Mbeya City imeanza vyema kampeni ya kujitetea kubaki ligi kuu baada ya kuikanda KMC mabao 2-1kwenye mchezo wa hatua ya kwanza ‘play off ‘ kwa timu za ligi kuu.

Katika mchezo huo ambao umepigwa leo Juni 13 kwenye uwanja wa Sokoine jijini Mbeya, kila timu ilihitaji ushindi ili kujiweka mazingira mazuri ya kukwepa kushuka daraja.

Baada ya mchezo huo, timu hizo zitakutana tena Ijumaa Juni 16 ambapo mshindi wa jumla atajihakikishia kubaki kwenye Ligi kuu msimu ujao, huku mwingine akisubiri kuvaana na Mashujaa FC inayoshiriki Championship.

Mabao katika mpambano huo yalifungwa na Gasper Mwaipasi dakika ya pili huku Sixtus Sabilo akifunga la pili kwa penalti dakika ya 40, huku KMC ikipata la kujifariji kwa Abdul Hilal Hassan kwa penati dakika ya 88.

Hizi ni dondoo za mechi hii.

Mbeya City inakuwa play off yake ya pili kwenye historia tangu ilipofanya hivyo msimu wa 2019/20 ilipoponea chupuchupu kwa kuinyuka Geita Gold jumla ya mabao 2-1.

Katika michezo hiyo, City ilianzia ugenini kwa sare ya 1-1 kabla ya marudiano kwenye uwanja wa Sokoine kushinda 1-0 na kunusurika kushuka daraja.

KMC inashiriki hatua hii kwa mara ya kwanza na sasa baada ya matokeo ya leo itasubiri dakika 90 ikiwa nyumbani kujua hatma yake ya kubaki au kucheza na Mashujaa kujipambania kubaki au kushuka daraja.

Timu hizo zinazomilikiwa na Halmashauri (Mbeya Jiji na Kinondoni Dar es Salaam) zimeangukia mchujo huo baada ya kumaliza nafasi ya 13 na 14 kutokana na kanuni za mashindano zinavyoelekeza kwa timu za ligi kuu.

KMC ilimaliza msimu katika nafasi ya 13 kwa pointi 32, huku City ikishika nafasi ya 14 kwa alama 31 huku Polisi Tanzania na Ruvu Shooting zikishuka moja kwa moja championship.

Hata hivyo, City itahitaji kupata ushindi au sare yoyote ili kubaki salama ligi kuu, huku KMC ilihitaji ushindi kuanzia bao moja ili kubaki kwenye michuano hiyo.

Kwa sasa Mashujaa ya mkoani Kigoma inasubiri mpinzani wake kutoka ligi kuu ili kuwania nafasi ya kupanda daraja baada ya kushinda kwenye play off dhidi ya Pamba kwa jumla ya mabao 5-4.

Kwa taarifa zaidi za michezo na usajili ligi mbalimbali duniani, tufuatilie hapa.

Leave A Reply


Exit mobile version