Moja kati ya tukio kubwa ambalo linazungumzwa sana katika mitandao ya kijamii bila shaka ni michuano ya mataifa barani Afrika yaani AFCON inayofanyika nchini Ivory Coast. Kwa ujumla hatua kubwa iliyofikia katika soka barani Afrika ni ya kushangaza haswa kwa namna timu zilivyojipanga katika michuano ya msimu huu huku timu kubwa zikikutana na vipigo wasivyokua wamevitarajia.

Mauritania kumtoa bingwa mara 2 wa michuano ya AFCON tena akiwa na wachezaji wenye uzoefu mkubwa ni moja kati ya jambo ambalo limekua likizungumzwa katika vijiwe vya soka na haswa kwa ukubwa ambao Algeria aliingia nao katika mchezo huu dhidi ya taifa dogo ambalo kwa kiasi kikubwa limezungukwa na jangwa.

Kama ulikua hufahamu tu nikutaarifu kuwa katika miaka 18  yaani kati ya mwaka 1995-2003 nchi ya Mauritania hawakuwahi kushinda mechi hata moja ya soka lakini mwaka 2010 walijiondoa kwenye kufuzu kwa michuano ya AFCON kutokana na mgogoro wa kifedha ambao walikua nao ambapo katika mwaka 2011 Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) waliiorodhesha kwa vitendo kuwa moja kati ya nchi maskini zaidi kisoka duniani ambapo mwaka huohuo Chama chao cha Soka kilimchagua Ahmed Yahya kuwa Rais wa shirikisho la soka la nchi hiyo yaani Football Federation of the Islamic Republic of Mauritania (FFIRM).

Kuingia kwake madarakani aliamua kwanza kwa kurekebisha ligi ya nchi yao ambapo akapanga timu za vijana na kufanikiwa kupata kampuni kubwa ya mawasiliano ya nchi hiyo kuwa mdhamini wa ligi jambo ambalo lilipelekea sasa mishahara ya wachezaji kupatikana katika ligi yao. Ushindi wao wa kwanza kimataifa katika soka waliupata mwaka 2014 ambapo waliweza kushinda mechi yao ya kwanza ugenini kihistoria wakiifunga nchi ya Liberia.

Tunafahamu namna ambavyo mara nyingi FIFA hutoa pesa mbalimbali za miradi kwa ajili ya malengo yao nan chi hii walifanikiwa kupata pesa hizo ambapo walitumia E10m zaidi ya Bilioni 12 kwa pesa za kitanzania kwa kuurekebisha uwanja wao wa kitaifa unaofahamika kama Uwanja wa Olympic lakini pia wakajenga makao makuu ya kisasa sana.

Hawakuishia hapo, Mauritania walijenga Kituo cha Mafunzo chenye vyumba vya hoteli na studio ya TV/Radio ambapo walifanya kambi kwa timu ya U-15 katika kituo hicho na kuanzisha programu ya maendeleo ya vijana. Katika ziara yake barani Afrika, Rais wa FIFA, Infantino, aliitupia sifa Mauritania kama mojawapo ya nchi chache za Kiafrika zenye uwajibikaji mzuri wa fedha za FIFA.

Mwaka 2019 waliweza kufuzu AFCON kwa mara ya kwanza ambapo hawakufanya vizuri lakini mwaka 2021 waliweza kufuzu kwa AFCON ya pili na kikosi chao kilijumuisha baadhi ya wachezaji wa vijana waliowaendeleza tangu 2015.

Mwaka huu hii ni AFCON yao ya tatu kufuzu huku wakishinda mchezo wao wa kwanza katika michuano hii ya AFCON kwa kulifunga taifa kubwa kisoka barani Afrika ambao pia ni mabingwa mara 2 wa michuano hii ya AFCON.

Hii ndio maana nimekuambia hawajafanya kwa bahati mbaya kumtoa Algeria bali uwekezaji mkubwa walioufanya kuanzia matumizi sahihi ya psa za miradi kutoka FIFA na kuwaandaa vijana kwa ajili ya timu yao ya Taifa.

SOMA ZAIDI: Kilichotokea AFCON Kwa Mataifa Makubwa Ni Somo

Leave A Reply


Exit mobile version