IlipoishiaWalipouvunja mlango walistaajabu sana, macho yaliwatoka kwa Mshangao. Japo walikua Maaskari polisi lakini washika vichwa vyao na wengine walishika viuno vyao, waliona jambo la ajabu lenye kutisha na kusisimua sana.”

Tuendelee 

SEHEMU YA 07

 

Walimkuta Kijana Michael mwenye miaka 27 akiwa amelala chali huku macho yake yakiwa yametobolewa, kando palikua na yule Paka ambaye naye alikua ametobolewa macho yake huku Michael na paka wakiwa wamevuja damu nyingi na Michael alikua amemkumbatia paka huyo anayeitwa Michael Junior.

Muda huo huo Jasusi Marcus aliingia, naye alishuhudia unyama huo. Alimtazama Michael kwa 

sekunde kadhaa tu kisha akarudi kwa Mama yake Michael ambaye hakua na taarifa ya kifo cha 

Mtoto wake, akamvuta nje kisha akamwuliza

“Kijana wako ni Mtu wa aina gani?” 

“Mjeuri, asiye na adabu. Hasikilizi lakini siku hizi amekua mwoga sana hasa baada ya kumaliza chuo, hatoki ndani anajifungia, muda wa kula naenda kumpa chakula.” 

“Uliwahi kumwona akijihusisha na Watu fulani ambao hata walikua wanakuja hapa?” aliuliza Marcus, 

Mama yake Michael akasema

“Ndiyo, kuna Msichana alikua anakuja hapa. Anasema anasoma naye, alikua anakuja dakika si chini ya tatu anaondoka” 

“Anafananaje” 

“Sikumzingatia, lakini ni mfupi hivi, mweusi kiasi” 

“Ok sawa, polisi watakupa taarifa kuhusu Michael” alisema Marcus kisha aliingia kwenye gari 

akaondoka zake.

 

Simu ya Kifo…

Siku ya Kuuawa kwa Bilionea Yusuf 

Mtu tajiri, mwenye Ushawishi kwa Serikali ya Tanzania alikua ofisini kwake akifanya kazi zake. Alikua bize sana akipiga Mahesabu huku akifwatilia ungiaji wa pesa kwenye akaunti kuu, Kompyuta kubwa iliyo mbele yake ilikua na Kolamu zenye kumwezesha kuona ni kiasi gani anaingiza kila baada ya Dakika moja.

Pesa zilikua zikiingia kutoka Mataifa mengi aliyowekeza na zote zilikua zikiingia kwenye akaunti moja. Wakati anafanya kazi yake alisikia simu yake ndogo ikiita kutoka kwenye mfuko wa koti lake la suti alilolitundika kwenye Kiti, alimalizia kwanza mahesabu yake kisha akaipokea Simu hiyo mara baada ya kupokelewa hapakusikika sauti yoyote ile isipokua ukimya, kutokana na ubize hakuijali sana akaikata, baada ya dakika moja iliita tena lakini alivyoipokea hapakua na sauti  yoyote ile iliyosikika.

 Iliita kila baada ya dakika moja lakini hapakua na Sauti yoyote aliyoisikia. Siku hiyo Jiiji lote liligubikwa na wingu zito lililoonesha wazi kua ingeshuka mvua kubwa mithiri ya Ghalika.

Mara zote Bilionea Yusuf alipendelea kurejea nyumbani mapema, akamwita Binti yake Sofia ambaye alimwamini sana kuliko Mtu mwingine kisha akamwambia

“Narejea nyumbani jitahidi nipate rekodi za Mauzo kuanzia sasa” alisema huku akichukua koti lake, ile simu iliita tena, safari hii hakuipokea alifunga Namba iliyokua ikimsumbua kisha akawasiliana na dereva wake, akaingia kwenye gari wakaanza safari ya kuelekea nyumbani.

Wakiwa kwenye gari Bilionea Yusuf alimweleza dereva wake kuwa ana Mashaka sana na Usalama wake.

“Eeeh Bosi kwanini usitoe taarifa Polisi ukapewa Ulinzi?” aliuliza dereva

“Nitaangalia kama hali ya kupokea simu isiyoongea kama itaendelea, tokea jana napokea hiyo simu, mpigaji hazungumzi” alisema. 

“Basi sawa Bosi jitahidi uwe Makini maana Maisha sasa yamebadilika sana, kwa hadhi yako 

unapaswa kua na dereva msomi pia walinzi” alisema Dereva, Alimfanya Bilionea Yusufu acheke huku akikohoa

“Unafikiri sithamini mchango wako Devie? Wewe ni muhimu japo hukusoma, unaniendesha salama nafurahia hilo, pia una familia inayokutegemea” alisema Mzee Yusuf, ilionesha namna Mzee huyo alivyokua mpole na mwenye huruma sana.

Walipofika nyumbani, Bilionea huyo alielekea moja kwa moja kwa Mjukuu wake Adela aliyekua chumbani, alimpenda sana Mjukuu wake huyo na kwa siri sana alimwandikisha utajiri mwingi alio nao, alifanya kwa siri hata Hamza na Sofia hawakulifahamu hilo.

Hata Adela alikua akimpenda sana Babu yake, wakaketi kitandani. Mzee Yusuf akamwambia Adela

“Ikitokea siku hunioni, tumia hizi namba, Fanya kua siri kwasasa hadi pale utakapokua hunioni 

sawa?”

“Kwanini iwe siri Babu?”

“Kwasababu Mimi na wewe tunapendana sana” 

“Ha!ha!ha!” wote walicheka, mara zote Mzee Yusuf alikua akimwita Adela Mke wake, ni kawaida  kwa Babu kumwita hivyo Mjukuu wa kike. Akampatia Adela kadi moja yenye Namba fulani, Adela akaificha kadi hiyo mahala pa siri sana.

Babu yake aliingia Chumbani kwake, alijipumzika bila kubadilisha nguo zake. Alilala hapo hadi Usiku wa saa tatu, alipokuja kushtuka alikuta kuna faili zimeletwa kwenye meza yake, faili hizo zililetwa na Binti yake Sofia, aliketi mezani na kuanza kuzipitia. Mvua kubwa iliyoshikana na radi ilikua ikinyesha, umeme ndiyo ulianza kusumbua, mara uwake, mara uzime.

Mzee Yusuf akawasha taa ya kuchaji ikiyosambaza Mwanga vizuri pale chumbani, akainamaa na 

kuendelea kupitia yale Mafaili, alishtuka alipohisi kuguswa kichwani, mdomo wa bastola ulielekezwa kwake, akafunga faili lake kisha akasema

“Nilijua utakuja” Baada ya kusema hivyo bastola ilishushwa, Mtu aliyeingia alivuta kiti na kuketi. Alikua ni Mwanamke aliyefunika sura yake kwa Barakoa, akiwa amevalia, jinzi nyeusi na kofia nyeusi. 

Mzee Yusuf akasimama na kuchukua Waini na glasi mbili ambazo wapelelezi walivikuta juu ya meza.Kisha aliporudi akaweka glasi kwenye meza, akamiminia waini kwenye zile Glasi kisha akamwuliza Mtu aliyekuja

“Umekuja kunimaliza Mwanangu?” Bilionea Yusuf alikua akifahamiana na Muuwaji aliyemuuwa

“Unahisi unastahili kuendelea kuishi baada ya yote?” alihoji Mwanamke huyo aliyeonekana kua 

Msichana wa makamo tu

“Sistahili kuendelea kuishi, Kifo ni Halali yangu. Lakini umefikiria baada ya kifo changu utabaki kuwa hai?” aliuliza Bilionea Yusuf kisha aligida Waini

“Sitojali hata kama nitageuka kuwa Muuwaji, nitauwa wote kwa ajili ya Kisasi changu kwako. Hakuna atakayebakia kua hai” Mzee Yusuf alitabasamu kisha akasema

“Kwa hakika nastahili kulipa kwa ukatili na tamaa zangu” Msichana huyo asiyetajwa jina lake 

akachomoa sindano kisha akaitia sumu ndani yake kisha akaitia sumu ndani ya glasi

“Kwa heshima yako ni vema ukaondoka taratibu bila purukushani” alisema Msichana huyo kisha 

Mzee Yusuf akagida kinywaji chenye sumu. Msichana aliketi hapo akimshuhudia Mzee Yusufu akifa kikatili kwa ile sumu Kisha akafungua Mlango na kutimka, dakika mbili baadaye akaingia Mtu mwingine na kumkita kisu Mzee Yusufu akiwa amelalia meza, Mtu huyo akasubiria kuona kama Mzee Yusufu angetapatapa lakini haikua hivyo, alipomtikisa aligundua ameshakufa.

Haraka akapekua mafaili kwenye Kabati kisha akatimka humo. Alikua amevalia Koti Jeusi

***

Kesi ya Kifo cha Bilionea Yusuf ilifufuka upya ikiwa kwenye mikono ya Jasusi hatari zaidi anayeitwa Marcus, alipotoka nyumbani kwao Michael Jomo alielekea moja kwa moja chuo Kikuu cha Dar-es-

salaam. Mwendo wa saa nzima alifika hapo, sasa akawa anaegesha gari yake mpya aina ya Kulger aliyokabidhiwa na Idara ya Ujasusi. Alikitazama sana Chuo cha UDSM, kisha alishuka kwenye gari akaifuata Ofisi ya Mkuu wa chuo ambaye alitoa taarifa kuhusu Michael Jomo.

Lakini kabla hata hajafika Ofisini alipishana na Msichana mmoja ambaye kwa namna alivyomtazama Msichana huyo alimwona akiwa na hofu sana, japo Marcus alimsalimia lakini hakujibu, alikua kama analia ndani ya moyo wake akiwa amekumbatia begi Marcus alimtazama vizuri yule Msichana akiwa anashusha ngazi akionekana kuondoka hapo Chuoni.

Alimsindikiza kwa Macho na kugundua Msichana huyo alikua na jambo zito ndani yake, jambo 

lililomfanya akose amani ndani yake. Alipohamaki na kutazama vizuri aliona alama za kiatu cha 

Msichana yule kilikua na damu, hii ilimshtua Marcus.

Akaacha safari ya kuelekea kwa Mkuu wa chuo na kuanza kumfuata Msichana huyo, alipofika eneo ambalo alimwona akiingia hakumwona yule Msichana, alizunguka kumsaka lakini hakumpata, sasa akaona ni Bora kwanza ajuwe ile damu ilikua ya nini, ndipo alipoanza kufwatilia mahala ambapo yule Msichana alitokea.

Alijikuta akienda kwenye majengo ambayo hayatumiki, majengo machakavu ya chuo ndiko ambako dama za viatu vya yule Msichana vilikua vimetokea, dama zilimfikisha hadi kwenye vyoo vya Majengo hayo, choo kimoja ndipo ambapo yule Msichana alitokea.

Alihisi hatari, akachomoa Bastola yake kisha taratibu akafungua choo hicho, alikutana na mwili 

wenye damu tena ukiwa umetobolewa macho yake, kifo kile kile ambacho Michael Jomo alikutwa nacho. Haraka Mpelelezi Marcus akaweka Bastola kiunoni kisha akatoa simu na kuupiga picha mwili huo uliolala kwenye Sinki la choo.

Kisha akachezea simu akionekana kutaka kupiga simu Mahali, pale pale akawekewa Bastola 

kichwani, Sauti ya kike ikasikika ikisema

“Weka mikono yako juu, ukifanya ujanja nabomoa Ubongo wako” alisema Msichana huyo, haraka akili ya Mpepelezi Marcus ikamwambia kua aliyesimama nyuma yake ndiye Muuwaji 

anayewasumbua wapelelezi, ndiye aliyeuwa Watu wote kuanzia Mzee Yusuf hadi Kijana Michael, na ndiye aliyepishana naye akionekana kujawa na wasiwasi.

“Unataka kunizuia?” aliuliza Msichana huyo kwa sauti ya upole sana, kama utaipima sauti yake 

pekee unaweza fikiria si Mtu katili, swali lake lilimpa uhakika Marcus kua alipata bahati ya kukutana na Muuwaji huyo.

Vita ya akili 

“Kwanini unauwa?” aliuliza Mpelelezi Marcus akiwa bado hajaiyona sura ya Msichana huyo. 

“Kwasababu wametaka niwauwe”

“Umemuuwa Yusuf?”

“Ndiyo, nitauwa hadi pale kisasi changu kitakapoisha dhidi yao” 

“Walikutendea nini hadi uwe na hasira dhidi yao” aliuliza Marcus akiwa anapanga shambulizi la 

kushtukiza, alishaona dalili na harufu ya damu, Mauwaji ya kikatili aliyoyafanya Msichana huyo 

yalimfanya aamini kuwa hakua sawa Kiakili hivyo dakika yoyote anaweza kufyatua Risasi.

“Hata ukijua huwezi kuzuia hiki nilichokianzisha Mpelelezi, unaonekana kua makini kuliko yule Daudi. Nimekuweka kwenye mpango wangu, ni lazima nikuuwe” alisema Yule Msichana, pale pale Mpelelezi Marcus akageuka upande na kuigeuza Bastola ya Msichana huyo, Bastola ikaanguka chini.

Nini Kiliendelea? Usikose Sehemu Ya 08

 

Jiunge WhatsApp Channel Ya KIJIWENI Ili Kuwa Wa Kwanza Kupata Updates Za RIWAYA Hii Kwa Kubonyeza Hapa 

SOMA Uchambuzi Na Makala Mbalimbali Kwa Kubonyeza Hapa

 

 

 

 

20 Comments

  1. Ebwana eeh muuwaji kaingia choo cha kiume 😅. Nataman kumjua ni nani maan taswira yake ishaanza kunsumbua 🤢😄

Leave A Reply


Exit mobile version