Kwa TFF kutojua wamiliki wa klabu zinazoshiriki mashindano yake ni kitu cha hatari na kinakaribisha zaidi vitendo vinavyoendelea vya klabu kubadilisha umiliki wake kiholela bila ya kuwepo na taarifa rasmi zinazoonyesha uuzwaji huo umegharimu kiasi gani na kilichosababisha mmiliki mmoja auze klabu kwa mwingine kana kwamba ni ile biashara ya zamani ya ‘mali kwa mali’kama ilivyokua kwa IHEFU.

Ukiliangalia hilo na lile lililokwamisha mchakato wa klabu ya Simba kuuza sehemu ya hisa zake kwa mwekezaji, utaona ni kwa nini Kamisheni ya Ushindani wa Haki (FCC) iliagiza Simba isubiri mwongozo utakaotolewa na TFF kuhusu umiliki wa klabu za Ligi Kuu kabla ya kukamilisha mchakato wake wa kuuza hisa kwa wawekezaji.

Ni sahihi kabisa kwamba sasa TFF haina budi kukaa chini na kutunga kanuni ambazo zitaongoza umiliki wa klabu zilizokuwa za wanachama, za watu binafsi na zile zinazomilikiwa na kampuni au taasisi ili pia kuwepo na uitaratibu ambao una uwazi katika kubadilisha wamiliki, kama ilivyofanyika kwa Singida Fountain Gate, ambayo awali ilikuwa Singida Big Stars, na Ihefu, ambayo muda si mrefu inaweza kubadilishwa jina.

Kama wanaoamini Mwigulu ameinunua Ihefu kuilainishia Yanga mechi dhidi ya timu hiyo ambayo hata msimu uliopita ilikuwa moja ya timu mbili zilizoishinda Yanga, wataachaje kuendelea kuamini iwapo Mwigulu ataachana na Ihefu na kuinunua klabu nyingine inayoonekana kuwa tatizo kwa Yanga na matokeo yakawa kama ya Ihefu? Kwa sababu hakuna kanuni zozote zinazoongoza uuzwaji wa klabu wala umiliki kulingana na kanuni za Leseni za Klabu.

Kama imani hiyo itasambaa na hakuna ilani yoyote, nani atamzuia mtu mwingine kununua klabu kwa lengo la kuilainishia klabu yake pendwa matokeo?

Kwa haraka haraka huoni hilo likitokea katika kipindi kifupi kijacho, lakini haitakiwi lisubiriwe hadi litokee. Wakati huu mzuri kuanza kudhibiti umiliki wa klabu kwa angalau TFF kuanza kuhakikisha kuwa kila klabu inawasilisha kwake vielelezo vya wamiliki wa klabu vilivyothibitishwa na serikali kabla ya kuanza kwa msimu au wakati mtu binafsi, taasisi au kampuni anataka kuinunua klabu.

Kwa wenzetu wa barani Ulaya, ambako watu hawataki tujilinganishe nao, ni rahisi kujua wamiliki kwa sababu klabu nyingi ni mashirika yaliyosajiliwa rasmi na hivyo yanawajibika kwa mamlaka za serikali kama zilivyo kampuni nyingine. Kwa sasa ili kulinda mpira, nchi kama Uingereza inaelekea kuwasilisha muswada ambao utazidisha udhibiti wa klabu kutokana na kuanzisha ofisi ya Msajili wa Klabu licha ya Chama cha Soka cha England kuwa na msajili wake.

Si kitu kizuri kwa klabu kumilikiwa na mtu aliye nyuma ya pazia na ambaye hajulikani kabisa, na ambaye hata akiamua kuondoka huwezi kumlazimisha abakie kwa sababu hukujua kama yupo. Matokeo yake yatakuwa kama ambavyo Singida United, ambayo pia iliaminika ilikuwa inamilikiwa na Mwigulu, ilisambaratika kwa mara ya pili baada ya ile Singida ya kwanza iliyokuwa ikimilikiwa na Mohamed Dewji.

Hii itasaidia kudhibiti hata maamuzi kama ya Alwxander Mnyeti ambaye aliamua kuiondoa klabu yake ya Gwambina kwenye ligi, akisema ni heri atumie uwanja wake kulisha mifugo kuliko kutumika kwa soka.

Hali kadhalika itadhibiti tabia ya klabu kuinunua klabu nyingine iliyo daraja la juu ili irejee kwenye ligi ya juu kirahisi kama ambavyo Pan African, Pamba, Moro United, African Lyon na nyingine zimejaribu kufanya na baadhi kufanikiwa.

Kwa kiasi fulani tumeshafanikiwa sana katika uendeshaji mashindano yetu kwa hiyo tunatakiwa tupige hatua nyingine kubwa ya kuanza kudhibiti umiliki wa klabu na kutaka uwazi katika mapato na matumizi ya fedha ili kuwa na uhakika zaidi katika uendeshaji na upangaji mipango mikubwa zaidi inayotaka uhakika wa uchumi wa klabu.

Kwa hiyo, kusema ni vigumu kujua wamiliki wa klabu kwa sababu wanafanya siri sana, hakutoi mwanga wa kumalizika kwa matatizo mengi yanayoonekana kuunyemelea mpira wa miguu, huku kukiwa na maswali mengi na yasiyo na majibu kuhusu uwezekano wa mechi kuchezwa nje ya uwanja kutokana na usiri huo.

SOMA ZAIDI: Simba Ana Nafasi Ya Kuendeleza Ubabe Dhidi Ya Ahly Kwa Mkapa

1 Comment

  1. Pingback: Mfumo Huu Utambeba Chama Kumuua Al Ahly Kwa Mkapa - Kijiweni

Leave A Reply


Exit mobile version