Ilipoishia Muhonzi akafanikiwa kukata kamba alivyofungwa, giza lilikua nene ndani ya Chumba  alichohifadhiwa, akajaribu kuchungulia dirishani kwa mtindo wa kuruka sababu dirisha  lilikua juu sana lakini hakuambulia kuona chochote kile, akajaribu kuita 

“Kuna nani hapo nahitaji Maji” aliita kwa makusudi huku akifahamu fika kua eneo hilo lina  ulinzi mkali kuhakikisha yeye hachomoki, akaita tena, ndipo aliposikia hatua za kiatu zikija  upande wake, akarudi haraka kuketi sakafuni alipokua ameketi. 

Mara taa ikiwashwa, kisha akatupiwa maji aliyoyataka. Endelea 

SEHEMU YA ISHIRINI NA SITA

“Nitakunywaje sasa na umenifunga kamba?” akauliza Muhonzi kwa ujanja huku akiwa tayari  ameshakata ile kamba, yule Mlinzi akamtazama sana Muhonzi 

“Ni kweli sasa nitakunywaje nina kiu sana Aaaaaahhh” akazidi kusema Muhonzi huku  akijibaraguza kama Mtu aliyefungwa mikono yake, yule Mlinzi ikamlazimu kufungua sasa  mlango wote kisha akaingia ndani ya chumba hicho, ndicho alichokua anakitaka Muhonzi. 

Akaoneshwa Bunduki, kisha akaambiwa 

“Huwezi kufanya ujanja wowote, nitakupa maji” alisema yule Mlinzi, akaiokota chupa ya  maji kisha akaifungua na kumsogezea Muhonzi ili amyweshe, hakujua kua alikua  ameshafanya kosa kubwa sana, pale pale Muhonzi akamtandika ngumi nzito ya pua, 

akamfwata kwa haraka na kumvunja shingo. Akaiyokota ile Bunduki kisha akaanza kutafuta  njia ya kutoka ndani ya Godauni. 

Akatembea kwa taratibu kwa mahesabu mazito sana ili asije rudi mikononi mwa Zagamba,  akasikia sauti ya TV, akajua fika kua Walinzi wengine walikua huko. Akasogea hadi eneo  hilo na kuwakuta walinzi wakiwa wanakunywa pombe na kuvuta sigara. 

Hakutaka kusema nao, akatafuta kona nzuri akapita ili alifikie lango kuu la kutoka ndani ya  Godauni hiyo iliyojaa giza zito. Taratibu sana Muhonzi akalisukuma lango kisha akatoka nje  ya Godauni, muda ulivyozidi kwenda ndivyo ambavyo wale Walinzi walivyoshtuka baada ya  kuona mwenzao harudi, akatumwa mmoja wao kwenda kuangalia, akamkuta akiwa  ameshakufa. Msako wa kutafutwa kwa Muhonzi ukaaanza ndani ya lile Godauni, walipokuja  kugundua kua alishatoka ndani ya Godauni tayari Muhonzi alikua ameshafika mbali kabisa. 

** 

Baada ya kuchomoka mikononi mwa Watu wa Zagamba, akakimbilia kwenye jumba la siri  ambalo alikua akilitumia kufanyia kazi zake, kichwa chake kikiwa kinawaka moto kwanza  alihitaji kujisafisha mwili mzima baada ya kukaa godauni kwa siku kadhaa. 

Maji ya Baridi yakakubali kuuufanyia Utakaso wa kutosha mwili wa Muhonzi, akili ilipokaa  sawa akawa tayari kujua ni wapi alipo Elizabeth, bado aliamini kuwa alikua hai. Jambo la  kwanza alilolifanya baada ya kuketi na kuwasha mitambo yake ni kuanza kusaka mara ya  mwisho simu ya Elizabeth ilizimwa wapi. 

“Picha ya Ndege” ndiyo sehemu pekee ambayo simu ya Elizabeth ilizimwa kwa mara ya  mwisho, aina ya simu aliyoitumia ilionekana lakini uzuri simu hiyo bado ilikua Hewani,  Usiku ulikua mwingi, akajipumzisha kwanza Kitandani ili akiamka aendelee na upekuzi  wake kwa njia ya Mtandao, masuala hayo ndiyo yaliyokoleza ukaribu wake na Elizabeth  Mlacha. 

** 

Saa 3 Asubuhi, Tanzania 

Muuwaji wa kuaminika alikua akipata chai ya asubuhi sehemu fulani ya Tanzania, safari  yake ya Usiku mzima ilikomea kwenye moja ya Hoteli, alipumzika hapo ili afanye safari ya  kuelekea eneo nyeti la Black Site. 

Baada ya kumaliza, aliingia kwenye gari kisha akaendelea na safari yake ya Masaa matatu  baada ya Chai, sasa aliushika Msitu mmoja, akaisweka gari eneo fulani, akachukua begi lake  na kupandisha kilima kimoja. Alionekana ni Mtu anayejua anachokifanya, kazi aliyopewa na  Waziri Mkuu ni kuhakikisha anamchukua Elizabeth kutoka Mikononi mwa Walinzi wa Balck  Site. 

Begi alilolibeba lilikua na silaha moja ya masafa marefu pamoja na Darubini, aliketi juu ya  kilele cha kilima hicho, huku macho yake akiyaelekeza eneo la umbali wa Kilomita Nane,  hapo ndipo ilipo Black Site.

Akatoa Ramani ya jengo la Black Site, ramani hiyo ilichukuliwa Ikulu baada ya Waziri Mkuu  kuikamata Ikulu, muuwaji akatabasamu. Kisha akalala usawa mzuri na kuiweka Bunduki ya  Masafa marefu vizuri, akachukua Darubini na kuanza kulikagua jengo hilo kwa uzuri. 

Akajifunika kofia nyeusi, kisha akairejesha Darubini ndani ya Begi, akaanza kuitumia  Darubini iliyo kwenye Bunduki yake, macho na hisia zake akayaelekeza ilipo Black Site,  eneo alilolala alikua akilitazama jengo hilo lenye vioo kwa uzuri sana. 

Aliona na kuhesabu idadi ya Walinzi walio ndani ya Jengo ambao ni Makomandoo wa  kuaminika aliokua akiwatumia Rais Lucas Mbelwa, alihitaji kuwamaliza kwanza. Ndani ya  jengo palikua na zaidi ya Makomandoo hamsini. Wote aliwapigia mahesabu, kisha akaikunja  Bunduki yake na kuizamisha ndani ya Begi, akarudi chini ya Kilima na kuanza kutembea  kwa kutumia barabara ya vumbi iliyokua ikielekea Black Site. 

Muuwaji huyo, alipokaribia aligundua kwa haraka uwepo wa ulinzi maalum wa Nyaya  nyembamba za Umeme ambazo ndizo zilizokua zikilinda eneo hilo, alishajiandaa sababu siri  za ulinzi wa ndani na nje ya Jengo alikua amezipata. 

Akachomoa kifaa kidogo chenye mfanano na Simu, kisha akauzima umeme huo ndani ya  sekunde ishiri akawa amezivuka nyaya hizo. Taratibu akakimbia na kujificha nyuma ya ukuta  wa jengo la Black Site, kuhusu idadi ya walinzi wa ndani ya Jengo hakua na wasiwasi nao  sababu alishawapigia mahesabu makali sana. 

Akasimama hapo kwa mahesabu mazito, kisha akachungulia, jengo hilo lililokua na vioo  vingi ambavyo vingefanya urahisi wa Muuwaji kujulikana kua amefika, akapiga hatua za  haraka na kuuwahi ukuta wa pili, akajificha kisha akatoa kamba kutoka ndani ya Begi lake,  akairusha kamba kuelekea juu, iliponasa akawa na zoezi moja tu la kuifuata paa ya jengo  hilo. 

Kisha taratibu akatembea juu ya paa la jengo huku akiwa anapiga mahesabu yake vizuri,  alikua na ramani nzima ya jengo hilo la Black Site, ilikua rahisi kwake kujua ni wapi ataweka  kambi hapo juu ya paa ya Jengo, akafika mahali ambapo palikua na pambo kubwa la saa,  eneo hilo lilikua karibu na mlango Mkuu wa Kuingia ndani ya Jengo hilo, kando ya jengo  ndimo walimokua wakikaa makomandoo. 

Kwake hao ndiyo kikwazo kikubwa kufanikisha kazi ya Kumchukua Elizabeth, akaiweka  vizuri kofia yake kisha akalala kwa ustadi mzuri huku akilitazama jengo ambalo  Makomandoo walikua wakipatikana. 

Akaishusha Bunduki yake ya Masafa marefu kutoka ndani ya Begi lake kisha, akaitega vizuri  kuelekea kwenye jengo, kichwani alikua na ramani yote. Kitu pekee alichohitaji kukifanya  hapo ni kuufunga mlango wa Umeme ambao ndio uliokua ukitumika na Makomandoo hao,  mwendo wa dakika ishirini awe tayari ameshamchukua Mateka wake kwani kupambana na  Makomandoo hao haikua kazi rahisi kwake. 

Akafunga kiwambo cha kuzuia sauti, kisha akalenga kitasa cha Umeme ambacho  kingemfanya atenganishe kati ya Makomandoo na Walinzi wa kawaida wa Black Site,  umbali wa jengo hilo ni zaidi ya Mita sabini.

Dakika moja na nusu ilimtosha kujihakikishia kua risasi atakayoiachia hapo itaenda kukata  mawasiliano ya jengo la Makomandoo na jengo la Black Site. Akavuta hewa nyingi kisha  akaiachia taratibu na kukaza mikono yake kisha kidole kikafanya kazi ya kusukuma risasi  

Haraka Alam ikalia kuashilia kua palikua na hitilafu mlangoni, hii ni baada ya Muuwaji huyu  kukita risasi mlangoni. Haraka walinzi wa Black site pamoja na Makomandoo walio ndani ya  jengo lililopigwa risasi wakawa kwenye taharuki nzito, akasubiria kwa sekunde kadhaa ili  Mlango wa Black Site ufunguliwe, alipousikua umefunguliwa akajirusha mithiri ya Nyani  mzee 

Akatua chini kama Buibui, haraka akaachia pigo takatifu la Risasi za mahesabu na  kusambaratisha walinzi watatu waliokua eneo la Mlango kisha akaingia ndani ya Jengo hilo. 

Elizabeth aliposikia Alam ikilia kuashiria kuna tatizo alishaanza kuhisi ujio wa Mtu mbaya  ndani ya Jengo la Black Site, japo alikua amechoka sana lakini akaweza kumwambia Mlinzi  kua amfungue kwani eneo hilo siyo salama kabisa 

“Usipofanya hivyo Utakufa” akakazia Elizabeth huku akijitingisha kwa nguvu chache  alizobakiwa nazo, yule Mlinzi hakutaka kumwelewa Elizabeth hadi pale aliposikia risasi  ikisikika karibu na Mlango wa chumba cha Mateso ambacho Elizabeth alikua amehifadhiwa. 

“Nifungue tafadhali” alisema Elizabeth, lakini akili ya yule Mlinzi ikajikuta imezubaa  kidogo, ghafla akapigwa risasi ya Kichwa, kisha Mlango ukafunguliwa, akaingia Muuwaji,  akamtazama Elizabeth kisha akatoa tabasamu la kufanikisha kazi yake. 

Hakutaka kupoteza muda akamzimisha kwa kumchoma sindano ya Usingizi, akamfungua na  kumweka begani, maiti za Walinzi zilikua za kutosha sakafuni, akatoka hadi nje ya Jengo la  Black Site wakati huo Makomandoo wakiwa wanahangaika namna ya kufungua ule Mlango  wa Umeme ambao kwa kawaida hufunguka baada ya dakika ishirini endapo utapata Hitilafu. 

Akauvuka uzio wa Umeme kisha akaanza kuzikata Kilomita kuelekea lilipo gari lake aanze  safari ya kurejea Ikulu, mara zote alikua akiitazama saa yake kwa maana zikitimia dakika  ishirini wale Makomandoo watatoka ndani ya jengo na kuanza kumsaka kila kona. Akaianza  riadha baada ya kugundua kua alikua amebakisha dakika tatu kumalizika kwa ule muda  aliokua ameupangilia kulifanya tukio la kuvamia Black Site. 

Ndani ya jengo tayari makomandoo walishajiandaa kutoka huku wakisubiria muda muafaka  ambao Mlango huo wa umeme utakapokua umefunguka, Muuwaji alikua akikimbia na  Elizabeth aliyepoteza fahamu, akapandisha kilima kidogo lakini kwa Bahati mbaya akatereza  na kujikuta akimtupa Elizabeth ambaye akavingirika na kutumbukia kwenye korongo, kwa  Bahati nzuri akanasa kwenye Mti. 

“Shit!!” akasema Muuwaji, akaanza harakati za kutaka kumtoa Elizabeth, lakini kelele za  Makomandoo zikasikika, akatazama saa yake na kuona tayari muda ulikuwa umekwisha na  tayari Makomandoo walikua wakija kwa kasi mahali ambapo Muuwaji alikua amesimama. 

Kwanza akatafuta mahali na kujificha ili Makomandoo wasiweze kumwona, akaangalia risasi  zilizopo kwenye Bastola yake, kisha haraka akaenda mbali na eneo lile, akauzunguka mlima  mmoja na kwenda kujificha huko kisha haraka akaitoa Bunduki yake kutoka ndani ya Begi.

Akaielekeza eneo ambalo Elizabeth alikua ametumbukia, alikua akihema kutokana na  kukimbia kwa muda mrefu, Makomandoo wakalipita lile eneo kisha walipofika mbele  walitawanyika ili kumsaka kwa uzuri adui yao baada ya kugundua adui yao hakuitumia  Barabara ya vumbi bali alizama Msituni. 

Muuwaji akautumia Mwanya huo kuuzunguka Mlima mdogo na kisha kutokea nyuma ya  Makomandoo kisha akapiganisha akili namna ambavyo anaweza kumchukua Elizabeth  kutoka juu ya Mti ulio korongoni, mara akasikia mlio wa gari ukija kutokea Upande wa kulia  ambapo ndiyo palikua na njia ya kutoka Black Site, haraka akajitupa Korongoni na kutua  kwenye ule Mti ambao Elizabeth alinasia kisha kwa haraka akamsomba na kushuka naye  chini ambako palikua Na Msitu wa kutosha. 

Akajipigiza bega kwenye jiwe, kila mmoja akatua upande wake lakini hakuna Hata  Komandoo mmoja aliyeshtuka kua Adui yao alikua Korongoni, wenge zito likamzonga  Muuwaji akiwa anajitafuta, akayaruhusu macho yake kutulia, akamwona Elizabeth akiwa  mita kadhaa kutoka alipo yeye. 

“Agggghhh” akagugumia kwa maumivu makali huku akinyoosha bega lake, lililo jaa damu,  kisha akajisomba na kumsogelea Elizabeth. Akasimama na kuvuta hewa ya kujituliza vyema  halafu akaangaza juu 

Jua lilikua likiwaka, ndege wa Msituni walikua wakipiga kelele za hapa na pale, Purukushani  eneo la juu zilikua za kutosha kisha akajishika kiuno chake na kujinyoosha vyema, hakuishia  hapo akachana tisheti lake na kujifunga eneo la Bega, kisha akiwa amebakiwa na vest nyeusi  akajitwika Elizabeth, akaanza kuisaka njia ndani ya Msitu wenye giza. 

Haikua rahisi kwake kujua alikua akielekea upande upi kwasababu alikua ameshapoteza  mwelekeo sahihi, akajikuta akisambaa Msituni kwa muda mrefu hadi pale Helkopta za Black  site zilipoanza Msako kila kona ya Msitu. 

** 

Kelele za popo na sokwe zilianza kusikika ndani ya Msitu wa Magoroto, hatua kubwa za  vishindo zilimfanya Benjamin Kingai aliye ndani ya pango atoke, kwanza alikutana na  Zandawe akiwa amevaa nguo za ngozi za wanyama. Pili alikua ameongozana na kundi  kubwa la Popo waliozingira eneo la juu ili kumpa kinvuli. 

Tatu, alikua ameshikilia Mkuki aliouchomeka chini, vyote hivi vikamfanya Benjamin  ashangae, lakini tabasamu la kuchanua lilikua likiongezeka kwenye sura ya Malkia Zandawe.  Taratibu Benjamin alisogea karibu na Zandawe na kumuuliza kwa utaratibu 

“Kuna nini?” alihoji kwa sauti ya chini ili adokezwe lakini Malkia Zandawe akajibu kwa  sauti. 

“Leo ni siku ya Ukombozi Benjamin, siku ambayo unaenda kurudisha kila ulichokipoteza”  alisema kisha alikaa kimya, akamfanya Benjamin atupe swali jingine 

“Unamaanisha nini kusema kila nilichokipoteza?” akauliza Benjamin Kingai, kisha akameza  funda zito la mate huku kivuli cha wale popo ambao ndiyo jeshi la kuaminika la Malkia 

Zandawe likiwa linamsaidia pia Benjamin kuikimbia mionzi ya jua ambayo ilianza kua  Mikali. 

“Umepoteza familia, umepoteza haki ya kuishi ndani ya Nchi yako, pia Mtoto na Mpenzi  wako.” Benjamin akatoa tabasamu lenye Maswali mengi 

“Unamaanisha……” kabla hajamaliza kusema alikuja ndege mpelelezi wa Zandawe kisha  akatua chini na kusema kwa Lugha ya ndege kisha Zandawe akamjibu Benjamin 

“Eneo uliloteswa imevamiwa” alisema Kama vile Mtu aliyejua haswa anachosema, taarifa  zote alipewa na ndege wake mpelelezi, hii ilimshtua sana Benjamin akajawa na taharuki 

“Vipi kuhusu Mtoto na….” 

“Mpenzi wako” akadakika Zandawe kisha akasema 

“Inatupasa kwenda sasa hivi huko kujua kinagaubaga, huo uvamizi hatuna hakika unafanywa  kwa lengo gani, lakini yupo Msichana aliyetoroshwa huko” alisema Malikia Zandawe kisha  alisubiria jibu la Benjamin, kabla hajajibu chochote Benjamin akamtazama yule ndege kisha  akainama na kumwambia ndege huyo 

“Ahsante” aliposimama akamuuliza Malikia Zandawe 

“Tunafikaje huko?” 

Malikia Zandawe akatabasamu kisha akamjibu kwa kumwambia nifuate, aliposema alikua  tayari amegeuka na kuanza kutembea huku wale Popo wakimfuata kwa juu, akamsogeza hadi  eneo la wazi ambalo lilikua halina Miti kabisa ila lilizungukwa na Msitu mkubwa wa  Magoroto. 

Katikati ya eneo hilo palikua na kitu kilichofunikwa Majani mengi makavu, Malkia Zandawe  akasogea hadi hapo kisha akaanza kuondoa yale Majani yaliyokuaa yamerundikana,  Benjamin alipata Mshangao mkubwa baada ya kuona Helkopta ikiwa ndiyo iliyokua  imefunikwa hapo. 

Pale pale kabla hata hajamaliza kushangaa akaletwa Mtu mmoja aliyefungwa mdomo wake kwa kitambaa, aliletwa na Sokwe Mkubwa ambaye ni rafiki wa Malkia Zandawe, Mtu huyo  alikua na mavazi ya Urubani, alionekana wazi kua ndiye aliyekua rubani wa Helkopta hiyo. 

“Nitakuacha Huru ukinifikisha nitakapo” alisema Malkia Zandawe kisha akamtoa kitambaa  eneo la Mdomo.  

“Siyo Mtu mbaya, ila mmenifanya nimekua Mbaya kwasababu hamtaki kuuheshimu na  kufuata Misingi na mila za Msitu huu” alisema Malikia Zandawe 

“Naomba tafadhali, mateso niliyopata yametosha kua funzo kwangu, naomba niende  nitawaeleze ukweli kuhusu huu Msitu, naamani hakuna mwingine atakayetia mguu kwenye  huu Msitu.Alisema yule rubani huku chozi likimbubujika, Malkia Zandawe akainama na  kumwambia

“Nimeshakwambia kua sina ubaya na wewe, hamkutaka kusikiliza onyo langu, ukawe chanzo  cha wengine kuupa heshima huu Msitu” Alisema kisha aliposimama akamwambia 

“Naamini hili litakua funzo kubwa kwenu, sikutaka kukuuwa kwa maana nilikua na Uwezo  wa kukufanyia ubaya kama niliowafanyia wengine walioingia ndani ya Msitu bila kufuata  utaratibu. Kuna viumbe vinaishi humu, vinahitaji utulivu n amani kama ambavyo nyinyi kila  siku mnapigania” alisema Malikia Zandawe, kidogo akaanza kulengwa na Mchozi. 

Benjamin akamsogelea Malkia Zandawe na kumtuliza kwa kumshika bega, hata yule rubani  wa Helkopta ya Kijeshi aliona wazi kua Binti huyo alikua akizungumza kwa hisia kali iliyomuumiza. Malkia Zandawe akafuta chozi lake kisha akamwambia ndege wake mweupe  aongoze njia, akamtaka na Benjamin aingie ndani ya Helkopta hiyo pamoja na sokwe wake  ampendaye. 

Kitendo cha ndege kuruka kiliwafanya na Popo kuzama Msituni zaidi kwa kukimbia kwa  spidi kali kisha Benjamin, rubani, Malkia Zandawe na Sokwe wakaingia ndani ya Helkopta  hiyo tayari kuelekea ndani ya Black Site kuikomboa familia ya Benjamin Kingai. Dakika  tano baadaye Helkopta ikawa angani ikimfuata ndege mkubwa mpelelezi aitwaye Gola. 

Nini kitaendelea? 

Usikose SEHEMU YA ISHIRINI NA SABA

Mpe Nguvu ADMIN Kwa ajili ya bando Kwa kumtumia Chochote aendelee kupost MSALA Hapa Kijiweni

Lipa Namba: 57900454
Jina: LIPA KIJIWENI TIPS
Mtandao: VODACOM  

SOMA RIWAYA YA KOTI JEUSI KWA KUBONYEZA HAPA 

SOMA RIWAYA YA FUNGATE KWA KUBONYEZA HAPA 

SOMA RIWAYA YA NILIPANGA NYUMBA MOJA NA MAJINI 

SOMA RIWAYA YA GORYANAH HAPA 

SOMA KISASI CHANGU HAPA  

JIUNGE NIPO KIJIWENI Kwa Kubonyeza Hapa

MSALA xx MSALAxx MSALA xx MSALA xx MSALA xx MSALA xx MSALA xx MSALA xx MSALA xx MSALA xx MSALA xx MSALA

9 Comments

Leave A Reply


Exit mobile version