Aprili 20, 2021 Kocha Nasreddine Nabi akitokea Tunisia alitua Dar es Salaam na kusaini mkataba wa mwaka mmoja na nusu kuitumikia Yanga na safari ya mafanikio ya timu hiyo ilianzia hapo.
Licha ya kuanza kwa kipigo alipotua katika mechi ya kwanza akifungwa dhidi ya Azam bao bao 1-0 na akaanza kuwapa furaha mashabiki akicheza mechi 49 bila kupoteza (unbeaten).
Kila chenye mwanzo hakikosi mwisho, Nabi ambaye ameipa Yanga mataji mawili Ligi Kuu, mawili Kombe la Shirikisho Afrika na fainali Kombe la Shirikisho Afrika jana Juni 14 safari yake imeishia akiachana na timu hiyo.
Uongozi wa klabu ya Yanga tayari umetoa taarifa ya kufikia makubaliano ya kuachana baada va kocha huyo kuomba kutoongeza mkataba mpya.
“Mkataba wa Kocha Nasreddine Nabi na Yanga umemalizika mwisho wa msimu huu, baada ya kumalizika kwa mkataba huo, Uongozi wa Yanga ulikutana na Kocha Nabi kwa ajili ya mazungumzo ya kusaini mkataba mpya lakini Nabi aliomba kuondoka ili akapate changamoto mpya” ilieleza taarifa hiyo ya Yanga iliyotoka jana usiku
Nabi akiwa Yanga amefanikiwa kutwaa mataji mawili ya Ligi Kuu, mawili ya Kombe la Shirikisho la Azam, mataji mawili ya Ngao ya Jamii na kuifikisha timu hiyo hatua ya fainali ya Kombe la Shirikisho la CAF
“Uongozi wa Yanga unamshukuru Kocha Nabi kwa mchango wake katika kipindi chote alichofanya kazi kwenye timu yetu na unamtakia kila la kheri katika safari yake,”
Katika taarifa hiyo Uongozi wa Yanga umesema umeanza mchakato wa kumpata Kocha mpya atakayechukua nafasi ya Kocha Nasreddine Nabi.
Soma hapa kwa taarifa zaidi za usajili.