akawaona Matilda na Mama  Naomi 

“Karibuni, sijui niwasiadie nini?” Aliuliza Mdada huyo mwenye  rasta asilia 

“Asante, Tunashida na James” alisema Matilda 

“Mmeongea naye kuwa mnakuja? Maana ametoka muda siyo mrefu” “Oooh ameeleekea wapi?” Aliuliza Matilda

“Nahisi atakuwa anaelekea kwake maana mara nyingi huwa  akitoka harudi hadi kesho yake” 

“Sawa Asante” 

“Haya karibuni tena” Alisema huyo Mdada, kisha alifunga  mlango, Mama Naomi na Matilda walitazamana maana majibu  waliyasikia kwa panoja, chozi lilimlenga Matilda 

“Usijali Matilda tusikate tamaa kwani kwa kufanya hivyo  hatutoweza kumsaidia Patra, cha msingi ni kumtafuta James,  hebu mpigie nitaongea naye” 

“Haya” 

Matilda akatoa simu na kumpigia James lakini simu  haikupokelewa kabisa, Matilda alikaa chini akaanza kulia kwa  uchungu 

“Matilda hapa ni ofisini kwa Watu, nyanyuka turudi  Hospitalini, tutamtafuta wakati mwingine sawa!!” 

“Lakini mwanangu Mama Naomi, kwanini Mimi tu kila siku,  nimemkosea nini Mungu?” Alisema kwa sauti iliyojaa kilio 

“Hakuna ulichomkosea Mungu Matilda, yeye anapanga na  kutekeleza, hii ni mitihani yake, hakuna kilio  kinachodumu….yataisha tu haya nyanyuka” Maneno ya busara ya  Mama Naomi yalimsukuma Matilda akaamka, wakaanza kuondoka  kurudi Magomeni mapipa. 

Walipofika Hospitalini Magomeni Mapipa, Mama Naomi alimuaga  Matilda sababu alikuwa na Mtoto mdogo, alihitaji kwenda  nyumbani lakini alimtaka Matilda kuwa jasiri sababu akilia  haitosaidia chochote kile. 

“Asante Mama Naomi, Mungu azidi kukubariki” Alisema Matilda ****** 

“James una hakika kuwa hii ni Mimba yako?” Lilikua ni swali  aliloulizwa James, walikuwa chemba na Mama yake wakimuacha  Neema akiwa sebleni 

“Ndiyo Mama kwanini unauliza hivyo?” Alihoji James akiwa  anamtazama Mama yake, alikua ameenda kumtambulisha Neema kwa  Mama yake huko Kiwalani 

“Nimekuuliza tu sababu imekuwa ghafla sana James” Nini Kitaendelea? Usikose Sehemu Ya Pili Ya PIGO TAKATIFU Msisahau COMMENTS Ziwe Nyingi

Mpe Nguvu ADMIN Kwa ajili ya bando Kwa kumtumia Chochote aendelee kupost RIWAYA Hapa Kijiweni

Lipa Namba: 57900454
Jina: LIPA KIJIWENI TIPS
Mtandao: VODACOM  

SOMA RIWAYA YA KOTI JEUSI KWA KUBONYEZA HAPA 

SOMA RIWAYA YA FUNGATE KWA KUBONYEZA HAPA 

SOMA RIWAYA YA NILIPANGA NYUMBA MOJA NA MAJINI 

SOMA RIWAYA YA GORYANAH HAPA 

SOMA KISASI CHANGU HAPA  

SOMA RIWAYA YA MSALA HAPA

JIUNGE NIPO KIJIWENI Kwa Kubonyeza Hapa

Pigo Takatifu xx Pigo Takatifu xx Pigo Takatifu xx Pigo Takatifu xx Pigo Takatifu xx Pigo Takatifu xx Pigo Takatifu xx Pigo Takatifu xx

28 Comments

Leave A Reply


Exit mobile version