IlipoishiaKwa kujiamini akasimama na kumvuta Bligedia kwa mbwembwe kisha akampa neno kwa sauti ya kuchombeza

“Tuma Askari hapo sasa hivi” alisema kisha aliachia tabasamu, Bligedia akabakia ameganda kama Mshumaa huku akimtazama Mwanamke huyo aliyerudi kuketi na kukunja nne huku akiwasha sigara yake ndefu na kuanza kuivuta. Haraka Bligedia akaita Askari zaidi ya Arobaini ili waelekee eneo la daraja ambako Bi. Sandra alipachorea duara.  Endelea 

SEHEMU YA KUMI NA SABA

Sekeseke!! Mkono Mtupu haulambwi

Kimya kimya Askari jeshi arobaini wenye silaha za Moto wameshatumwa Darajani, ndege tunduni wawili walikua hapo wamepumzika. Mzee Kimaro alikua amejilaza kama Mfu anayesubiri kuingizwa mwana Ndani, Elizabeth akagutuka baada ya kusikia vishindo kadhaa, kutokana na Mafunzo yake aliyoyapata akagundua vishindo hivyo vilikua vya Askari waliokua wakibadilishana nafasi kutoka kushoto na Kulia.

Wanajeshi wengine walilizunguka daraja kutokea Porini, maji yalikua yakiririka, magari ya Wajenzi yalikua yamesuswa hapo baada ya Mashambulizi kadhaa Kijijini Mwambisi. Palitulia kwa sikio la kawaida lakini kwa Elizabeth alishashtuka kua usalama ulikua mdogo sana hapo.

Akamtonya Digidigi aliyelala kama Mfu kando yake, Mzee Kimaro alipogutuliwa kitu cha kwanza kilikua ni Bunduki yake aina ya M2 Carabine, Bunduki maalum kwa ajili ya vita ikiwa na sifa ya kumwaga risasi kama njugu mawe.

Elizabeth akazidi kumkubali Mkongwe huyo aliyekataa kuzeeka Maini, hapakua na maongezi zaidi ya wote kutega vizuri masikio yao.

Giza halikuwapa nafasi ya kuona zaidi, wote walipitia mafunzo ya Ujeshi hivyo zoezi la hisia halikua tatizo kwao. Wakazisoma vyena hatua za Askari huku wakiwahesabu na kugundua walikua kumi na tano juu ya daraja, kimbembe kilikua kuchomoka hapo.

Wakati wanapiga hesabu waligundua pia uwepo wa Askari wengine porini, nyasi zilikua zikicheza cheza kama zinasukumwa na Upepo.

Elizabeth akachomoa Bastola zake mbili kutoka kiunoni, akafunga vizuri kiremba chake, akamtonya Mzee Kimaro kila Mmoja akatafuta njia kwenye eneo lake, njia zote mnbili za kutokea darajani zilizingirwa na Wanajeshi.

Mzee Kimaro akachapa kwanza risasi porini ili kumshtua adui yake, zikarindima risasi kama mvua, wote wakalala chini huku wakiwa wameshajua maadui zao walipo, Mzee Kimaro akazitupa risasi za kutosha kuelekea porini, zikajibiwa na wale walio juu ya Daraja.

Majibizano yakaanza wakati huo Elizabeth alikua ameshachumpa na kutua kando ya jiwe kubwa lililo mficha vyema na mashambulizi ya Watu wa chini, akawapa mgongo na kuanza kuwapigia mahesabu walio juu ya daraja ambao walikua na uchu na Mzee Kimaro aliyekua akishambulia kwa kasi ya ajabu kama Kipanga aliyenasa kifaranga cha Kuku, alikua hodari wa kutumia Bunduki hiyo aliyoizoea tokea enzi za vita ya Uganda na Tanzania.

Ufundi na uharaka wa kupanga risasi na kuziachia aliwamaliza walio porini kwa upande wake, akajikunja ndani ya daraja huku akipiga Mahesabu ya kuchomoka ndani ya daraja, wote walishajua kama watatumia muda mrefu kushambuliana na wale askari basi vikosi vitaongezeka hapo watazidiwa.

Elizabeth akaona ni bora aseme na walio juu, akaweka vizuri Bastola zote mbili alizozishikilia kama Mapaja ya Kuku wa Kienyeji, akiwa amewapa Mgongo walio porini kwa upande wake akaanza kuwadondosha walio juu kimya kimya sababu Bastola zake zilifungwa kizuia sauti, alipo wapunguza vya kutosha akarudi tena ndani ya daraja, akaichukua Bunduki ya Mzee Kimaro, haraka akatoka nayo na kuanza kuwashambulia walio porini, alizimwaga za kutosha hadi pakawa kimya.

Ukawa ndiyo muda mzuri wa wao kuchomoka ndani ya daraja lakini tayari taa za Magari ya jeshi zilikua zinakaribia hapo kwa spidi ya ajabu, hawakutaka kupoteza muda.

Walianza kuisaka Kiluvya kwa mwendo wa spidi wakikatiza Mashambani, Askari walipofika eneo la tukio walikuta Miili ya kutosha ikiwa chini, Bi. Sandra akashuka kutoka kwenye gari nyeusi ndogo aina ya Benz, akaikagua ile miili, akakutana na maganda mengi ya risasi, akaliokota moja kisha akasogea nalo karibu na taa ya gari akalichunguza vyema.

“Mabibi na Mabwana, ni M2 Carabaine, hayuko peke yake. Wanaswe haraka” akasema kwa sauti kubwa Bi. Sandra, haraka Kikosi kikazama Mashambani kuwasaka Elizabeth na Mzee Kimaro.

SIKU MOJA KABLA YA KIZAA ZAA

Jua lilikua likichomoza, Jiji la Dar-es-salaam lilifunikwa na mwanga mkali ulioashiria ilikua ni siku yenye joto kali kuliko kawaida. Japo Umande uliwafanya wengi kuvalia Makoti asubuhi hiyo lakini ndani ya vichwa vyao walijua ifikapo saa Nne watavua makoti hayo na kuyaona kama Mizigo.

Muhonzi alikua akipata kifungua kinywa, Mtu wa kwanza kumpigia Asubuhi hiyo alikua ni Elizabeth ambaye alikua akijigaragaza kwenye mashuka ya Hoteli, hapo Hotelini alipaswa kukaa kwa siku mbili kisha atorokee Uskochi kama alivyoambiwa na Rais ili kukwepa mkono wa Usalama wa Taifa, Usalama wa Taifa walipanga kummaliza Elizabeth, aliyeusuka mpango huo wa siri uliovuja alikua ni Bosi wa Idara ya Usalama wa Taifa Bi. Sandra ambaye ni Mtu wa karibu wa Rais.

Alipanga hivyo ili kulinda siri nyingi ambazo kama Rais ataendelea kua na Mchepuko huyo kungekua na hatari ya kuvuja kwasababu alishikwa pabaya sana na Msichana huyo, Kingine Bi. Sandra aliona viashiria vya mapema kuwa Elizabeth alikua Jasusi, siku moja aliwahi kumweleza Rais hilo lakini Rais Mbelwa akalibishia kutokana na namna alivyompenda Elizabeth, ndipo Mpango wa kuuawa kwa Elizabeth uliposukwa lakini ulivuja ambapo Rais alipanga kumtorosha Elizabeth kuelekea Uskochi mafichoni.

Tusonge sasa…

“Naelekea PIZA HUNT sasa hivi, nitakujulisha” alisema Muhonzi, mara nyingi simu zao hazikua na maneno mengi. Elizabeth alikaa kimya kisha simu ilikatwa, akaendelea kuvinjari kwenye Mashuka mazito huku akiwa na furaha kubwa sana, alifikiria namna ambavyo wangetia kibindoni Bilioni 30 kutoka kwa Mke wa Rais kupitia kwa Zagamba.

Kazi hiyo walipewa na Mke wa Rais kwa kushirikiana na Zagamba ambaye ni kiongozi wa chama Kikuu cha Upinzani cha TUYTA.

Unaweza jiuliza Mke wa Rais alipata wapi pesa zote hizo, kabla hajaolewa na Rais alikua waziri wa Madini kwenye serikali iliyopita, alikusanya kiasi kikubwa cha pesa ambacho kiasi kidogo alimwezesha Rais kukalia kiti hicho, Mke wa Rais alikua ni miongoni mwa Mafisadi ambao waliibia Tanzania kwa kiasi kikubwa sana, alificha pesa nyingi Benki ya Ufaransa.

Baada tu ya Rais kukalia kiti walifunga ndoa, aliamini kumsaidia Mbelwa kushika madaraka kutamfanya aendelee kuiibia Nchi, lakini akatulizwa na kuporwa madaraka, akafutwa kwenye Chama Tawala, akapotezwa kwenye ramani, akafungiwa Ikulu kwa Mtumwa.

Mbelwa akahakikisha hakuna mwingine anayeiibia Nchi isipokua yeye mwenyewe na washirika wake wachache, akatesa na Kuuwa Watu ndani ya Ikulu, akamgeuza Mke wake kuwa Kijakazi ndani ya Ikulu, akampa Ujauzito mdogo wake Mke wake kisha akamuuwa ili kuificha siri hiyo ambayo aliamimi ingemchafua, ndipo Mke wa Rais alipoamua kupanga njama za Kumg’oa Mbelwa kwa kushirikiana kwa siri na chama Pinzani.

Udhaifu wa Rais ulikua kwenye nyaraka zake za siri alizozificha kwa ulinzi Mkali mdani yaIkulu, Mke wa Rais akawatumia walinzi wa Ikulu kupiga picha na kuchukua video eneo lasiri analotumia Rais kufanya Mauwaji ndani ya Ikulu, akahakikisha anatengeneza ushahidi ili zikipatikana nyaraka za siri basi zivuje na Video hizo.

Muhonzi alifika Piza Hunt kwa lengo la kulichunguza eneo hilo lililoonekana kua la kawaida lakini eneo la chini palikua na siri nzito iliyofichwa humo, akaegesha Pikipiki yake mbali na pale kisha akatembea kwa hatua kadhaa akaingia ndani ya jengo hilo la kisasa lililojaza Raia wengi wa kigeni.

“Karibu Kaka, nakusikiliza” alisema Mrembo mmoja aliyevalia sare za wahudumu, Muhonzi alimtalii kidogo kama Mtalii huko Serengeti, kisha akatabasamu

“Nahitaji Piza moja na Soda yoyote nyeusi” alisema Muhonzi, Mhudumu aliguna. Kisha

aliondoka hapo akiwa ameshaandika ni kitu gani Muhonzi alikua ameagiza. Akili na macho ya Muhonzi vilikua vikiwaza ni namna gani anaweza kuzama ndani zaidi ya jengo hilo, eneo la jiko alihisi huwenda ndiko kwenye mlango

Aliketi akiwa hatulii, hakunwona hata Mhudumu alipokua amefika “Kaka” akaita Mhudumu akiwa anatabasamu

“Mbona kama kuna Mtu unamtafuta hapa?” akauliza

“Nilikua naangalia kilipo choo, mimi ni mgeni, ni mara yangu ya kwanza nafika hapa usije ukanicheka” akasema Muhonzi, yule Mhudumu akazidi kufurahia vituko vya Muhonzi, Pepsi nyeusi na Piza vilikua tayari juu ya Meza yake

“Nifuate nikuelekeze” akasema Msichana huyo, Muhonzi akanyanyuka na kuanza kumfuata kwa nyuma, hatua zake ndefu za taratibu zilimpa uhuru zaidi

“Ukikunja kulia utaviona” akasema Yule Mhudumu

“Ahsanteee” akasema Muhonzi, yule Muhudumu alipompa mgongo Muhonzi, akairejesha sura yake ya kazi, alinyanyua kwanza macho yake juu kuhesabu kamera, alipata idadi ya kamera sita zilizotegwa karibu karibu, akajua fika kuwa anarekodiwa.

Haraka akabadilisha uelekeo, akaifuata korido moja iliyo kimya sana, ni sauti ya kiatu chake ndiyo iliyokua ikisikika. Alitembea kwa dakika moja tena kwa mwendo wa taratibu kama Kinyonga, akaanza kuhisi harufu za vyakula.

Akapiga mluzi wa maana, sauti za kukaangiza zilisikika pia, akazidi kupiga hatua ndefu kusonga mbele, akakuta mlango mmoja ambao sauti zote alizozisikia zilitokea huko, akili yake ikawaza haraka kuwa huko ndiko lilipo jiko.

Kando ya Mlango palikua na Boksi moja, alipochungulia alikuta sare za wapishi zenye rangi nyeupe, akaichukua moja na kuipachika mwilini, kisha taratibu akausukuma mlango, mahali alipotokea palikua jikoni, ndipo alipohitaji kufika.

Harufu za Vyakula zilianza kupenyeza taratibu kwenye pua za Muhonzi, kila Mmoja ndani ya jiko alikua bize sana kiasi kwamba hakuna aliyeshtuka kuwa ndani ya Jiko aliingia Mtu asiye husika.

Muhonzi aliutumia mwanya huo kudandaza macho yake vyema, hatimaye akauwona Mlango Mmoja ambao alihisia huwenda ndiyo wenye kumiliki korido yenye kumfikisha chini ya Mjengo.

Akabeba kisu, akakiweka kiunoni, akajitomasa vizuri kuikagua Bastola yake iliyo kiunoni, kisha akabeba trei yenye mahitaji kadhaa ya mapishi, alifanya hivyo ili pasitokee Mtu atakaye Mtilia shaka. Taratibu akiwa anawaangalia wapishi alianza kuusogelea mlango, lakini ndani pale palikua na Mpishi mmoja aliyemwona Muhonzi akiwa kama anakagua jambo, alishamtilia shaka kwa kaisi kikubwa sana.

Akavua Mask yake kisha akaanza kufwatilia nyendo za Muhonzi, alimchunguza kwa siri hadi Muhonzi alipoutikisa mlango na kuufungua kwa wepesi sana kisha akatokea upande wa pili, yule Mpishi akaitoa simu mfukomi kisha akapiga Mahali na kutoa taarifa.

Ukimya ulikua wa kutosha sana baada ya Muhonzi kuingia kwenye korido asiyoifahamu, alipepesa macho yake, hapakua na chochote upande wake wa kulia na kushoto, isipokua mbele ambapo aliona kuna Bango lenye mishale inayoelekeza kulia na mwingine kushoto. 

Nini kitaendelea? Usikose sehemu ya 18 ya MSALA ndani ya SEASON 2 

Mpe Nguvu ADMIN Kwa ajili ya bando Kwa kumtumia Chochote aendelee kupost MSALA Hapa Kijiweni

Lipa Namba: 57900454
Jina: LIPA KIJIWENI TIPS
Mtandao: VODACOM  

SOMA RIWAYA YA KOTI JEUSI KWA KUBONYEZA HAPA 

SOMA RIWAYA YA FUNGATE KWA KUBONYEZA HAPA 

SOMA RIWAYA YA NILIPANGA NYUMBA MOJA NA MAJINI 

SOMA RIWAYA YA GORYANAH HAPA 

SOMA KISASI CHANGU HAPA  

JIUNGE NIPO KIJIWENI Kwa Kubonyeza Hapa

MSALA xx MSALAxx MSALA xx MSALA xx MSALA xx MSALA xx MSALA xx MSALA xx MSALA xx MSALA

7 Comments

Leave A Reply


Exit mobile version