IlipoishiaMithiri ya Umeme uwashwapo, ndivyo fahamu za Benjamin zilivyorudi huku mapigo ya Moyo wake yakiwa yanaenda mbio sana, zaidi ya siku nzima alikua kwenye Usingizi mzito wa kifo, alijikuta mahali penye kutisha sana, alimeza funda zito la mate huku akisikiliza mapigo yake ya moyo yalivyokua yakienda kwa kasi kubwa.

Alitumia sekunde thelathini kudhibiti hisia zake, sekunde ya arobaini aliituma akili yake idadisi eneo alilokuwepo Usiku huo, miale ya moto ilikua imezunguka, haraka aligundua miale hiyo iliwekwa kwa ajili ya kulipatia mwanga eneo hilo, akaruhusu macho yake kuangaza huku na kule.  Endelea 

SEHEMU YA KUMI NA SITA

Wakati anageuka kushoto akahisi maumivu makali sana, ndipo akaukumbuka Mkasa wake wa kuruka juu ya Helkopta na kuzama ndani ya Bwawa moja, hisia na mwili wake vilinusa hatari akaona mahali alipo siyo salama kwake, akiwa anashangaa aligundua alikua ndani ya pango moja lenye nafasi kubwa.

Pembeni palikua na kapu dogo lililotengenezwa kwa miyaa, ndani yake mlikua na matunda yaliyotokezea hadi juu, hapo haraka akajua kua matunda hayo yalikua yake lakini swali alilojiuliza

“Nani amenileta hapa, nimekaa kwa muda gani?” alijiuliza akiwa anahema kwa kutumia mdomo wake, pua zake zilikua zimeziba kwa mafua ya ghafla yaliyomshika. Akausukuma mkono wake taratibu ili ufike mahali ambapo palikua na kapu hilo lenye matunda, kabla hajaufikia walitimka Popo kutoka kwenye shimo moja lililo juu ya eneo alilokua ameketi baada ya kuamka.

Alishtuka, lakini popo hao hawakumdhuru isipokua walifanya safari ya kuzama zaidi ndani ya pango hilo, Benjamin akaushikilia moyo wake uliostuka nusura utoke kifuani, funda jingine la mate likapita kwenye koo lake huku matundu ya pua yake yakizibuka kutokana na ule mshituko, akaweza kuhema vizuri kwa pua zake.

Akiwa katika tafakari nzito ya eneo hilo alisikia sauti ya mikanyago mizito ikija alipo, macho yake aliyelekeza eneo ambalo sauti hizo zilikua zikitokea, kadili sauti zilivyokua zikisogea ndivyo alivyokua katika hali ya woga zaidi.

Kilitokea kiumbe kikubwa chenye manyonya mengi, haraka aligeuza shingo yake asiweze kutazama zaidi, alitamani ardhi ipasuke aingie humo.

Kiumbe hicho kwa ukubwa wake kiliinama wakati kinavuka eneo hilo lililokaa kama mlango kisha likajiachia vizuri na kufanya umbo lake kuonekana vizuri.

Alikua sokwe mkubwa sana, Benjamin alijikaza kumtazama, Sokwe huyo alipogongana macho na Benjamin alitabasamu, mara alitokea Msichana mmoja mweupe mwenye nywele nyingi zilizojisokota, alikua na urefu wa Wastani, alivalia mavazi yaliyotengenezwa kwa ngozi, msichana huyo alikua ameongozana na Sokwe huyo Mkubwa.

Wote walisimama wakimtazama Benjamin, kisha Msichana alisogea karibu na Benjamin, pumzi za Benjamin zilionesha wazi alijawa na hofu sana, msichana huyo anayekadiliwa kuwa na Miaka 23 hadi 25 alilitambua hilo kisha akamwambia Benjamin

“Usiogope, Mimi siyo Mtu mbaya” alisema akiwa ameshamfikia Benjamin, namna alivyokua akimtazama Benjamin alikua akimshangaa na kutabasamu, eneo la kifua la Benjamin lilikua wazi haraka alivuta nguo iliyo kando akajizuia kisha akamwuliza Msichana huyo.

“Wewe ni Nani, nimefikaje hapa, na hapa ni wapi?” aliuliza maswali kwa mkupuo, msichana huyo alijiuma mdomo wake kabla ya kumpa jibu

“Hapa ni Magoroto Tanga, ulianguka kutoka juu ya Helkopta. Nilikusaidia kuokoa uhai wako” alisema Msichana huyo aliyejawa na tabasamu zuri na sauti laini isiyo na mikwaruzo, kitovu chake kilikua nje kutokana na aina ya Mavazi aliyokua ameyavaa, macho yake makubwa yalikua usoni kwa Benjamin, Msichana huyo aliachwa mbali sana kiumri na Benjamin

“Wewe ni Nani?” akauliza Benjamin, hisia zake zikamfananisha Msichana huyo na Elizabeth Mlacha aliyemwingiza kwenye sekeseke la kutisha.

“Naitwa Zandawe, Malkia wa Magoroto. Mmiliki wa kila kilichomo ndani ya Msitu huu” alisema,

“Zandawe?”

“Ndiyo, Baba na Mama yangu walinifundisha kuutawala Msitu huu na kuongoza kila kiumbe ndani ya Msitu. Upo salama usiwe na hofu Benjamin”

“Benjamin, umelijuaje jina langu?” alishtuka Benjamin, Msichana huyo alilifahamu jina la Benjamin, kitu kilichomshangaza sana.

“Nimeona umechora jina hilo kwenye bega lako” alisema akitabasamu, ni kweli Benjamini alikua na mchoro wa jina lake Begani, kidogo hofu ilianza kuondoka. Zandawe akazamisha mkono wake wa kushoto ndani ya kapu akatoa Tunda na kumpatia Benjamin

“Kula kwa mkono wako, unapaswa kua na nguvu. Nakutakia Usiku mwema, tutaonana asubuhi” alisema Zandawe, Msichana huyo alimpatia Tunda Benjamin kisha akamwacha hapo akaondoka na Sokwe aliyekuja naye, Sokwe aligeuka nyuma na kumuaga Benjamin, ilimfanya Benjamin atoe tabasamu la wasiwasi akiwa ameshikilia tunda mkononi.

***

Mvinyo ulikua unashuka kwenye glasi, mkono ulioshikilia chupa ya Mvinyo ulikua ukitetemeka, saa ya gharama ilikua mkononi. Ukimya ulitawala, mbele ya Mtu huyo waliketi wanaume watano, mmoja ni IGP Hassan Kitulo, wa pili aliyeketi upande wa pili ni Mkuu wa majeshi, waziri wa Mambo ya ndani Ignas Zakaria Balozi Juma Nguvu mbili na Mwanamke pekee kati ya wanaume hao aliyeitwa Bi Sandra Mengi ambaye ni Mkuu wa Idara ya Usalama wa Taifa, jina la utani aliitwa Kisu cha Bucha.

Jina hilo la utani halikuja kwake kwa Bahati mbaya, yeye alitumika sana na Rais Mbelwa kumaliza wote walioenda kinyume na Rais, tena kazi ya kuwamaliza aliifanya mwenyewe kwa mikono yake, akapewa jina hilo kutokana na uhodari wake bila kuangalia Mtu huyo alikua na uzito wa namna gani alimfyeka.

Sauti ya mvinyo kupenya shingoni pa Rais Mbelwa kila mmoja aliisikia, aliwaonesha ni jinsi gani alikua na hasira, aliusukuma mvinyo kwa nguvu bila kujali ukali wake kisha akaitupa glasi juu ya meza kwa kishindo huku akihema, mkono wake akautumia kuwahesabu walio mbele yake kisha akasema

“Nyinyi wote watano mnanizamisha kwenye shimo nikiwa hai, mnanizika bila huruma. Haiwezekani Msichana mdogo kama yule eti hadi sasa hajanaswa?” alisema kwa kufoka kila alivyokua akizidi kuongea, kila mmoja aliinamisha kichwa chake chini

“Au mnataka Dunia ianze kuandika yanayoendelea Tanzania, operesheni ya Siku moja inawaumiza kichwa kiasi hicho, jeshi mnalo, mamlaka mnayo, mnataka nini kingine niwape”

Hakuna aliyepaza sauti wala kuchezesha japo midomo yake, hasira aliyonayo Rais Mbelwa hakuna aliyeweza kukabiliana nayo. Halafu akamgeukia Bi Sandra, kwa sauti iliyopoa akamwambia

“Tumefanya mengi Sandra, umefanya operesheni zangu nyingi, nakuamini. Namtaka Elizabeth akiwa hai au akiwa amekufa, nataka nyaraka” alisema Rais Mbelwa, alionekama kuanza kuzidiwa na Mvinyo mkali aliokua akiugika kutwa nzima bila kula chochote, aliishiwa nguvu, pale pale walinzi wake walimtoa na kumpeleka chumbani kwake.

Sasa kazi hiyo akakabidhiwa Bi. Sandra, Mama Katili mwenye nywele fupi zilizojaa karikiti.

Saa Saba Usiku, Picha ya Ndege.

Gari nyeusi yenye usajili maalum iliwasili kwenye kambi ya muda mfupi iliyowekwa na Askari kwa ajili ya Msako, alishuka Bi. Sandra ambaye muda mfupi uliopita alikua Ikulu ya Rais Mbelwa, Askari walimpa heshima yake.

“Mmefikia wapi?” aliuliza baada ya kukutana na Mkuu wa kambi hiyo Bligedia Antony Kesi, mkononi alikua na ramani ya eneo zima la Picha ya ndege pamoja na Kijiji cha Mwambisi, akampatia ramani hiyo Bi. Sandra

“Bado anatafutwa, hakufa kwenye shambulio lile” akasema Bligedia, siri ya kwanini Elizabeth anasakwa ilifichwa na viongozi wakubwa wa Kijeshi, kiremba cha Ugaidi ndicho ambacho Elizabeth alifichwa nacho, wengi wakiamini anasakwa kwasababu ni Gaidi.

“Hisia zetu zinasema yupo hapa Picha ya ndege, hawezi kurudi nyuma wala kwenda mbele hata kwenda Barabara ya Bagamoyo, kote wamesambaa askari” akasema tena Bligedia huku akiwa anakatwa jicho kali na Bi. Sandra, wengi walikua wakimwogopa kigogo huyo wa Usalama wa Taifa kutokana na ukaribu wake na Rais Mbelwa, hata namna alivyokua akifanya Mauwaji ya kutisha ilijenga picha ya kuogofya zaidi.

“Kama hawezi kwenda mbele, hawezi kurudi nyuma aliwezaje kutoka Mwambisi akafika  hapa Bligedia?” aliuliza Bi. Sandra, nyodo na dharau vilikua kama mapacha na tabia yake ya ujivuni, kigauni chake chenye mpasuo kilionesha ni namna gani aligoma kuzeeka.

Licha ya Usiku kua mwingi lakini aliweza kupaka rangi midomo yake myembamba kama ganda la ndizi, masikioni aliweka hereni zenye msalaba, kwa asiyemjua akikutana naye anaweza cheka kwa kufikiria ni kituko lakini ni Mtu hatari anayetumainiwa sana na Rais Mbelwa kwenye mipango ya Siri.

Kwanza aliketi na kukunja nne, akaidandaza ramani hiyo juu ya meza kisha akaongeza mwanga wa taa, akatoa kalamu nyeusi, haraka akachora duara eneo fulani la Picha ya ndege, hapo palikua na daraja jipya linalojengwa, daraja hilo ndilo lilikua mwisho wa Mpaka wa Picha ya ndege.

Kwa kujiamini akasimama na kumvuta Bligedia kwa mbwembwe kisha akampa neno kwa sauti ya kuchombeza

“Tuma Askari hapo sasa hivi” alisema kisha aliachia tabasamu, Bligedia akabakia ameganda kama Mshumaa huku akimtazama Mwanamke huyo aliyerudi kuketi na kukunja nne huku akiwasha sigara yake ndefu na kuanza kuivuta. Haraka Bligedia akaita Askari zaidi ya Arobaini ili waelekee eneo la daraja ambako Bi. Sandra alipachorea duara.

Nini kitaendelea? Usikose sehemu ya 17 ya MSALA ndani ya SEASON 2 

Mpe Nguvu ADMIN Kwa ajili ya bando Kwa kumtumia Chochote aendelee kupost MSALA Hapa Kijiweni

Lipa Namba: 57900454
Jina: LIPA KIJIWENI TIPS
Mtandao: VODACOM  

SOMA RIWAYA YA KOTI JEUSI KWA KUBONYEZA HAPA 

SOMA RIWAYA YA FUNGATE KWA KUBONYEZA HAPA 

SOMA RIWAYA YA NILIPANGA NYUMBA MOJA NA MAJINI 

SOMA RIWAYA YA GORYANAH HAPA 

SOMA KISASI CHANGU HAPA  

JIUNGE NIPO KIJIWENI Kwa Kubonyeza Hapa

MSALA xx MSALAxx MSALA xx MSALA xx MSALA xx MSALA xx MSALA xx MSALA xx MSALA xx MSALA

13 Comments

  1. Story bombaa sana, ila mwanzon ilikua Benjamin ndo anatusimulia wasomamaji ila xax haipo hivyo ni ww mwandishi ndo unatusimulia ila ni ya motoo sanaa

Leave A Reply


Exit mobile version