IlipoishiaAkavua Mask yake kisha akaanza kufwatilia nyendo za Muhonzi, alimchunguza kwa siri hadi Muhonzi alipoutikisa mlango na kuufungua kwa wepesi sana kisha akatokea upande wa pili, yule Mpishi akaitoa simu mfukomi kisha akapiga Mahali na kutoa taarifa.

Ukimya ulikua wa kutosha sana baada ya Muhonzi kuingia kwenye korido asiyoifahamu, alipepesa macho yake, hapakua na chochote upande wake wa kulia na kushoto, isipokua mbele ambapo aliona kuna Bango lenye mishale inayoelekeza kulia na mwingine kushoto.  Endelea 

SEHEMU YA KUMI NA NANE

Hadi afike hapo ilimhitaji kupiga hatua zisizopungua kumi na tatu. Alipaza macho yake zaidi, hapakua na Kamera yoyote ile eneo hilo.

Uchu wa kuipata Bilioni 30 ulianza kumsukuma kupiga hatua kwenda mbele, lakini kisu kilikua Mkononi mwake, alikishika vyema sana. Sekunde kadhaa baadaye zilimkuta akiwa amefika eneo lenye bango, hapo palikua na makutano ya Korido moja ndefu, kushoto na kulia, upande wa kulia palikua na katazo la Mtu yeyote kuelekea huko, upande wa kushoto hapakua na katazo lolote, haraka akajua anachokitafuta kipo upande wa kulia.

Korido ilikua ndefu kiasi tena isiyo na mlango wowote ule hafi mwisho, Muhonzi aliamua kuifuata Korido hiyo huku akiwa tayari amechomoa Bastola yake, aliishikilia kwa utayari wa Ambushi yoyote itakayojitokeza

Akatoa simu yake, kitu cha kwanza alichokigundua baada ya kutoa simu mfukoni ni simu kupoteza uwezo wa kufanya mawasiliano.

Akili yake ikamwambia kwa haraka sana kua anaingia sehemu nyeti zaidi, akaukaza moyo wake akazidi kusonga mbele huku akiwa makini kuliko wakati wowote ule.

Muhonzi alizidi kusogea mbele, eneo la mbele lilikua likipigwa na taa angavu zaidi, hakuogopa akapiga moyo konde. Alifika mwisho wa korido hapo akakutana na Korido nyingine lakini pakiwa na njia ya kushuka chini, akaitumia ngazi taratibu na kwa umakini zaidi, hakuruhusu kiatu chake kitoe sauti anapokua anapiga hatua kushuka chini.

Palikua kimya sana, alipofika chini alikutana na Mlango mmoja wa aluminiamu, akatega sikio lake ili kusikia sauti yoyote itakayo mpa mashaka. Hapakua na sauti yoyote ile, akajaribu kuutekenya mlango

Taratibu mlango ulisukumika, ndani palikua kimya sana na palionekana kua na Maktaba ya vitabu, akaangaza huku na kule, ukimya ulikua unamfuata Muhonzi huku akianza kuhema kwa nguvu sana.

Akaufunga ule mlango taratibu huku Bastola ikiwa mkononi, akajikuta ndani ya Maktaba isiyo na mwanga mkali, giza la wastani lakini palikua kimya sana.

Muhonzi alipojaribu kupiga hatua kadhaa mbele ghafla taa zenye mwanga mkali ziliwaka, akiwa katika taharuki

tayari askari walishamzunguka kila upande tena wakiwa na silaha kali za moto.

Msako

“Stupid Kids (Watoto wapuuzi” alisema Bi. Sandra akiwa ameshikilia sigala mkononi, mbele yake aliona Askari wakizama mashambani kuwasaka Mzee Kimaro na Elizabeth, maiti za askari zilitosha kuwapa ujumbe kua Wanayemsaka siyo Mtu mwepesi.

Bi. Sandra alitabasamu kisha alirudi ndani ya gari, akaipekua ramani aliyoitandaza vyema kwenye siti ya nyuma ya gari yake, kisha akamwita Brigedia Antony Kesi

“Huyu Mtu anaelekea Dar-es-salaaam, inavyoonekana kuna mambo anayahitaji kuyakamilisha” alisema Bi Sandra akiwa anamtazama Brigedia aliyezidiwa maarifa.

“Unafikiria watakua wanapitia wapi?” akahoji Brigedia, Bi. Sandra akamkata jicho kali Brigedia Antony kisha kwa kebehi iliyovuka mipaka akamuuliza “Wewe ni Brigedia wa namna gani ambaye hadi sasa hujajua Huyu Binti ni Komandoo?”

Hapakua na jibu kutoka kwa Brigedia, akaongeza

“Hatuwindi kuku, tunamwinda Mtu mwenye ujuzi. Hii operesheni haiitaji Watu kama wewe” Mchaka mchaka ndani ya Mashamba ulizidi kua Mkubwa, Elizabeth alihitaji kusonga mbele zaidi afike kiluvya, mambo mawili yalimsukuma kwenda mbele, moja alihitaji kumkomboa Muhonzi ambaye alikua ameshikiliwa na Mwenyekiti wa chama cha TUYTA na jambo la pili ni namna ambavyo nyuma alikua akisakamwa na Jeshi la Tanzania.

Usiku huo, Bi. Sandra akaagiza Chopa mbili kuranda randa juu ya Mashamba ili kuwanasa Mzee Kimaro na Elizabeth ambao walikua katika mwendo kuhakikisha wanajiweka salama, moja ya chopa aliidandia yeye Bi. Sandra, aliamua kulivalia njuga kama ambavyo Rais alimkabidhi jukumu la kuhakiiisha anamnasa Elizabeth.

“Shusha karibu” alisema Bi. Sandra kwa sauti iliyopotezwa na upepo, kwa hasira akarudia kauli yake, taa kutoka juu ya Chopa zilifanya eneo zima kua na mwanga Mkali. Chopa ilishuka usawa wa karibu zaidi, licha ya kua na Uhakika kuwa Elizabeth alizama ndani ya mashamba lakini hapakua na dalili kua alikua hapo, Msako mkali ulifanywa na Askari kwa takribani nusu saa, hakuna aliyemwona Elizabeth wala Mzee Kimaro.

Ndani ya pango moja dogo ambalo si rahisi kwa Askari kushtuka kua Watu wawili wanaowasaka walikua wamejificha hapo, walikua kama Popo namna walivyojibanza. Sauti ya Chopa na upepo mkali wa Pangaboi ulisaidia kulaza kila kitu ndani ya Shamba lakini hawakufanikiwa kugundua mahali walipojificha.

Bi. Sandra akahitaji kushuka chini kukagua kwa macho yake ya karibu, alishushwa hadi chini, kisha chopa ikarudi juu kwa ajili ya kulifanya eneo lote liwe na mwanga Mkubwa kama Mchana.

“Mkuu tumetafuta kila kona, lakini hatujaambulia chochote” alisema Askari mmoja tena kwa sauti kubwa ili kwenda sawa na sauti ya Helkopta. Bi. Sandra hakumjibu chochote, akasogea hadi juu ya jiwe moja kubwa mahali ambapo aliita Askari wote, mara moja walijikusanya

“Mnasikia, huyu Mtu hatakiwi kwenda mbali zaidi ya Hapa, akitoka hapa ataingia Kiluvya kisha Mbezi. Hatupaswi kulikubali hilo sababu tutamkosa rasmi” alisema huku akigonga gonga jiwe kwa kutumia Buti lake kubwa.

“Fanyeni Msako wa maana kila kona” alisema kisha Helkopta ilishuka na kumchukua, muda huo huo Mzee Kimaro na Elizabeth walichomoka kwenye pango dogo na kuchumpa upande wa pili ambapo palikua na msitu.

Helkopta iliyombeba Bi. Sandra ilirejea Ikulu ya Dar-es-salaam, dakika chache ilikua tayari inatua kwenye kiwanja kidogo cha kutua Helkopta ndani ya viunga vya Ikulu, Rais Mbelwa alikua juu ya varanda akitazama namna Mama huyo Mtu mzima alivyokua akitembea na Buti zake kuelekea ndani ya Ofisi ya Rais, hapo hapo Rais Mbelwa alibinya midomo yake kwa hasira kisha akarudi Ofisini kuzungumza na Bi. Sandra.

“Rais, siyo rahisi kumnasa yule Binti. Kikosi kilicho eneo la tukio siyo kikosi kinachoweza kufanikisha hili, tafadhali naomba kikosi maalum kutoka Black Site” alisema Bi. Sandra akiwa ameishikilia mkononi kofia yake. Ndilo jambo la kwanza alilolinena akiwa mbele ya Rais Mbelwa, hakuona kama Brigedia Antony na kikosi chake wangefanikisha mpango huo wa kumnasa Elizabeth.

Macho yalimtoka pima Rais Mbelwa, akabonyeza simu yake ya Mezani akiwa anahema, presha yake ilikua siyo ya kawaida. Kwa mambo ambayo yalikua yakiendelea Tanzania kwa wakati huo moja kwa moja yalimtia doa Rais na vyombo vyake vya Usalama. 

Ni masaa kadhaa yalipita huku Mtandao wa intaneti ukiwa umezimwa Tanzania kwa maagizo ya Rais Mbelwa, alitegemea kumnasa Elizabeth kusingelichukua muda mrefu hivyo.

Kwa sauti ya kukoroma iliyotokana na mvinyo mkali, Rais Mbelwa alipiga simu Black Site na kutoa agizo la kuhitaji Makomandoo wa kutosha kuelekea eneo la Tukio, tabasamu lilimtoka Bi. Sandra, alikiamini kikosi hicho hatari ambacho kilikua silaha ya mwisho ya Rais Mbelwa.

Alipiga saluti mbele ya Rais asiyesema chochote kisha aligeuka na kuondoka haraka, kabla hajaingia kwenye chopa alipigiwa simu, alisita kuipokea, simu hiyo iliyotoka kwa Waziri Mkuu wa Tanzania Haji Babi, akaipokea, akasikiliza maelezo yaliyoambatana na wito maalum wa waziri Mku Haji Babi katika kisiwa cha Mbudya.

Alipoingia ndani ya Helkopta aligeuka na kuitazama Ikulu kwa dakika zaidi ya moja, kisha akamwambia rubani,

“Tuelekee Mbudya sasa hivi” haraka Helkopta ilipaa na kuelekea Kisiwa cha Mbudya.

**

Zaidi ya Helkopta sita zenye Makomandoo kutoka Black Site zilikua zikikatiza juu ya Msitu wa Magoroto Tanga, mahali ambapo Benjamin Kingai alidondokea na kusaidiwa na Malkia Wa Msitu huo anayeitwa Zandawe.

Sauti hizo zilimgutua Benjamin akiwa pangoni, mara Sokwe Mkubwa pamoja na Malkia Zandawe walifika hapo kwa Benjamin haraka sana Usiku huo, wote walisimama mbele ya Benjamin ambaye naye alishtuliwa na sauti za Helkopta hizo. 

Wewe ni Nani?” aliuliza Malkia Zandawe, alijawa na jazba, hasira iliyomfanya amtolee macho Benjamin. Mkononi alikua ameshikilia mkuki mdogo aliouelekeza kwa Benjamin

Kichwa cha Zandawe kilizungushiwa shanga nyekundu moja kama urithi wa Umalkia ndani ya Msitu huo wa kutisha, Msitu ambao aliishi na Wazazi wake wawili ambao walifariki akiwa mdogo.

“Mimi ni Benjamin, kwani kuna nini?” alihoji Benjamin akiwa anatetemeka.

“Kwanini wanakutafuta?” swali hili lilimkumbusha wakati ambao alikua na Elizabeth, alikua

akimuuliza swali hili mara kwa mara Benjamin alipepesa macho yake yaliyokaribia kutoa chozi, akamweleza Malikia Zandawe mkasa mzima, taratibu Mkuki ulishuka chini, hata ile hasira ilirudi nyuma.

“Mtoto wako yupo wapi?” aliuliza Zandawe

“Sijui alipo, ila Mpenzi wangu yupo eneo la siri.”

“Huyo Elizabeth yuko wapi?” alihoji Malkia Zandawe 

Akajibu Benjamin “sijui chochote, huwenda hadi sasa wanamtafuta. Inaonesha hawajakata tamaa kuhusu Mimi

pia, wanaamini kuna mambo ninayoyajua kuhusu hiyo M21

“Hiyo M21 ni kitu gani?” alidadisi Zandawe akiwa anamtazama Benjamin, kabla hajatoa jibu alitikisa kichwa chake

“Sijui chochote kama nilivyokweleza, Mtu pekee anayejua hiyo M21 ni yule Msichana Elizabeth, Mimi ni kivuli tu” akasema Benjamin, Zandawe akatoka ndani ya pango akaelekea nje ambako Sokwe na Popo walikua wakiranda randa, moja ya Helkopta ilikua juu ya Msitu wa Magoroto, kama alivyosema Benjamin bado Askari walikua wakifanya Dolia ili kuona kama wanaweza kumpata yeye au askari zaidi ya Mia moja ambao wamepotea kwenye Msitu huo.

Malikia Zandawe akatoa amri kwa popo kuishambulia Helkopta iliyo juu ya Msitu wa Magoroto, haraka msafara wa Popo wakubwa mfano wa Bata Mzinga, waliruka na kuivamia Helkopta ya Kijeshi iliyokua kwenye doria, wakawauwa askari wote pamoja na Rubani anayeiendesha kisha Helkopta ikaangukia ndani ya Msitu wa Magoroto, haraka Malkia Zandawe akarejea ndani kwa Benjamin

“Kama ni hivyo unapaswa kuisaidia familia yako Benjamin, unajua mahali ilipo Balck Site?” alihoji Malikia Zandawe, Ilimpa tafakari ya haraka Benjamin, akapata nguvu ya kuketi huku akiituma akili yake ikumbuke namna Mikimbio ya Helkopta ilivyokua Usiku ule alipokua ametolewa Black Site

Akaitumia elimu yake ya Urubani kutafuta jibu la Haraka, kisha akaibuka

“Ndio naweza kupafahamu, nitafikaje kule?” akahoji Benjamin

“Hili niachie Mimi Benjamin, Mimi ni Malkia wa Magoroto, huu ni Msitu wangu” alisema, kisha akaongeza

“Twende tukaikomboe familia yako” alisema Zandawe, ilikua kama kauli isiyo na nguvu kwa Benjamin, alichokisikia aliona kama kilijaa utani na dhihaka ya hali ya juu, hakuamini hata kidogo kama Msichana huyo anaweza akaikomboa familia yake kwenye eneo lile lenye ulinzi wa kutosha tena ni eneo nyeti la Serikali ya Tanzania.

“Twende Black Site?” akauliza Benjamin akiwa anamkodolea macho Zandawae

“Nimesema twende” aling’aka Zandawe akionekana kumaanisha anachokisema. Japo Benjamin alihitaji sana kumkomboa Mpenzi wake lakini kurudi ndani ya Black site lilikua ni jambo gumu kwake, akikumbuka namna alivyokatwa kidole na kuteswa hakuhitaji kuishia mikononi mwa lile jeshi, akazuga kidogo

“Sawa lakini nahitaji kukumbuka zaidi kuhusu lile eneo, naona kama kichwa changu kinazidi kunipa majibu tofauti” alisema huku akisikiliza jibu la Zandawe ambaye alianza kupoa, kwa haraka haraka Benjamin aligundua Zandawe alikua ni Mtu aliyejawa na hasira na kisasi fulani ndani yake

Basi Zandawe akarejea kuketi mahali alipo lala Benjamin kisha akamwambia

“Pengine hujui nina nguvu kiasi gani Benjamin, nifuate” alisema Zandawe haraka akanyanyuka na kuanza kuondoka Pangoni, jukumu la Benjamin lilikua ni kumfwata Malkia Zandawe kwa nyuma, bado ulikua usiku mwingi.

Walitoka hadi nje wakiongozwa na Sokwe Mkubwa aliyepewa jina la Yubo, alikua ni Sokwe mwenye akili sana, alikua rafiki mkubwa wa Zandawe. Wakaongozana hadi sehemu moja iliyo na jiwe Kubwa, yule Sokwe akalisogeza lile jiwe, likaonekana pango

Benjamin akawa anashangaa, taratibu wakaingia ndani ya pango hilo huku akiwa na shahuku ya kutaka kujua ni kitu gani anbacho Malikia Zandawe alihitaji kumwonesha. Walizidi kwenda ndani, giza lilikua jingi lakini halikufanya safari hii kusita.

Popo walianza kuruka ruka walipokua wanazidi kwenda mbele ndani ya Pango hilo lenye ukubwa wa kutosha, walifika mahali Zandawe alisimama kisha yule sokwe akasugua kucha zake kwenye jiwe, ukatoka moto akaweka kwenye kifaa kilichopo kwenye jiwe, Naam! Hapo palikua na tambi iliyoshika moto haraka na kufanya pango liwe na mwanga, Benjamin alishtuka alipowaona Popo wakubwa mfano wa Bata Mzinga wakiwa wametulizana

“Usiogope” alisema Zandawe, haikua rahisi kwa Benjamin lakini alihitaji ujasiri wa ziada ili kusonga mbele zaidi, Benjamin alizituliza pumzi zake na mapigo yake ya moyo yaliyokua yakienda ‘Songombingo’

Waliendelea mbele kwa zaidi ya hatua ishirini huku yule Sokwe akiwa ameshikilia ule utambi unaowapa Mwanga. 

Nini kitaendelea? Usikose sehemu ya 19 ya MSALA ndani ya SEASON 2 

Mpe Nguvu ADMIN Kwa ajili ya bando Kwa kumtumia Chochote aendelee kupost MSALA Hapa Kijiweni

Lipa Namba: 57900454
Jina: LIPA KIJIWENI TIPS
Mtandao: VODACOM  

SOMA RIWAYA YA KOTI JEUSI KWA KUBONYEZA HAPA 

SOMA RIWAYA YA FUNGATE KWA KUBONYEZA HAPA 

SOMA RIWAYA YA NILIPANGA NYUMBA MOJA NA MAJINI 

SOMA RIWAYA YA GORYANAH HAPA 

SOMA KISASI CHANGU HAPA  

JIUNGE NIPO KIJIWENI Kwa Kubonyeza Hapa

MSALA xx MSALAxx MSALA xx MSALA xx MSALA xx MSALA xx MSALA xx MSALA xx MSALA xx MSALA

 

12 Comments

  1. Johnson Kajuna on

    Sema mtunzi yuko vizuri…big up sana kwa kujua kuwaunda wahusika. Haikuwa bahati mbaya Benjamin juwa rubani…najua mengi ya kusisimua na kufungua macho yanakuja🔥🔥🔥

Leave A Reply


Exit mobile version