Ilipoishia ” Nilimsimulia kila kitu cha siku ile tu lakini, sikugusia mambo ya nyuma.

“Du! Kwa hiyo mimi nikusaidieje?”

“Naomba tuingie wote ndani, nataka nikachukue simu yangu tu nimpigie huyo jamaa.”

“Da! Itakuwa ngumu kidogo, unajua mimi nina haraka sana leo,” alijitetea yule mtu ambaye kwa umbo ni bonge la mtu. Nilijua ni uoga tu, hakuwa na kuwahi wala kuchelewa “

Endelea SEHEMU YA NANE (08)

Alipopita, akatokea mwingine, mzee mmoja, kichwa chote kilichafuka kwa mvi. Nilimsalimia huku nikimwonesha ishara kwamba nataka kuzungumza naye.

“Mzee samahani sana.”

“Bila samahani kijana.”

Naye nikamsimulia tukio la siku ile,  lakini wakati ananisikiliza, mara nilimwona anatupia macho dirishani na mimi nikageuka kuangalia, sikuona mtu.

“Umeona nini mzee wangu?”

“Nimeona msichana ananizomea.”

“Kweli?”

“Ee. Ndiyo hayo mambo unayosema?”

“Ndiyo hayo mzee.”

“Twende,” alisema, nikaanza kutangulia mbele, mzee akanifuatia kwa nyuma. Hatukuwa tukiongea chochote, najua sababu. Kila mmoja alikuwa anaiwaza hatari ya mbele.

Tuliingia ndani, tukafika sebuleni, lakini sikuiona simu kwenye kochi.

“Ona sasa mzee, simu niliitupia hapa, lakini haipo.”

“Au unayo mfukoni kijana?”

“Hapana, nina uhakika,” nilisema huku nikijipapasa mifukoni, hakukuwa na simu.

“Nitajie namba nijaribu kuibipu,” yule mzee aliniambia huku akitoa simu yake mfukoni. Nilimtajia namba zote, akawa anaziandika, kisha akapiga huku simu akiwa ameiweka kwenye sikio lake la kulia. Nilishtuka sana  kusikia simu yangu inaita kutokea kwenye chumba cha wale wapangaji wenzangu.

“Si hiyo?” yule mzee aliniambia akiniangalia kwa mshangao.

Mzee alikata kisha akapiga tena, ikaita tena kutokea kulekule, nilizidi kuogopa, nikamwambia tutoke lakini uzee kweli dawa, aliniambia hakuna haja ya kutoka dawa ni kupambana tu.

Alinisogelea na kuniambia kwa sauti ya chini:

“Niwagongee mlango?”

“Si watakasirika?”

“Sasa kama unaogopa watakasirika, unadhani simu yako utaipataje?”

“Haya wagongee. Lakini subiri, kwa nini tusiende kwanza chumbani tukajua nani alikuwa anachungulia nje?”

“Kijana unaonekana muogamuoga sana, we mwanaume bwana, jifunze kukabiliana na hali kama hii, sawa?”

“Sawa mzee.”

“Haya twende huko chumbani kwako unakotaka tukaone huyo msichana.”

Tulifungua mlango wa chumbani, hakukuwa na mtu, ila shuka nililoliacha kitandani asubuhi silo, lilitandikwa jingine pia la kwangu.

“Khaa!” nilishangaa.

“Nini?”

“Hili shuka.”

“Limefanyaje?”

“Silo nililolitandika asubuhi.”

“Lakini la kwako?”

“Ndiyo langu.”

Niliangalia mazingira mengine ya mle ndani na kubaini kwamba, kuna vitu vingi sana vilikuwa ndivyo sivyo.

“Si umeona hayupo?” yule mzee aliniuliza, nikamjibu ndiyo, akasema twende tukachukue simu yetu kwenye kile chumba ambacho ilikuwa inaita.

Moyo wangu ulikuwa mzito sana, nilihisi kizunguzungu, nilitamani kukaa chini na kumwomba yule mzee asichukue uamuzi wa kuifuata ile simu, lakini ningeipataje simu yangu wakati ina namba kibao?

“Kijana, ngoja nikuoneshe dawa moja ya hao viumbe wasiotaka kuonekana,” alisema yule mzee, nikamuuliza ni ipi hiyo.

“Tulia wewe,” alisema huku akiingiza mkono mfukoni na kutoa kimfuko kidogo, akakifungua akatoa kitu. Nilipomuuliza ni nini akajibu:

“Ni bangi.”

“Sawa kabisa, hiyo ndiyo dawa, ngoja nikupe kiberiti.”

Katika mambo yaliyonishangaza ni hilo, tulitafuta kiberiti chumbani hadi sebuleni lakini hakikuonekana, mbaya zaidi mimi nilikuwa na kawaida ya kununua viberiti bunda zima, lakini pia sikuona popote.

“Kweli una kiberiti ndani?” yule mzee aliniuliza.

“Kiberiti kipo na uzuri ni kwamba, nina bunda zima, pia silioni.”

Nilimwona yule mzee akisimama wima na kunyoosha mikono juu kama mtu anayeomba dua kwa Mungu.

“Kijana nimejua sasa, ngoja kidogo,” alisema huku akitoka na mimi nikimfuata kwa nyuma.

Wakati tunapita kwenye korido jirani na vyumba vile vya wenzangu, nikaisikia simu yangu ikiita.

“Mzee mzee, hiyo bwana,” nilisema, mzee akasimama na mimi nikasimama nyuma yake, tukasikia sauti ya mwanaume ikipokea simu yangu:

“Haloo…Juma…Juma gani wewe? Nakuuliza Juma gani maana mimi ndiyo mwenye simu hii, huyo unayemsema simjui na wala hajawahi kumiliki simu hii,” sauti ya kiume ilisema, ukapita ukimya kidogo kisha sauti hiyohiyo ikasema:

“Kama unabisha siyo simu yangu ongea na mke wangu huyu hapa.”

Mara nikasikia:

“Haloo…ni kwa nini mnapenda sana kumfuatafuata mume wangu, mara mzungumzie bangi, mara mtusemee kwa watu.”

Nilitamani sana kumwambia asiniache katika safari yake maana kwangu kwa muda ule palishaharibika, ningeuawa na watu wasioonekana.

“Wewe nisubiri kijana,” mzee aliniambia akiendelea kwenda nje sikukubali.

“Mzee humu ndani mimi sikai, nimeshajua sasa.”

“Umejua nini?”

“Huyo Juma anayetajwa hapo nafanya naye kazi na ilikuwa aje na bangi kwa ajili ya hawahawa watu wa humu ndani.”

Mzee aliniangalia, akaniuliza:

“Wewe kijana unaye Mungu?”

“Ninaye.”

“Huwa unakwenda kusali?”

“Sana.”

“Lini umekwenda mara ya mwisho?”

“Ungeniambia tatizo ni kusali au?”

“Si hilo tu, ila una matatizo mengi. Hivi hapa tumesimama, nyuma yako nimemuona yule msichana amekuinamia akikung’ong’a kama mara tatu kwa harakaharaka.”

Nilitimua mbio kuelekea kusikojulikana, nikaenda kufunga breki kwenye mtaa mmoja ambao ukienda kushoto kwangu unakwenda kutokea kwenye barabara ya kwenda Kigogo Mbuyuni.

Baadhi ya watu walioniona nilivyo walitambua nina tatizo zito kichwani, mzee mmoja aliniuliza kama nakimbizwa nimefumaniwa.

 

“Sijafumaniwa mzee, lakini kwa tatizo langu afadhali ningefumaniwa.”

Huyu mzee alikuwa amebeba kibegi kidogo mgongoni, alivaa suti nyeusi huku akionekana ni mzee mwenye heshima kubwa katika jamii inayomzunguka.

“Tatizo nini, hebu nisimulie kidogo tu,” alisema huku akinivutia pembeni. Nilimsimulia kila kitu, alichokuwa akinishangaza sasa, kila hatua ya maelezo yangu alikuwa akiachia tabasamu hata pale nilipoamini kwamba ninachokisema kwa wakati huo asingetabasamu na uso wake ungeonesha kushtuka.

Nilipomaliza nikanyamaza na kumwangalia kwa woga, nilitaka kuamini ni yule mwanaume aliyepokea simu yangu kule nyumbani amenibadilikia ili nisiweze kumtambua.

Moyoni nilisema kuwa, kama kweli ni yeye atakapojidhihirisha  tu kwangu nitoke mbio na kwenda kuingia kwenye nyumba ya mtu yeyote mbele yangu.

“Tatizo ni hilo dogo tu?” aliniuliza.

“Ni hilo tu mzee wangu. Ukiweza kunisaidia nitashukuru sana.”

“Nyumba yenyewe iko wapi?”

“Kule nyuma nyuma.”

Nilimwona akiingiza mkono mfukoni na kuchomoa simu nyeusi ndogo, wengi wanaziita za tochi kisha akabonyezabonyeza na kuiweka sikioni. Moyoni nilisema yaleyale.

“Si ajabu anawasiliana na yule mwanamke wa kule nyumbani.”

 Nikamsikia akiuliza:

“Isdory, bado mpo hapo?”

Nadhani huyo jamaa alisema yupoyupo maana nilimsikia huyo mzee akisema: “Unaweza kuja na akina Tino hapa kwenye kibanda tulichotuma pesa asubuhi ya leo? Haya njooni.”

Niligeuzageuza kichwa na kukiona kibanda cha kutuma pesa kwa kupitia mitandao mbalimbali ya simu. Nikajua amewaita watu waje pale.

Baada ya dakika kama tatu, wakafika watu kama saba, wanne wanawake, watatu wanaume akiwemo Isdory na Tino.

“Huyu bwana anaitwa,” alianza kusema yule mzee akiniangalia nikajua anataka nijitambulishe jina mimi mwenyewe, nikafanya hivyo. Nilipomaliza, ndipo yule mzee akawaambia wenzake kisa chote cha kwangu, mwanzo hadi mwisho kama nilivyomsimulia awali.

“Ndugu, sisi wote walokole, kazi hiyo tunaimudu kwa vile mara nyingi huwa tunatumia jina la Bwana na Mwokozi wetu kufukuza uchafu kama huo, sasa itabidi utupeleke kwenye hiyo nyumba,” alisema yule mzee.

Nilianza kutembea mimi na wao wakawa wananifuata kwa nyuma. Wale wanawake niliwasikia wakizungumzia mwanamke mmoja aliyeangushwa chini na mapepo akawa anataka kupigana na wale waliokuwa wakimwombea. Moyoni nikasema:

“Leo huko sijui.”

Tulifika nje ya nyumba, kitendo cha kwanza ambacho si cha kawaida, nilimwona yule kijana muuza maji akitoka ndani. Alivaa kama siku alivyokuja nikamwingiza ndani.”

Nilishtuka sana, yeye hakushtuka, ila aliponiona akaniambia:

“Bro nashukuru sana wamenilipa pesa zangu.”

Sijui ni nini kilinipata nilijikuta nikisema sawa, sikuongeza neno jingine lolote lile.

“Ni humu waheshimiwa,” niliwakaribisha wale watu nikiwa nimeshapishana na yule kijana.

Waliingia wote ndani, wakasimama katikati ya korido kisha wakawa wananiangalia, yule akaniuliza:

“Hivyo vyumba ni vipi?”

Sikumjibu kwa sauti, nilinyoosha mkono kuelekea kwenye vyumba vyote viwili. Vilioneshwa kufungwa kwa ndani lakini hakukuwa na sauti ya muziki wala maongezi yao.

“Baba katika jina la Yesu,” yule mzee alianza ghafla.

“Amiiiin,” walijibu wote aliofuatana nao, tena walijibu kwa sauti ya juu kisha wakatulia kimya.

Akaanza kusali akitaja maneno ya kutisha, nilimsikia akisema, choma moto roho mtakatifu, mara Malaika Michael shuka na panga likatalo kuwili.

Kifupi yule mzee alisema maneno ya ki-Mungu kwa jinsi nilivyoelewa mimi. Ikafika mahali akasema:

“Paaza sauti yako.”

Ndipo wengine nao wakapokea kwa kila mmoja kuomba kivyake. Wengine walisikika wakisema wanaangusha na kuvunja ngome za ibilisi, wengine wanachoma moto makazi ya shetani, wengine wanamwagia damu ya Yesu pale ndani. Nilianza kuhisi amani iliyoje, niliamini ukombozi umefika tayari kwani sauti tu niliisikia ikipenya hadi kwenye mbavu zangu.

Waliomba sana, kuna wakati mimi nilihisi kuchoka lakini wao waliendelea tu hadi moyoni nikasema kweli ni watu wa Mungu.

Ghafla nilianza kuona moshi mweusi ukitoka chini ya milango yote ya wale ndugu, mlango wa sebuleni kama sikikosei na mlango wa chumbani. Moshi ulikuwa mzito kiasi kwamba, kuna wakati nilihisi kupaliwa na kukohoa kwa nguvu lakini wao hawakuonesha dalili ya kusumbuliwa na moshi huo. Nini Kiliendelea? Usikose sehemu ya 09

Tafadhali Unapomaliza Kusoma Acha Na Comment Yako Hapo Chini

SOMA RIWAYA YA KOTI JEUSI KWA KUBONYEZA HAPA 

SOMA RIWAYA YA FUNGATE KWA KUBONYEZA HAPA 

Una Enjoy Nyumba Ya Majini? Mtumie ADMIN Ahsante

Lipa Namba: 57900454
Jina: LIPA KIJIWENI TIPS
Mtandao: VODACOM 

Wewe Ni Mwandishi? Unapenda kuendeleza Taaluma yako ya uchambuzi kwenye masuala ya michezo? Mtandao wa uchambuzi wa michezo kijiweni.co.tz unakupa uwanja wa kuendeleza kipaji chako na kufikia maelfu ya wapenzi wa michezo Tanzania na nje ya Tanzania.

Tutumie makala au uchambuzi wa michezo katika barua pepe hii editor@kijiweni.co.tz  

29 Comments

  1. Daaah! Kama ni ukweli basi dunia kweli ina mambo! Sema admin unazingua 😂 weka hata mbilimbili kila siku aisee..

  2. Washampiga sana kizinga sasa wameyatimba🤣🤣🤣🤣🤣🤣 sema ninaogipa hadi kuamka prepo kusoma kisa adith

  3. Admin unatutumia usiku ili na sisi wengine ni waoga, ah admin punguzaa sisi wengine tupo peke yetu, mimi naeka kiporo bana

  4. Mtunzi nimekuelewa zaidi unapo ikwepa bangi katika kutumiwa big na haijatumika police pia walimpa onyo kali kuhusu bangi unafundisha pia licha tu kua ni story yakuchangamsha ubongo🏆

  5. 😪😭😭😭💔ni nin lkn mie adii naogopa ahahaha siwaamini wapangaji wenzangu ani baada ya kusoma hii story naota ota🤣🤣… yaaniii nkiamka asubuh nawaangalia wapangaji wenzangu mara mbili mbili

  6. 😂😂😂 m nikajua labda akifika pale atakosa zile nyumba (atakuta nyumba hazipo) 🤣🤣🤣 ila admini ww upo kama LAMATA yaan unatoka nje ya fikra zetu kabisa 😅😅😅 tunaomba uachie mwendelezo mapema sana.

Leave A Reply


Exit mobile version