Ilipoishia “Nje, nilikuta taa inawaka, ndani pia taa inawaka, lakini si sebuleni bali kwenye korido. Hii iliashiria kwamba, wale wapangaji wenzangu walisharudi kutoka kwenye biashara zao.

Nilishusha vyombo kwa kusaidiwa na wasaidizi wa dereva wa lile lori, lakini nilishangaa sana kuona kila nikiingia na mizigo, wale wapangaji wenzangu wanacheka sana chumbani kwao. Maana yangu ni kwamba, kwa kawaida walitakiwa hata watoke na kunisalimia ili tufahamiane. Tena kwa wengine, mume angetoka na kunisaidia kubeba hata stuli tu.”

Endelea Sasa 

SEHEMU YA PILI (02)

Ilifika mahali, wale vijana waliokuwa wakinisaidia waliniuliza:

“Hivi hao majirani zako mbona hawatoki, wanacheka tu chumbani.”

Niliwajibu mimi mwenyewe sijui, lakini sikumaindi sana. Akaja mama mmoja aliyesema anaishi nyumba ya pili, akasalimia na kuniuliza maswali.

“Hamjambo wanangu?”

Tuliitikia wote, akauliza nani anahamia pale kati ya sisi wote, tulikuwa watano mbali na dereva.

“Ni mimi.”

“Ooo, mzima baba?”

“Mimi mzima mama.”

“Unaitwa nani?”

“Humuli Samaki.”

“Unahamia peke yako au uko na mke na watoto?”

“Peke yangu mama.”

“Humuli Samaki ni mwenyeji wa wapi?”

“Usukumani.”

“Haya, naamini uliaga wakati unaondoka nyumbani.”

“Hilo lilikuwa la kwanza mama.”

“Haya, kila la kheri.”

Tuliendelea na kazi ya kuingiza vyombo ndani hadi tukamaliza. Wale wenye gari wakaondoka, nikabaki mimi peke yangu.

Nilijiwekea malengo kwamba, nihakikishe naweka sawa kila kitu ili kesho yake nisiwe na kazi hiyo zaidi ya kwenda kazini. Niliifanya kazi kwa muda wa saa tatu, mpaka kwenye saa saba na nusu usiku nikamaliza.

Nilibadili nguo, nikavaa taulo na kwenda kuoga. Nilikuta bafu limetoka kutumika kama dakika kumi nyuma, sikushangaa kwani si kuna wapangaji wengine ambao tulitakuwa tunatumia bafu moja.

Usiku kabla ya kuzima taa, nilizima taa, nikapanda kitandani. Kabla sijapata usingizi, niliwasikia wenzangu wakicheka sana na kuongea huku wameweka muziki. Lakini ule muziki haukuwa wa kiarabu, kizungu wala kiswahili.

Hata maongezo yao, mimi nilisikia sauti tu lakini kusema walikuwa wanatumia lugha gani si rahisi. Kuna wakati kama walikuwa wakiongea kihindi, pia niliwasikia kama wanaongea kiarabu, nikajua ni watu wa namna hiyo.

Lakini sikulala mpaka nikampigia simu dalali kumuuliza kama wale wapangaji wenzangu ni weupe au waswahili kama mimi, akasema hata yeye hajui kwani hakuwahi kuwaona hata siku moja.

Basi, nililala. Asubuhi niliamka nikiwa nimechoka sana. Wakati nakwenda bafuni kuoga niligundua ni mimi peke yangu ndiye niliyekuwa nimetangulia kuamka, kwani bafuni hakukuwa na maji yaliyomwagika kwa muda huo.

Baada ya kuoga nilirudi chumbani kwangu kujiandaa kwenda kazini. Wakati najiandaa, nilisikia mlango ukifunguliwa, nikajua ni wenzangu wanakwenda kuoga au chooni kama ilivyo kawaida kwa wanadamu wakiamka asubuhi.

Niliamua kutumia nafasi hiyo kuwatambua. Nilivizia pale niliposikia mlio wa maji bafuni na mimi nikatoka kwenda kupiga mswaki kwa mara ya pili. Sehemu niliyosimama, mtu akitoka bafuni kwenda ndani ilikuwa lazima nimuone kwani ilikuwa kiasi cha kugeuka tu.

Lakini cha kushangaza, nilikuwa sisikii maji kumwagika, nikageuka na kuona mlango wa bafuni upo wazi. Mbali na mlango kuwa wazi, pia chini nikaona alama za kandambili nne zikiwa zimekanyaga, nikajua wametoka.

“Lakini wamepitaje hapa?” nilijiuliza.

Nilirudi ndani, mlangoni kwao nilikuta kandambili pea mbili zikiwa bado na majimaji kwa mbali, jambo hili lilinifanya nijiulize sana.

Nilijipa ujasiri na kuamua kuchungulia ndani ya chumba hicho kwa kutumia nafasi ya katikati ya mlango ambapo niliweza kuona hadi kitanda lakini sikumwona mtu mwingine.

Niliingia kwangu, nikaweka mswaki, nikavaa vizuri na kuondoka zangu. Nilitegemea wenzangu nimewaacha ndani, kwani nilipofika mlangoni nilikuta umefunguliwa na upo wazi. Nilirudi ndani hadi kwenye mlango wao.

“Wa ndugu,” niliita kwa sauti.

“Jamani wa ndugu.”

Ukimya ndiyo ulinifanya nibaini walishaondoka. Kwani kulikuwa kimya sana na kandambili zilikuwa pembeni ya mlango si pale pa kwanza.

Nilifunga mlango mkubwa nikaondoka, mbele nilimwona yule mama aliyekuja usiku kuniuliza maswali. Alikuwa amesimama nje ya nyumba yake, aliponiona akashutuka na kuita majina mawili ya watu. Wakatoka watoto wake wawili, ni mabinti wenye miaka kama kumi na nane na ishirini na mbili hivi.

“Hujambo kijana?” yule mama alinisalimia kwa furaha.

“Sijambo mama, shikamoo.”

“Marhaba.” Kisha akawaambia kitu wale watoto wake nao wakanikazia macho.

“Mama umewaona majirani zangu hapa?”

“Majirani zako akina nani?”

“Wapangaji wenzangu.”

“Kijana, kua uyaone ya dunia. We si umeshakua, utayaona ya dunia.”

Kauli hiyo iliniogopesha sana, nikashtuka na kumuuliza mama.

“Mama una maana gani?”

“Sisi hatutaki umbeya kijana.”

“We si umeambiwa utayaona kwa hiyo subiri tu,” alidakia binti yake mkubwa.

Miguu ilitetemeka, mwili uliisha nguvu, nikajikuta nataka kukaa, lakini sikuweza. Nilichoamua ni kuondoka huku nampigia simu yule dalali.

“Vipi hujambo bwana?”

“Mimi sijambo.”

“Za makazi mapya.”

“Si nzuri bwana.”

“Kwa nini tena?”   

“Sielewielewi.”

“Kivipi?”

“Kuna mambo kama si ya kawaida.”

“Yapi hayo?”

“Wale wapangaji wenzangu siwaelewi kabisa.”

“Kivipi?”

“Ah! Watu gani mimi mgeni nimehamia washindwe kutoka kunisalimia ili angalau tufahamiane?”

Dalali alicheka sana kisha akasema:

“Wale ndivyo walivyo bwana, si unajua tena malezi, mwingine kalelewa vile, mwingine hivi. Ila ulichokisema ni kweli, haiwezekani nyumba mnayoishi mpate mgeni halafu msitambuane, sasa mkikutana njiani je?”

“Si ndiyo hapo sasa,” nilisema nikijifanya lawama zangu ni kwa ajili ya hilo tu, lakini kumbe nilikuwa na zaidi ya hapo.

Kazini siku hiyo nilishinda sina amani, sina raha, mwili ulikuwa kama umetoka kufanya kazi nzito ambayo sijawahi kuifanya kwa siku nyingi, wenyeji wa Pwani wanaita mavune.

Kwa upande mwingine nilitamani sana jioni ifike ili nikaone siku hiyo kitatokea kitu gani kipya kwenye nyumba ile. Jioni ilifika, nikaondoka kazini, sikutaka kupitia popote, dukuduku langu lilikuwa kwenda nyumbani tu.
Baada ya kufika nyumbani ilikuaje? Usikose Sehemu ya Tatu

SOMA RIWAYA YA KOTI JEUSI KWA KUBONYEZA HAPA 

SOMA RIWAYA YA FUNGATE KWA KUBONYEZA HAPA 

31 Comments

  1. Unajuwa mimi sio mpenzi wakusoma hadithi sema hadithi zako nimezielewa sana ukianzia ile ya fungate ndo imenivutia niwe sahabiki wako namba 1 BIG UP 🫡

  2. Alikuwa hajui mizamwamwa eeeeh 😂😂😂😂😂😂😂 hapana chezea misoweto 😂😂😂😂😂😂😂🙌🙌

  3. Em tupe mda maalumu maana unatuacha na shauku San Asee af unachelewa sana kuweka mwendelezo ila stor n tamu balaaa

Leave A Reply


Exit mobile version