IlipoishiaTulirudi kule kwenye ghorofa la Tancot House ambapo ndiyo  tulilala usiku uliopita, Nilijaribu nguo zote ikapatikana  moja tu ambayo ilionekana kuwa nzuri sana na yenye  kunipendeza zaidi 

“Wow!! Hii ndiyo yenyewe Jojo, nina uhakika hawezi kuchomoka,  sasa unapaswa kuwa makini sana sababu ni lazima akuchukue  kama kimada wa kulala naye Usiku, ndipo utakapo iba hayo  madini, utachunguza kujuwa yalipo, baada ya kufanikisha  zoezi, utafungua dirisha sababu chumba chake kipo mashariki  mwa jengo hilo, utayatupa madini kwa kutumia kifaa ambacho  kitakuwa kimehifadhi kisha utayachukua baada ya kushuka, kuwa  makini sana vinginevyo unaweza ishia huko Hotelini, pia ni  lazima ukamilishe zoezi ili uwe huru” alinieleza Sarafina. Endelea

SEHEMU YA KUMI

“Sawa” niliitikia ili kuondoa ngoma juani sababu nilishajua  utakuwa ni mtihani mzito sana kufanya hivyo. 

Basi tulienda kula na tuliporudi tulilala, asubuhi alinipa  kadi maalum ya kuingilia Hotelini kwa ajili ya Hafla hiyo. 

“Kila la kheri Jojo” Alisema Sarafina, sikuwa na maneno mengi  ya kuzungumza sababu nilishapewa maelekezo yote na  nikayaelewa 

“Upande ambao utayatupa madini kuna bustani ya mauwa hivyo  kuwa makini sana uyatupe mahali ambapo utaweza kuyaokota  kirahisi, utayatupa sababu hutoweza kupita nayo mlangoni  walinzi wake watakukagua” 

“Ok sawa!” 

Japo niliikubali kazi ile ili niwe huru ila nilikuona cha  mtema kuni maana jukumu lilikuwa zito sana, niliendelea  kupiganisha akili yangu, nilifikiria jambo kwa pale kwenye  hoteli kuna kamera hivyo itakuwa rahisi mimi kuonekana,  niliwaza nifanye nini maana kama nitaonekama nitatafutwa na  kukamatwa kwa kosa ambalo litawafaidisha wengine, wakati naendelea kutafakari niliona picha ya paspot pembeni, ilikuwa  ni picha ya Sarafina. Niliivuta kwa mguu bila Sarafina  kushtuka kisha niliiweka kwenye mkoba wangu huku nikijuwa  ndani ya akili yangu nitafanya nini ili kuwa salama. 

Jioni mishale ya saa 12 Jioni, Sarafina alinieleza kuwa ndiyo  muda wa kuelekea Hotelini kwa ajili ya kuiba hayo madini,  nilijiangalia kwenye kioo nilijikuta nikitabasamu licha ya  hatari iliyo mbele yangu, uzuri wangu, nilifanana sana na  Marehemu Mama yangu. 

Tulitoka, nje alinipakiza kwenye gari moja ya kifahari sana  nyeusi. 

“Mimi siwezi kwenda huko sababu kadi ni moja tu ambayo  nimekupa wewe, ifanye kazi uwe huru Jojo, ukitugeuka basi  juwa msala huu utakuwa wako peke yako” alinisistiza Sarafina 

“Nimekuelewa Sarafina” Basi, nilifunga mlango kisha safari  fupi sana ya kuelekea Hotelini ilianza, ilituchukua dakika  nne kufika Hotelini, nilishuka kwenye gari baada ya  kukaguliwa kama Mwana Malikia vile kumbe nilikuwa mwizi tu. 

Mlango Mkuu wa Kuingilia nilitakiwa kuonesha ile kadi,  nilifanya hivyo kisha niliruhusiwa kuelekea ndani ambako  kulikuwa na hiyo Afla iliyo hudhuriwa na viongozi kadhaa na  wafanya biashara wakubwa wa Tanzania. Sikuwahi kuingia sehemu  nzuri na ya kifahari kama ile katika Maisha yangu, ilinifanya  niwe muoga kiasi chake japo hakuna aliyeshtuka. 

Hadhi niliyovishwa ilikuwa kubwa sana, mavazi niliyovaa  yaliakisi ukubwa wangu na hadhi yangu, nilionekana ni mwenye  Maisha mazuri, mzuri na mrembo kuliko Wanawake wote  waliohudhuria kwenye Afla hiyo. 

Niliketi kwenye meza ambayo haikuwa na Mtu yeyote yule huku  Watu wakiwa bize na mazungumzo ya Hapa na pale, nilimuona  huyo Bilionea wa Madini akiwa ameketi anazungumza. Mahali  nilipochagua kuketi palikuwa na urahisi wa yeye kuniona pindi  atakapogeuza shingo yake, Wanaume wengi walikuwa bize  kunitazama nami nikajifanya bize na Afla hiyo ambayo ilikuwa  ikiendelea. 

Walikuja Wanaume kadhaa kuniuliza maswali fulani ambayo  nilijuwa lengo lilikuwa ni kunihitaji kimapenzi ila  niliwakatalia hata kuketi karibu na Mimi sababu kufanya hivyo  kungemfanya Bilionea pindi atakaponiona asiwe na wazo la  kunihitaji.

Bilionea huyo alikuwa Kijana mtanashati, kichwa changu  kilikuwa na maelekezo yote kutoka kwa Sarafina na Mkuu wa  Magereza juu ya kuiba hayo Madini yenye thamani kubwa sana  japo nilijuwa haitokuwa rahisi kufanya hivyo, nililetewa  Vinywaji na chakula nikawa ninakula ila akili na macho yangu  yakiwa kwa huyo Bilionea Kijana. 

Nililetewa vimemo kadhaa vya Wanaume vyenye namba, nilivisoma  na kuvitupa sababu hakuna hata kimoja kilichotoka kwa Mlengwa  wangu, niliendelea kusubiria kwa masaa kadhaa huku akionekana  bize sana kucheka, Moyo wangu ulihitaji uhuru hivyo niliona  

kazi hiyo ingenifanya niwe huru na kurudi Tabora. 

Nilizuga kufanya vitu kadhaa ikiwemo kwenda chooni ilimradi  anione lakini haikuwezekana hadi pale dakika za mwisho ambapo  aligeuka akaniona kidogo alafu akarudisha macho kwa aliyekuwa  akiongea naye, nilihisi labda hakuuona uzuri wangu, nilianza  kukata tamaa kumbe alikuwa ameniona ila alikuwa akitafuta  engo nzuri ya kunitazama, nikiwa nimeshakata tamaa nataka  kunyanyuka. Niliona nimtazame kwa mara ya mwisho huku  nikijiambia 

“Geuka unitazame basi” Nilisema kwa hisia na kwa kumaanisha  kabisa, ile namtazama nilikutana naye ana kwa ana tena  akionekana alikuwa akinitazama kwa muda mrefu, basi  nilijitingisha kidogo alafu nikatazama chakula changu, nikawa  na uhakika kuwa ameniona na alikuwa akiniangalia kwa  kunitamani. 

Basi, Dakika chache alikuja mlinzi wake akaniambia 

“Bosi anahitaji kuzungumza na wewe” Alisema, ili nisionekane  mrahisi nilimwambia 

“Mwambie akome sikuja hapa kwa ajili ya Mtu yeyote yule”  Nilisema, yule Mlinzi aliganda kidogo kisha akasema 

“Dada usipoteze bahati yako, Bosi wangu ni Bilionea Mkubwa wa  Madini, amekuwa akikuangalia kwa muda mrefu sana” Alisema  tena, sasa niliona nikubali maana kujizugisha wakati  kilichonileta kilikuwa ni hicho niliona ni Ujinga 

“Yupo wapi?” niliuliza kanakwamba nilikuwa simjui 

“Yule Pale kwenye ile Meza” Alisema kisha nilipeleka macho  huko, niligongana naye macho akiwa ananikodolea sana, moyoni  nikasema 

“Umenasa Bosi”

Basi, nilinyanyuka taratibu nikaelekea kwenye hiyo Meza,  alitoa walinzi wake akaniambia 

“Kuwa huru, karibu Naitwa Bilionea Vitalis Kyando” Alisema  kisha alinipatia Mkono wake, nilimpa wangu tukashikana 

“Naitwa….Juliana” Nilifikiria kusema jina langu halisia  nikaona inaweza niletea shida baadaye, niliamuwa kumdanganya. 

“Ooh Juliana! Nimefurahi kukufahamu, hakika Mungu alikuumba  kwa utulivu sana, muda mrefu nimekuwa nikikutazama alafu  akili yangu ilikosa utulivu, unastahili kila kilicho bora  Juliana, Niambie unataka nini” Aliniuliza Swali kwa ujasiri  Mkubwa sana, niliwaza vingi kwa haraka sana, nikakumbuka  kauli ya Msonjo kuwa Mimi ni mzuri sana ninapaswa kuishi Dar,  Nilifikiria nifanyaje na nipo kwenye mpango wa kumuibia ili  niwe huru 

“Asante! kukufahamu pekee ni kitu kinachonitosha” Nilisema  japo nafsi ilikuwa ikinisuta na kuniita Zuzu wa Mwisho 

“Juliana Usiogope kama unahitaji Biashara, Nyumba, gari zuri  la kutembelea niambie tu kuwa huru labda hujajuwa unaongea na  Mtu gani….Hebu nifuate” Alisema huyo Bilionea, alinyanyuka  kisha nami nilinyanyuka nikajiuliza alikuwa anataka  kunionesha kitu gani, Basi nilimfuata huku walinzi wake  wakija kwa nyuma. 

Tulipanda Lifti hadi ghorofa ya nne ambapo ndipo alipokuwa  amechukua chumba. 

“Kama walinzi wangu wanakufanya usiwe huru Juliana niambie  sawa?” Alisema Bilionea Vitalis Kyando, niliitikia kwa ishara  ya Kichwa tu hata sikusema chochote huku moyo ukianza  kunienda mbio maana hao Walinzi walikuwa kama Saba tena  walioshiba sasa nikawaza endapo nitagundulika naweza kuuwawa  hapo kisha ndoto yangu ya kuwa huru ikazimwa. 

Tulipofika karibu na Chumba chake aliwaambia walinzi wake. 

“Msijali nipo sawa” Aliwaambia kisha Sisi tuliingia Chumbani  kwake, angalau moyo wangu ulichanua kidogo 

“Juliana, pamoja na pesa zangu na umaarufu nilio nao ila  sijawahi kumuona Mwanamke mzuri kama wewe, nikikusifia sana  naona nitakufuru ila Hakika Mungu alikupendelea sana” Alisema  akiwa ananisogelea,, nilishajuwa alichokiwa anakihitaji  kwangu na niliambiwa udhaifu wake upo kwa Wanawake wazuri  weupe

“Unamaanisha nini? na huku umenileta kufanya nini?”  Nilimuuliza Bilionea Kyando 

“Oooh Ok!!” Alisema kama Mtu aliyesahau kitu, alielekea  kwenye kabati alifungua akatoa kibegi kidogo, kisha alikuja  nacho karibu yangu alikifungua akatoa madini ambayo Mkuu wa  Magereza na Sarafina waliniambia, Moyo wangu ukasema 

“Wow!!” 

“Katika Maisha yako umewahi kushika madini Juliana….hebu  yashike” Alinishikisha yakiwa kwenye mfuko maalum, kiukweli  ilikuwa ndiyo mara yangu ya kwanza kushika madini tena mengi  kiasi kile, Nilibakia kinywa wazi huku nikipiga hesabu  nafanya nini ilia nimeweza kuyaona kirahisi hivyo. 

Bilionea aliongea Kama Mtu aliyerukwa na akili kabisa ndiyo  nikaamini udhaifu wa Mtu haujalishi ana nyazifa gani. 

Aliyachukua madini akayarudisha kwenye kabati, kisha alirudi  nilipokuwa nimesimama 

“Ndiyo maana nimekwambia sema unataka nini Juliana, Mwanamke  mzuri kama wewe unastahi kilicho bora, nipo tayari kukupa  kilicho bora na kukutunza hata ukitaka kuishi Kama Mtoto wa  Malkia” Alizidi kusema, Nilimwambia 

“Nahitaji uhuru, hao walinzi wako wananiogopesha sana,  sijawahi kuishi hivi kabisa sina amani” Nilisema huku  nikijuwa jibu lake linanipa ishara ya kufanikiwa au  kutokufanikiwa kwa mpango wangu wa kuina Madini yake 

“Unataka waende wapi na kwanini wakati wapo kwa ajili ya  Ulinzi wangu” Alisema kwa kukaza sauti hadi niliogopa  nikahisi kama amenishtukia hivi 

“Siyo lazima tubishane Mr. Bilionea, kama haiwezekani naomba  niende” Nilisema kwa sauti yenye kujiamini mno 

“Ok Sawa!!” alikubali niondoke, sasa vitu viwili vilinipinga  na kunilaumu. Moyo ulisema Hapana, miguu ikawa tayari  kuondoka pale Chumbani kwake, Ningefanyaje na tayari  nimeshaweka uamuzi basi nilipiga hatua kama tatu fupi  kuuelekea Mlango ghfla akasema 

“Juliana!! wewe ni wa thamani huna haja ya kuondoka” Nikiwa  nimesimama nilifurahi sana ndani ya nafsi yangu, alikuja  mlangoni akafungua kisha akawaambia Walinzi wake 

“Nendeni Chini hadi nitakapowaita”

“Lakini Bosi…”ilisikika sauti ya Mlinzi wake mmoja kisha  Bilionea alimkatisha 

“Mmh!! hakuna cha lakini, nitawapigia simu” Alisema kisha  aliwatazama wakiondoka alafu akafunga mlango. 

“Umefurahi? naamini sasa utakuwa huru kunipa uzuri wako”  Alisema Bilionea huyo ambaye kwenye akili yangu nilimuita  Bilionea Mwendawazimu, anaruhusu vipi Walinzi waondoke kisa  Mwanamke ambaye hata hamjui, niligeuka na kurudi 

Niliketi kitandani, hayo yote nilifundishwa na Sarafina  sababu kazi hizo alikuwa ameshazizoea. 

“Nahitaji kuoga kidogo” Nilisema 

“Oooh Sawa Juliana” Alisema kama kichaa yaani Daah!! kweli  udhaifu hasa kwenye mapenzi ni kitu kibaya sana, 

“Nikimaliza na wewe unapaswa kwenda kuoga” Nilisema, basi  aliachia tabasamu ila hakusema chochote. Nilibadili nguo  nikaenda kuoga Bafuni nikamuacha pale Kitandani. Basi nilioga  kwa kuzuga kama dakika kumi hivi, kisha nilitoka. Nilimkuta  akiwa kitandani, alikuwa ameshabadilisha nguo zake na kuvalia  pensi tu. 

“Nenda kaoge” Nilisema. 

“Tofauti yako na Malaika ni Majukumu tu, wao wanamsaidia  Mungu na wewe upo na Mimi hapa” Alisema Bilionea nikiwa  ninajifuta Maji, niliishia kutabasamu tu. 

“Leo ni siku adhimu sana kwangu Juliana, nina uhakika itakuwa  ni siku ya Kumbukumbu kubwa” Alisema, nilicheka tuu huku  nikivaa chupi yangu, kisha nilijitupa kitandani kama Mzoga 

“Ngoja nioge haraka” Alisema Bilionea Kisha aliingia Bafuni  kuoga, kitendo bila kuchelewa nilivalia gauni langu kisha  nilielekea kwenye Kabati ambapo alihifadhi madini, Mbinu zote  nilifundishwa na Sarafina. 

Nilikagua pale nilipoona aliweka lakini hayakuwepo, hapo  ndipo niliposhtuka kuwa hata yeye alikuwa haniamini, nilianza  kuyatafuta Fasta fasta huku nikimsikia akiwa anaoga huku  akiwa anaimba. 

Nilifanya Haraka mno, nilikagua kabati zima bila mafanikio,  kwa jinsi ambavyo nilikuwa nimevurugua vitu pindi atakapotoka  Bafuni ni lazima nitakamatwa tu, Nilifikiria nikasema ni lazima niondoke hata kama madini sikuyapata, nilichukua ile  picha ya Sarafina kisha nikaitupa chini, ile nataka kutoka  nililiona lile begi likiwa kwenye ubavu wa kabati, haraka  nililichukua. Nikaenda kufunga mlango wa Bafu kwa nje kisha  nikafungua dirisha, nilipoangalia chini niliiyona ile Bustani  kisha niliyatupa yale madini yakiwa ndani ya Mfuko tu sababu  sikutaka kulitumia lile begi lake. 

Wakati naelekea mlangoni nilisikia akiniita nimfungulie,  nilifungua mlango nikatoka ndani Mbio mbio huku nikiwa  nimeziba sura yangu, nilishuka kwa mguu bila lifti, sasa ile  nafika floo ya mwisho niliwaona wale walinzi wakipandisha  juu, nilijificha mahali kisha nilisubiria hadi walipopita  wakiwa wanapiga stori, mmoja wao akiwa anasema 

“Hivi Bosi ana shida gani? hawa wanawake watakuja kumponza  siku moja” Sikutaka kuendelea kuwasililiza badala yake  nilikimbilia nje, mlinzi wa Hoteli aliniuliza vipi mbona Hai  hai? 

“Kuna kitu nimeangusha” Nilimjibu kisha nilizunguka nyuma  nikachukua madini nikayatia kwenye Mkoba wangu. 

“Umekipata?” aliniuliza yule Mlinzi 

“Ndiyo kwaheri” Nilisema nikiwa na haraka sana maana nilijuwa  tu wale walinzi wakifika kule juu kila kitu kitaharibika kama  nitakuwa sijaondoka. 

Kulikuwa na tax pale iliyomleta Mtu, niliitumia kuondoka,  kisha nilienda kushuka kwenye kanisa la Azania Front  nikamlipa pesa yake yule Dereva, sasa wakati nataka kuekea  pale nilipomuacha Sarafina niliona askari, sijui askari hao  walikuwa wakimitafuta mimi au walikuwa kwenye majukumu yao ya  Usiku, ile Hofu nikajikuta naita Bajaji nikamwambia anipeleke  Dar City Sinza. 

ilikuwa ni mishale ya saa 5 Usiku, nilikuwa na hofu maana  mzigo wa madini nilionao ulikuwa na thamani kubwa sana tena  hata haukustahili kupanda Bajaji. Mwendo wa dakika 45  tulifika Sinza 

Nilimlipa pesa kisha nilienda hapo Dar City, nilimuulizia  Shonaa nikaambiwa zamu yake ni asubuh hadi mida ya Jioni  hivyo yupo kwake, niliomba namba maana sikuwa na simu, ile  nataka kutoka si nikakutana na Sarafina akiwa na Mkuu wa  Magereza, nilijificha maana nilijuwa taarifa ya kuibiwa  madini yule Bilionea iliwafikia alafu sikwenda kuwapa.  niliwaza nijitoe ili niwape au nifanye nini, nikakumbuka nilichokifanya kule Hotelini niliweka picha ya Sarafina hivyo  kwa vyovyote Sarafina atatafutwa ili Mimi nipatikane, wao  waliponipita bila kuniona Mimi nilitoka ndani nikakimbilia  kwenye Bajaji nikamwambia dereva nipeleke Mbele 

“Mbele gani?” aliniuliza 

“Twende tu hapo mbele haraka” Nilimsistizia yule dereva, basi  aliondoa Bajaji pale akawa anaelekea mitaa ya kumekucha,  nikamuomba dereva 

“Naomba uipige hii namba” Nilisema 

Aliichukua ikiwa kwneye karatasi akampigia Shonaa, alipokea  nikaongea naye nikamwabia 

“Nipo kwenye matatizo Shonaa, nielekeze Ulipo nije haraka”  Nilisema, Shonaa alimuelekeza dereva wa Bajaji na uzuri  mazingira hayo hayakuwa mageni ila mwanzo nilijichanganya  kujuwa hiyo sehemu inaitwaje ndiyo maana sikurudi nilipopata  matatizo kule Ubungo. 

“Una matatizo gani Dada yangu?” aliniuliza 

“Mazito hata nikikwambia huwezi kunielewa” Nilimwambia yule  dereva ambaye baada ya kumjibu hivyo hakuuliza kitu kingine  tena. 

Tulifika alipokuwa anaishi Shonaa, nilimlipa yule Dereva wa  Bajaji maana nilikuwa na pesa fulani nilizopewa na Sarafina  wakati naenda kufanya kazi ya kuiba Madini. 

Niligonga mlango wa Shonaa kwa kitambo sana bila kuitikiwa,  akaja yule Mama aliyewahi kunidekisha choo kipindi kile 

“Aah kumbe ni wewe, yumo humo ndani si umewahi kuishi hapa  sasa si uingie” Alisema, yaani alikuwa Mshakunaku vibaya mno.  Nilisubiria hadi alipoondoka ndipo niliposukuma mlango, kweli  Mlango ulifunguka. 

Taa zilikuwa zinawaka, pale sebleni hakukuwa na Mtu,  nilifunga mlango kisha nilienda chumbani kwa Shonaa,  niligonga napo sikuitikiwa, nilifungua mlango, nilikutana na  kitu kilichonishtua sana, Shonaa alikuwa amelala kitandani  damu zikiwa zimetapakaa 

“Shonaa! Shonaaa!” Nilimuita, niliona akiwa bado mzima

“Ngoja nikupeleke Hospitali Shonaa umekumbana na nini Mama”  Nilisema nikiwa kwenye heka heka ila Shonaa alinipa ishara ya  kutulia kwanza kisha aliniambia 

“Jojo aliyefanya hivi ni Sarafina, anakutafuta wewe una mzigo  wa Madini. Nenda mbali sana na Jiji hili vinginevyo utauwawa”  Alisema Shonaa kwa shida sana 

“Siwezi kukuacha Shonaa ukiwa katika hali hii ngoja  nikakuache Hospitali” Nilisema huku chozi likinibubujika 

“Hapana huna muda Jojo, ondoka. Nikifa nitakufa nikiwa  nakupambania, Kimbia Jojo” Alisema Shonaa, Mwanga ukamulika  dirishani, nikachungulia nikaona Watu wakija uelekea wa  Chumba cha Shonaa. 

Haraka nilimwambia 

“Naenda Shonaa nakupenda” Niliielekea ilipo swichi ya Taa ya  nje, niliizima kukawa na giza kisha nikatoka haraka nikapitia  mlango wa uwani nikakimbia eneo lile. 

Nilikimbia sana Usiku ule huku nikiwa ninahofia kuhusu  usalama wa Shonaa maana alikuwa akivuja damu nyingi sana. 

Nilichukua pikipiki nikamwmabia dereva anipeleke Ubungo,  nilichotaka sasa kilikuwa ni kurudi Tabora tu. Hali ilikuwa  mbaya sana kwangu ndani ya Jiji la Dar, nilijiingiza kwenye  janga zito sana ambalo lilihatarisha maisha yangu moja kwa  moja, nilijilaumu sana ni bora hata ningekubali kumalizia  kifungo changu kule Gerezani 

Tulipofika Ubungo nilikata tiketi kisha nilienda kulala ndani  stendi karibu na gereji ndogo iliyokuwa ikitengeneza mabasi,  nilijikunyata kama kifaranga cha kuku, nilimuomba Mungu  aliyenisahau anikumbuke ili niweze kuondoka salama kuelekea  kwetu Tabora maana hali ilizidi kuwa mbaya. 

Sikupata Usingizi, madini yalikuwa kwenye mkoba wangu, zaidi  ya Bilioni 20 nilikuwa nimekaa nayo pale bila Mtu yeyote yule  kujuwa kuwa nilikuwa na utajiri Mkubwa sana ambao ulkuwa na  uwezo wa kubadilisha maisha ya Watu wote walio stendi kwa  Usiku ule. 

Baridi lilikuwa kali sana pale Ubungo lakini halikunizuia  kuwa makini, gari niliyokata tiketi nilikuwa nikitazamana  nayo macho. Alfajiri mapema sana nilikurupuka, pembeni  kulikuwa na bomba la Maji, nilifungulia nikapata kuosha uso  wangu ili kuondoa uchafu wa pale nilipokuwa nimekaa.

Macho yangu yalikuwa makali sana kuangalia huku na kule ili  nisije ingia mikononi mwa Watu wanaonitafuta, Picha yangu  ilikuwa imesambazwa kila kona ili nikionekana tu nikamatwe,  Alfajiri hiyo nilienda kwanza kujisaidia kule chooni.  Niliporudi niliona makundi ya Askari, hofu niliyonayo  ilinifanya nisimame sehemu ili kuangalia Askari wale walikuwa  wanafanya nini? Nilipoona wameenda mbali kidogo na nilipokuwa  naenda Mimi nilisogea kwenye gari, muda huo tayari walikuwa  wameruhusu Watu kuingia. 

Sasa wakati naingia humo niliona picha yangu na ya Sarafina  kuwa tunatafutwa atakayetuona atapata Donge nono, niliziba  uso wangu nikashuka kwenye gari, nilirudi pale nilipokuwa  nimekaa usiku kucha. 

Hofu ilinijaa upya, niliona kabisa safari ya Tabora inaweza  kufa tena, nikiwa naendelea kutafakari nilihisi kuguswa  kwenye bega langu. Nilipogeuka nilikutana na Mtu ambaye  alikuwa ana picha yangu, nahisi Mtu huyo alinihisi kuwa ndiye  Mimi ila kutokana na giza alisema 

“Samhani nilikufananisha” Alisema kisha alisonga mbele,  nilitumia mkoba wangu kuficha sura yangu, nilionelea ni bora  nitoweke Ubungo maana kuendelea kuwa Ubungo kungeniletea  Shida kubwa sana, nilisogea geti dogo nikapita nikatokea nje  kabisa, kulikuwa na kigiza fulani hivyo ile hali ilinisaidia  kujificha ili nisionekane. 

Polisi walisambazwa kila kona ya Jiji na maeneo ya nje ya  Jiji kutusaka Mimi na Sarafina, kutokana na lile tangazo  nilijuwa wazi kuwa Sarafina alikuwa hajakamatwa. Madini bado  nilikuwa nayo kwenye pochi langu. Niliona ni bora nitembee  kwa Mguu kuliko kupanda Usafiri maana tayari nilikuwa  natafutwa Nchi nzima na atakayeniona aliahidiwa kupewa zawadi  Nono. 

ilikuwa ni safari ya Jojo na Madini yangu, nilitembea kama  Kichaa nikiifuata barabara ya Morogoro, nilipoona Askari  nilichekupa na kuzama ndani kisha baadaye najitokeza na  kuendelea na safari, kulipo pambazuka nilinunua kofia  nikaivaa angalau ilinisitiri kwa kiasi fulani. 

Nilibakiwa na pesa kidogo sana ambayo hata isingenifikisha  Morogoro ila nilikuwa na mzigo wa madini yenye thamani ya  Bilioni 20 kwenye Mkoba wngu. Kila mara nilifungua na  kuangalia kama madini yalikuwepo, basi nilipojisikia njaa na  kuchoka nilienda sehemu nikanunua chakula ila sikula pale  nilienda kukaa chini ya Mti mmoja nikapata chakula. Maisha  yangu yalipoteza nuru ila kile kiasi cha madini kilinipa nguvu ya kuzidi kusonga mbele, mida ya Jioni nilifika Kibaha  Maili moja miguu ikiwa haitamaniki ilikuwa ikiuma sana. 

“Ooh Mungu nimechoka sasa” Nilisema nikiwa ninakaa kando ya  eneo la Mnada wa nguo, nilikaa hapo hadi giza lilipoingia.  Chupi ilikuwa ikiniumiza kutokana na Uchafu wa kuivaa kutwa  nzima, kwasababu eneo lile lilikuwa giza basi niliondoa ile  chupi pale mnadani, pia kulikuwa na ronya za nguo ambazo  ziliachwa nilitafuta pensi nikavaa pia tisheti niliipata  nikaavaa na wala sikujali nitaonekanaje ila nilichotaka ni  kwenda mbali na Jiji la Dar. 

Sikutaka kupumzika Kibaha niliendelea mbele, Watu  niliopishana nao walikuwa wakiongea kuhusu Mimi kuiba Madini  bila kujuwa waliokuwa wakimzungumzia walikuwa wakipishana  naye. 

Zile nguo nilienda kuzitupa kwenye daraja moja ambalo  lilikuwa linapitisha maji mengi kisha niliendelea na safari  yangu, gari za polisi zilikuwa zikipita kwa wingi kama vile  kulikuwa na msafara wa Rais wa Nchi kumbe ulikuwa ndio msako  wangu na kwavile nilipita barabara ya vumbi nikiwa naitazama  Barabara kuu kwa Mbali niliona jinsi msako ulivyokuwa  ukiendelea. 

Nilipochoka nililala Kwenye kichaka fulani hadi asubuhi kisha  safari iliendelea, kadiri nilivyokuwa natoka nje ya Jiji  ndivyo nilivyoanza kuhisi kuwa tayari nimejikwamua kutoka  kwenye msako ule mkali, Nilichofikiria sasa kilikuwa ni  madini na pesa nitakayoipata. 

Pesa ilikuwa imeniishia kabisa, nilipofika mbele kidogo  niliona sonara ndogo. Nilikaa sehemu nikapekua yale madini  nikatafuta dini dogo sana yaani kakipande fulani tu ambacho  nilihisi kuwa pesa yake isingekuwa kubwa sana, niliingia humo  ili niuze. Nilijitahidi sana kukwepa macho ya Mtu wa Sonara 

Nilimpa lile dini, kwanza alishtuka sana maana lilikuwa ni  dini lenye thamani kubwa tofauti na nilivyofikiria, alilipima  na kugundua kuwa lilikuwa lenyewe siyo feki kisha aliniambia 

“Dada yangu pesa sina, hili nenda kauze Kwa wale wenye Sonara  kubwa kabisa” Alikuwa Kijana mmoja wa Kipemba 

“Linagharimu shilingi ngapi?” Nilimuuliza maana nilikuwa  sijui kuhusu Madini 

“Hili siyo chini ya Milioni 45 ndiyo maana nasema sina hela  ya kukupa” Alijibu yule jamaa, sasa nilifikiria niende huko  anakosema nilihisi nitakamatwa nikamwambia

“Wewe nipe uliyonayo, ukiuza nitakuja kuchukua hela kwako”  Nilisema kama vile mzoefu wa hiyo Biashara. 

“Alivyoskia hivyo alihangaika akafungua droo akatoa milioni  mbili akaniambia 

“Ipo hii ila nakuhakikishia hadi kufikia jioni litakuwa  limeuzika, tena nitaenda Mjini kuliuza” Alisema. 

Sikumjibu nilichukua zile pesa nikazitia kwenye Mkoba bila  hata kuhesabu 

“Ungezihesabu kwanza Dada yangu” 

“hata Usijali nakuamini” Nilisema kisha niliondoka pale,  Kumbe nyuma yule Dogo alipiga simu sehemu ambapo angeuza hilo  dini, sasa taarifa zangu zilikuwa zimesambazwa kwa Wauza  madini nchi nzima, yule jamaa aliambiwa anikamate. 

Ile anatoka nje tu Mimi ndiyo kwanza nilikuwa nitoka na  Bodaboda, nilipogeuka nilimuona akihangaika kujuwa nimeelekea  wapi, ni wazi alikuwa hajaniona. Nilimwambia dereva aingie  njia nyingine ili asionione kabisa, kweli dereva alinipitisha  njia nyingine tukaenda kutokea Barabara Kuu. 

Nilimlipa kisha nilichukua Pikipiki nyingine nikamwambia  anisogeze mbele kwa kutumia njia za vumbi za Shoti kati,  mbele ya pesa kila kitu kiliwezekana hadi nilifika Mbele  zaidi, nikapanda gari ndogo ya abiria hadi Chalinze. Hapo  nilikodi Pikipiki inifikishe Morogoro. 

Nilifika Morogoro mishale ya saa 10 Jioni, nilitafuta gest ya  vichochoroni nikala kisha nikalala zangu bila hata hofu kuwa  ninatembea na mzigo mkubwa wa Madini. Hofu yangu ilikuwa kwa  polisi pekee, nikiwa hapo nilipata kuona taarifa ya Habari  kuwa Sarafina na Mkuu wa Magereza walikuwa wamekatwa baada ya  Sarafina kumtaja Mkuu huyo, Sasa kupitia kamera za Kule  Hotelini siku ya tukio la kuiba madini sura yangu ilionekana  nikawa natafutwa Kila kona huku akina Sarafina wakiwa kwenye  mikono ya Polisi, kilichotakiwa kilikuwa ni Madini ya yule  Bilionea. 

Nilizima TV ili nisiendelee kuangalia habari hiyo, Nililala  hadi Asubuhi, Mapema sana nilianza safari ya kuelekea Tabora  kwa kutumia Basi. Nilifika Tabora usiku sana, nilichukua  pikipiki hadi nyumbani kwetu, Nilimgongeshea mlango Mama  Rafia ambaye ndiye jirani yetu kule Tabora nikamwambia

“Nifungulie tafadhali Mama Rafia” Nilisema nikiwa bado nina  hofu ya kukamatwa, Mama Rafia alifungua kisha aliniuliza 

“Kulikoni Jojo? taarifa zako zimeenea kila kona, Tobra nzima,  imekuwaje Mwanangu” Alisema Mama Rafia,, 

“Mama laiti kama ningelijuwa nisingelienda Dar, Maisha yangu  yameharibika baada ya kufika huko” Nilisema 

“Ni kweli umeiba Madini Mwanangu?” aliniuliza, alikuwa ni  jirani pia rafiki wa Marehemu Mama yangu, nisingeliweza  kumficha. Nilimwambia ukweli na nilimuonesha madini 

Tuliingia ndani kwake maana alikuwa akiishi peke yake kisha  alinieleza 

“Msonjo amekamatwa Jana Mchana, inasemekana kuwa yeye  anahusika na anajuwa ulipo” 

“Hapana Mama, Msonjo sijawasiliana naye kwa zaidi ya miezi  yote niliyokuwa Dar, nimepata mitihani mikubwa sana Mama”  Nilisema 

“Sasa Jojo, haya Madini ni mali ya Watu hivyo muda wowote  unaweza kukamatwa, kuliko ukamatwe kwa kosa dogo ni bora  ukamatwe kwa kosa kubwa” Alisema Mama Rafia 

“Unamaanisha nini Mama” 

“Yafiche kiasi alafu mengine kaa nayo ili ukikamatwa  uyaoneshe! utakapotoka huko utajuwa pa kuanzia” Alisema Mama  Rafia, nilimuamini yeye hivyo nilimpa kiasi cha Madini kisha  mengine niliondoka nayo usiku huo na kwenda nyumbani. 

Asubuhi Mapema Mlango uligongwa, Sauti ya Mama Rafia  niliisikia. 

“Nakuja Mama” Nilisema, kisha nilivaa vizuri maana nilikuwa  nimelala. Nilipofungua mlango nilikutana na Askari wakiwa  wameongozana na Mama Rafia 

“Huyu hapa!! kiukweli Askari Mimi sitaki Matatizo kabisa,  huyu Binti anayo hayo madini yanayotafutwa” Alisema Mama  Rafia, kiukweli nilipigwa na Butwaa 

“Mamaaa” 

“Siyo Mama, kiukweli Jojo sitaki matatizo na Mtu ndiyo maana  nimewaambia polisi, ningekaa kimya ningekuja kukamatwa na Mimi” Wale Polisi waliingia ndani wakachukua mkoba wenye  Madini, Chozi lilinibubujika sana. 

“Basi Mama nipe yale madini niliyokupa ili tumrudishie  mwenyewe” Nilisema huku chozi likinivuja 

“Madini? kuna madini uliyonipa Mimi Jojo? ndiyo maana  niliyakataa mapema haya nikaamuwa kusema kwa polisi” Masikini  nililia sana Aisee, Mama Rafia alinikana mbele ya Wale  askari. Nilikamatwa kisha nilirudishwa Dar 

Nikiwa kituo cha polisi nilikutana na Sarafina na yule Mkuu  wa Magereza pia nilikutanishwa na Biliona niliyemuibia  Madini. Alihakiki madini akaona hayajatimia hivyo niliteswa  sana ili niseme yalipo, nilimtaja Mama Rafia ila alinikataa  mbele ya Askari, Tulipelekwa mahakamani kila mmoja na kosa  lake, Mimi nilikuwa na kesi ya wizi wa Madini, Sarafina  alihusika na kifo cha Shonaa pia kupanga njama ya wizi wa  madini, Mkuu wa Magereza alikuwa na kesi nzito zilizoihusu  magereza yake, kifo cha Shonaa na Njama za kuiba Madini. 

Binafsi nilihukumiwa kwenda jela Miaka Mitamo, Sarafina  alienda jela miaka 25, Mkuu wa Magereza alifungwa kifungo cha  Maisha Jela sababu alikutwa na kesi nyingi za mauwaji. 

Kila mmoja alipelekwa Gereza lake kutumikia adhabu.  Nilimpoteza Mama yangu, Nilimpoteza Shonaa, Nilipoteza  thamani yangu, pia nilimpoteza Mama Rafia kisa Madini. Siku  moja nilitembelewa na Msonjo nikiwa gerezani aliniambia kuwa  Mama Rafia amejenga jumba la kifahari, ana Biashara nyingi  anafanya tena ameahama kabisa Tabora anaishi zake Dodoma. 

“Msomjo Mimi Mungu amenisahau” Lilikuwa ndiyo neno langu la  Mwisho kulisema, sikuhitaji kuonana na Mtu mwingine tena.  Hadi sasa unaposoma hadithi hii Mimi ninatumikia adhabu mwaka  wa 8. 

MWISHO

Mwisho wa HADITHI Hii Ndio Mwanzo Wa HADITHI NYINGINE…. Kukiwa na COMMENTS Nyingi Mpya Inaanza Mapema Tu

Mpe Nguvu ADMIN Kwa ajili ya bando Kwa kumtumia Chochote aendelee kupost RIWAYA Mpya Hapa Kijiweni

Lipa Namba: 57900454
Jina: LIPA KIJIWENI TIPS
Mtandao: VODACOM  

SOMA RIWAYA YA KOTI JEUSI KWA KUBONYEZA HAPA 

SOMA RIWAYA YA FUNGATE KWA KUBONYEZA HAPA 

SOMA RIWAYA YA NILIPANGA NYUMBA MOJA NA MAJINI 

SOMA RIWAYA YA GORYANAH HAPA 

SOMA KISASI CHANGU HAPA  

SOMA RIWAYA YA MSALA HAPA

JIUNGE NIPO KIJIWENI Kwa Kubonyeza Hapa

 

 Mungu Amenisahau xx  Mungu Amenisahau xx  Mungu Amenisahau xx  Mungu Amenisahau xx  Mungu Amenisahau xx  Mungu Amenisahau xx  Mungu Amenisahau xx  Mungu Amenisahau xx  Mungu Amenisahau xx  Mungu Amenisahau xx   Mungu Amenisahau xx   Mungu Amenisahau xx   Mungu Amenisahau xx  Mungu Amenisahau xx  Mungu Amenisahau xx 

 

  

10 Comments

  1. Hongera sana admin kwa kweli inasisimua sana😭hadi kusoma unaogoa😢
    Mwisho wa riwaya hii ndio mwanzo mzuri🌹wa riwaya nyengine
    Kila lenye kheir liwe kwako ni nzur san hii riwaya☑️💯

Leave A Reply


Exit mobile version