Ilipoishia “Sijapata kumwona Mwanadamu Mbishi na Mgumu kama huyu” aliutupa mkono wake uliojaa damu kwa hasira sana kisha akarudi kuketi kitini akitafakari ni namna gani afanye ili apate taarifa nyeti. Haraka akanyanyuka kutoka kitini kwa hasira akamfwata tena Elizabeth, akamwambia
“Ukiendelea kuwa jeuri utamfuata Rais alipo” alisema kisha akaondoka ndani ya chumba hicho, haraka Elizabeth akatambua fika kua Rais alikua ameshauawa na kilichokua kinaenda kufanyika ni Uasi mkubwa wa kuitawala Nchi.
Elizabeth akiwa ananing’inia akaukumbuka Usiku wa Heka Heka. Endelea
SEHEMU YA ISHIRINI NA TANO
MSATA. SAA TANO USIKU
Elizabeth alifika Msata akiwa amebadilisha mwonekano wake kama Msichana mwenye mambo mengi mjini, aliweka kope Bandia, akaweka kucha, alivalia gauni fupi lenye mg’ao, juu aliweka Wigi fupi ambalo lilimfanya aonekana kama siyo yeye, eneo ambalo alielekezwa na Zagamba wakakabidhiane Nyaraka M21 lilikua ni Msituni.
Akaiweka gari kando ya Barabara kisha taratibu akaingia Msituni, Hapo aliambiwa kua atakutana na Mtu wa Zagamba aliyepewa kazi ya kupeleka Nyaraka kwa Zagamba, alipoanza kukaribia aliona tochi, akajua ndiye anayepaswa kuonana naye hapo. Akaiweka sawa Bastola yake ndogo aliyoitoa kutoka kwenye mkoba wake
Akatembea taratibu tena kwa tahadhari kubwa sana, hakutaka kumwamini yeyote. Mkononi alivalia kifaa chenye GPS ambayo ilikuwa inamwezesha Muhonzi kuona mitembeo ya Elizabeth na kujua yupo wapi. Alipofika hapo alikutana na mwanaume mmoja aliyevalia koti jeusi, ndani zaidi ya Msitu mzito wenye kiza kizito kisicho na nuru kabisa
Chini ya Mti mmoja ndipo alipokuwepo Mtu huyo.
“Una mzigo?” aliuliza Mwanaume huyo, Elizabeth akamjibu kwa umakini “Siwezi kukupa mzigo bila kuona namna utakavyonipa pesa”
“Binti, Bilioni 30 ni ngumu sana kutembea nazo hata kama zipo kwemye mfumo wa Dola. Nimeziacha ndani ya gari, naomba nione hizo nyaraka kwanza ndipo nikupe pesa yako” Mazungumzo haya yalikua Mubashara kwa Muhonzi.
Elizabeth akatoa Flashi akampatia Mwanaume huyo asiye mfahamu, kisha Mwanaume yule akawasha kifaa chenye mfanano na Kompyuta Mpakato akaiingiza Flash na kuhakiki, akatoa tabasamu la kuchanua ambalo lilimpa ishara Elizabeth kua Mtu huyo hakua na lengo zuri kwake, hakuishia hapo aliangusha kicheko.
Haraka Elizabeth akaichomoa Flash kutoka kwenye kompyta kisha akamnyooshea Bastola Mwanaume huyo.
“Pesa nikupe Nyaraka” alisema, mkononi alikua na tocho ndogo lakini alipommulika vizuri alimwona Mwanaume huyo akiwa na mavazi ya Usalama wa Taifa, akajua wazi kua alikua ameingia Mtegoni.
“Oooh taratibu Elizabeth, pesa yako ipo ndani ya gari. Ok, ongozana na Mimi” alisema Mwanaume huyo, Elizabeth akaongeza umakini wa kutosha baada ya kugundua hapo Msituni hapakua eneo salama kwake.
Akayaangaza macho yake kama Paka mwizi, kisha akamsukuma mbele yule Mwanaume ili amtumie kama chambo cha yeye kutoka pale Msituni, akilini mwake alishaiuwa Biashara ya Nyaraka zile za siri baada ya kuona dalili za uwepo wa hatari. Hatua za yule Mwanaume zilikua za mahesabu makali sana, Elizabeth alishaligundua hilo sababu alikua Jasusi
Sauti ya Muhonzi ikasikika Masikioni mwa Elizabeth, ikamwambia
“Naona uwepo wa Watu zaidi ya Mmoja hapo Msituni, haraka Ondoka” alisema kisha Elizabeth akajibu kwa Ukimya huku sauti za Majani makavu yaliyokanywagwa zikiendelea kusikika. Moyo wa Elizabeth ukaanza Riadha ya haraka, nywele zikamsisimka vya kutosha huku vipele vidogo vidogo vya Tahadhali vikianza kumtoka.
Hatua ya sita ya yule Mwanaume ilimfanya Elizabeth ashuhudie teke kali likimuelekea, kwakua tayari alishaanza kuzihesabu hatua za yule Mwanaume na kujua hatua hizo alilikwepa teke kwa haraka huku akiukunja mgongo wake kuelekea mbele, aliporudi alikutana na kipande cha mti kilichotua eneo la tumbo na kumjeruhi.
“Mshenzi unafanya nini?” aliuliza Elizabeth, hapo akajua fika kua taarifa za yeye kua ndani ya Msitu zilishauzwa muda mrefu hivyo kituo kinachofwata ni kukamatwa na kuuawa kikatili na Wanaume hao wenye sare za Ikulu, kwa haraka akili yake haikuchekecha vyema na kujua ni Nani aliyeuza mpango huo, akajikaza ili atoke ndani ya Msitu.
Bastola ilikua imeshamtoka, kutokana na giza zito hakufanikiwa kuiyona mahali ilipo dondokea, mkononi alikua na Flashi yenye nyaraka, akaisweka haraka ndani ya chupi na kuifunga kwa zipu kisha akajiweka sawa kukabiliana na Mwanaume huyo aliyekua na tambo za kutosha kua angemmaliza Elizabeth hapo Msituni.
Tochi ilikua pembeni, Elizabeth alipoutoa mkono tumboni alihisi uwepo wa damu Mbichi yenye harufu, ikampa hasira, akamvaa Mwanaume yule mwenye ngumi nzito.
Akashusha mvua ya ngumi nyepesi alizolenga sehemu moja, kisha akaachia pigo zito kwa kutumia skuna yake iliyomtoboa yule Mwanaume eneo la shavu. Akatema damu huku akigugumia kisha akapiga filimbi ya kuita Watu wengine walio pale Msituni, dakika moja tu alishajua kupambana na Elizabeth isingelikua kazi rahisi kuifanya.
Tochi zikaanza kutapakaa pale Msituni, Elizabeth akamshushia na teke takatifu lililomlaza yule Mwanaume kisha akaanza kukimbia ili kuokoa Maisha yake huku akivuja damu, eneo ambalo alikatisha lilikua na Miiba ya kutosha iliyomkwangua kila eneo la mwili wake na kumchania nguo.
Alikatiza ndani ya Msitu wenye giza nene huku akijua fika kua hapakua na Umbali mrefu kutoka hapo kuelekea Barabarani alipoacha gari yake, lakini haikua rahisi kufika Barabarani, ilimtaka atumie nguvu zake zilizoanza kumsaliti. Alikimbia huku akifukuzwa na Wanaume kadhaa wenye tochi
La haula!
Akafika Barabarani lakini hapakua na gari yoyote, eneo ambalo alitokea halikua lile eneo aliloingilia, akaanza kuifukuza ile Barabara asijuwe anasonga mbele au anarudi nyuma, giza
lilikua la kutosha na hapakua na dalili ya kutokea kwa gari au Pikipiki, akamwambia Muhonzi
“Sijui kama nitachomoka salama Muhonzi, hali yangu siyo nzuri” akasema kisha akakitupa kifaa chake cha Mawasiliano, Bahati nzuri akamulikwa na taa ya gari kutokea nyuma yake, akasimama na kupungia mkono gari isimame.
Ndani ya gari alikuwamo Benjamin Kingai, rubani wa Shirika la Air Tanzania aliyekua akitokea Arusha kwa Mpenzi wake, gari iliposimama akafungua mlango na kuingia haraka kisha akamwambia yule dereva kua
“Ondoa gari Haraka” Benjamin akiwa mwenye taharuki akawaona wanaume wenye Silaha wakitokea Msituni, haraka akaliondoa gari bila kuuliza swali lolote.
**
Ndani ya Ikulu. Saa 9 Alhasiri.
Waziri Mkuu Haji Babi, alielekea eneo la siri ambalo Rais alikua akitesa na kuuwa Watesi wake, akaingia kwenye moja ya chumba ambacho alikuwamo Mke wa Rais Lucas Mbelewa, hakutaka kutangaza kifo cha Rais Bila kupatikana kwa Nyaraka za siri ambazo zilikua mikononi mwa Elizabeth.
Alipofika alimkuta Mke wa Rais akiwa ameketi sakafuni, Haji Babi akasogea na kuchuchumaa mbele ya Mke wa Rais kisha akamwambia
“Masaa machache yajayo nitatangazwa kua Rais wa Nchi hii, hakuna Mtu wa karibu wa Lucas atakayebaki kua hai. Una nafasi moja ya kuishi, nieleze unafahamu nini kuhusu Nyaraka M21?” alihoji Haji Babi akiwa amekaza macho yake kuelekea alipo Mke wa Rais. Hofu ya Haji Babi ni kua Nyaraka hizo zina siri zake pia kwani viongozi wengi wa ngazi za juu walikua kwenye nyaraka hizo.
Mke wa Rais alikua kimya huku akilini akijiuliza ni jambo gani lililomfika Rais, akiwa katika tafakari akanyanyuliwa na kupelekwa kwenye chumba kingine ambacho kilikua na jokofu la kuhifadhia Maiti, humo ndimo mwili wa Rais Lucas ulikuwa umehifadhiwa.
Mke wa Rais akawa anatetemeka, ujanja wote akautia mfukono, waziri Mkuu Haji Babi alionesha wazi kua alikua siyo Mtu mzuri, japo Mke wa Rais alihitaji Rais atoke madarakani lakini hakutegemea kama angetolewa kwa njia hiyo ya Uwasi, jokofu lilipofunuliwa akaambiwa
“Nenda kaangalie kuna nini ndani yake” alisema Waziri Mkuu, kisha akatoa tabasamu pana huku akisigina kiatu chake sakafuni, Mke wa Rais akasogea hadi kwenye jokofu, aliiyona maiti ya Rais. Mwili huo ulikua na matundu ya Risasi, alijikuta akiishiwa nguvu, Waziri mkuu akamdaka
“Sasa unapaswa kua upande wangu Mke wa Rais, nitayafungulia Maisha yako yaliyokua yamefungwa na Lucas, nyota yako itawaka tena kwenye Siasa” akasema Waziri Mkuu huku akiwa anamwonesha tabasamu pana sana, alionekana kujua siri nyingi za Maisha ya Marehemu Rais Mbelwa na Mke wake.
Akaagiza Mke wa Rais awekwe kwenye chumba kingine kwa uangalizi mkubwa, akawekwa kwenye chumba kizuri ambacho alipewa kila kitu isipokua simu, Mpango wa Waziri Mkuu ukawa ni kutaka kuitawala Nchi, aliporudi ndani ya Ofisi ya Rais akampigia Simu Muuwaji wake wa kuaminika, akamtaka awasili hapo Ikulu jioni hiyo ili ampe kazi ya kusafisha wote anaowahisi watakua kikwazo kwenye Utawala wake.
**
Hatma!!
Baada ya kutoka Black Site akiwa amechoka sana Bi. Sandra alikua akiegesha gari lake kwenye jumba moja la ghorofa ambamo ndimo alimokua akiishi, Ulikua usiku umeshaingia, nywele zake alizozifunga kwa nyuma zilikua zikimfuata kila aendako.
Palikua kimya sana, kichwani alikua na mawazo tele, kwanza alihitaji hizo nyaraka za siri ambazo Elizabeth alikua nazo na pia alifikiria sana kuhusu Mauwaji aliyoyafanya kwa Rais Lucas Mbelwa. Kwa kiasi kikubwa alianza kujiona mwenye hatia
Akalisogeza gari hadi maegesho, alipomaliza alishuka ili aelekee juu ambako alikua akiishi, eneo la maegesho lilikua na magari mengi, pia palikua na giza la wastani lakini ambalo haliwezi kuyashinda macho yake, akapiga hatua kadhaa lakini akahisi uwepo wa Mtu nyuma yake, akasimama kisha haraka akageuka lakini hapakua na Mtu yeyote yule.
Akashusha pumzi nzito ya wasiwasi, palikua kimya kuliko kawaida. Alipogeuka mbele alimwona Mtu mmoja aliyevalia suruali ya Jinzi ya Bluu, shati jeupe alilolichomekea vizuri. Akapata ahueni, akatabasamu kisha akaendelea mbele.
Yule Mtu alikua Mwanaume aliyeenda hewani, mweusi mwenye mwili uliojengeka vizuri, alipokaribiana na Bi. Sandra alianza kutafuta kitu mfukoni mwake lakini kwa Bahati mbaya aliangusha Karatasi alizokua amezibeba, akainama kuokota, Bi Sandra akajikuta tu akimsaidia kuziokota maana zilikua zimetawanyika sana.
Namna ambayo Bi. Sandra alikua akiishi ni ngumu sana kugundua alikua Muuwaji wa kuaminika.
“Ooh Ahsante sana” alisema Mwanaume huyo baada ya Bi Sandra kumpatia karatasi alizokua ameziokota.
“Siku nyingine uwe makini” akasema Bi. Sandra akiwa anampa tabasamu Mwanaume huyo aliyemzidi umri parefu sana. Alipotaka kuachana naye Mwanaume yule akamwambia Bi. Sandra
“Samahani Naitwa Skanda” alisema huku akitabasamu kama Mtu aliyehitaji ukaribu na Bi. Sandra, hakujua Mtu aliyekua akizungumza naye alikua Mtu wa namna gani, haraka Bi. Sandra akajua Mwanaume huyo alihitaji ukaribu, alizungumza akiwa amempatia mkono Bi. Sandra.
Bila Hiyana Bi. Sandra alirudisha tabasamu pamoja na Mkono, akampa Mwanaume huyo. Sekunde moja tu ikabadilisha kila kitu, yule Mwanaume akaubana mkono wa Bi. Sandra kwa nguvu huku akitabasamu,kwa kutumia ujuzi wake Bi. Sandra akajitoa
Alipojiangalia aliona ana tundu dogo linalotoa damu, kisha ghafla nguvu zilianza kumwisha, akachomoa Bastola yake ili amshambulie Mwanaume huyo aliyekua amesimama mbele yake, cha ajabu Mwanaume yule hata hakujitingisha, pale pale Bi. Sandra alianguka na kuanza kutapa tapa, yule Mwanaume akaangalia huku na kule kisha akauvuta mwili wa Bi. Sandra na kuuingiza chini ya gari yake, halafu akajikung’uka vumbi
Akaitoa simu kutoka mfukoni kisha akapiga mahali.
“Nani anafuata?” akauliza Mwanaume huyo, Naaam!! Mpango wa Waziri Mkuu Haji Babi ulianza kufanya kazi, tayari Muuwaji alikua kazini kufyeka wote anaowahofia kwenye Utawala wake. Maisha ya Bi. Sandra yakaondoka kizembe.
**
Waziri Mkuu Haji Babi, akaketi kwenye kiti cha Rais akiwa anagida mvinyo, muziki wa taratibu ukiwa unamburudisha huku Muuwaji wake akizidi kufanya Mauwaji Usiku huo, hakuishia kwa Bi. Sandra, akammaliza Balozi akiwa ndani ya gari kwa kutumia kitambaa chenye Sumu.
Mauwaji haya yalifanyika kwa siri nzito na uharaka wa ajabu sana, kipaumbele sasa kikawa ni kupata Nyaraka za siri zilizopewa jina la M21, akamtuma Muuwaji wake wa kuaminika kwenda Ilipo Black Site kumchukua Elizabeth Mlacha. Akampa ramani ya mahali ilipo Black Site, akaondoka Usiku huo huo na gari ndogo aina ya Carrina C4 kuelekea Black Site.
Kitu pekee kilichobakia kwa Waziri Mkuu ni kupata nyaraka ili kifo cha Rais kitangazwe, Upande wa pili ndani ya Godauni
Muhonzi akafanikiwa kukata kamba alivyofungwa, giza lilikua nene ndani ya Chumba alichohifadhiwa, akajaribu kuchungulia dirishani kwa mtindo wa kuruka sababu dirisha lilikua juu sana lakini hakuambulia kuona chochote kile, akajaribu kuita
“Kuna nani hapo nahitaji Maji” aliita kwa makusudi huku akifahamu fika kua eneo hilo lina ulinzi mkali kuhakikisha yeye hachomoki, akaita tena, ndipo aliposikia hatua za kiatu zikija upande wake, akarudi haraka kuketi sakafuni alipokua ameketi.
Mara taa ikiwashwa, kisha akatupiwa maji aliyoyataka.
Nini kitaendelea?
Usikose SEHEMU YA ISHIRINI NA SITA
Mpe Nguvu ADMIN Kwa ajili ya bando Kwa kumtumia Chochote aendelee kupost MSALA Hapa Kijiweni
Lipa Namba: 57900454
Jina: LIPA KIJIWENI TIPS
Mtandao: VODACOM
SOMA RIWAYA YA KOTI JEUSI KWA KUBONYEZA HAPA
SOMA RIWAYA YA FUNGATE KWA KUBONYEZA HAPA
SOMA RIWAYA YA NILIPANGA NYUMBA MOJA NA MAJINI
JIUNGE NIPO KIJIWENI Kwa Kubonyeza Hapa
MSALA xx MSALAxx MSALA xx MSALA xx MSALA xx MSALA xx MSALA xx MSALA xx MSALA xx MSALA
8 Comments
wakwanza kuisoma
Ni mimi
🔥🔥
😋😋😋
Msalaa 🐐🐐
Weeeee weee hatar na nusu
Jaman masala ni moto wa quotes mbali admin umeweza
Nzuri