Daktari Mkuu wa Simba, Edwin Kagabo ameshusha presha kwa mashabiki wa timu hiyo kuhusiana na hali ya kipa, Aishi Manula aliyeko nchini Afrika Kusini kwa ajili ya matibabu ya nyama za paja.

Kipa huyo na daktari huyo wapo Afrika Kusini, baada ya Uongozi wa Simba kufanya maamuzi hayo ya haraka kwa kuhakikisha anakuwa fiti ili aweze kurejea uwanjani kabla ya msimu ujao kuanza tena.

“Niwatoe hofu kuhusu Aishi Manula kwamba atarejea uwanjani kucheza haraka iwezekanavyo ingawa siwezi kusema wazi ni kwa muda gani, kikubwa mashabiki waendelee kumuombea ili apone vizuri,” alisema.

Aidha Kagabo aliongeza anaamini matibabu hayo yataleta manufaa makubwa kwa Manula kwani malengo yao ni kumuona mchezaji huyo akirejea kucheza haraka kutokana na umuhimu wake kikosini na hata timu ya taifa.

Majeraha hayo yamemfanya kukosa michezo saba mfululizo tangu alipoumia katika mchezo wa robo fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) dhidi ya Ihefu FC uliopigwa kwenye Uwanja wa Azam Complex, Aprili 7.

Kuumia kwa Manula imetoa fursa kwa kipa namba tatu, Ally Salim kupata nafasi ya kuanza golini mbele ya Beno Kakolanya katika michezo mbalimbali ikiwemo ya Ligi Kuu Bara na Ligi ya Mabingwa Afrika.

Endelea kutufatilia zaidi hapa.

Leave A Reply


Exit mobile version