IlipoishiaBasi Maisha ndani ya Gereza yaliendelea, siku moja baada ya  kazi ilikuwa ni majira ya saa 7 Mchana, ulikuwa ni muda wa  kupata Chakula. Tulikuwa tukipanga mistari miwili kwa ajili  ya kupata Chakula, msitari wa kwanza nilikuwepo Mimi, sasa  katika tazama tazama nilistaajabu nilimuona Sarafina, yule  Mdada ambaye alifukuzwa na Shonaa kisa Mimi, nilitamani  kumuita ila nilikumbuka kuwa alikuwa na hasira na Mimi,  nilimgeukia Isabela nikamuuliza 

“Yule yupo hapa kwa muda gani?” Nilimuonesha kidole Sarafina 

“Nimemkuta hapa, anaonekana kahukumiwa muda mrefu ila  inasemekana aliiba pesa kwa tajiri mmoja” 

“Vipi unamjuwa?” 

“Ndio namjuwa” Basi baada ya kuwa tumeshachukua chakula  tulienda kula, Isabela aliniuliza 

“Unamjua vipi yule”  Endelea 

SEHEMU YA NANE

“Wakati nakuja hapa Dar ndio nilionana naye ila tuliachana  kwa shari, aliniona mbaya akidai nimesababisha amefukuzwa  pale alipokuwa anaishi” Nilisema 

“Mh! Sasa itabidi ujiadhari maana yule ana kundi lake hapa  gerezani ambalo linaendesha ubabe mwingi, akijuwa kama upo  hapa utaishi kwa shida sana” Alisema Isabela. 

“Ni kweli lakini nitamkwepa vipi wakati tunaishi kwa uwazi  hivi, ikiwa mimi nimemuona nina imani na yeye ataniona tu.” 

“Cha msingi ni kumkwepa vinginevyo utateseka sana hapa Jojo” 

“Mh! Tutaona itakavyokuwa” Tulipomaliza kula tulirudi  kuendelea na kazi za Shamba, jioni tulihesabiwa kisha  tulikula na kurudishwa kwenye vyumba kwa ajili ya kulala,  kila chumba kilikuwa na wafungwa 8 ambao tulikuwa tukilala  humo. Bahati nzuri chumba chetu hakikuwa na muhuni hata  mmoja, kumbe taarifa ya Mimi kuwepo Gerezani alikuwa nayo  Sarafina, kama Isabela alivyoniambia kuwa Sarafina alikuwa na  kundi la ubabe pale gerezani. 

Usiku tukiwa tumelala tena fofofo maana kazi za pale Gerezani  zilikuwa ngumu mno hivyo Mtu akilala anakuwa kama amekufa.  Nilishtuka geti la chumba chetu lilikuwa likifunguliwa alafu  tochi ilinimulika Usoni, aliingia mdada mmoja ambaye hakuwa  Askari, aliniambia nimfuate. 

Niliamka kisha nilimfuata, niliingizwa kwenye chumba kimoja  kisha kilifungwa, kilikuwa ni chumba chenye giza mno kiasi  kwamba sikuweza kuona chochote kile 

“Nipo wapi?” Nilijiulza kwa sauti ya chini huku nikipapasia 

“Dada yangu kwanini umenileta huku?” Niliuliza, sauti  ilijirudia tu katika kile chumba, sikujibiwa. Mara taa  iliwashwa, nilikutana na macho ya Sarafina 

“Sarafina” Niliita kwa mshituko maana sikutegemea kama  ningekutana naye katika Mazingira yale, kwa vyovyote vile  aliyenileta alijuwa nini anafanya. 

“Karibu Jojo, Mungu wangu alinisikia kilio changu, hatimaye  nimekutana na wewe” Alisema Sarafina akipiga hatua ndogo  ndogo kusogea nilipokuwa nimesimama. 

“Sarafina sikufanya chochote kibaya dhidi yako, sikutegemea  kama ingekuwa vile. Nisamehe tafadhali, tuyamalize”

“Pengine umesahau Jojo, nilikuokoa yule Mwanaume asikubake,  nilimpiga mbele yako kukuonesha kuwa sikupenda alichokifanya.  Wema wangu kwako ndiyo uliozaa matunda yale, sikuwa na pa  kwenda, nilikuacha pale lakini nilisema ipo siku  nitakuonesha. Siwezi kuwa na haraka na wewe sababu upo kwenye  himaya yangu” Alisema Sarafina akiwa anazunguka huku na kule 

“Sarafina tafadhali sana, nisamehe hujui ni mambo mangapi  magumu nimekutana nayo, nimeishi Maisha magumu sana, hukumu  niliyopewa ni adhabu tosha kwangu…” Nilisema kwa uchungu  sana 

“Lakini sio adhabu yangu, yangu itakuwa zaidi ya hiyo hukumu  uliyopewa, wema wangu ukageuka kuwa udhalilishaji, siri ya  ugonjwa wangu iliwekwa wazi, namjuwa Sana Shonaa kuliko  unavyomjuwa wewe ni lazima alinianika kwenye kila jambo”  Alisema Sarafina akiwa amefika karibu zaidi na Mimi 

Nilipiga goti nikamuomba Sarafina asinifanye chochote kibaya  maana kama aliweza kupata funguo ya chumba chetu maana yake  alikuwa na uwezo hata wa kuniuwa na hakuna ambaye angesema  chochote kile. 

“Magret” Aliita, yule Mdada aliyekuja kunichukua alikuja  ndani 

“Mrudishe, nitamalizana naye” Alisema Sarafina kisha  nilirudishwa kwenye chumba chetu cha gereza. 

Nilikuta Watu wa Chumba chetu wakiwa macho ni dhahiri kuwa  walisikia Wakati Mimi ninaondolewa pale gerezani. Mtu wa  kwanza kuniuliza alikuwa ni Isabela 

“Ulienda wapi Jojo?” Nilivuta pumzi nikamueleza nilipokuwa 

“Itabidi uwe makini sana Maana Sarafina ni Mtu mkorofi mno  hapa gerezani, ipo namna anaweza akafanya maisha yako yakawa  si kitu hapa gerezani” Alisema Isabela akadakia Mwanamke  mwingine akasema 

“Wakati anafika aliwahi kupigana na askari Watatu na  akawadhibiti vizuri sana, tokea siku hiyo amekuwa na urafiki  na Mkuu wa Gereza hili, mara kadhaa amekuwa akitoka na kurudi  haijajulikana wana ajenda gani, hivyo unapaswa kuwa makini  sana Jojo vinginevyo hata sisi tutakuwa hatarini. Ana kundi  lake hapa na linatambulika na Mkuu wa Gereza, wao hawafanyi  kazi yoyote ile zaidi ya kutoka na kurudi” Yalikuwa ndiyo  maelezo yake kuhusu Sarafina, hilo la kupiga Askari  halikunitisha sana maana nilikumbuka aliwahi kumpiga yule  Mwanaume aliyetaka kunibaka.

“Ina maana anaishi humu gerezani kwa uhuru bila kubugudhiwa  na chochote?” 

“Ndiyo! Ni Mtu hatari sana, anaendesha biashara ya kuuza  Bangi na Unga hapa Gerezani, anachumba maalumu cha kulala na  anapewa mahitaji yote ayatakayo” alielezea huyo Mwanamke  mwingine, kiukweli nilijawa na woga sana, nilipitia kote ila  niliona dhahiri Maisha yangu yataishia ndani ya gereza,  nilimuuliza Isabela 

“Ndugu zako wanakuja kukuona?” 

“Hapana nahisi hawajaambiwa chochote na Mume wangu”  Alinijibu, lengo langu lilikuwa kama wanafika niwape maelezo  waende nyumbani kwetu Tabora wakauze kibanda chetu ili waje  kunikomboa pale gerezani, nilichoka sana. 

Wao walilala maana ulikuwa ni usiku mwingi, ila Mimi nilikuwa  macho hadi Alfajiri ambapo tuliamshwa kwa ajili ya kazi, siku  zote nilikuwa napewa kazi nafanya na wenzangu ila siku hiyo  ilikuwa tofauti sana, kwanza nilipelekwa kwenye kuvunja mawe  adhabu ambayo hupewa Wafungwa waliofungwa kwa kosa la  Mauwaji. Pili niliambiwa natakiwa kuwa peke yangu, basi  nilipelekwa huko na Askari mmoja, kulikuwa ni eneo lenye Mawe  yaliyochimbuliwa, nilipewa nyundo kubwa nilianza kazi ya  kuvunja mawe, Mchana ulipoingia nilisikia kengele kwa ajili  ya kwenda kupata Chakula lakini yule askari alinizuia  akaniambia siruhusiwi kula kwa siku hiyo. 

Nilikubaliana na hali halisi, nilifanya kazi kwa bidii sana  bila hata kutegea sababu nilijuwa yalikuwa ni maelekezo ya  Sarafina, Jioni nilipelekwa kulala kwenye chumba cha peke  yangu, chumba hakikuwa na taa wala sehemu ya kulalia,  palikuwa pamemwagwa maji kwenye sakafu. Basi niliketi, japo  nililoa lakini ilinilazimu kwani nisingeliweza kusimama kwa  muda wote 

Kweli aliyesema Maisha ni popote, msemo ulikuwa na maana  kubwa sana, licha ya kutokula chochote lakini nililala kwenye  sakafu yenye maji, niliuchapa Usingizi kutokana na zile kazi  ngumu. Usingizi ulinipitiliza hadi asubuhi sana, jua lilikuwa  limeshatoka nilipata kuushuhudia mwanga wake kupitia  kidirisha kidogo ambacho kilikuwa juu pale kwenye kile  chumba, mazingira ya chumba yalikuwa maalum, kilionekana kuwa  ni chumba spesho. 

Tofauti na vyumba vingine, chumba hicho kilikuwa na geti  lisiloonyesha nje, kilikuwa na michoro ukutani na harufu kali  sana ya uchafu, wadudu walikuwa wakitembea kwenye ukuta, nilijiinua na kuketi pembeni nikiwa nimeegemea ukuta,  nilijiuliza kwanini sikuamshwa siku hiyo, masaa yalisogea  njaa ilizidi kuniuma, kiu ilizidi kunishika maana tokea  nilivyokula na kunywa maji siku iliyopita sikula wala kunywa  maji tena. 

Siku iliisha bila geti langu kufunguliwa, giza liliingia, Kiu  ilinibana sana na njaa ilizidi kuniuma, niligonga nifunguliwe  lakini hakuna aliyefungua mlango na hakukuwa na dalili  iliyoonesha kuwa kulikuwa na Watu karibu. Siku hiyo iliisha,  Usiku uliingia, nilijaribu kuutafuta Usingizi lakini  sikuupata, nilikaa macho hadi kulipopambazuka, mwili ulikuwa  na alama za kung’atwa na Wadudu na mbu. 

“Mnifungulie nitakufa jamani” Nilisema kwa sauti isiyo na  nguvu kabisa, siku mbili bila kula tena nikitoka kufanya kazi  haikuwa rahisi kwangu kukabiliana na hali ile, haikusikika  sauti yoyote upande ule, niligumia kwa muda mrefu hadi  nilikata tamaa ya Mtu kunisikia, nilirudi nikakaa chini  nikaegemea ukuta nikiwa nimechoka sana 

Baadaye kidogo nilisikia sauti ya geti langu kufunguliwa,  niliamka haraka, ilitupwa bakuli moja kisha palifungwa,  nilikimbilia kwanza getini kisha nilisema 

“Mnitoe humu nitakufa, kwanini mnakuwa wakatili kiasi hicho,  mnanitendea hivi kama nimeuwa?” Nilisema kwa sauti ya juu,  sauti ya Mtu kutembea ilikoma kisha ukimya ulisikika,  niligeuza macho yangu kwenye ile bakuli 

Nilisogea kuangalia kulikuwa kuna nini, niliifungua kisha  niliona Mchuzi mwepesi sana na kipande kidogo cha Muhogo  kilicho pikwa. Nililishika lile bakuri huku moyo ukiniuma  sana, yaani kukaa siku mbili bila kula alafu niletewe mchuzi  na kipande kidogo cha muhogo? Nilitamani nimwage tu maana  sikuona kama nilistahili, ila nilipokumbuka kuwa nipo Jela  nilifakamia mchuzi huo kisha nilikula muhogo. 

Angalau kidogo nilikuwa nimekata kiu lakini njaa ilibakia  pale pale. Sekunde chache nilikuwa nimemaliza kula kisha  nilikaa chini, Muda ulizidi kwenda, siku zilienda nikiwa  ndani ya chumba hicho cha Mateso. 

Macho yangu yakazoea giza, Uchafu ukatawala mwili wangu,  nilikojoa humo humo na kujisaidia haja kubwa humo humo, njaa  iliponizidi nilikula kinyesi changu sababu nilikuwa  nikiletewa supu kila baada ya siku mbili, nilianza kukonda na  kudhohofika, sura yangu ilinyauka kutokana na kukosa chakula.

Usiku mmoja nilikuja kuchukuliwa nikiwa hoi bin taabani, hali  yangu ilikuwa mbaya kupita maelezo, nilikuwa nimelegea sana  hata kuongea siwezi, nilichokuwa nasubiria ni ujio wa Malaika  mtoa roho pekee aje anichukue maana sikuwa na tumaini tena la  kuendelea kuishi. 

Nilipelekwa kwenye chumba kimoja ambacho kilikuwa na taa,  mbele yangu kulikuwa na meza iliyokuwa na chakula cha  kutosha, niliambiwa nile nishibe. Taratibu nilianza kula  chakula kile ambacho kilikuwa cha moto hivyo kilinipa nguvu  sana. 

Angalau nilipata unafuu sana, mwili uliingia nguvu hadi  nilipata uwezo wa kumuuliza Mdada aliyekuja kunichukua kule  kwenye chumna chenye mateso 

“Kwanini mlitaka kuniuwa?” Nilimuuliza kwa sauti ya uchovu  kiasi 

“Majibu utayapata muda siyo mrefu” Alisema, niliendelea kula  huku nikisubiria hayo majibu. Punde aliingia Sarafina 

“Jojo” Alisema kisha aliketi kwenye kiti, alichukua chakula  kidogo akala kabla ya kusema chochote kile, nilimtazama sana  Sarafina 

“Kwanini ulitaka kuniuwa Sarafina, ni kosa gani ambalo  halisameheki hadi kufikia hatua ya kutaka kuondoa uhai  wangu?” Nilimuuliza Sarafina huku chozi likianza  kunibubujika. 

“Kiukweli sikutegemea baada ya muda huo uliokaa kule ungetoka  ukiwa hai Jojo, hakika wewe ni miongoni mwa wachache wenye  roho ngumu sana, wengi walifia mle ila wewe umetoka, Hongera”  Alinipongeza Sarafina, ila niliona kama ananikaidisha tu 

“Unanipongeza kwa lipi ikiwa ulitaka nife? Wewe ni mnyama  Sarafina…hadithi ya Maisha yangu imebadilika ghafla sana”  Nilisema huku nikiwa ninafuta chozi langu 

“Sarafina, kama kifo changu kitakuwa furaha kwako usisite  kunimaliza ili nipumzike hii mitihani mizito ambayo imekuwa  ikiniandama baada ya Mama yangu kufa, sitaki kuingia kwenye  mtihani mwingine, imetosha, nimeteseka sana Mimi Sarafina,  ona nimedhohofika sina hata nguvu” Nilisema kwa uchungu sana  huku nikiwa ninabubujikwa mchozi. 

Sarafina alifuta chozi lake lililokuwa linaanza kumtoka,  stori yangu ilimfanya alie kidogo japo baadaye alijifanya  haijamuumiza

“Sikia Jojo, ukiishi kwa kuhitaji huruma ya wengine utaishia  kuishi Maisha ya hovyo sana. Lengo la kukutoa mle ni kutaka  kufanya na wewe baadhi ya Majukumu kisha utaachiliwa huru”  Nilishtuka sana kusikia kuna majukumu nataka kupewa, nilifuta  chozi kisha nilimuuliza 

“Majukumu?” 

“Ndiyo! Kwasasa angalia Afya yako kwa mwezi mzima kisha  utakapokuwa sawa nitakuchukua tena” Hakunipa hata nafasi ya  kumuuliza chochote kile, aliondoka zake. Yule Mdada mwingine  alisogea akaniambia 

“Unapaswa kwenda Hospitali” Alininyanyua kisha alinitoa pale,  Ulikuwa ni usiku mwingi sana, nilipelekwa Kwenye hospitali ya  pale pale Magereza.  

Nini Kitaendeea?  Nione COMMENT NYINGI LEO au MSHAICHOKA TUACHE KUIPOST? 

Usikose SEHEMU YA TISA ya MUNGU AMENISAHAU bila kuacha comments hapo chini

Mpe Nguvu ADMIN Kwa ajili ya bando Kwa kumtumia Chochote aendelee kupost RIWAYA Mpya Hapa Kijiweni

Lipa Namba: 57900454
Jina: LIPA KIJIWENI TIPS
Mtandao: VODACOM  

SOMA RIWAYA YA KOTI JEUSI KWA KUBONYEZA HAPA 

SOMA RIWAYA YA FUNGATE KWA KUBONYEZA HAPA 

SOMA RIWAYA YA NILIPANGA NYUMBA MOJA NA MAJINI 

SOMA RIWAYA YA GORYANAH HAPA 

SOMA KISASI CHANGU HAPA  

SOMA RIWAYA YA MSALA HAPA

JIUNGE NIPO KIJIWENI Kwa Kubonyeza Hapa

 

 Mungu Amenisahau xx  Mungu Amenisahau xx  Mungu Amenisahau xx  Mungu Amenisahau xx  Mungu Amenisahau xx  Mungu Amenisahau xx  Mungu Amenisahau xx  Mungu Amenisahau xx  Mungu Amenisahau xx 

 

7 Comments

Leave A Reply


Exit mobile version