Ilipoishia “Gari ndogo iliyombeba Muhonzi iliwasili ndani ya godauni moja, akashuhswa na kuburuzwa hadi ndani ya Chumba kimoja kilicho kitupu, akamwagiwa Maji ili azinduke. Maji yalimzindua Muhonzi akajikuta ndani ya kiza kizito, akawakumbuka wale wanaume akataka kuleta vurugu lakini aligundua kua Mikono yake ilikua imepigwa kudu ya nguvu sana.  Akiwa hajatuliza akili vyema ilisikika sauti ya kiatu ikija walipo, wote waligeuka nyuma. Endelea 

SEHEMU YA KUMI NA TANO

Uhafifu wa mwanga ndani ya chumba haukumpa nafasi ya haraka Muhonzi kumtambua aliyekua akifika hapo, ilimbidi asubiri asogee zaidi. Hakuamini macho yake kwa Mtu aliyemwona hapo tena akionekana kua ndiye aliyeagizwa yeye atekwe, alikua ni Kiongozi Mkuu wa chama cha Upinzani cha TUYTA, Ndiye aliyewapa kazi akishirikiana na Mke wa Rais Mbelwa ili kuiba nyaraka huku wakiahidiwa kitita cha Bilioni thelathini.

“Wewe ndiye uliyeagiza ninaswe?” aliuliza Muhonzi kwa hasira, kiongozi huyo anayejulikana kwa jina la Zagamba Edward, alichuchumaa kisha akavua kofia yake aliyokua akiipendelea zaidi kuivaa, kisha akairusha rusha huku akiwa amebana midomo yake, aliposimama alimwambia Muhonzi

“Mnazificha nyaraka, ni sawa. Tulikubaliana si ndiyo, sasa hivi Elizabeth hapatikani, wewe uko bize sana. Ndiyo kusema mmeenda nyuma ya muda tuliopanga kufanya makabidhiano, sasa sijui nataka kusema nini” alisema Zagamba mwenye urefu wa zaidi ya Futi sita, mweusi‘tii’

Aliranda randa ndani ya chumba akiliza funguo za gari kisha haraka akarudi kuchuchumaa alipo Muhonzi halafu kwa sauti iliyojaa utani na kebehi akasema

“Nimepata wazo, kwanini nisikushikilie wewe ili nipate nyaraka, Ooooh!! Ndiyo…tena nitapata nyaraka bila kutoa Burungutu” alitabasamu Zagamba ambaye nia yake kubwa ilikua ni Kuingia Ikulu kama Rais wa Tanzania kuelekea Uchaguzi Mkuu ujao.

“Unasemaje wewe, hebu nifungue tafadhali. Tulishakubaliana kua tunakupa nyaraka unatupa Pesa, mnataka kutugeuka si ndiyo?” alihamaki Muhonzi akiwa anapurukuta pale chini lakini kudu aliyopigwa ilikua ya kiufundi sana hakuweza hata kuichezesha.

“Oooh ni kweli, sasa nitafanya nini jamani” alisema Zagamba akionekana kujawa na kebehi ya hali ya juu, akaiweka sura yake kama Mtu anayetaka kulia kisha akaangusha kicheko cha nguvu.

“Makubaliano, tulikubaliana ndiyo lakini nimefikiria kwenda kinyume, Bilioni 30 kutoka kwa Mke wa Rais zitakua zangu, nyaraka zitakua mali yangu. Ndiyo vyote ni vyangu, kisha nitakalia kiti cha Urais na kuongoza nitakavyo” alisema Zagamba, alishajionesha wazi mbele ya Muhonzi kuwa ataiongoza Tanzania kwa Mabavu zaidi ya Rais Mbelwa aliye Madarakani.

“Mshenzi Mkubwa wewe” alipaza sauti Muhonzi, akaambulia kofi kali lililomsukumiza hadi chini, kisha akainuliwa na Zaganba kwa kutumia Mkono mmoja akamwambia Muhonzi

“Nazitaka nyaraka na Maisha yenu, Mfungeni hapa asitoke” alisema Zagamba kisha akajikung’uta vumbi. Akaondoka ndani ya Godauni hiyo iliyopo Ubungo Maziwa.

Mzee Kimaro na Elizabeth walifanikiwa kufika Picha ya ndege, kilichobaki kilikua ni kuwasiliana na Muhonzi, namna alivyojitanda usingeliweza kumtambua Jasusi huyu hatari anayelitingisha Taifa, Upekuzi ulikua wa kutosha kila kona. Mzee Kimaro aliificha Bunduki yake kwenye Kiroba chakavu kisha akakipachika Begani, ukimwona Mzee huyu unaweza fikiria ni wale Vichaa wanaookota Makopo na kwenda kuuza, ndevu zake zilizokosa ushirikiano na nywele zake zilizojaa mvi, mavazi yake viliakisi makubaliano ambayo Elizabeth na Mzee Kimaro waliyaweka kabla ya kuingia Mtaani wakitokea Msituni.

“Tutajifanya hatufahamiani, lakini jicho lako liwe kwangu, nami nitalielekeza langu kuja kwako” yalikua ni maneno ya mwisho ya Elizabeth kwa Mzee huyu mwenye simulizi tata ya kuuwa Wamang’ati huko Mashambani.

Hatua za Mzee Kimaro zilijaa ukichaa usiovuka mipaka, alinena kwa lugha isiyoeleweka ili aonekane ni Kichaa, haikua rahisi kugundulika sababu aliyekua anatafutwa ni Msichana wa Miaka 21 ambaye picha yake ilisambazwa kila kona ya Tanzania, ili kama kuna atakayemwona atoe taarifa, akavishwa kiremba cha Ugaidi.

Kijijini Mwambisi hapakupatikana mabaki ya mwili wake, hapakua na dalili ya Msichana huyo kuteketea kama ambavyo Rais Mbelwa aliagiza, hivyo Msako wa Maana ulifanywa kila kona kumsaka, akitajwa kama Gaidi.

Wanawake walikaguliwa zaidi ya Wanaume, alitakiwa kupatikana haraka kama Rais alivyotaka.

Mzee Kimaro alivuka viunzi vya askari, alipishana nao bila kumtambua, tena alikua na kiroba chenye makopo na Bunduki iliyowekwa sawa kwa ajili ya Mashambulizi. Elizabeth hakumwacha Mzee Kimaro afike mbali maana alimtegemea kama msaada endapo Ambushi itaanza, naye hakukaa kizembe alikua na Bastola Mbili alizozificha kiunoni.

Kazi iliyo mbele yao ilikua ni kuchomoka Picha ya ndege, alifika mahali akaomba kutumia Choo, lengo lake lilikua ni kuchomoa laini kutoka kwenye chupi ili atafute simu awasiliane na Muhonzi ampe taarifa ya wapi alipo kusudi aje amsaidie.

Alipotoka alimwomba simu kijana mmoja aliyekua ameketi nje ya nyumba hiyo. Akapatiwa simu kisha akaweka laini yake akampigia Muhonzi, simu ya Muhonzi ilipokelewa na Zagamba ambaye alikua ameshamteka Muhonzi na kumfungia Godauni, Elizabeth alimtambua Zaganda baada ya sekunde kadhaa za kuzungumza naye, akapewa sharti la kupeleka nyaraka za siri ili Muhonzi aachiwe, hadi kufikia hapo Elizabeth aligundua kua alikua akifanya kazi ambayo haina malipo yoyote, kwani walishageukwa na Mtoa kazi.

Alikata simu, akaganda akiwa ameishikilia, roho ilimuuma huku hasira ikiwa imemshika. Akatoa laini yake kisha akamrudishia simu yake yule Kijana.

“Ahsante” alisema Elizabeth aliyejitanda vizuri kama Mwana Mwali kisha alianza kutembea akitafuta namna ya kuwakwepa askari waliokua wamezagaa kila kona, wakati anatembea akaliona gari la Polisi lililokua likija mbele yake tena likiwa limejaza askari wenye silaha kali za moto na Bendera nyekundu ya Tahadhari.

Elizabeth akapata wazo la kuwakwepa, akakunja kulia mahali ambapo palikua na Upenyo fulani uliojificha, akiwa ndani ya Mpenyo huo alikutana na askari Mmoja mwenye silaha.

Haraka yule askari aligundua ufanano wa Msichana anayemwona na picha ya Msichana anayetafutwa, akamsimamisha baada ya kupishana naye kidogo, akaitoa picha ya Elizabeth, akagundua Msichana anayesakwa alikua amesimama nyuma yake, akataka kuhakiki kwanza.

Pakiwa pana ukimya wa hali ya juu sana, Askari huyo alisogea na kumtaka Elizabeth ageuke, kwa tahadhari akamnyooshea Bunduki. Elizabeth alijikuta akiwa hana ujanja, mgongo wake aliompa Askari haukumpa nafasi ya kutambua namna ambavyo Askari huyo alikua amekaa.

Moyoni alijiambia

“Nikifanya ujanja sichomoki hapa, Mzee Kimaro uko wapi?”

“Geuka taratibu” alisema Askari huyo huku akiwa makini sana, nyuma ya Askari alitokea Mzee Kimaro kama Mzimu, alikua na kazi moja ya kumlinda Elizabeth ambaye alishampa ahadi ya kumkatia kitita cha pesa kama watafanikiwa kukabidhi nyaraka kwa Zagamba,

kitendo cha Askari kugeuka nyuma alikua amepoteza kila kitu. Haraka Mzee Kimaro alimkita askari huyo ngumi nzito ya kichwa, kabla hajafanya chochote tayari Elizabeth alishaikamata shingo yake na kuinyonga haraka, kisha akautupa mzoga wa askari kama mzigo wa kuni, Mzee Kimaro akauburuza na kuusogeza kichakani.

Elizabeth akamkubali Mzee Kimaro kuwa ni Mtu wa kazi ambaye anaweza kumvusha kutoka hapo ukizingatia tayari Muhonzi alikua ametekwa na Zagamba, baada ya tukio kila mmoja akaingilia upande wake, kila kona ya picha ya ndege palikua na Askari wenye silaha ambao walikua wakifanya upekuzi wa kutosha.

Kila hatua iliyopigwa ilikua na mahesabu makali sana, walikata mtaa kwa Mtaa kukwepa macho ya Askari waliotapakaa, hadi jua linazama walikua wakiranda randa

 

Picha ya ndege.

Wadudu wa Usiku walikua wakipiga kelele, sauti za Helkopta zilikua zikisikika kwa mbali juu ya Msitu wa kutisha wa Magoroto, Wilaya ya Muheza ilikua katika kazia nzito.

Wanajeshi Mia moja Hamsini walikua wamepotea Msituni, Popo wa Maajabu waliwazamisha na habari zao zilifutika katika Uso wa Dunia.

Msitu wenye simulizi ya kutisha ndimo alimo potelea Rubani Benjamin akiwa anatolewa eneo nyeti la Serikali lijulikanalo kama ‘Black Site’

Giza nene, lilikua limeifunika Tanga na wilaya zake zote. Ngurumo za radi na rasharasha za manyunyu zilikua zinaanza, Watu waishio karibu na Msitu wa Magoroto walikua wakilala mapema sana kwa kile walichokua wakikisema kuwa nyakati za Usiku vilisikika vishindo

Ushahidi wa nyayo zilezile walizoziona wale wanajeshi zilionekana pia katika vijiji kadhaa vilivyo karibu na Msitu huo, watafiti wengi walizifananisha na unyayo wa Binadamu lakini ukubwa wa nyayo hizo ulibaki kua kitendawili kizito sana kwa watafiti kuweza kuthibitisha kuwa walikua ni Binadamu au wanyama wenye mfanano na Binadamu.

Mtafiti mmoja kutoka Australia anayejulikana kama Victor Bonteras aliwahi kuweka kambi kijiji kimoja kilichopo karibu na Msitu wa Magoroto, aliweka vinasa picha ili kuviona viumbe hivyo vyenye nyayo kubwa lakini hakufanikiwa zoezi lake, asubuhi zilionekana nyayo lakini kamera yake haikunasa chochote, kwa miezi minne ilimtosha kuhitimisha Uchunguzi wake na kufanikisha kuandika Makala kwenye jarida la New Evolution huku akiuita Msitu huo ‘Nusu Msitu Nusu kuzimu’

Mithiri ya Umeme uwashwapo, ndivyo fahamu za Benjamin zilivyorudi huku mapigo ya Moyo wake yakiwa yanaenda mbio sana, zaidi ya siku nzima alikua kwenye Usingizi mzito wa kifo, alijikuta mahali penye kutisha sana, alimeza funda zito la mate huku akisikiliza mapigo yake ya moyo yalivyokua yakienda kwa kasi kubwa.

Alitumia sekunde thelathini kudhibiti hisia zake, sekunde ya arobaini aliituma akili yake idadisi eneo alilokuwepo Usiku huo, miale ya moto ilikua imezunguka, haraka aligundua miale hiyo iliwekwa kwa ajili ya kulipatia mwanga eneo hilo, akaruhusu macho yake kuangaza huku na kule. 

Nini kitaendelea? Usikose sehemu ya 15 ya MSALA ndani ya SEASON 2 

Hatma ya Mzee Kimaro na Elizabeth itakuaje? vipi kuhusu Muhonzi?

Mpe Nguvu ADMIN Kwa ajili ya bando Kwa kumtumia Chochote aendelee kupost KISASI CHANGU Hapa Kijiweni

Lipa Namba: 57900454
Jina: LIPA KIJIWENI TIPS
Mtandao: VODACOM  

SOMA RIWAYA YA KOTI JEUSI KWA KUBONYEZA HAPA 

SOMA RIWAYA YA FUNGATE KWA KUBONYEZA HAPA 

SOMA RIWAYA YA NILIPANGA NYUMBA MOJA NA MAJINI 

SOMA RIWAYA YA GORYANAH HAPA 

SOMA KISASI CHANGU HAPA  

JIUNGE NIPO KIJIWENI Kwa Kubonyeza Hapa

MSALA xx MSALAxx MSALA xx MSALA xx MSALA xx MSALA xx MSALA xx MSALA xx MSALA xx MSALA

11 Comments

  1. Rachel Richard on

    Mh hisia zangu zinaniambia huo msitu ndo siri zenyew za rais ila mh ngoja tuone kiukwel hadith tamu balaaaa❤️

Leave A Reply


Exit mobile version