Usiku mmoja, Mwanaume mmoja alikuwa akitoka Hospitalini, alionekana kwenda hapo kwa ajili ya kumuona Mtu mmoja aliyemfahamu sana tena alikuwa Mtu wa karibu sana kwake. Mwanaume huyo alionekana kuwa mwenye mawazo fulani kichwani pake, alikuwa amevalia koti la suti na jinzi chini akipigilia raba kali yenye mg’ao.
Ilitosha kujiridhisha kuwa Mwanaume huyo alikuwa na hela za kutosha, tembea yake ilikuwa ya taratibu mno, ukimtazama vizuri utagundua alikuwa na vita kichwani pake, alipofika kwenye korido aligeuka na kutazama nyuma kisha alitaja jina moja
“Mandy!” Alilitaja jina hilo kisha alihema kiasi, kisha aliendelea mbele kuuelekea mlango wa kutoka Hospitalini hapo. Alikutana na nesi mmoja akiwa amebakisha hatua chache kutoka, nesi huyo alimuita Mwanaume huyo jina lake
“Desmond!!” Alipomuita ni kama alimzindua kutoka Mawazoni, Mwanaume huyo aliyeitwa Desmond alijichekesha kidogo kabla ya kusalimiana na nesi huyo
“Aaah!! Lucia, Habari yako!” Alisalimia Desmond
“Nzuri mbona una mawazo hivyo au kuna taarifa yoyote mbaya kumuhusu Mandy?” Aliuliza nesi huyo aliyeonesha kumfahamu Vizuri Desmond
“Aaah! Hapana hali yake ipo vilevile, nimechoka tu na majukumu ya hapa na pale” Alisema Desmond
“Pamoja na yote Desmond, wewe ni Mwanaume mzuri sana, unajali mno maana huishi kuja kumuona Mandy kwa kipindi chote ambacho amekuwa hapa” Alisema Lucia
“Ndiyo jukumu langu, nahitaji kwenda sasa” Alisema Desmond, waliagana hapo kisha Desmond aliondoka zake huku Lucia akimtazama Desmond kwa jicho la kuhitaji kumwambia kitu lakini alishindwa.
Yalikuwa ni majira ya saa tano za Usiku, muda huo mvua ilianza kuchapa kidogo na kumfanya Desmond akimbilie kwenye gari yake, aliondoka Hospitalini hapo Usiku huo huku akiwa kwenye gari alionekana kukumbuka jambo liliomuumiza, sauti ya daktari ilijirudia kichwani pake
“Mandy anaweza kupata ufahamu ndani ya siku chache zijazo, hii ni habari njema Desmond” Alionekana kutofurahishwa na taarifa ya Mgonjwa huyo kuwa sawa, alipiga usukani kwa hasira kisha alielekea moja kwa moja kwenye jumba lake la kifahari lililopo karibu na fukwe, ndipo alipokuwa akiishi.
Alipoingia alitazama ukutani, aliiyona picha aliyopiga yeye na huyo Mgonjwa aliyeitwa Mandy, mgonjwa huyo alikuwa wa kike, picha hiyo ilieleza kuhusu Mandy na Desmond, Naam! Walikuwa ni wana ndoa, Desmond aliitoa picha hiyo akaitupa kutoka juu ya ghorofa hilo hadi chini
“Mandy huwezi kuwa hai tena ni lazima nikumalize” Alisema Desmond kwa hasira na hisia kali huku akionesha wazi kuwa kulikuwa na jambo ambalo lilijificha kuhusu Yeye na mke wake huyo aliyeitwa Mandy.
Alikunywa pombe sana usiku huo huku simu yake ikiwa bize kuita lakini hakuipokea kabisa, alikunywa na kulewa sana akawa hajitambui, alilala hapo sebleni hadi asubuhi.
**********
Ilikuwa ni asubuhi ya siku iliyofuata, ndani ya ofisi moja alikuwepo Mwanamke mzuri sana aliyeitwa Noela, Mwanamke huyu alikuwa ni Mwanasheria. Alikuwa akifanya kazi yake hapo ofisini huku akili yake ikionesha wazi kuwa haikuwa na utulivu, mara zote alikuwa akijaribu kupiga simu bila kupokelewa, baadaye alikuja jamaa mmoja aliyeitwa Zanda, walikuwa ni marafiki waliokuwa wakifanya kazi ofisi moja ya Wanasheria wa kujitegemea, mara moja Zanda aligundua Noela hakuwa sawa aliketi akamuuliza
“Vipi Noela una tatizo?” Alihoji Zanda huku akimtazama Usoni Noela
“Aaah! Nipo sawa Zanda usijali” Alijibu Noela
“Noela nimefanya kazi na wewe kwa muda mrefu hivyo nakujuwa vizuri sana, leo haupo sawa” Alisistiza Zanda, Noela alimkubalia Zanda kuwa hayupo sawa ila ni mambo madogo tu atayatatua.
Baada ya kupita muda kidogo Noela aliondoka ofisini akiaga kuwa anajisikia vibaya. Zanda alimshangaa sana Noela, alimkodolea macho akiwa anaondoka na gari yake kisha alitikisa kichwa chake, Noela aliendelea kupiga simu bila kupokea majibu yoyote yale hadi anafika nyumbani kwao, alikuwa akiishi na Mama yake Mzazi ambaye alipendelea sana kumuita Mlami
Mama yake ( Mlami ) aligundua haraka kuwa Noela hayupo sawa kifikra, alimuuliza akiwa amejilaza sofani
“Kuna nini Noela huonekani kuwa sawa kabisa, unaonekana ni mwenye mawazo mengi kichwani mwako” Alihoji Mama yake Noela huku akimkata jicho la udadisi binti yake huyo wa pekee ambaye alikuwa akimpenda sana baada ya Baba yake kufariki.
“Ni Joshua Mama, tokea jana hapokei simu zangu. Sijui yuko wapi” Alijibu Noela kama vile alikuwa amechokozwa na Mama yake, alimpigia tena huyo Joshua
“Ulijaribu kwenda kwake?” Aliuliza Mama yake, Noela alimtazama Mama yake kwa jicho la kukata tamaa kisha akatikisa kichwa ishara ya kuwa hakwenda nyumbani kwa Joshua kisha alimwambia Mama yake
“Msichana wake wa kazi anasema hakurudi tokea alipotoka jana asubuhi” Alijibu Noela
“Sasa atakuwa wapi na kwanini hapokei simu zako jamani” Alisema Mama yake Noela
“Mama tokea jana nimechanganikiwa kabisa, ngoja tu nikapumzike maana nimeshindwa hata kufanya kazi leo kwasababu yake” Alisema Noela
“Haya sawa Mwanangu! Usijali sana huwenda yupo bize” Alisema Mama yake Noela kisha Noela alionesha tabasamu feki akaelekea chumbani kwake.
Ndani ya jumba la kifahari la Desmond, alikuwa ndiyo anaamka kutoka usingizini, alikuwa amelala palepale sebleni kutokana na pombe kumzidia. Aliamka akiwa mchovu sana lakini alipoamka tu alitaja jina la Mke wake Mandy kisha alitafuta simu yake ambayo ilikuwa kando yake kisha akapiga Hospitalini kwa Nesi Lucia
“Vipi hali ya Mke wangu” Aliuliza Desmond huku akiwa na hofu sana
“Mandy anaendelea na matibabu, bado hajapata ufahamu Desmond” ilisikika sauti kutoka upande wa pili, ilikuwa ni sauti ya Nesi huyo iliyotoka kwa kubembeleza sana
“Asante! Kwa lolote unitaarifu mapema sana” Alisema Desmond kisha alikata simu bila kusikiliza kingine kutoka kwa Lucia
“Mandy kwanini hukufa? Kwanini upo hai? Kwa vyovyote vile huwezi kutoboa siri nitakuuwa tu” Alisema Desmond kwa jazba kisha alikagua vizuri simu yake, alikutana na simu nyingi ambazo hazikujibiwa, moja ilikuwa ya Noela, alikutana na meseji nyingi kisha alitabasamu tu. Akaelekea kuoga kisha alitoka kwenye jumba hilo ambalo alikuwa akiishi hapo
Safari ya Desmond ilikuwa ni kuelekea nyumbani kwa Noela, kitendo cha Mama kusikia mlio wa gari kilimfanya achungulie, alipoliona gari la Desmond haraka alikimbilia chumbani kwa Noela akamwambia
“Joshua amefika” Alisema Mama huyo, Noela hakuamini alichokisikia naye alikimbilia nje, alimuona Desmond ambaye yeye alikuwa akimfahamu kwa jina la Joshua.
Alimkimbilia na kumkumbatia kwa furaha sana kisha chozi lilimbubujika, alionesha ni wazi kuwa alikuwa akimpenda sana Mwanaume huyo kisha alimuuliza
“Joshua nimekutafuta sana ulikuwa wapi Mpenzi, nimeingiwa na hofu mno” Desmond alicheka kidogo
“Nimeamini kuwa unanipenda sana Noela, nilifanya kusudi ili nipime upendo wako” Alisema Huyo aliyefahamika kwa jina la Joshua lakini kule Hospitali alijulikana kama Desmond, hebu tusonge na Uhondo wa Hadithi hii.
Mama yake Noela alisimama akiwaangalia wapendanao hao, kisha moyo wake ulikubali kuwa walikuwa wakipendana sana, alitabasamu alafu akatangulia ndani huku Desmond ( Joshua ) na Noela wakifuatia.
Walishinda hapo pamoja siku hiyo, walikula, walicheza pamoja na kupeana mapenzi motomoto kisha baadaye waliondoka na kuelekea kwenye nyumba ambayo Desmond alikuwa akiishi, hii ilikuwa ni nyumba tofauti na ile aliyokuwa akiishi na Mke wake.
TURUDI MIAKA KADHAA ILIYOPITA
Ndani ya Kijiji kimoja, kulikuwa na familia moja iliyoishi kwa shida sana. Familia hii ilikuwa ya Watu wawili tu, Baba na Mwanaye. Walikuwa wameketi nje ya Banda lao, ukimya ulikuwa umetawala sana hapo, Mtoto huyo mwenye miaka 11 alimuuliza Baba yake.
“Baba tutaenda wapi?” Aliuliza akiwa anamtazama Bba yake aliyekaa juu ya gogo la Mti
“Unafikiria tutaenda wapi Desmond? Kifo cha Mama yako kimeleta mkosi sana kwetu kila kitu kimeharibika” Alisema Baba huyo, Mtoto huyo aliyeitwa Desmond ndiye huyu ambaye ni Mume wa Mandy aliyeko Hospitalini, kumbe jina lake halisi ni Desmond na siyo Joshua.
“Usiseme hivyo Baba! Huwenda Mungu alipanga iwe hivi” Alisema Mtoto Desmond
“Alipanga tufukuzwe hapa Kijijini? Una mawazo ya kipumbavu sana, huu ni mkosi aliouleta Mama yako!! Leo utakula Hizo kauli zako” Alisema Baba yake huyo kisha aliondoka zake na kumuacha Desmond akizidi kutafakari. Maisha yao yalikuwa Duni sana, Desmond alidondosha chozi kisha alikimbilia kwenye kaburi la Mama yake ambalo halikuwa mbali na banda lao, alipiga magoti kisha alisema
“Mama si hujakosea si ndiyo? Kwanini Baba anakuhukumu hivi….Mama nauchukia umasikini, nakuahidi sitokufa masikini” Alisema Desmond kisha aliondoka kaburini hapo.
TURUDI MAISHA YA SASA
Hiyo ilikuwa ni kumbukumbu ambayo Desmond alikuwa akiikumbuka alipokuwa akiitazama picha ya pamoja aliyopiga na Mama yake. Aliichukua picha hiyo iliyo ndani ya waleti yake kisha alisema
“Mama natamani ungekuwepo uone Maisha ninayoishi, nimekuwa tajiri nina kila kitu ila sina Baba wala Mama, Baba yangu alikufa kwa pombe kali….” Alipokuwa akiyasema maneno haya Noela alikuwa akiingia chumbani, Desmond hakushtuka kama Noela alikuwa ameingia, Noela alimsikia Desmond akisema
“Kipo kirusi Mama, nahangaika kukiondoa ili niwe huru zaidi” Alisema Desmond lakini ghafla alihisi kuna Mtu anamsikiliza, ni kweli alipogeuka alimuona Noela akiwa anamtazama, Desmond alionekana kuwa mwenye siri nzito sana ndani yake, siri ambayo hakutaka Mtu yeyote aijuwe huku lengo lake kuu likiwa ni kumuuwa Mke wake.
“Kirusi? Ukiondoe?” Aliuliza Noela, Desmond alimtazama Noela kwa Makini sana akagundua alikuwa hajaelewa lakini macho ya Desmond yalikuwa yakivujisha chozi, Noela alimpatia kitambaa Desmond ili afute chozi hilo, aliketi akamuuliza tena
“Kirusi gani untaka ukiondoe?” Aliuliza Noela, Desmond alifuta chozi kisha alimwambia Noela
“Mimi na marehemu Mama yangu tulikuweka ahadi kuwa nitakuwa na pesa nyingi sana na pia nitaowa, pesa ninazo lakini sijaowa, kwangu nachukulia kama kirusi kwenye ahadi yangu” Alisema Desmond, Basi Noela alitabasamu tu
“Kubali nikuowe Noela ili uwe wangu peke yangu, jinsi ninavyokupenda nahisi Dunia yote nimeiweka kiganjani pangu” Yalikuwa ni maneno matamu sana aliyoyatoa Desmond ili kumfanya Noela asihisi chochote kile, kweli Noela alihama kihisia akasahau kila kitu
“Naanzaje kukataa Joshua? Nipo tayari uniowe hata kesho. Nikikumbuka jinsi tulivyokutana moyo wangu unajawa na furaha na amani sana. Nakupenda pia Joshua” Alisema Noela kisha alimkumbatia Desmond.
Sura ya Desmond ilibadili taswira kutoka kutabasamu hadi kuwa mtu aliye siriazi na jambo lililo akilini mwake.
Majukumu ya kazi yaliendelea kwa pande zote yaani kwa Desmond na kwa upande wa Noela, kumpata Desmond kulimpa furaha sana Noela akawa anachapa kazi zake.
Mchana wa siku hiyo, Desmond alienda Hospitalini kama kawaida, alipewa nafasi ya kumuona Mke wake Mandy. Alikuwa na hasira na Mwanamke huyo. Mandy alikuwa amepoteza fahamu kwa zaidi ya miezi mitano hivyo kwa kipindi chote alikuwa Hospitalini tu, Desmond alisogea akaketi kwenye kiti kimoja ambacho kilikuwa kando ya kitanda cha Mke wake, alikunja nne kisha akamwambia Mandy
“Nina uhakika unanisikia Mandy! Katika vitu sitamani kuona katika Maisha yangu basi ni uhai wako, natamani uwe umekufa na usiamke tena hapo Kitandani” Alisema Desmond akiwa amevalia suti nyeusi zilizomkaa vizuri, alikuwa kijana mwenye muonekano mzuri sana. Desmond alisimama kisha alimsogelea Mandy
“Siri unayoijuwa kuhusu Mama yako ibaki kuwa siri ya Ulimwengu mzima, sipo tayari kuyaharibu Maisha yangu kwasababu yako. Asante kwa utajiri mkubwa ulioniachia Mandy, nasikitika sababu uliyemuamini siku zote hakuwa na mapenzi na wewe, sikuwahi kukupenda Mandy….Nilizipenda pesa zako tu” Alisema Desmond kisha alivuta pumzi zake huku chozi likimlenga, licha ya uamuzi huo mgumu bado alionesha kuumia ndani ya Moyo wake
Ghafla aliona Mandy akitingisha kidole, hii ilimshtua sana Desmond, miezi yote Mandy hakuwahi kutingisha hata kope za macho yake, ilionesha wazi hata alichokizungumza Desmond alikuwa akikisikia. Akiwa anaendelea kushangaa Desmond aliona macho ya Mandy yakifunguka huku yakibubujikwa na mchozi, Mandy alikuwa ni Mwanamke mzuri mwenye weupe wa asili, chozi la Mandy lilionesha wazi kuwa lilibeba maumivu makali sana
“Mandy umeamka? Ina maana siri yangu utaisema!! Hapana Unakufa” Alisema Desmond ndani ya moyo wake huku akiwa amevurugwa sana, aliangalia huku na kule kisha alichukua mto na kumziba pumzi Mandy ili afe pale kitandani. Mandy alihangaika kwa nguvu chache aliyokuwa nayo lakini hakuweza kufanya lolote zaidi ya kuziona pumzi zake zikifika mwisho, Desmond alidhamiria kumuuwa Mandy mchana huo ili hiyo siri yake isijulikane.
Mara Desmond alisikia chupa ikivunjika, alipogeuka alimuona nesi Lucia akiwa anaokota vipande vya vyupa pale mlangoni. Haraka aliacha jaribio la kutaka kumuuwa Mke wake Mandy. Aliuweka mto pembeni, alikuwa akitokwa na jasho jingi kisha alimtazama Mandy alionekana kuzima, Desmond aligeuza macho alimuona nesi Lucia akisogea hapo
“ooh Desmond” Alisema Nesi Lucia huku akiwa anaweka vifaa juu ya meza iliyo pembe ya ukuta, alipomtazama vizuri Desmond alimuona akiwa anatokwa na jasho jingi sana, alishangaa kisha alipeleka macho yake kwenye AC, kisha alirudisha kwa Desmond. Alionekana kushangaa jasho la Desmond lilitoka wapi ikiwa chumba hicho kilikuwa hakina joto kabisa
“Kulikoni Desmond mbona unavuja jasho hivyo” Aliuliza Nesi Lucia akiwa anamtazama kwa makini Desmond
“Aaah- aaah…Jasho….unajuwa!! Lucia sijisikii vizuri naomba nipumzike nje” Alisema Desmond kisha alitoka lakini Nesi Lucia aliendelea kujiuliza maswali yasiyo na majibu, mwisho alipuuzia jambo hilo.
Alienda kumtazama Mandy, alionekana kupowa huku mapigo ya moyo yakienda sawa kwa maana Desmond hakufanikiwa jaribio la kuondoa uhai wa Mandy, alibadilisha dripu na kufanya mambo mengine kisha naye alitoka. Hali ya Mandy haikujulikana kwa wakati huo kuwa ataamka lini wala saa ngapi laiti kama taarifa ya kuamka kwake ingewafikia madaktari basi tumaini lingekuwa kubwa sana.
Akiwa nje ya wodi ile, Desmond aliendelea kutafakari kuhusu usalama wa Mandy, alifikiria kama Mandy alikuwa amekufa au alikuwa hajafa na kama hajafa basi siri yake iliyojificha kuhusu Mama yake Mandy ingefichuka, akiwa hapo alisikia sauti ikimuita
“Mr Desmond” Alipogeuka alimuona Mtu mmoja akiwa amemsimamia, alishtuka sana sababu hakutarajia kumuona Mtu huyo kwa wakati huo
“Mbona umeshtuka au hukutarajia kuniona?” Alihoji Mtu huyo aliyekuwa Mwanaume mwenye sauti nzito
“Hapana ila nilikuwa mawazoni ndiyo maana nimeshtuka” Alisema Desmond kisha aliketi vizuri ili Mwanaume huyo naye aketi
“Hali ya Mkeo vipi?” Aliuliza Mwanaume huyo
“Mke wangu anaendelea…Hali yake bado ipo vile vile” Alijibu Desmond
“Mkeo ni shahidi namba moja wa kifo cha Mama yake, mara ya mwisho alituma ujumbe kituo cha polisi kuwa anamjuwa Muuwaji wa Mama yake, baada ya hapo ndiyo tukio la wewe kupigwa risasi na Mke wako kupigizwa ukutani lilipotokea, Mkeo ni Mtu muhimu zaidi katika kesi ile” Alisema Mwanaume huyo ambaye sasa alitambulika kuwa ni askari
“Yaah! Ni kweli, ilikuwa ni siku ngumu sana katika Maisha yangu ni kama nilimpoteza Mke wangu tokea siku ile hadi hivi leo” Alijikakamua Desmond kisha alijibu, huyu Desmond alionekana wazi kutambua juu ya kifo cha Mama yake Mandy lakini kwanini hakutaka ukweli uwekwe wazi? Au yeye ndiye aliyemuuwa Mama yake Mandy? Kwanini Amuuwe? TUSONGE MBELE
“Kwa lolote usisite kutujulisha Mr. Desmond” Alisema Askari huyo kisha aliondoka hapo. Kumbe nesi Lucia alikuwa anamuangalia Desmond akizungumza na polisi kisha alipoondoka yeye alimfuata Desmond alipokaa
“Desmond najuwa unavyojisikia, najuwa unaumia sana lakini Mkeo atakuwa sawa tu siku moja mtarudi kuwa kama zamani” Alisema Nesi Lucia, Desmond alimtazama Lucia kisha alijisemea moyoni
“Ungejuwa ninavyotamani afe wala usingesema hayo maneno” Kabla hajamjibu chochote Lucia alipokea simu ya Noela
“Hello” Alisema Desmond baada ya kupokea simu hiyo
“Desmond nakusubiria Mgahawani” Alisema Noela kisha Desmond alijibu
“Sawa nakuja”
“Unaenda wapi?” Alihoji Lucia
“Mjini”
“Hata mimi ninaenda huko kwa ajili ya chakula, tafadhali nipe lifti” Alisema Lucia
“Haya sawa!” alisema Desmond kisha waliongozana hadi kwenye gari ya Desmond na safari ya Kuelekea Mjini ilianza.
Wakiwa barabarani Nesi Lucia macho yake yote yalikuwa kwa Desmond, alimpenda sana Mwanaume huyo lakini alishindwa kumwambia sababu alikuwa Mume wa Mtu istoshe alikuwa akimuuguza Mke wake huyo.
Desmond aligundua hilo akamuuliza Lucia
“Kwanini unaniangalia hivyo?”
“Desmond wewe ni Mzuri sana, Hakika Mke wako anajivunia kuwa na Mwanaume kama Wewe” Alisema Lucia kisha Desmond alitabasamu kidogo alafu hakusema chochote kile hadi anafika eneo ambalo Lucia alikuwa akienda. Ilikuwa ni kwenye mgahawa huo huo ambao Desmond alienda kukutana na Mpenzi wake Noela
“Eeeh ajabu kumbe nawe ulikuwa unakuja hapa?” Aliuliza
“Yaah! Kuna Mtu naonana naye mara moja kisha niendelee na majukumu mengine”
“Haya asante kwa Lifti” Alisema Lucia kisha alishuka akaingia kwenye mgahawa huo ambao ulikuwa wenye hadhi kubwa na pia ulikuwa mkubwa mno, Desmond alienda mahali ambapo alipanga kuonana na Noela.
Nini Kitaendelea? USIKOSE SEHEMU YA PILI
Mpe Nguvu ADMIN Kwa ajili ya kuendelea kutuma SIMULIZI Mpya Na Kuipost HAPA Kwa kumtumia Chochote kupitia
Lipa Namba: 57900454
Jina: LIPA KIJIWENI TIPS
Mtandao: VODACOM
SOMA RIWAYA YA KOTI JEUSI KWA KUBONYEZA HAPA
SOMA RIWAYA YA FUNGATE KWA KUBONYEZA HAPA
3 Comments
Hakika hujawahi kutuangusha
Love and Pain
Inaonyesha ni Story nzito yenye burudani na Mafunzo ndani yake.
Asante sana Kaka Mkubwa
More Love from Kenya ♥️
NAOMBA KWA SIKU ZIWE SEHEMU 2.
Kali sana