Ilipoishia “Kazini siku hiyo nilishinda sina amani, sina raha, mwili ulikuwa kama umetoka kufanya kazi nzito ambayo sijawahi kuifanya kwa siku nyingi, wenyeji wa Pwani wanaita mavune.

Kwa upande mwingine nilitamani sana jioni ifike ili nikaone siku hiyo kitatokea kitu gani kipya kwenye nyumba ile. Jioni ilifika, nikaondoka kazini, sikutaka kupitia popote, dukuduku langu lilikuwa kwenda nyumbani tu.”

ENDELEA: SEHEMU YA TATU-03

Nilichukua kama saa moja kutoka kazini hadi kufika nyumbani. Nje nilikuta mfuko wa rambo  mweusi, ndani yake ulionekana kuwa na kitu kwani ulikuwa umetuna sana. Niliinama kuipekenyua ili nijue ndani kulikuwa na nini, nilishangaa kuona ni vipande vya nyama za kuchoma tena vilikuwa vya moto.

“Kha! Atakuwa nani ameweka?” nilijiuliza mwenyewe, nikauacha palepale, mimi nikapanda ngazi za kuingia ndani. Mlango ulikuwa wazi hali iliyoashiria kwamba, wenzangu walisharudi. Nilisukuma mlango, nikaingia. Nilikutana na harufu ya pafyumu, nikahisi walikuwa wakijiandaa kutoka.

“Jamani za leo?” nilisalimia kwa sauti ya juu licha ya kwamba, mlango wao ulikuwa umefungwa, hakuna aliyeniitikia, hilo sikulijali sana kwani niliamini kwa kuwa walikuwa ndani, isingekuwa rahisi wasikie salamu yangu.

Niliingia sebuleni kwangu, kisha nikaenda chumbani, kuna kitu kilinishangaza, nikasimama kwa mshtuko. Nilikuta sehemu nilipoweka kiberiti asubuhi siyo, nilikiacha juu ya meza, nikakikuta juu ya kitanda. Niliacha kioo na kitana juu ya kitanda, lakini nikavikuta kwenye stuli, niliguna!

Nilikishika kioo na kukiangalia kwa umakini kama kina mabadiliko yoyote, lakini sikuona, nikashika kitana. Nilipokigaua sana pia sikuona kitu cha tofauti, nikaamua kuchania, nikahisi kuguswa na kitu kama nywele ndefu kama za mtu aliyefuga. Nilikiweka kitana juu usawa wa dirishani, nikaona nywelenywele nene, nyeusi, mwili wote ukasisimka.

Ninavyojua mimi, mwanamke mwenye nywele nyingi akichania kitana, ndiyo huacha nywele, sasa mimi nilikuwa na nywele fupi sana zisingeweza kuacha nywele ndefu kwenye kitana.

“Mh! Hapa kuna kinachoendelea,” nilisema moyoni huku nikikaa. Nilishtuka zaidi kuona soksi zikiwa kwenye msumari nyuma ya mlango wakati niliacha chini.

“Huyu ni nani?” niliuliza kwa sauti ya ukali.

Ghafla nikasikia kicheko kutoka chumbani kwa wale wenzangu.

Nilikaa kwenye kochi, nikaanza kuangalia sehemu mbalimbali za mle ndani ambazo niliamini naweza kuona mabadiliko mengine mbali na yale ambayo nilishayaona, lakini sikubahatika.

Nilitoka, nikaenda sebuleni ambako nako nilianza kuangalia kila kona ya sebule. Nilishangaa kuona glasi ya maji ya kunywa ambayo niliitumia asubuhi kisha nikaacha maji yamejaa, ikiwa haina hata tone la maji mbaya zaidi, iliwekwa juu ya kabati ambapo mimi niliiweka kwenye meza ya katikati ya sebule.

“Mh! Hii kali sasa,” nilijikuta nikisema kwa sauti, mara nikasikia kicheko tena kutokea upande wa pili kule kwa wenzangu. Sasa nikaanza kama kuhisi kitu kuhusu watu hao. Ni kwa nini kila nilipoongea kwa sauti ndipo na wao waliangua kicheko?

Niliamua kujaribu tena, nikasema kwa sauti:

“Nitakuja kuua mtu, kweli tena.” Nikasikia kicheko tena, safari hii kilidumu kwa muda.

Moyoni nikasema naanza kufanyia kazi uhusiano wa maneno yangu na vicheko vya wale majirani. Nilitoka kurudi chumbani, wakati napita kwenye korido, nilisimama jirani na mlango wao. Walikuwa wakiongea, lakini niliposimama mimi, kukawa kimya ghafla kama hakuna watu.

Nilipozama chumbani, nyuma wakaanza kuongea tena. Sikufunga mlango ili niweze kusikia wanachokiongea, lakini jamani kwa kusema ule ukweli wa Mungu, sikujua walikuwa wakitumia lugha gani katika kuwasiliana hata pale nilipojitahidi kutega masikio kwa umakini wa hali ya juu sana.

Kuna wakati utadhani wanatumia sana neno dotikom, lakini ukisema usikilize zaidi unasikia wakisema sana kotoko au kiburate, wakati mwingine sauti ya kike ilisema kaunto, ya kiume ikarudia hivyohivyo, kaunto.

Nia yangu kubwa ilikuwa kuwaona kwa sura na kufahamu kama ni ngozi nyeusi au nyeupe. Hilo peke yake lingenipa mwanga ni watu wa aina gani naishi nao pale ndani ya nyumba.

Nilisikia mlango wa chumbani kwao ukifunguliwa na mimi nikatoka haraka sana, cha ajabu sikuona mtu akitoka lakini mlangoni kulikuwa na kandambili pea moja tu wakati zilikuwa pea mbili.

Hilo lilimaanisha kwamba, mmoja wao alitoka kwenda chooni, nilichofanya ni kuamua kusimama katikati ya mlango wangu ili huyo aliyekwenda chooni akirudi nimuone. Ni kweli mmoja wao alikwenda chooni kwani nilisikia mlio wa maji.!!

Nilijitahidi kusimama mlangoni kwangu kumsubiria. Kwa ramani ya nyumba ile ilivyo, asingeweza kutoka chooni bila mimi kumwona hata kama angekuwa anataka kutoka kwenda nje au uani.

Mlio wa maji ulikosa kusikika, nikawa natumbulia macho kule huku moyoni nikisema:

“Leo ndiyo leo, asemaye kesho mwongo, hata afanyaje, hawezi kunichenga hapa hata kidogo kwenye hii nyumba,” nilisema moyoni, ingawa wakati huo mapigo ya moyo yalikuwa yakinienda kwa kasi.

Nilipoanza kuhisi muda unakwenda na hakuna mtu aliyetoka, nikampa dakika tatu kwamba lazima atakuwa anavaa ndiyo maana anachelewa:

“Labda alikuwa anajisaidia haja kubwa, maana wengine huwa wanavua nguo zote, lakini mimi nipo, siendi kokote,” nilisema moyoni nikiwa bado nimesimama mlangoni kwangu.

Baada ya muda, nikasikia watu wakiongea chumbani kwao, nikashtuka, nilijikuta nikisema:

“Haa!”

Haraka sana nilitupa macho mlangoni kuangalia kandambili, nikazikuta pea mbili, nikashangaa:

Nini Kiliendelea? Usikose sehemu ya nne

SOMA RIWAYA YA KOTI JEUSI KWA KUBONYEZA HAPA 

SOMA RIWAYA YA FUNGATE KWA KUBONYEZA HAPA 

Una Enjoy Nyumba Ya Majini? Mtumie ADMIN Ahsante

Lipa Namba: 57900454
Jina: LIPA KIJIWENI TIPS
Mtandao: VODACOM 

Wewe Ni Mwandishi? Unapenda kuendeleza Taaluma yako ya uchambuzi kwenye masuala ya michezo? Mtandao wa uchambuzi wa michezo kijiweni.co.tz unakupa uwanja wa kuendeleza kipaji chako na kufikia maelfu ya wapenzi wa michezo Tanzania na nje ya Tanzania.

Tutumie makala au uchambuzi wa michezo katika barua pepe hii editor@kijiweni.co.tz  

31 Comments

  1. Zeyy Tabasamu✨🥰 on

    😂😂😂Aaah Mhandishi una sifa sanaaa imagen mtu unaogopa kwa kitu cha kusoma Yan Unavuta picha🤣😂🤣Big up kwakooo

Leave A Reply


Exit mobile version