Ilipoishia “Benjamin yuko nje anatusubiria” kabla hata hajamaliza kusema alichokua amekikusudia,  zikasikika buti mlangoni, kisha Sauti ya risasi ikasikika, damu ikamwagika ikapenya chini ya  Mlango. Malkia Zandawe akaivuta bunduki yake na kuanza kujibu mashambulizi ya Risasi  za mfululizo.

Alipiga risasi nyingi mlangoni ili awatishe waliokua hapo waone sasa kua aliye ndani alikua  amejipanga, Malikia Zandawe hakujua nje kwenye korido palikua na Walinzi na  Makomandoo wa kutosha. 

Mwili wa rubani ulikua ni miongoni mwa miili iliyolala kando ya Mlango, Suzan alikua  mwingi wa kugumia kila aliposikia risasi zikilia… Endelea 


SEHEMU YA ISHIRINI NA NANE

“Unatakiwa kutulia ili tutoke hapa tukiwa hai, ukipiga kelele haisaidii zaidi itatufanya  tuangamie mapema zaidi” alisema Malikia Zandawe akiwa anapiga mahesabu namna ya  kutoka ndani ya chumba hicho. Chumba hicho kilikua na dirisha moja dogo lililo juu zaidi,  mahesabu hapo ilikua ni kulitumia dirisha hilo kuchomoka hapo. 

Haraka akaivuta meza iliyo jirani akaisogeza hadi eneo lilipo dirisha akapanda na kuangalia  kwa nje, bado chumba hicho kilikua katikati ya jengo la Black Site, yaani hata kama  watafanikiwa kuchomoka basi bado watakua ndani ya Black Site, lakini akili ya kwanza ya  Malkia Zandawe ilikua ni kuchomoka hapo 

“Sikia inabidi upite hapa kwenye dirisha, nitakukuta upande wa pili” alisema Malkia  Zandawe kisha akatumia kitako cha Bunduki kuvunja kioo cha dirisha hilo halafu akashuka  na kumpisha Suzan apande hapo, taratibu Suzan alianza kulipenya dirisha hilo lenye vipande  vya vioo vilivyoanza kumkata lakini alivumilia hadi alipodondokea upande wa pili, Zandawe  akiwa ndani ya chumba bado alianza kuhisi pua zake na macho vikiwasha sana, akagundua  kua tayari sumu ilikua imetupwa ndani ya chumba hicho kwa njia ya moshi. 

Akawafyatulia risasi kadhaa za kuwaaminisha kua yeye bado yupo ndani ya chumba hicho  kisha naye akapanda dirishani na kuchumpia upande wa pili akakutane na Suzan ili waanze  kutafuta namna ya kuchomoka hapo. 

** 

Maji yalikua yakifoka kwa sauti kubwa, yalikua yakiporomoka kutoka juu kuelekea chini  mbali sana. Muuwaji alikua amesimama hapo huku sauti za Mbwa zikizidi kusogea kwa kasi  kuashiria kua Walinzi wa Black Site walikua wakimfikia hapo, begani alikua amembeba  Elizabeth. 

Aliwaza afanye nini, kurudi nyuma ni sawa na kujikabidhi mikononi mwa Walinzi hao lakini  kusonga mbele ni kuyaweka Maisha yao hatarini kwani chini ni mbali mno na palikua na  mawe makubwa makubwa. Eneo hilo hakulifahamu, hapakua na dalili ya kuja kwa Msaada  kutoka kwa Waziri Mkuu Haji Babi, mara ghafla akiwa anatafakari ikasikika sauti nyuma  yake ikisema 

“Simama hapo hapo” ilikua ni sauti nzito ya Mlinzi wa Black Site aliye mbele ya kundi  kubwa la Askari. Mbwa walikua wakimfokea Muuwaji, kisha akaambiwa tena 

“Jisalimishe kwasababu huwezi kwenda popote umefika mwisho” Kauli hii ilimtia ghadhabu  Muuwaji, hakutaka kuishia mikononi mwa Walinzi hao pamoja na Makomandoo wa Black  Site, kwa vyovyote atauawa. Akapiga mahesabu mazito huku kwa siri sana akitazama namna  poromoko hilo lilivyo kaa.

“Geuka!” ikasema sauti ile tena kwa Msisitizo mkubwa sana, Muuwaji akajiweka sawa kisha  ghafla kila mmoja hakuamini alichokifanya, akadanda juu ya jiwe kisha akajiachia akiwa na  Elizabeth Begani, siyo tu walishangaa bali walikunja nyuso zao na macho yaliwatoka 

Mwanaume akashuka kwenye maporomoko akiwa anapigwa na Maji lakini hakutaka  kumwachia Elizabeth, kwa Bahati mbaya wakati wanashuka chini wakipigwa na yale maji,  Elizabeth akazinduka kutoka katikati ya Usingizi mzito wa sindano. 

Akajishuhudia akiwa kwenye bega akishuka chini kwa kasi ya ajabu. 

Upande wa pili ndani ya Black Site, Malikia Zandawe na Suzan walizidi kutafuta njia ya  kutoka ndani ya jengo hilo lililojengwa kistadi sana, walijikuta wakianza kupotea kwasababu  hawakua na ramani ya kuwatoa ndani ya jengo hilo lenye mfanano mkubwa kwa kila kitu  kuanzia korido hadi vyumba. 

Walijitahidi kukimbia lakini walihisi kama walikua wakizunguka ndani ya jengo hilo la ajabu  sana, nje ya jengo Benjamin pamoja na sokwe walikua wakimsubiria Malkia Zandawe atoke,  walijificha kwenye Bustani karibu na lango kuu ambalo waliamini Zandawe angetokea hapo. 

Muda ulizidi kwenda Upande wa Waziri Mkuu, mara zote alikua akijaribu kuwasiliana na  Muuwaji wake anayemtumainia ili kujua alipo kusudi kikosi maalum cha uokozi kimchukue  lakini alikua hapatikani kabisa. 

“Shit!” alisema Waziri Mkuu Haji Babi, kisha akawaita Washirika wake waliobakia,  akawaambia kua waandae taarifa ya kifo cha Rais Lucas Mbelwa ili masaa 24 baadaye  aapishwe kua Rais wa Tanzania kama katiba inavyotaka, alihitaji kuapishwa haraka ili  asimame kama Rais na asiweze kuguswa na Mamlaka yoyote endapo nyaraka M21 itavuja.  

Alihisi dalili mbaya kua Muuwaji wake alikua amenaswa, ikafanyika hivyo. Taarifa rasmi  ikaruka kwenye runinga ya Taifa kua Rais Mbelwa alishambuliwa na kuuawa akiwa Ikulu,  baada ya kurusha matangazo alisubiria kusikia namna taarifa hiyo itakavyopokelwa na wengi 

Pale pale akavuta simu na kumpigia Mwanasheria Mkuu wa Serikali ili aandae nyaraka  maalum za uapisho. 

** 

Helkopta zilizidi kuranda randa juu ya Msitu kuwatafuta Elizabeth na Muuwaji, Elizabeth  alikua wa kwanza kurejesha ufahamu baada ya kuanguka kwa kasi kwenye maji, alijikuta  akiwa amesukumwa na Maji hadi eneo kavu la Bonde. 

Sauti za mbwa zilikua zikisikika kuashiria kua Msako ulikua ukiendelea ndani ya Msitu huo,  kumbukumbu zake zilimwambia kua mara ya mwisho alikua na Mtu wakianguka kwa  pamoja 

“Yule Mtu yuko wapi?” alijiuliza huku akiwa anageuka huku na kule, alichokiona kilikua ni  begi la yule Muuwaji, begi hilo lilikua na Bunduki ya Masafaa marefu na darubini, akajiokota  taratibu

Kisha kwa mwendo wa kupepesuka alisogea karibu na Begi, alipofika hapo ndipo  alipomwona Mwanaume aliyekua akianguka naye yaani yule Muuwaji, alikua amepasuka  vibaya kichwani huku damu nyingi zikiwa zimemtoka akiwa amefichwa na jiwe moja kubwa. 

Hakumjua Mtu huyo lakini alijua kua alikua akimsaidia kutoroka ndani ya Black site,  akasogeza gauni lake na kufungua chupi, akaiyona Flashi yenye nyaraka M21. Kisha  akairudisha ndani ya chupi lakini hata kabla hajafanya chochote walitokea makomandoo  kutoka Black site. 

Dakika moja tu akawekwa chini ya ulinzi na moyo wake ukamripuka kwa hofu na wasiwasi  ukizingatia alikua mchovu kutokana na Mateso ndani ya Black Site, akaamriwa kupiga  magoti ili anaswe. Taarifa za Elizabeth ziliwafanya Makomandoo kua makini naye kwani  naye alikua na mafunzo kama yao. 

Taratibu Elizabeth alipiga goti kwa maumivu makali ndani ya moyo wake, tumaini la  kuondoka likawa linafia hapo mbele ya Makomandoo, kisha ikapigwa simu ili Helkopta  ishuke kwa ajili ya kumchukua Elizabeth. Makomandoo kumi na tano walikua  wamemzunguka Elizabeth. 

Ghafla Komandoo mmoja akaanguka, damu ikaruka kama Kuku aliye chinjwa, wakiwa wana  tahamaki ikaja mvua ya Risasi zilizokua zikipigwa kwa mahesabu makali eneo la shingo la  Kila Kimandoo. Mpigaji alipiga risasi sawa na idadi ya Makomandoo na kuwaangusha,  akambakiza Elizabeth tu ambaye alikua mwenye wasiwasi. 

Kwakua Elizabeth alikua na mafunzo maalum ya Kijeshi alijua ni wapi risasi hizo zilitoka,  akageuka kutazama Juu ya kilima kimoja akamwona Mtu mmoja aliyevalia nguo za Njano na  kofia akishuka kwa spidi kali kama Kipanga mwenye mpango wa kunasa Kifaranga. 

Hakua na Wazo la kwenda popote alisimama akimtazama Mtu huyo aliyeshikilia Begi ndefu  linalohifadhi silaha aliyoitumia, hadi anafika chini Elizabeth aligundua Mtu huyo alikua  amevalia kinyago cha Simba, akatetemeka na kuanza kurudi nyuma ili ajihami huku akipiga  mahesabu ya kuokota Bunduki moja ya Komandoo aliye jirani. 

Mtu huyo alimfikia Elizabeth kisha akamnyooshea Bunduko na kumuuliza 

“Iko wapi nyaraka M2?” alihoji kwa sauti nzito isiyo ya kawaida, Elizabeth aligundua Mtu  huyo alikua akifahamu mengi kuhusu Faili hilo na alikua akimfwatilia kwa kila Hatua, alizidi  kutetemeka kwa hofu, kisha Mtu huyo Mwanaume akavua Kinyago. 

Elizabeth hakuamini macho yake, Mtu huyo alikua ni Muhonzi, tabasamu lililoambatana na  machozi likamtoka Elizabeth 

“Umejuaje niko hapa?” Aliuliza Elizabeth, Muhonzi akatoa rimoti fulani mfukoni iliyo  mwashilia Elizabeth kua aliwekwa kifaa maalum cha GPS, Kisha muhonzi akamnyooshea  kidole Elizabeth eneo la chini akimaanisha pale alipoificha Ile flashi ndipo Elizabeth  alipogundua kua Muhonzi alitega GPS kwenye ile flash, kwa furaha alimkumbatia Muhonzi  huku chozi likimtoka.

Uchovu wote ukamwisha Elizabeth, sauti ya Helkopta ikasikika kwa juu kisha mvua ya  Risasi ikaanza kuwaandama, haraka Elizabeth na Muhonzi wakakimbilia kwenye mawe  makubwa kujificha. Elizabeth akaichukua Bunduki kutoka kwenye begi la Muhonzi 

Utaalam wa kulenga haukua tatizo kwake, akaiweka vizuri Bunduki hiyo kisha akamlenga  rubani wa Helkopta hiyo iliyo juu ikizidi kuwaandama kwa risasi za Mfululizo, akatuliza  akili yake kisha akamwambia Muhonzi 

“Kimbia” Bila hata kuuliza Muhonzi alijua nini ambacho Elizabeth alikua akikitaka kutoka  kwake, alitaka kumtoa Muhonzi chambo ili amdungue rubani kwa Urahisi zaidi, kweli  Muhonzi akachomoka hapo akipandisha mlima. Ile Helkopta ikabadili mpango na kuanza  kumwandama Muhonzi kwa risasi za kutosha ambazo zilikua zikimkosa 

Haraka Elizabeth akasimama na kuiweka Bunduki juu ya jiwe kisha haraka akaachia Pigo la  Mwana Ukome, akapiga Risasi moja na kusambaratisha Watu wawili, mmoja alikua ni  Mdunguaji aliyekua akimshambulia Muhonzi na wa pili ni Rubani, kisha Helkopta ikapoteza  uelekeo na kujikuta ikienda mrama kisha ikaaguka na kulipuka, Muhonzi akatoa tabasamu  pana kuashiria kua alikua akimkubali sana Elizabeth kwenye Mission za kivita. 

Haraka Muhonzi akashuka Mlimani 

“Tunafanya nini sasa?” akauliza Muhonzi 

“Nyaraka M21 haiuziki tena sababu kila kitu kimegeuka, tunasakwa kila kona bila faida  yoyote ile. Tutoke hapa Msituni kwanza lakini nataka turudi ndani ya jengo nililokua  nimehifadhiwa, nafikiria kuna vitu tunapaswa kua navyo”  

“Ulihifadhiwa wapi?” 

“Nafikiri ni kambi ya siri ambayo sikuwahi kuijua, nimefanya Ujasusi mwingi lakini sikupata  kufikiria kama kuna kambi ya siri ndani ya huu Msitu” 

“Hiyo kambi iko wapi?” 

“Juu ya haya maporomoko, nakumbuka ndipo tulipotokea. Yatupasa kua makini sana  Muhonzi sababu siyo sehemu rahisi, panaonekana kua na siri nyingi za kutisha” akasema  Elizabeth kisha wakaziokota Silaha zilizo watosha kuelekea Black Site. 

Haraka wakaanza kuupandisha mlima mrefu wenye mawe makubwa kuelekea juu ambako  ndiko iliko Black Site. 

** 

“Nimechoka siwezi kwenda mbele” alisema Suzan baada ya kukimbia kwa muda mrefu bila  mafanikio ya kuiyona njia. 

“Ukichoka utafia ndani ya jengo hili, nafikiri ni mita kadhaa kuelekea nje ya jengo, hatuna  Budi bali kusonga mbele”

“Lakini tunakimbia bila kujua tunaelekea wapi” alisema Suzan, ghafla risasi zikaanza  kusikika zikiwafwata tena kwa kasi sana, Suzan mwenyewe akajiokota na kuanza kukimbiza  Maisha yake, Malkia Zandawe hakutaka kuwa mnyonge akaanza kujibu mapigo kuelekea  walipo Walinzi na Makomandoo wa kambi hiyo ya Black Site. 

Wakajibanza mahali kwa ajili ya mviziano mkali wa risasi, eneo walilojibanza lilikua ni  chemba ya kuhifadhia vifaa, kulia na kushoto Walinzi walikua wakisogea na wote walijua ni  wapi ambapo Zandawe alikua amejificha. 

“Sikia, kosa lolote hapa tunakufa” alisema Zandawe huku akiangalia kiasi cha Risasi  kilichobakia, kilitosha kupambana na Walinzi lakini aliona ugumu wa kukabiliana na walinzi  hao wote kwa Mara moja. Sauti za Buti zilisikika kinyemera kuashiria walikua jirani 

Kabla hata Zandawe hajatupa pigo lolote zikasikika risasi za kutosha chini ya dakika moja  pakawa kimya kabisa kisha Sauti za Watu wawili zikasikika 

“Nafikiri ni kule mbele japo sina kumbukumbu sawa sawa” sauti hiyo ilikua ya Elizabeth,  kisha wakawa wanataka kuelekea mbele, ghafla Zandawe akajitokeza na kuwaweka chini ya  Ulinzi Muhonzi na Elizabeth. 

“Weka silaha zenu chini, nyinyi ni akina Nani?” akauliza Malkia Zandawe, Muhonzi na  Elizabeth wakatupa Bunduki zao kutii agizo la Zandawe. Kisha wakatazamana, machoni pa  Zandawe Watu hao hawakuonekana kua ni Wanajeshi wa kambi hiyo 

Suzan alipomtazama vizuri Elizabeth alimkumbuka kwa haraka sababu picha ya Msichana  huyo aliwahi kuoneshwa. 

“Wewe ndiye Elizabeth si ndiyo?” akahoji huku akiwa anamtazama kwa Makini, hata  Elizabeth alishangaa Mwanamke huyo amemjuaje. 

“Ndiyo, umenijuaje?” 

“Niliona Picha yako, Benjamin yuko wapi?” akahoji 

“Huyu ndiye aliyemwingiza Benjamin kwenye huu Msala” alisema Suzan akimwambia  Malkia Zandawe, pale pale Zandawe akashusha Bunduki maana Simulizi hiyo aliwahi  kuisikia kutoka kwa Benjamin, akajua Msichana huyo hakua Mbaya. 

“Nafikiri kwasasa tufikirie namna ya kutoka ndani ya Kambi hii kwanza” akasema Zandawe,  hakutaka maongezi zaidi lakini hapo hapo wakasikia kiashiria cha Bomu kubwa  linalotarajiwa kulipuka baada ya dakika tatu, kisha Milango ikaanza kujifunga 

Taharuki ikawa kubwa, wakaanza kurudi nyuma ambako Elizabeth na Muhonzi walitokea ili  waweze kuikwepa hatari iliyo mbele yao, joto likawa linazidi kua kali ndani ya jengo hilo, na  hapakua na Mtu yeyote aliye hai zaidi yao ndani ya jengo 

Walinzi na Makomandoo walikua wameuawa vya kutosha, walifika hadi lango la kutoka  ndani ya jengo lakini Mlango huo wa umeme ulikua umefungwa, walijaribu kuusukuma  lakini Mlango huo haukufunguka, wakaanza kuita huku wakiangalia nje kwa kutumia vioo 

vizito vilivyo eneo hilo lakini hawakumwona yeyote yule hata Benjamin na Sokwe  hawakuwepo hapo. 

“Tunafanya nini?” akauliza Muhonzi huku dakika zikiwa zinayoyoma, jesho likawa  linawatoka. 

“Huu ndiyo mlango pekee ambao tunaweza kuutumia kwa haraka kutoka humu, lakini  umefungwa unafikiria tunafanya nini?” akauliza tena Muhonzi akiwa anasubiria majibu, kila  mmoja alichanganikiwa na hapakua na jibu lolote lililotoka, wakajaribu kutumia Bunduki  kuuvunja Mlango huo lakini haikuwezekana 

Dakika zikawa zinazidi kwisha huku joto kali likizidi kuongezeka, Zandawe akaona ni bora  amwite Gola hapo, akamwita kihisia. 

Naaam!! 

Gola akafika nje ya jengo, akampa maagizo ya hisia amtafute Sokwe alipo ili aje kuwasaidia,  kila mmoja alimshangaa Zandawe ni Mtu wa aina gani, iliwafikirisha sana lakini kwao  muhimu ilikua ni kutokana ndani ya Black Site. 

Haraka Sokwe alifika hapo akiwa ameongozana na Gola muda uliobakia ulikua ni dakika  moja tu ya kuhesabu, Sokwe akawa na kazi ya kuhakikisha anauvunja mlango kutokea kwa  nje ili wao watoke, akawa anasukuma kwa nguvu zake na kuanza kuutikisa mlango huo wa  umeme ulio anza kutoa shoti. 

Sekunde zikiwa zinayoyoma, ghafla Helkopta tatu zikawa mbele ya Mlango huo tayari  kushambulia ili asitoke yeyote, Sokwe akachanganikiwa, kila mmoja akashikwa na Butwaa.  Katika hali ya kustaajabisha kundi kubwa la Popo likszivamia Helkopta na kuanza  kuwashambulia wanajeshi walio ndani yake. 

Sokwe akaendelea kuusukuma mlango hadi akauvunja, wote wakatoka huku Helkopta zikiwa  katika purukushani nzito za wale popote wanaokula nyama za watu.  

“Nani anajua kuendesha Helkopta?” akauliza Zandawe, Suzan alikua ni rubani pia hivyo  kwake haikua kazi ngumu, akaingia ndani ya Helkopta iliyokua mbele ya jengo kisha  wakazama wote na kuanza kuitoa Helkopta hiyo, ikafika usawa wa juu ndipo Zandawe  alipokumbuka kua Benjamin hakuwamo ndani ya Helkopta. 

“Benjamin” akasema, kila mmoja sasa akatambua kua kuna aliye sahaulika, kweli  walipotazama kwa chini walimwona Benjamin Kingai akiomba Msaada, wakati huo jengo  likianza kulipuka 

Ikawa ngumu kwa Helkopta kushuka chini kumchukua Benjamin kutokana na moto mkali,  ikawalazimu kupanda juu zaidi ili kuukwepa moto Mkubwa uliokua ukiwaka kutokana na  Mlipuko wa Majengo yote ya Black Site. Chozi lilimbubujika Zandawe, Suzan naye  alidondosha chozi, waliamini Benjamin atakua amefia kwenye ule moto 

“Tuondoke” alisema Elizabeth akiwa anasikitika kumpoteza Benjamin, Helkopta ikabadili  uelekeo ili kuondoka huku Zandawe akiwaongoza ni Wapi wanapaswa kuelekea, alihitaji  kurudi kwanza kwenye Msitu wa Magoroto.

Katika hali ya kustaajabisha, wakiwa wanaamini Benjamin amefia kwenye Mlipuko  walimwona akiwa juu ya ndege Mkubwa aitwaye Gola, tena Gola akiiongoza Helkopta hiyo  kurudi Magoroto, tabasamu lililojaa huzuni na maumivu liliwajaa wote.  

Benjamin aligeuka na kumtazama rubani Suzan kisha akatabasamu akiwa amejishikiza juu ya  Ndege Gola. Jua lilikua likianza kuzama 

** 

Wakati giza linaingia, Helkopta ndiyo ilikua ikiingia Msituni Magoroto Tanga, wasiofahamu  eneo hilo walistaajabu kuona Bado wanatua Msituni lakini Zandawe aliwaambia 

“Naitwa Zandawe, Mimi ndiye mmiliki wa huu Msitu. Najua mnahitaji kupumzika, kesho  mtaendelea na safari yenu” alisema 

“Zandawe?” alihoji Elizabeth. Hadithi ya Msichana huyo aliwahi kuisoma kwenye kitabu  kimoja cha Hadithi za Watoto lakini hakujua kama ilikua ni Hadithi iliyomhusu Mtu aliye hai tena alikua akiishi hapo hapo Magoroto. 

Basi waliingia pangoni wakiwa wenye kustaajabu, wakapata chakula Usiku huo kisha  Zandawe akawauliza 

“Mna mpango gani?”  

“Kuzuia mapinduzi na Utawala wa kidharimu” alidakia Muhonzi, kisha alisimama na kuwapa  taarifa kua tayari Rais Mbelwa alikua ameshauawa na Mtu anayetarajiwa kushika hatamu ni  waziri Mkuu Haji Babi ambaye ataapishwa siku ya kesho yake. 

“Kama ni hivyo ni lazima siri hizi zilizo ndani ya Flash zianikwe hadharani ili kuuzuia  mpango wake” alisema Elizabeth. 

“Unafikiria ni rahisi?” akauliza Zandawe 

“Najua, lakini nilipotoka na huu mpango hadi nilipofikia siwezi kukubali kupoteza nguvu  bure. Lazima mpango wa mwisho ufanye kazi” alisema Elizabeth.  

“Vipi kuhusu Mtoto wako Benjamin?” akauliza Zandawe 

“Nina hakika yupo salama, nahisi hakuwamo ndani ya lile jengo, kama kumuuwa wangeanza  na Suzan” alisema Benjamin, basi wakatazama tu. 

**  

Uapisho wa Rais Mpya kikatiba ulianza baada ya mapambazuko kama katiba ilivyokua  ikitaka, Waziri Mkuu ndiyo mwenye kushika hatamu. Alihitaji jambo hilo kufanyika mapema  zaidi akiamini bado zile nyaraka zinaishi mikononi mwa Msichana Elizabeth, akajiandaa siku  hiyo huku akipongezwa na Watu wake wa karibu kua anaenda kua Rais muda mchache ujao.

Ulinzi ukaimarishwa kila kona ya Jiji kuhakikisha panakua salama zaidi, Nchi nzima kila  mmoja alikua akifwatilia matangazo kwa njia ya Redio, Televisheni hata Mitandao  mbalimbali. 

Waziri Mkuu akaondoka na Msafara wake kutoka Ikulu kuelekea eneo la uapisho akiamini  mambo yanaenda kua mazuri muda machache Ujao, wakati yeye akielekea eneo la Uapisho. 

Msitu wa Magoroto palikua na safari ya Helkopta iliyotarajiwa kuanza dakika kadhaa tu,  Malkia Zandawe akawaaga Elizabeth, Benjamin, Muhonzi na Suzan ambao wao  walikubaliana kurejea Dar-es-salaam kuzuia uapisho 

“Naamini mtafanikiwa, Benjamin asante kwa kumbukumbu nzuri” alisema Malkia Zandawe  akiwa anatabasamu, Benjamin akasogea na kumpa kumbato Zandawe akamwambia 

“Tutaonana tena Malkia” kisha aliachia Tabasamu, safari ya kuelekea Kwenye Helkopta  ilifwata kisha Zandawe aliwaaga kwa huzuni, hatimaye Helkopta ilipaa kuelekea Dar-es salam. 

** 

MBIVU NA MBICHI 

Idadi kubwa ya Wanajeshi ilijitokeza kwenye Uapisho huo ulioteka macho na masikio ya  wengi. Waziri Mkuu Haji Babi alifika eneo hilo akiwa amevalia suti, alifika akiwa na  msafara wa Magari sita meusi, magari mengine yalikua na walinzi wake maalum  aliowaandaa  

Baadhi ya viongozi walikua hapo kushuhudia tukio hilo ambalo lilihudhuriwa na wanajeshi wengi wenye Silaha. Hotuba fupi ikatolewa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali ambaye  alipewa vitisho vya kutosha na Waziri Mkuu Haji Babi, alikuwa mwoga na mwenye  kutetemeka na kutokwa na jasho wakati anatoa maelekezo ya kisheria ni Nani atavaa viatu  vya Urais 

Baada ya Kumaliza, alishuka na kwenda kuketi huku akishushia na maji mengi, Waziri Mkuu  alitabasamu huku akiamini kila jambo linakwenda sawa sawa, akapanda Waziri kula kiapo  cha Utii, alipomaliza alitia saini nyaraka kisha Mtu wa Mwisho alikua ni Mwanasheria mkuu  wa Serikali. 

Naye Mwanasheria Mkuu akapanda na kupewa nyaraka atie saini. Alionekana kusita kufanya  hivyo 

“Fanya haraka tia Saini” alisistiza Waziri Mkuu akimwambia kwa sauti ya chini 

“Unajua unachokifanya siyo kitu sahihi, hulioni hilo?” akauliza Mwanasheria kwa sauti ya  chini pia, ni wawili tu ndiyo waliokua wakisikilizana hapo hakuna mwingine aliyekua  akisikiliza. Eneo hilo la kiunga lilikua tulivu sana kila mmoja akisubiria hatua hiyo ya  mwisho. 

“Unasubiria nini?” akahoji Waziri Mkuu akijikuta anaanza kutahamaki, ghafla ikasikika sauti  ya Helkopta, wote wakaiyona Helkopta ya jeshi inashuka. Walikua kimya wakitaka kujua 

Jeshi walikua na lengo gani kuja hapo, akageuka na kumtazama mmoja wa wakuu wa  Majeshi kisha akarudisha macho yake mbele 

“Tia saini haraka” akasema Waziri Mkuu, Mwanasheria akamwambia Waziri Mkuu. 

“Nitakachofanya kitagharimu Maisha ya wengi kwa muda mrefu, kizazi na kizazi. Sitaki kua  sehemu ya Laana hiyo” kisha akachana nyaraka hizo huku Viongozi wakisimama na  kushangaa, Mwanasheria akavuta Maiki ili aongee lakini pale pale akapigwa risasi na  Walinzi maalum wa Waziri Mkuu, tafrani ikawa nzito kati ya Wanajeshi na Walinzi maalum  wa Waziri Mkuu. 

Risasi zikarindika huku wakihitaji kumtoa Waziri Mkuu baada ya kuona mambo yanaanza  kuharibika, Elizabeth na Muhonzi ndiyo waliokua na jukumu la kufichua taarifa zile za siri.  Wakati purukushani zikiendelea, Elizabeth akakimbilia jukwaani kumtafuta Mtu mmoja  aliyekua akimfahamu 

Akamkuta Mzee Mmoja ambaye alikua ni Mshauri wa Masuala ya Kisiasa, Mzee huyo alikua  akimfahamu Elizabeth kiundani, kisha Elizabeth akampatia Flashi Mzee huyo. 

“Tafadhali ondoka hapa na hiyo Flash, utakachokiona humo ndiyo silaha nzito ya kumaliza  yote haya. Ukiamua kukaa kimya ni wewe na ukiamua kusema kwa ajili ya Taifa ni wewe,  Nakuamini” alisema Elizabeth kisha aliondoka hapo na kumwacha Mzee huyo na Maswali  mengi sana, kisha akaingia kwenye mpambano wa kuwasaidia jeshi kupanmbana na waziri  Mku ambaye alijiandaa kushinda mpambano huo 

Pamoja na uwingi wa Wanajeshi hapo lakini Waziri Mkuu alitimka na gari moja nyeusi huku  akiwaacha Walinzi wake waendeleze vita ili yeye aikimbie Nchi mana sri zake zikishatoka  atasakwa na Mamlaka kama Muasi. 

Dakika kadhaa tu Walifanikiwa kuwazimisha Walinzi wote wa Waziri Mkuu, sasa kibao  kikamwangukia Elizaberh maana tayari Mamlaka zilimtambua kama Gaidi, akakamatwa ma  kuondolewa hapo kwa ulinzi Mkali sana. 

Muda huo, Muhonzi, Benjamin, na Suzan walikua wameshalikimbia eneo hilo wakimfukuzia  Waziri Mkuu kujua alikua akielekea wapi. Nusu saa baadaye Nyaraka M21 ilianza kusambaa  kila kona na kuzua gumzo kubwa sana. 

Siri nyingi za viongozi zilivuja kwa kasi akiwemo Marehemu Rais Mbelwa na washirika  wake, hata siri za Waziri Mkuu nazo zilikuwamo ndani ya Nyaraka M21. Upekuzi mkubwa  ukafanyika Ikulu na kugundua palikua na miili mingi eneo la siri la mateso ndani ya Ikulu,  hata Mke wa Rais Mbelwa alikutwa kwenye moja ya vyumba 

Akatoboa siri ya Waziri Mkuu kumuuwa Rais Mbelwa, kuanzia hapo sasa Msako wa  kumsaka Waziri Mkuu ulianza. Muhonzi akatoa siri ya wapi alipo Waziri Mkuu, akavamiwa  ndani ya makazi yake ya Siri akiwa anajiandaa kutoroka. 

Viongozi wote waliokuwamo ndani ya Nyaraka M21 walinaswa haraka sana na Mamlaka  husika, Elizabeth akiwa katika kituo cha Polisi ilitoka amri ya kumwachia, amri hiyo  ilitolewa na Mshauri wa Kisiasa ambaye ndiye aliye zivujisha Nyaraka.

Elizabeth hakua na kesi ya Kujibu, kutokana na Msaada alioutoa kwa Serikali ya Tanzania,  Elizabeth na timu yake wakapewa kiasi kikubwa cha pesa kama shukurani kwa kazi hiyo  nzito ya kulikomboa Taifa, wakapanga safari ya kuelekea Nchini Moroco kama sehemu ya  Mapumziko lakini kabla hawajaondoka Elizabeth alihitaji Kummaliza Zagamba Mtu  aliyewageuka dakika za mwisho. 

HITIMISHO 

Baada ya kuvuja kwa zile nyaraka Zagamba alianzisha mijadala kwenye mitandao ya  Kijamii, akaonesha hadi picha alizopiga na Elizabeth kama Ushahidi kua alikua nyuma ya  Mpango huo, alifanya hivyo siyo kwamba alikua anajisafisha tu bali alihitaji kupata nafasi  ndani ya Serikali kupitia chama chake cha TUYTA 

Usiku Mmoja aliwaarika marafiki zake nyumbani kwake, naye alitajwa kua mmoja wa Watu  waliosaidia kuvuja kwa Nyaraka M21, walikunywa na kufurahi pamoja Usiku huo. 

Hakujua kua Usiku huo ulikua ndiyo Mwisho wa Maisha yake, Mtoa roho alikua amesimama  kwenye korido akimsubiria Amtoe roho, Elizabeth alikua hapo akiwa amevalia Mask 

Kama kawaida ya Pombe ilivyo, Mkojo ni kitu cha kawaida sana, wengi walipta hapo  Elizabeth akiwa amejificha akimsubiria mlengwa wake, alipopita Zagamba akiwa amelewa  alimfuata huko huko chooni, akamtokea kama Mzimu kwenye kioo, Zaganba alipogeuka  alimwona Mtu akiwa amevalia Mask 

“Nani wewe?” aliuliza Zagamba huku pombe ikianza kutoka. Elizabeth akatoa Mask 

“Hatimaye tumekutana tena baada ya usaliti ulioufanya kwetu” alisema Elizabeth, pale pale  Zagamba akataka kumshambulia Elizabeth kwa kutumia koki ya maji yenye waya lakini  Elizabeth alimwonesha Zagamba ufundi alionao, akajizungusha kisha akaikwepa halafu  akaidaka na kuizungusha waya wa koki shingoni, kwa spidi ya ajabu akamnyonga Zagamba  kwa kutumia waya huo hadi kufa. 

Kisha akavalia Mask yake kisha akaondoka kwenye Makazi hayo, nje alikua akisubiriwa na  Muhonzi, Benjamin, Mtoto wa Benjamin, pamoja na Suzan ambao walikua ndani ya gari 

Kila mmoja alijua wanaenda Moroco kupumzika lakini Elizabeth aliwaambia 

“Naenda kuishi Magoroto kufurahia Rasilimali za Nchi yangu” alisema kila mmoja  alistaajabu, katika hali isiyo ya kawaida wakajikuta wote wakikubaliana kwenda kuishi  Msituni na Malkia Zandawe kama sehemu ya Mapumziko yao. 

MWISHO

Ahsante Kwa Kuwa Na Mimi Mwanzo Mpaka Mwisho Wa RIWAYA Hii Ya MSALA kuanzia Season 1, Season 2 na hii SEASON 3. Comments zikiwa nyingi tunaanza riwaya mpya kesho

Mpe Nguvu ADMIN Kwa ajili ya bando Kwa kumtumia Chochote aendelee kupost RIWAYA Hapa Kijiweni

Lipa Namba: 57900454
Jina: LIPA KIJIWENI TIPS
Mtandao: VODACOM  

SOMA RIWAYA YA KOTI JEUSI KWA KUBONYEZA HAPA 

SOMA RIWAYA YA FUNGATE KWA KUBONYEZA HAPA 

SOMA RIWAYA YA NILIPANGA NYUMBA MOJA NA MAJINI 

SOMA RIWAYA YA GORYANAH HAPA 

SOMA KISASI CHANGU HAPA  

JIUNGE NIPO KIJIWENI Kwa Kubonyeza Hapa

MSALA xx MSALAxx MSALA xx MSALA xx MSALA xx MSALA xx MSALA xx MSALA xx MSALA xx MSALA xx MSALA xx MSALA xx MSALAxx MSALA xx MSALA xx MSALA xx MSALA xx MSALA xx MSALA xx MSALA xx MSALA xx MSALA xx MSALAxx

27 Comments

  1. Big up admin👊🏼 Story n ya moto sana 😂😂nmecheka elizabet amezima alafu anazinduka yupo hewan anaanguka😂 ah unaeza ukazimia tena huko huko hewan aniii😁 admin umetisha sana sanaaa🔥🙌

  2. Kubababake!!!!!!!!

    Sijawahi kusoma riwaya yenye action zinazoonekana kama hivi hakika ndugu Mwandishi umenikosha

    Kongore kongore kongore kongore kongore kongore kongore kongore kongore kongore

    Stress free zone

Leave A Reply


Exit mobile version