Ilipoishia “Tulikwenda kusimama pembeni ya nyumba akaanza kuniambia:

“Sikiliza, kama unaishi nyumba ya namna hiyo, unachotakiwa kufanya, kila siku asubuhi na jioni au usiku unapuliza bangi ndani ya nyumba, kama ni majini, mapepo sijui nini, utaona mambo poa kabisa.”

Sikuamini maneno hayo, nikamuuliza mara mbilimbili kama ni kweli.

ENDELEA SEHEMU YA SITA 

“Khaa! Nina mjomba’ngu aliwahi kuishi kwenye nyumba ya hivyo, akaenda sehemu akaelekezwa dawa ni hiyo, akaitumia, mpaka sasa anaishi kwa raha hakuna cha majini wala mapepo,” alisema.

Nilimsikiliza nikianza kuamini kwa mbali, lakini nilifika mahali nikamuuliza hiyo bangi mimi nitavuta au nitaiwasha ili itoe moshi yenyewe?

“Ukishaiwasha, utaiweka mezani au popote ndani kwako, lakini angalia isizimike ili moshi wake usambae chumba kizima au sebule nzima.”

“Hilo linawezekana,” nilimwambia nikimtumbulia macho.

Kwa sababu nilikuwa nimeshaaga, ilibidi niondoke tu na kurudi baadaye. Nilikwenda mtaani, nilitafuta bangi nikapata maeneo ya Kariakoo, nikaitia mfukoni.

Nilizurura sana siku hiyo, saa tisa kamili nilikuwa njiani narudi kazini. Nilipiga hesabu za kufika kazini na kuondoka, maana muda wa kazi ni saa tisa na nusu.

Wakati napita pale Kituo cha Polisi Msimbazi, fujo zikazuka, kuna machinga wawili walikuwa wanapigana kwa sababu ya kugombea sehemu ya kufanyia biashara, katika ugomvi huo mimi nilibaini mmoja wao ndiyo mwenye kosa.

Nikampa laivu kuwa yeye ndiye mwenye tatizo, alikuja juu, akachukua boksi lenye viatu na kunirushia, likanipata kwenye bega la kulia, sikukubali, nikaokota jiwe na kumrushia, likampata mkononi.

Polisi walifika haraka sana, wakanikamata mimi, yeye na yule machinga niliyeona anaonewa, tukapelekwa Msimbazi polisi.

Tulipofika pale, afande aliyetukamata alituamuru kuvua viatu, mikanda, simu kuweka pembeni. Halafu mmoja alianza kutusachi mifukoni. Wakati tendo hilo linaanza kwa wenzangu, ndipo nikakumbuka mimi mfukoni nina vipisi viwili vya bangi.

Nilitaka kutoka mbio kituoni hapo, lakini sehemu tuliyokaa, ningesema nitoke, nisingefika nje au hata kama ningefika ningekamatwa au kupigwa risasi kama mhalifu, nilitetemeka, mwili uliisha nguvu.

Ilipofika zamu yangu kusachiwa, askari mwenyewe alishangaa kuniona nachezesha miguu kama niliyebanwa na haja ndogo, akaniuliza:

“We vipi, unaumwa?”

Nikamjibu naumwa afande.

“Unaumwa nini?”

“Sijui, nadhani homa.”

Hakunijibu, alianza kwa kutumbukiza mkono kwenye mfuko usiokuwa na kitu, akahamia wa nyuma ambao una waleti, akapeleka wa kulia kwangu ambao ndiyo wenye bangi, aliposhika, akakunja sura, alipotoa akashtuka sana na kusema:

“Haa! Hii bangi siyo?”

Sikumjibu kwani niliamini ameshaijua, wenzake waliokuwa kaunta wakaacha mambo yao na kunigeukia mimi, nao wakashangaa sana. Mmoja alikuwa amekaa juu ya stuli, akashuka huku akiniangalia kwa kunikazia macho.

“Unakuja kituo cha polisi na bangi, wewe unatutafuta nini sisi?” aliuliza yule aliyeshuka kwenye stuli.

Niliambiwa nafunguliwa kesi ya pili, ya kwanza kupigana na kujeruhi ya pili kukutwa na bangi!

Nilijitetea nikisema bangi ile si kwa ajili ya kuvuta bali nilikuwa nina shida nayo.

“Wewe usitufanye sisi watoto wadogo, tunawajua ninyi raia,” alisema yule afande aliyenisachi.

Lakini afande mmoja wa kike ambaye muda wote alikuwa akiangalia tu, akawaambia wenzake:

“Lakini huyu kaka mbona hafanani na kuvuta bangi, muulizeni ana shida nayo gani?”

Wale wenzake wakanigeukia na kuniuliza:

“Haya, wewe mwananchi, raia kabisa, unaweza kuwa na shida gani na bangi mbali na kuvuta?”

Niliwasimulia kila kitu, tena nilifika mahali nikawaambia kama kuna asiyeamini, tuongozane hadi nyumbani, Magomeni akaone maajabu ambayo hayahitaji kuelekezwa sana ili kuamini kama yapo au la!

Palipita ukimya wa sekunde kadhaa, mmoja wao akaniuliza:

“Kama ni kweli au tufanye ni kweli, ni kwa nini umemuumiza huyu?”

Nilisema kilichotokea, yule chinga niliyemsaidia naye akanitetea kwa kusema hivyohivyo, lakini afande mmoja akasema nilijichukulia sheria mkononi ambapo ni kosa kisheria.

Niliomba sana wanisamehe kwa yote, nikasingizia kwamba ni kwa sababu kichwa changu hakipo sawa kwa kuishi nyumba moja na majini.

Namshukuru mmoja wao aliniambia niondoke lakini nihakikishe situmii bangi katika kujitibu kwani serikali haiamini kama bangi ni dawa.

Nilipotoka, nilikwenda kununua nyingine, lakini akili iliingia hisia kwamba, huenda yule dada wa ajabu mle ndani ndiye anayecheza michezo ili kunikwamisha kwenda na bangi ndani ya nyumba, nikasema moyoni ngoja ninunue hii nione kitakachotokea, nikanunua tena misokoto miwili.

Nilitembea kuelekea kituo cha daladala. Njiani nilimpigia simu yule mfanyakazi mwenzangu aliyenijulisha kuhusu dawa ya kutibu nyumba yenye majini, nikamwambia sitaweza kurudi kwani nilipata wakati mgumu kidogo njiani.

Alinielewa, akaniuliza kama nimepata, nikamjibu kila kitu kimekwenda sawa, lakini sikumwambia kuhusu timbwili lililojitokeza.

Nilipanda daladala nikashuka Magomeni, niliingia ATM kutoa fedha kidogo, kisha nikatoka. Wakati natafuta mwelekeo wa kwenda nyumbani, nilimkumbuka dalali, nikampigia simu.

“Halo.”

“Halo habari za kazi bwana?”

“Nzuri, pole na kazi na wewe mwenzangu?”

“Nimepoa. Bwana vipi kuhusu nyumba?” nilimuuliza.

“Nyumba imefanyaje?”

“Si nilikusimulia matatizo yake, umesahau?”

“Kwani ulisema matatizo yake yakoje vile?”

Nilimwelezea kwa kirefu, nikafika mahali nikamwambia hadi nilivyompigia simu halafu ikapokelewa na sauti ya ajabuajabu, alicheka sana.

“Wewe bwana acha kunichekesha.

“Kwa nini unasema hivyo?”

“Yaani simu yangu mimi halafu apokee mtu mwenye sauti ya ajabuajabu, kwa nini sasa?”

“Mimi pia sijui.”

“We ulikosea namba.”

“Labda bwana mi siwezi kukazania sana,” nilimjibu kwa kinyongo kwani namba yake niliisevu na ninapompigia huwa nasachi jina tu, sasa nilikosea kivipi?

“Enhe, unasemaje bwana?” aliniuliza.

“Nimeshakwambia bwana.”

“Kwa hiyo unashauri nini?”

“Nataka pesa zangu nikapange kwingine.”

“Da! Hilo halitawezekana kirahisi bwana, maana mpaka nimpate mpangaji mwingine atoe fedha ndipo nikulipe wewe na mpangaji atakayekuwa tayari kutoa fedha lazima akute nyumba tupu, sasa wewe utalikubali hilo?”

 

“Naweza kulikubali, ila tuandikishiane.”

“Kwamba?”

“Kwamba unajikomiti nikiondoka, akiingia mpangaji mwingine tu unanilipa pesa zangu.”

“Ngoja nitakupigia,” alisema dalali na kukata simu.

Nilipokuwa nakaribia nyumbani, nikakutana na yule msukuma mkokoteni wa maji.

“Kaka za kazi?”

“Nzuri, vipi wewe?”

“Niko sawa, ndiyo unarudi?”

“Ndiyo.”

“Najua jamaa hawajarudi, nitakuja muda uleule tuliopanga.”

“Sawa, karibu sana.”

“Asante sana.”

Niliingiza funguo ili kufungua mlango, lakini nikagundua kwa ndani kulikuwa na funguo nyingine maana nilichungulia.

Nilipousukuma, ulifunguka. Hii ina maana wale watu wa ajabu walikuwa wamesharudi, wako ndani. Niliingia ndani, nikafungua mlango wa sebuleni, nikaingia humo.

Nilifikia kwenye kochi kubwa, nikajilaza. Sikuangalia kama kweli wenzangu walikuwa wamesharudi, ila nilisikia sauti ya muziki wa redio, nikajua wapo.

Mara nikasikia mlango wao mmoja ukifunguliwa, nikasikia mtu akitoka. Kwa mara ya kwanza nilisikia akisema:

“Kama utamkamata anavuta bangi apelekwe polisi, ndiyo dawa yao watu wa aina hii.”

Nilishtuka, nikakaa. Nikawaza kama ninachosikia ni cha kweli au?

Huyo aliyekuwa akisema hayo ni mwanamke na ilionekana alitoka kuelekea uani. Nikatoka ghafla, nikaona kisigino cha mguu mmoja kikimalizia kuingia chooni. Nilirudi chumbani huku najiuliza kama hawa watu walisema vile kwa sababu wamejua mimi nimenunua bangi au? Na ni kwa nini wazungumze Kiswahili kwa mara ya kwanza siku hiyo? 

Baada ya dakika mbili, nilimsikia akirejea chumbani kwake huku akisema:

“Mimi mtu anayevuta bangi siku yoyote na mahali popote pale, nikimwona nampeleka polisi ajue mimi ni nani. Haiwezekani watu wawe wanavuta bangi hovyo tu.

Moyoni nikasema hata iweje, hii bangi leo lazima niichome humu ndani. Mkienda polisi msipoenda mtajua wenyewe.

“Mimi siwezi kuishi katika mazingira magumu namna hii wakati pesa ni yangu. Kwa nini ustaarabu usiwepo?” nilisema moyoni nikipeleka mkono mfukoni ili kutoa ile bangi niliyonunua mara ya pili.

 Niliipata, nikaitoa. Niliiweka kwenye meza kisha nikaendelea kulala nikiusaka usingizi kwa nguvu zangu zote maana nilijisikia kuchoka sana. Hapo nilikuwa sijaenda chumbani kwangu.

Sikumbuki ni muda gani nilipitiwa na usingizi, ila nakumbuka wakati nalala ilikuwa saa kumi na moja. Nilipokuja kushtuka ilikuwa saa kumi na mbili na nusu. Ina maana nililala kwa saa moja na nusu.

Jicho langu moja kwa moja lilitua kwenye bangi pale mezani, sikuiona.

Nilihamaki kwa kusema ha! Nani amechukua bangi yangu? Sikujibiwa na mtu, ukimya ulitawala huku akili ikiniambia wale wapangaji wenzangu watakuwa wanahusika moja kwa moja.

Baada ya muda nilitoka mle sebuleni, nikaenda chumbani. Nilifungua mlango na kusimama kwanza kabla ya kuzama ndani. Niliangaza kila kona, nikabaini kitu. 

Mambo ameyatibua zaidi.. Nini kitaendelea? 

SOMA RIWAYA YA KOTI JEUSI KWA KUBONYEZA HAPA 

SOMA RIWAYA YA FUNGATE KWA KUBONYEZA HAPA 

Una Enjoy Nyumba Ya Majini? Mtumie ADMIN Ahsante

Lipa Namba: 57900454
Jina: LIPA KIJIWENI TIPS
Mtandao: VODACOM 

Wewe Ni Mwandishi? Unapenda kuendeleza Taaluma yako ya uchambuzi kwenye masuala ya michezo? Mtandao wa uchambuzi wa michezo kijiweni.co.tz unakupa uwanja wa kuendeleza kipaji chako na kufikia maelfu ya wapenzi wa michezo Tanzania na nje ya Tanzania.

Tutumie makala au uchambuzi wa michezo katika barua pepe hii editor@kijiweni.co.tz  

 

 

51 Comments

  1. Ambros Mchau on

    Kaka hii storry ni nomaaa yaani huchoki kuisoma ni burudani,yaani hii sehemu ya 6 nimejikuta nasoma huku nacheka hatarii,daahh ni moto

  2. Official DG on

    Admini hili igizo kwenye sinema zetu jmn🤣🤣🤣. Badilisha bana. Lete mambo kama fungate . hili nalikumbuka kbs kwenye sinema zetu azam tv

  3. Zeyy Tabasamu✨🥰 on

    Ndo nmepata mda sahzi ila sisomiiii ng’ oooooooo🤣😂🤣NALALA pekeaangu nasoma keeesho Comment zmejieleza ya Leo Noma stry inazid kutisha🙌

  4. Weeeh! Kwa kweli hii story sijaribu kusoma usiku nisije na mimi nikapata mauzauza 😂🙌 ila Admin 🫡 salute sana kwako maana story inazidi kunoga kila siku ❤️

Leave A Reply


Exit mobile version