Kipa wa Real Madrid, Thibaut Courtois amekiri kwamba nafasi yao ya kushinda LaLiga imekamilika, kufuatia kipigo cha mabao 2-1 kutoka kwa Barcelona Jumapili.

Matokeo hayo yamewaacha Los Blancos wakiwa nyuma ya vinara wa ligi hiyo kwa pointi 12.

Madrid walitangulia katika uwanja wa Camp Nou shukrani kwa bao la kujifunga la Ronald Araujo.

Lakini Sergi Roberto alisawazisha kabla ya muda wa mapumziko, kabla ya Franck Kessie kufunga katika muda wa nyongeza.

Matokeo hayo yanamaanisha kuwa Barca wako mbioni kutwaa taji lao la kwanza la ligi tangu 2019.

“Ndio, tunapaswa kuwa wakweli,” Courtois aliiambia Movistar, alipoulizwa ikiwa mbio za ubingwa zimekamilika.

“Tulitaka kupigana hadi mwisho, lakini sasa ni tofauti ya michezo minne … Wangepoteza michezo minne, na itabidi tushinde yote. Hakuna lisilowezekana, lakini ni ngumu sana.”

Leave A Reply


Exit mobile version