Mchezo wa mpira wa miguu nchini Tanzania umekua ni moja kati ya kitu ambacho kinawakutanisha watu wengi sana kwa wakati mmoja na kuweza kushuhudia mchezo wenyewe lakini pia na kujadiliana kuhusu mambo mbalimbali kabla na baada ya mchezo husika kuisha.

Kuwa kwake moja ya kitu ambacho kinapendwa na watu wengi basi mchezo huu umegeuka kuwa kama njia mojawapo ya wanasiasa kutumia mwanya huo kama njia mojawapo ya kuonesha namna ambavyo wanatoa hamasa katika mchezo huo au kupenyeza agenda zao za kisiasa.

Uwepo wa wanasiasa katika mpira wa miguu sio kosa, shida hutokea pale ambapo kupitia namna ambavyo wanajishughulisha na michezo katika njia ambayo wanakua wanawapa presha wachezaji kwani ni hii baada ya kutembelewa na wanasiasa wengi makambini huko lakini pia katika viwanja vya mazoezi.

Siku zote tunatakiwa kufahamu kuwa Mpira sio siasa za kutaka kutafuta watu watakaokupigia kura baadae bali mpira ni uwekezaji mkubwa sana ndio maana yapo mataifa ambayo zamani yalikua yanafungwa sana na Tanzania lakini wao waliamua kuweka siasa pembeni na kufanya uwekezaji.

Uwekezaji katika soka la Tanzania unaweza kuleta mabadiliko makubwa, si tu katika uwanja wa michezo bali pia katika uchumi wa nchi. Kwa kuvutia wawekezaji, kuboresha miundombinu, na kuhakikisha maendeleo ya vijana, tunaweza kuleta soka la Tanzania kwenye jukwaa la kimataifa. Kwa pamoja, tunaweza kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha michezo, uwekezaji, na mafanikio ya kitaifa.

Tusidanganyane kwa matokeo ya nchi nyingine katika michuano hii wakati tunafahamu namna ambavyo nchi kama Morocco imefanya uwekezaji mkubwa katika soka la nchi yao na mpaka hapo walipo sasa.

Morocco imefanya uwekezaji mkubwa katika soka la nchi yao ambapo wameweza kuchukua hatua mbalimbali kwa lengo la kuimarisha miundombinu, kuendeleza vipaji vya vijana jambo ambalo limewapa mafanikio katika medani ya kimataifa.

Ukianzia katika suala ambalo linatusumbua sisi kama Tanzania ni miundombinu na viwanja wakati wenzetu wao wamewekeza sana katika ujenzi na ukarabati wa viwanja vya michezo na miundombinu inayohusiana na soka. Wamefanya ukarabati wa viwanja vya zamani na kujenga viwanja vipya vya kisasa, hivyo kuwa na uwezo wa kuandaa matukio makubwa ya kimataifa. Viwanja kama vile Stade Mohammed V huko Casablanca vinaonyesha dhamira ya Morocco kutoa mazingira bora kwa michezo.

Ukuaji na matumizi yao ya vijana katika michuano mbalimbali umepelekea kukua zaidi kwa soka lao kwani wameanzisha akademii za Soka kote nchini kwa lengo la kugundua, kukuza, na kutoa mafunzo bora kwa vipaji vya vijana. Akademii hizi zinatoa fursa kwa wachezaji wa vijana kuendeleza ujuzi wao, kutoa mazingira bora ya mafunzo, na kuwawezesha kushiriki katika mashindano ya kimataifa. Hapa ni kuonesha namna gani wameacha Sias ana kukimbilia uwekezaji wa soka.

Kupitia uwepo wa wawekezaji Morocco imechukua hatua hii muhimu kuboresha na kuendeleza ligi yao ya soka na vilabu. Kwa kushirikiana na wawekezaji wa ndani na wa kimataifa, wamefanya juhudi za kuimarisha ushindani wa ligi na kutoa motisha kwa vilabu kufanya vizuri katika mashindano ya ndani na kimataifa.

Wakati sisi tukiwa tunaendelea kujitafuta katika ligi kuu ya wanawake ikumbukwe kuwa nchi ya Morocco imeonyesha dhamira ya kukuza soka la wanawake kupitia uwekezaji katika miundombinu na programu za maendeleo. Wanajitahidi kuimarisha ligi za wanawake, kuendeleza vipaji vya wanawake, na kutoa fursa sawa za mafunzo na ushiriki.

Ni wakati wetu sasa kama nchi ya Tanzania kuhakikisha kuwa tunaonesha dhamira kubwa ya uwekezaji na kuacha mambo ya siasa kwani mpira huwa haujifichi na siku zote mpira ni uwekezaji ambapo ni muhimu sio tu kwa mafanikio ya timu ya taifa, bali pia kwa maendeleo ya michezo nchini kote. Kwa kuimarisha miundombinu, kuendeleza vipaji vya vijana, na kushirikiana na wadau wa kitaifa na kimataifa. Kwa kufanya hayo tufahamu kuwa tutaleta mapinduzi ya soka na la kimataifa na kuleta heshima kwa taifa.

Endelea kusoma zaidi kwa kugusa hapa.

1 Comment

  1. Pingback: Watanzania Mwacheni Kocha Afanye Kazi Yake - Kijiweni

Leave A Reply


Exit mobile version