Chozi lilikuwa likinimwagika, nilikuwa nikimuaga Mama yangu  kwa mara ya Mwisho Mkoani Tabora. 

“Mama! Umeniacha Mama yangu, nimebaki mwenyewe” Nilisema kwa  sauti iliyowaumiza wengi, alikuja Mama mmoja alinishika  vizuri akaniambia 

“Jojo usilie sana utakufuru, Muache Mama yako apumzike kwa  Amani” Alisema kwa sauti iliyojaa maumivu pia sababu alikuwa  ni jirani yetu. Hadi Mama anafariki hakuwahi kunionesha  mahali ambapo ndugu zake walikuwa wakiishi hata hivyo alikuwa  hapendi kuzungumza kuhusu ukoo wao. 

Mama yangu alizikwa katika Ardhi ya Tabora, ukawa mwisho  wake, nilikumbuka maneno yake kuwa Kila siku Binadamu  wanakufa, walio hai wanakuwa kwenye hiyo foleni, kila mmoja  ataenda huko ambako Wafu huenda na hawarudi, alisema 

“Jojo ipo siku tutatengana hatuta onana tena, nikitangulia  ishi vizuri na Watu, niombee Mama yako” Alisema siku moja  akiwa anaumwa, japo sikupenda sana kusikiliza kauli za Mama  ambazo zilikuwa zikiniumiza. Hatimaye maneno yake yalitimia,  aliniacha nikiwa bado namuhitaji sana. 

Huzuni ilinijaa, siku mbili zilipita. Nilimkumbuka Mama  yangu, alikuwa ni ndugu yangu pekee katika hii Dunia, baada  ya Mama walifuata majirani zangu sababu hata Baba yangu  nilikuwa simjui. 

“Pole Jojo, Mungu atakurudishia tabasamu lako siku moja”  Alisema jirani mmoja ambaye alikuwa akichuma mboga katika  Bustani yake ndogo iliyo kando ya nyumba yetu iliyo Bomoka  upande mmoja. Nilimtazama Mama Rafia, niliangalia nyumba yetu  kisha nilitabasamu 

“Ndio, Mungu hawezi kukusahau Jojo, amekupa kila kitu” Mameno  ya Mama Rafia yalizidi kunipa tabasamu kidogo, nilikuwa  nimejikunyata nilimfuata alipokuwa anachuma mboga za majani

“Chukua kidogo ikusaidie leo” Alisema tena Mama Rafia 

“Nashukuru Mama Rafia” Nilisema, Basi nilichuma kiasi kidogo  cha mboga kisha nilirudi ndani, Maisha hayakuwa mazuri pale  nyumbani, sikuwa na kazi yoyote ile. 

Nilikagua Mkaa haukuwepo, Mafuta wala chumvi vyote  havikuwepo, niliingia chumbani nilipekuwa kwenye begi  nilikuta pesa kama Shilingi elfu tatu na senti zake. Nilienda  kununua Mkaa wa shilingi Elfu moja na mahitaji mengine madogo  kisha Unga robo ili nisogeze Mchana huo. 

Wakati narudi nilikutana na Mama Rafia, alikuwa ni Mama  Mcheshi sana, alikuwa anapenda utani mno. Kila nilipomuona  nilijihisi kupona maumivu yangu 

Nilipika chakula changu vizuri, nilikula, nilipata muda wa  kupumzika na kutafakari nini nifanye. Umri wangu wa miaka 28  haukunitosha kuhisi naweza nikajikwamua, nilishusha pumzi  zangu maana kila nilichokuwa nakifikiria hakikunipa majibu  yenye uhakika, nilijiegesha Kitandani nikiwa natazama matundu  ya paa la bati alafu nilijikuta nikicheka maana ilikuwa kama  chujio la tui la nazi vile. 

Mara nilisikia sauti ya Mtu akiniita huko Nje, ilikuwa ni  sauti ya Mkaka aliyeitwa Msonjo 

“Abee! Nakuja” Nilisema, nilijikurupusha kisha nilitoka  ndani, alikuwa Mkaka fulani hivi mcheshi na alikuwa maarufu  sana mtaani kwetu, alikuwa akiyajuwa fika Maisha yetu. 

“Muarabuuu wa Tabora” Alisema Msonjo kwa utani, nilikuwa na  asili ya uarabu 

“Abee!” Niliitika nikiwa nafunga khanga yangu vizuri “Pole kwa kifo cha Mama yako Jojo” Alisema Msonjo 

“Nimeshapoa ndiyo Maisha, wacha apumzike ameumwa sana”  Nilisema kisha nilifuta chozi 

“Sasa Jojo, kwa jinsi ulivyo hupaswi kuishi Tabora, unatakiwa  kwenda kuishi Dar sababu huko ndio kuna Maisha mazuri ya  kuishi wewe na rangi yako” Alisema Msonjo, nilijiweka makini  kumsikiliza 

“Una maanisha nini?” Nilimuuliza

“Kuna Bosi anatafuta wafanyakazi yupo Dar nikasema siwezi  kukuacha ndugu yangu, ni bora ukatafute Maisha huko Mjini”  Maneno yake yalinifanya nikumbuke nilichokuwa nakiwaza nikiwa  ndani. 

“Kazi gani hiyo?” 

“Mmh! Yeye ni tajiri tu sina hakika sana ila anahitaji  Wafanyakazi, utalipwa vizuri Jojo hebu angalia maisha yako,  Mama hayupo tena unafikiri utaishi Maisha ya dhiki hadi lini”  Alisema tena Msonjo 

“Nimekuelewa Msonjo ila nahitaji muda kupona kwanza kutokana  na maumivu ya kumpoteza Mama kisha nikiwa tayari nitakuambia”  Nilisema 

“Mh! Haya…Maamuzi ni yako wewe! Ukiwa tayari utasema, alafu  upo na nani?” 

“Hahaah! Msonjo hebu niache sitaki kucheka” Nilisema kisha  niliingia ndani 

“Jojo mimi sina Mke kwahiyo kama ukiona vipi wewe niambie tu”  Alisema kwa utani akiwa anaondoka, nilishamzoea kwa utani  wake. 

Nilipofika chumbani nilikaa kitandani nikatafakari  alichokisema Msonjo, ni kweli sikuwa na kazi na sikuwa na  tumaini lolote Tabora, kuhusu uzuri ni kweli nilikuwa mzuri  mno ila sasa uzuri ndio uwe kigezo cha Mimi kuishi Maisha  mazuri na kupata kazi? Nilicheka kidogo. 

Siku zilienda, Maisha yalizidi kunichapa Tabora, nililala  njaa, nilikula mlo usio na shibe, Mwezi mzima ulikatika.  Nilimtafuta Msonjo kuhusu masuala ya kazi huko Dar.  Alinieleza kazi yenyewe hadi mwili ulichoka yaani, ilikuwa ni  kazi ya kuwa Baamedi 

“Hiyo siwezi Msonjo nina shida lakini hiyo kazi hapana”  Nilimwambia Msonjo huku nikiwa ninakaa juu ya Tofali 

“Sasa kipi bora ulale njaa hapa Tabora au ukale Maisha Dar?  Wewe kule unaenda kwa mipango na malengo yako, hauendi kuishi  Maisha ya Kibaamedi” Alisema Msonjo 

“Mh lakini Msonjo hakuna kazi nyingine?” 

“Jojo, Mchagua jembe siyo Mkulima” Alisema Msonjo akawa  anaondoka, nilifikiria nikaona ni bora nikubali

“Msonjo” nilimuita, alisimama kisha alisogea nilipo “Nakusikiliza” Alisema 

“Nipo tayari” nilisema 

“Hayo ndiyo Maneno niliyotaka kusikia kutoka kwako Jojo, hapo  umenifurahisha ngoja nimpigie huyo Bosi” Alimpigia huyo Bosi,  ilitumwa nauli muda huo huo, nilipaswa kujiandaa ili kesho  yake nianze safari kutoka Tabora kwenda Dar 

Nilirudi nyumbani, nilimpa taarifa Mama Rafia, alinitafutia  Mtu wa kuishi pale kwa kipindi chote ambacho nitakuwa Dar,  Nilijiandaa, Usiku Msonjo alinieletea Tiketi ya Basi kisha  alinipa kiasi cha pesa kwa ajili ya matumizi nikiwa safarini,  moyo ulikuwa ukinienda mbio, sikuwahi kwenda Dar ilikuwa  ndiyo mara yangu ya kwanza. 

Alinipa namba ya huyo Bosi wa kazi, alikuwa ni Mwanaume, kwa  jinsi alivyonielekeza Msonjo Bosi alikuwa ni Mmiliki wa  migodi huko kusini mwa Tanzania katika Mkoa wa Lindi. 

Alfajiri safari ya kuelekea Dar ilianza. Ilikuwa ni safari  iliyojaa mawazo, nitaishi vipi, hiyo kazi sijui kama  nitaiweza. Tulipofika Dar, nilikuja kupokelewa na Mdada mmoja  ambaye alijitambulisha kwangu kama Shonaa, alikuwa na umri  sawa na Mimi, ulikuwa ni usiku. 

Tulienda moja kwa moja anapoishi Shonaa akaniambia kesho yake  atanipeleka kwa huyo Bosi, nilikuwa nimechoka hivyo sikuwa na  maswali mengi zaidi ya kuhitaji Kupumzika tu, kweli  nilipumzika hadi asubuhi kulivyo pambazuka. Shonaa aliamka  mapema sana, alikuwa amepangisha chumba kimoja na sebule,  nilienda hadi sebleni nilimsalimia 

“Mambo Dada?” Aliacha alichokuwa anakifanya kisha alitabasamu  akanijibu 

“Poa tu umeamka salama?” Aliniuliza 

“Ndiyo nipo sawa! Umedamka hivyo?” Nilimuuliza 

“Si unajuwa tena Maisha ya Mjini ndugu yangu, ukiendekeza  Usingizi utakufa masikini” Alisema kisha tulicheka, niliona  nimepata Mtu wa kuzungumza naye na kumuuliza maswali yangu 

“Jana ulisema utanipeleka kwa Bosi asubuhi hii” “Usijali, subiria nimalize kupasi nguo zangu” Alijibu Shonaa 

Nini Kitaendelea? Usikose SEHEMU YA PILI ya MUNGU AMENISAHAU bila kuacha comments hapo chini

Mpe Nguvu ADMIN Kwa ajili ya bando Kwa kumtumia Chochote aendelee kupost RIWAYA Mpya Hapa Kijiweni

Lipa Namba: 57900454
Jina: LIPA KIJIWENI TIPS
Mtandao: VODACOM  

SOMA RIWAYA YA KOTI JEUSI KWA KUBONYEZA HAPA 

SOMA RIWAYA YA FUNGATE KWA KUBONYEZA HAPA 

SOMA RIWAYA YA NILIPANGA NYUMBA MOJA NA MAJINI 

SOMA RIWAYA YA GORYANAH HAPA 

SOMA KISASI CHANGU HAPA  

SOMA RIWAYA YA MSALA HAPA

JIUNGE NIPO KIJIWENI Kwa Kubonyeza Hapa

 

 Mungu Amenisahau xx  Mungu Amenisahau xx  Mungu Amenisahau xx  Mungu Amenisahau xx  Mungu Amenisahau xx

3 Comments

Leave A Reply


Exit mobile version