Ilipoishia jana ” Mkononi Mzee huyo alikua ameshikilia Bastola nyeusi ndogo, hapa Daudi akashindwa kufasili kwa haraka haraka ni kwanini alikua na Bastola ambayo haikuonekana kutumika. Pia ilionekana kwenye kabati la kuhifadhia makabrasha palikua pamepekuliwa sana, hii ikamfanya Daudi ahitimishe uchunguzi wa awali kua muuwaji alihitaji kitu fulani kutoka kwa Mzee huyo, lakini swali aliloondoka nalo ndani ya Chumba hicho lilikua

“Nani amemuuwa Mzee huyo tajiri?”

Tuendelee Sasa

SEHEMU YA PILI (02)

Sasa ni saa moja Asubuhi, familia yote ya Mzee Yusuf ilifikishwa kituo cha polisi Oystebey, Daudi Mbaga aliwaeleza. “Hapa tunazungumzia kifo cha Mtu wenu, toeni ushirikiano kwa mnayoyajua ili tubaini Muuwaji ni Nani” alisema Daudi, kwa jicho lake la kipelelezi na aling’amua jambo, mmoja wa wanafamilia ile alikua na wasiwasi sana. 

Ni yule Bi Choro ambaye aliiyona ile damu kwa mara ya kwanza “Nitaanza na wewe Bibi, wengine msubirie hapa” alisema Daudi kisha aliongozana na Bibi huyo kuelekea chumba Maalum cha Mahojiano. 

Kwanza Daudi alimpatia Bibi huyo kikombe cha Kahawa akiamini kutokana na umri wa Bibi huyo angelikua mpenzi wa Kahawa, kweli Bi Choro aliinywa kahawa akiwa anatetemeka.

“Najua wewe si Muuwaji, ila Muuwaji yupo ndani ya familia ile na wewe unamjua, hebu nieleze ni nani aliingia chumbani kwa Mzee Yusuf Usiku wa tukio?” aliuliza Agent Daudi Mbaga huku akiwa amemkazia macho Bi Choro ambaye alijitahidi sana kutokumtazama Agent Daudi Mbaga. 

Alibaki kimya bila kumjibu Daudi “Ni rahisi nikahitimisha kesi hii ndogo iliyojaa utoto kwa kusema kua wewe Bibi ndiye Muuwaji na utahukumiwa kifungo cha Maisha jela” alisema Daudi kisha akaweka mtego hapo, akajifanya anaandika maelezo ya kuhitimisha uchunguzi, haraka yule Bibi akasema “Mimi sijauwa” alisema huku chozi likimbubujika, Daudi akaacha kuandika kisha akamdunga swali 

“Kama si wewe ambaye ndiye uliyeita wengine ni Nani?” Bi Choro akaamua Kumsimulia Daudi 

Mbaga kile kilichotokea Usiku ule, akasema

“Niliamka baada ya kuhisi kiu ya Maji, nilitembea taratibu sababu miguu yangu ina maumivu, nilisikia mlango ukifungwa kwa nguvu” Daudi Mbaga alimkatisha Bi Choro na kumwuliza

“Mlango uliofungwa kwa nguvu ulikua wa chumba cha Nani?” sura ya Bi Choro ilionekana kutokua tayari kusema lakini alibanwa na mpelelezi huyo, akasema

“Adela Mjukuu wa Mzee Yusuf” 

“Ni yule Binti wa Miaka 13?”

“Ndiyo”

“Baada ya hapo?”

“Ndiyo niliona hata mlango wa Mzee Yusuf ukiwa wazi, ndipo niliposogea kujua kwanini upo wazi, ndiyo niliiyona damu ikitiririka” alisema Bi Choro, alipandikiza maswali ya kipelelezi kichwani kwa  Agent Daudi, akafikiria jambo

Akafikia kukubaliana na akili yake kua Binti yule wa miaka 13 asingeliweza kutenda yale Mauwaji,  lakini akafikiria upande wa pili kua huwenda Adela alimwona Muuwaji akitoka chumbani kwa Mzee Yusuf, ndiyo sababu alifunga mlango kwa nguvu kutokana na ile hofu. Sasa alionesha tabasamu huku akikenua meno yake yaliyojipanga vizuri, aliona wazi anaenda kumfahamu Muuwaji kwa haraka sana.

Aliwaacha wengine wakiendelea kuwahoji akina Adela, alikua na akili sana sababu alijua kosa moja analoweza kufanya linaweza kuvuruga ushahidi wote, hakutaka kumhoji Adela bali aliondoka kwa kutumia Pikipiki yake hadi nyumbani kwa marehemu Mzee Yusuf.

Aliingia hadi ndani, sasa alikua akifika kwenye chumba cha Mzee Yusuf, alishaelekezwa na Bi Choro ni chumba gani ambacho kilifungwa kwa nguvu, alihitaji kutumia akili yake vizuri. Chumba kinachotajwa kua ni cha Adela kinatazamana moja kwa moja na chumba cha Mzee Yusuf hivyo kama muuaji alikua akitoka humo basi Adela aliweza kumwona bila tatizo.

Akasogea na kusimama mlango wa chumba cha Adela, alichokifikiria ndicho alichokutana nacho, engo hiyo ilitosha kumshawishi kua Adela alimwona Muuwaji, lakini akajiuliza swali moja, kwanini Bi Choro hakumwona Muuwaji?

Maana yake Muuwaji alibakia ndani ya nyumba hiyo na pengine alijificha mahali, sasa swali moja zito alilojiuliza ni kuwa Muuwaji aliondokaje hapo ikiwa palikua na korido moja tu ambayo Bi Choro ndiyo alikua akitembea na kwa mazingira yale isingelikuwa rahisi Muuwaji atoke alafu Bi Choro asimwone. 

Hapa alianza kumtilia shaka Bi Choro kua kuna jambo lingine aliliona na alichagua kukaa kimya ndiyo maana alijawa na hofu sana.Hakuishia hapo Agent Daudi Mbaga kijana mrefu kiasi, mweupe na msomi aliyeingia kwenye idara ya Polisi kama Mpelelezi aliona ipo haja ya kurudi Chumbani ambako Mauaji ya Mfanyabiashara Yusuf yalifanyika.

Michoro mbalimbali ya namna ambavyo Mzee Yusuf alilala baada ya kuuawa ilikua imechorwa pale chini ili kuweka kumbukumbu ya eneo la tukio, alisogea kwenye ile meza huku akijua fika kua mwili wa Mzee Yusuf ulikua Hospitali ukifanyiwa vipimo na baadhi ya vitu vilivyokutwa eneo la tukio la Mauaji.

Alituliza akili yake, meza ndogo ilikua hapo, hii ndiyo meza ambayo Alilalia Mzee Yusuf baada ya Kuuawa, aliikagua meza hiyo, sasa akafikisha macho yake chini ya meza akiwa ameinama. Alikuta kitu cheupe mfano wa karatasi kikiwa kimebandikwa kwenye meza hiyo kwa chini, aliibandua na kufungua karatasi hiyo ngumu iliyoonekana kwa hakika kabisa kua ni Picha ya Mnato.

Agent Mbaga aliifungua picha hiyo, ilikua ni picha ya zamani sana ambayo Mzee Yusuf alipiga na familia yake. Aliona watoto watatu, wawili wa kike na Mmoja wa kiume. Aliona wazi picha hiyo haikua na mahusiano yoyote na upelelezi wa kesi hiyo lakini hakuiacha aliikunja na kuitia mfukoni. 

Wakati anatoka simu yake iliita, Dokta Sekwa ndiye aliyekua akimpigia

“Agent Daudi” ilisema simu hiyo baada ya kupokelewa

“Ndiyo”

“Njoo Hospitali mara moja”

“Hapana shaka nitakua hapo dakika chache zijazo” alisema kisha aliikata simu hiyo iliyopigwa na 

mtaalamu wa kuchunguza Maiti. Alifunga mlango wa chumba hicho kwa kutumia funguo kisha 

alishusha ngazi hadi nje.

Alikutana na familia ya wafiwa ikiwa inaingia hapo, macho yake akayapeleka kwa Mtoto wa miaka 13 anayeitwa Adela, alimwona Mtoto huyo akiwa na hofu sana, alikua ameshikwa na Mama yake ambaye ni Sofia Mtoto wa Mzee Yusuf, Sofia alimwamuru Adela kuzama ndani

“Naelekea Hospitali kupata majibu ya uchunguzi wa Maiti na vyote vilivyokutwa eneo la tukio, 

nitarudi kuzungumza na nyie” alisema Daudi Mbaga kisha aliondoka na kuicha familia hiyo ikiingia ndani.

                                                                          ***

Sofia alimfuata Binti yake hadi chumbani kwake alikokimbilia, Adela alikua akilia. Mama yake akamfuata na kumkumbatia huku akimwambia “Usiseme chochote kile Adela, sitaki uingie matatizoni sawa?” Adela mwenye kulia alimjibu Mama yake kwa kichwa tu kuwa hatosema chochote, baada ya kutoka hapo Sofia alimfuata Bi Choro aliyesimama jikoni

“Bi Choro nakuomba sana usije ukamwingiza Adela kwenye hili, tafadhali sana acha polisi 

wachunguze tukio hili. Nina hakika Adela hakumwona Muuwaji, sitaki aathirike na hili ukizingatia Salma anarudi Tanzania” alisema Sofia kwa sauti ya kukaza, Bi Choro akajawa na hofu akamwuliza “Huoni kama utakua unampa mzigo mzito Binti yako, ni bora atoe alicho kiona kusaidia uchunguzi Sofia”

“Usichokielewa ni nini hapo Bi Choro? Nimesema sitaki Binti yangu ahusishwe, umri wake hapaswi kushiriki hili linaloendelea. Polisi watabaini Ni Nani Muuwaji” alisema Sofia kisha aliondoka hapo na kuelekea chumbani kwake, alichukua stuli na kupanda ikamfikisha juu kabisa ya kabati lake la kuhifadhia nguo, huko alikuta faili akalichukua kisha akafikiria nini cha kufanya, akaamua kulizika faili hilo nyuma ya nyumba mahali ambapo palikua na zizi la Mbwa. Alipomaliza alirudi Ndani na kuingia bafuni kuoga.

***

Agent Daudi Mbaga alifika Hospitali kwa Dokta Sekwa, baada ya kupaki pikipiki yake alipaki akatembea hadi ofisini, akamkuta Dokta Sekwa akiwa anamsubiria kwa hamu sana ili ampe ripoti ya uchunguzi.

Alipofika tu alisogezewa faili asome kwa kina maelezo kuhusu Marehemu na shahidi za mazingira zilizokutwa eneo la tukio. Ripoti ilisema

“Mwili wa Mzee Yusuf ulikutwa na sumu, hiyo ikatoa ishara kua kilichoondoa uhai wake kwa haraka 

ilikua ni hiyo sumu, sumu hiyo ilikutwa kwenye moja ya Glasi mbili zilizokutwa eneo la tukio. Hata hivyo macho ya Mzee huyo Marehemu yalimrekodi Marehemu katika hatua ya mwisho alipomtazama, chini ya maelezo ikawekwa hiyo picha iliyopatikana kwenye mboni za Macho ya Mzee Yusuf.

Picha hiyo haikutosha kuonesha sura ya Muuaji kwani ilionesha mikono tu ya Muuwaji” 

Alipomaliza kuisoma ripoti hiyo fupi alihitaji maelezo ya mdomo kutoka kwa Dokta Sekwa ambaye alikua na jicho moja tu huku lingine likiwa ni Bandia, umri wake wa Miaka 60 ulitosha kuonesha alikua na uzoefu kiasi gani kuchunguza Maiti na kubaini mambo kuhusu Maiti.

“Sijaona kuhusu kisu katika ripoti yako” alisema, Dokta Sekwa akamweleza Agent Daudi Mbaga kua“Hakuna mahusiano kati ya kisu kilichokutwa mgongoni na kifo cha Mzee huyo, kwani Mzee huyo alikufa kwanza ndipo akachomwa kisu Mgongoni muda mfupi baada ya kifo chake” taarifa hii kutoka kwa Dokta Sekwa ilianza kumkanganya Agent Daudi Mbaga.

“Inawezekanaje, ina maana Muuaji hakua na uhakika kua ameuwa akaamuwa kumkita na kisu cha Mgongo? Alipata wapi huo muda?” akauliza Agent Daudi kisha akamshukuru Dokta Sekwa kisha akaondoka na maelezo hayo hadi Ofisini kwake, akapata muda wa kutuliza akili yake na kufikiria zaidi katika mambo aliyoamua kuyapatia maelezo ili aanze uchunguzi aliamua kuweka dhana kuwa pengine kulikua na wauwaji wawili waliotenda tukio kwa nyakati mbili zilizorandana tena bila kujuana, kwa maana isingelikua rahisi kumpa sumu kisha akamchoma na kisu mgongoni akiwa tayari ameshakufa.

Pili alifikia maamuzi ya kukubali kuwa Muuaji aliyapanga vizuri Mauaji hayo kwa maana aliweza kufuta picha kadhaa kwenye Mboni ya Mzee Yusuf na kuacha moja ambayo haitoshi kutoa taswira halisi kua ni nani Muuaji?

Usikose kusoma SEHEMU YA TATU ya KOTI JEUSI

KAMA HUKUSOMA SEHEMU YA KWANZA ISOME HAPA

 

26 Comments

  1. Pingback: KOTI JEUSI ( Sehemu Ya Tatu) KOTI JEUSI – 03 - Kijiweni

  2. Pingback: KOTI JEUSI (Sehemu Ya Kumi Na Tatu) KOTI JEUSI – 14 - Kijiweni

  3. Pingback: KOTI JEUSI (Sehemu Ya Kumi Na Tano) KOTI JEUSI – 15 - Kijiweni

Leave A Reply


Exit mobile version