Ilipoishia Jana ” Haraka Salma alichukua Taxi akarejea nyumbani kwake, alikuta bado ndugu wapo wakimsubiria  maana alishapiga simu kua ameachiwa huru. “

Tuendelee Sasa

SEHEMU YA NNE (04)

“Mama Naogopa” alisema Adela usiku ulipoingia, alikua chumbani na Mama yake tu

“Unaogopa nini Adela, polisi hawawezi kukuuliza chochote kile sababu tayari nimeongea na Bi Choro asiseme chochote” alisema Sofia wakiwa kitandani amemkumbatia Adela ambaye alikua 

akilikumbuka tukio la Usiku ule

“Kwani ilikuaje, uliona nini Adela?” aliuliza Sofia.

“Mtu mmoja akitoka chumbani kwa Babu, alikua amevalia koti jeusi, naogopa sana” aliongea Adela akionekana kuzidi kua na hofu zaidi

“Mtu mmoja amevalia Koti jeusi?” 

“Ndiyo Mama”

“Pole Mwanangu, hakuna kibaya kitakachokupata nitakulinda kwa gharama yoyote ile” alisema Sofia huku akionekana kuizidi kuitafakari kauli ya Binti yake, mara mlango uligongwa, alipofungua alikutana na Martha

“Dada Sofia, sisi tunarejea nyumbani maana Usiku ni mwingi sasa” alisema.

“Sawa mfike salama, pia poleni”

“Usijali, niagie Adela” 

“Haya” alisema Sofia kisha alirejea chumbani, Martha alikitazama sana Chumba cha Mzee Yusuf kisha akashusha ngazi na kuondoka hapo.

****

Baada ya siku kadhaa kupita, Agent Daudi akiwa nyumbani kwake ameshamaliza kuoga na sasa 

alikua akijiandaa kujitupa Kitandani, mara simu yake iliita. Namna alivyochoka alijisikia uvivu hata kunyanyuka, alijilazimisha hadi akafika kwenye simu na kuinyanyua kisha akaipokea

“Hello?” alisema Daudi Mbaga baada ya kua amekwishaipokea, alijibiwa na ukimya kutoka upande wa pili kwa zaidi ya sekunde kumi kisha ikasikika sauti ya Kike iliyochezewa ikisema

“Agent Daudi, najua unahangaika kumjua Muuwaji. Huna haja ya kumtafuta Muuwaji wa kwanza wa Mzee Yusuf sababu yupo Muuwaji wa pili ambaye hata Mimi namtafuta pia” ilisikika hiyo sauti nyororo ikisema, Daudi alishtuka akaiangalia vizuri namba hiyo iliyoonekana kupigwa kutoka nje ya Nchi ya Tanzania

“Nani wewe na umeyajuaje yote hayo?”

“Huna haja ya kunifahamu, ila nakutegemea sababu na Mimi nataka kumjua Muuwaji wa pili 

aliyemchoma kisu Mzee Yusuf ni Nani, ukishampata utanijulisha” alisema Mwanamke huyo, uzuri simu ya Agent Daudi ilikua ikionesha mahala ambapo simu hiyo ilitoka, ilikua ni Liverpool Nchini Uingereza.

Simu ilipokatwa ilimwacha Daudi Mbaga akiwa na maswali mengi kumhusu Mwanamke huyo, 

kwanza alijiuliza ni Nani ambaye anazijua taarifa za ndani za Uchunguzi wa maiti ya Mzee Yusuf, pili kwanini anataka kumjua Muuwaji wa pili wakati wa kwanza hajamjua. Haraka akahisi kua huwenda huyo ni Muuwaji wa kwanza aliyempa sumu Mzee Yusuf.

Haraka akaandika jina la mahali ambapo simu hiyo ilipigwa, namba hakuiyona tena sababu simu 

ilipigwa kwa mfumo wa siri yaani Private. Akaunganisha doti juu ya Salma Mke wa Marehemu Mzee Yusuf ambaye naye alitokea Uingereza, sasa yale maneno ya Sofia kua Salma alikua na ugomvi na Mzee huyo yalijirudia tena 

Akapata hofu kubwa kua huwenda Salma ndiye aliyemtuma Muuwaji huyo mtaalamu ambaye alifuta hata picha za mboni ya macho ya Mzee Yusuf, kwa maana hiyo aligundua Muuwaji alikua Profeshino kweli kweli na si kazi rahisi kumbaini, kichwa kikawaka moto kwa Agent Daudi, Usingizi na uchovu vilimuisha.

Akawasha kompyuta Mpakato na kupitia taarifa za Salma Mke wa Mzee Yusuf, aligundua mara 

nyingi alikua akifanya safari zake kuelekea Uingereza hasa katika Jiji la Liverpool na Manchester ambako ndiko ziliko Biashara nyingi za Mzee Yusuf, hapa akiwa kama Mpelelezi akatabasamu kidogo maana uelekeo wa kesi ulianza kwenda vizuri, akapanga ratiba ya kuanza kumpeleleza Salma. Ile simu ya ajabu ilimfanya akune kichwa kwa kujiamini kua Muuwaji alifanya kosa kubwa kupiga simu.

Asubuhi Mapema sana Mpelelezi Daudi Mbaga alielekea kwenye kasri la Mzee Yusuf, lilikua ni jumba la kifahari mno. Alipokua nje Daudi alisadiki kua Marehemu alikua tajiri haswa na huwenda kifo chake kimetokana na utajiri alio nao, akapiga honi, mlinzi akamfungulia geti maana kwa siku hizo alizofika hapo tayari mlinzi alishamzoea Mpelelezi huyo.

Lakini kabla hajaelekea ndani alihitaji kuzungumza na Mlinzi ambaye hakuna hata mmoja aliye 

muhoji baada ya tukio hilo. Alimuuliza

“Palikua na mgogoro wowote kati ya marehemu na Mke wake?”

“Ndiyo” alijibu mlinzi, hivyo kama mlinzi tu alilifahamu hilo basi haukua mgogoro wa kawaida. 

“Unasemaje walikua na mgogoro wakati mara zote upo getini, ina maana ulikua mgogoro mkubwa 

kiasi hicho?”

“Siku moja asubuhi, kila mmoja alitoka kwa gari yake. Kila mmoja alivyopita hapa alikua akizungumza kuhusu mwenzake kwa hasira sana”

“Ilikua ni kipindi gani hicho?”

“Wiki moja kabla ya tukio hili”

“Je, usiku ule kuna Mtu yeyote aliingia na kutoka?”

“Hapakua na Mtu yeyote yule, hali ilikua shwari na hakukua na viashiria kua kuna aliyeingia na 

kutoka japo palikua na giza na mvua kubwa lakini sikuona dalili yoyote ile” alisema Mlinzi

“Haya sawa Ahsante” alisema Mpelelezi Daudi akataka kuondoka lakini yule Mlinzi akamuuliza

“Je umefanikiwa kumpata Muuwaji?”

“Nitawajulisha” alisema Daudi kisha aliingia ndani, akiwa anapandisha ngazi alikutana na Mtoto wa Sofia aliyeitwa Adela akiwa anashusha ngazi akionekana anaelekea shuleni, alipomwona Mpelelezi Daudi alionekana kua na hofu kubwa ya kumwogopa Mpelelezi huyo.

Daudi hakushangaa sababu alishapewa taarifa na Bi Choro kua huwenda Adela alimwona Muuwaji

“Hujambo Adela?” 

“Ndiyo, shikamoo” alisema Adela akiwa anashusha ngazi kwa haraka sana. Daudi akatabasamu tu 

kisha akaendelea juu ambako alikutana na Sofia akionekana anamsimdikiza Binti yake shuleni

“Oooh Mpelelezi, za Asubuhi. Naona leo umetuvamia mapema” alisema Sofia akiwa mwingi wa 

tabasamu lisilo na shaka kua lilitoka ndani ya uvungu wa moyo wake

“Nimekuja kuzungumza na Salma, kuna taarifa nimezikusanya”

“Zipi hizo?”

“Kuna Mtu amenipigia simu jana na kuniuliza kuhusu Muuwaji, namna alivyouliza anaonekana kujua mambo mengi kuhusu kesi hii, kilichonipa Mashaka ni kwamba Mtu huyo amepiga simu kutokea Uingereza, hivi mara nyingi Salma huenda Mji gani kule?” 

“Liverpool na Manchester, ndiko ziliko Biashara za Mzee”

“Mpigaji alipiga kutokea Liverpool sasa hofu yangu huwenda kukawa na mahusiano na yeye”

“Lakini hata hivyo Salma hayupo hapa, nasikia aliondoka Usiku sana na hajarudi hadi sasa” taarifa hii ilimshtua sana Mpelelezi Daudi

“Aliondoka Usiku sana?”

“Ndiyo, na kwa mujibu wa mlinzi ni kwamba alikua akizungumza na Mtu kwenye simu. Hajarudi hadi hivi sasa” alikazia Sofia

“Nipatie namba yake” aliomba Mpelelezi Daudi, Sofia alitoa namba ya Salma

“Daudi kwakua una kazi ya kufanya hapa basi wacha nimwaishe Mtoto shule, tutawasiliana” alisema Sofia huku akishusha ngazi, Daudi akajaribu kumpigia simu Salma lakini alijibiwa kua Namba ya Salma ilikua haipatikani, akajaribu kupiga zaidi ya mara tatu hadi alipothibitisha kua hakukua na tatizo la Mtandao bali simu ya Salma ilikua haipatikani

“Ups!” akiwa amesimama alishusha pumzi zake, kila alilolifikiria aliona haliingii akilini mwake, hofu na mashaka juu ya Mwanamke huyu vilipanda ndani yake Mpelelezi Daudi aliyeaminika na Serikali  kwa namma alivyokua akipambana na kesi nyingi na kuzishinda.

HADI kufikia saa tisa alhasili hapakua na dalili ya Salma kuonekana, hakupatikana popote pale na kuzidi kukoleza taarifa ya kua Muuwaji miongoni mwa wapelelezi hasa Mpelelezi Daudi Mbaga ambaye moja kwa moja alimweka alama Salma kua ni Mtu anayemhisi kuusuka mpango wa kifo cha Mzee Yusuf.

Kukawa na nadharia moja kubwa kua Bilionea huyo aliona wazi pesa zake namna zilivyokua 

zikichotwa na Mwanamke huyo na kupewa huyo Mwanaume mwingine anbaye ndiye chanzo cha ugomvi baina ya wanandoa hawa, huwenda Mwanaume huyo wa Salma ndiye aliyemshawishi Salma kumuuwa Mume wake ili apate utajiri zaidi.

Mishale ya saa kumi na moja jioni, wingu zito lililoashiria kua ilitarajiwa kushuka mvua kubwa 

iliyoambatana na upepo mkali, Mwanaume mmoja wa makamo aliyekua akifanya kazi ya kukatisha tiketi za maegesho ya Magari maeneo ya Mwenge Vinyago aliliona gari moja aina Vogue C8 nyeusi likiwa limesimama kwa muda mrefu sana tangia asubuhi alipolikatia tiketi na kuliruhusu kupaki hapo hadi muda huo lilikua halijaondoka.

 

Alilazimika kusogea ili kuzungumza na Mtu aliye ndani ya gari hilo maana muda wote huo 

palionekana kua na Mtu ambaye ndiye aliyekua akiliendesha gari hilo, aliposogea aligundua kua Mtu aliye ndani ya gari alikua kimya sana, akalazimika kumchunguza huku akimgongea. Mwanzo alifikiria huwenda alikua amelala lakini baadaye alipata hisia ya fofauti kabisa

Ukimya ulikua mkubwa sana, lakini alipomtazama vizuri aliona wazi kua alikua hapumui, aliona wazi ukimya eneo la kifua na tumbo ndipo alipowaita polisi wa Barabarani, kwa pamoja walifikia maamuzi 

ya kuvunja kioo, ndipo walipomkuta Mwanamke mmoja wasiye mfahamu akiwa amekufa ndani ya gari hilo.

Polisi mmoja aliyetambulika kwa jina la Mbegu alipiga simu kituo cha polisi, lakini kwa uchunguzi mdogo alioufanya aligundua kuwepo kwa viashiria kua Mwanamke huyo alikua ameuawa, alikutwa na kamba nyembamba sana mfano wa mshipi wa kuvulia samaki eneo la shingoni, nywele za Mwanamke huyo zilikua zimetimka hali iliyoashiria kua alikua katika varangati zito kabla ya kuuawa.

Taarifa ikasambaa haraka ikamfikia Mpelelezi Daudi na Timu yake ya wapelelezi ambao waliagiza Maiti hiyo isitolewe eneo la tukio hadi wao watakapokua wamefika. Dakika chache baadaye Agent Daudi Mbaga alifika eneo la tukio akiwa na timu yake, Mshituko mkubwa aliupata baada ya kuitazama Maiti, aligundua Mwanamke huyo aliwahi kufika kituo cha polisi na alifanya naye mahojiano, maiti hiyo ilikua ya Salma Mke wa marehemu Bilionea Yusuf.

“Namfahamu huyu, ni miongoni mwa washukiwa wakuu wa kifo cha Bilionea Yusuf. Huyu Muuwaji aliwezaje kumuuwa Mwanamke huyu eneo hili la wazi, basi ni profeshino kweli maana eneo hili ni la wazi mno” alisema Daudi akizungumza na mmoja wa vijana wake kisha akawaagiza Madaktari kuibeba maiti kama ilivyo waipeleke Hospitalini kwa daktari wake aliyeitwa Sekwa ambaye alikua ni Mzee mwenye uzoefu Mkubwa wa kuchunguza maiti tata.

Daudi Mbaga alijiegemeza kwenye Mti mmoja, akamwita Mwanaume aliyekua akifanya kazi ya 

kukatisha tiketi ambaye ndiye aliyewaita polisi wa mwanzo kabisa.

“Unasema ulimhudumia Mwanamke yule?” aliuliza Daudi

“Ndiyo lakini alionekana kua mchovu sana, macho yake yalionesha kua alikua amelia mno maana yalivimba pia yalikua mekundu na alikua akizungumza mfano wa Mtu mwenye Mafua hivi” alielezea Mwanaume huyo.

“Hakuonekana Mtu mwingine ndani ya gari” 

“Hapana alikua peke yake, sijui nini kiliendelea kwake maana baada ya kumhudumia niliendelea na kazi nyingine” alisema, lakini aliposimama Daudi Mbaga alikua akiitazama sheli moja ya Engen, kwa namna wahudumu wa sheli hiyo walivyosimama hakua na shaka kua walikua wakiliona vizuri gari hilo. Akawafuata, akajitambulisha kua ni Askari mpelelezi 

“Mnaliona lile gari pale?” aliwaonesha ile Vogue, tayari Madakatari walishaondoka na mwili wa 

Salma

“Ndiyo”

“Imekua pale kwa muda gani?”

Mmoja wao akajibu

 

“Ni muda sana imesimama pale, nilimhudumia mafuta asubuhi, ndipo ikaegeshwa pale” alisema 

mhudumu huyo wa kiume

“Kuna aliyeingia mle na kuondoka?” Kila mmoja pale hakua na uhakika wa swali hilo, jibu la uhakika kutoka kwao ni kua hawakua makini kulitazama muda wote hivyo Daudi Mbaga alikosa jibu la kueleweka, akarudi kwenye lile gari na kulichunguza likiwa pale pale

Ndani ya gari palikua na pesa nyingi zilizokadikiwa kufikia Milioni 32 ambazo zilikua kwenye Boksi kubwa, siti ya nyuma kulionekana kua na alama za kiatu, hiyo ikaashiria kua Muuwaji alikua nyuma ya gari. 

Daudi Mbaga akavaa Gloves kisha akaliondoa gari hapo na kulipeleka kituo cha polisi huku akiweka kiporo taarifa rasmi kwa familia kua Salma amekutwa akiwa ameuawa, Daudi akaendelea kulichunguza gari akiwa kituo cha polisi

Mbali na fedha hizo pia palikua na Bastola kwenye mkoba wa Salma, Daudi Mgaba kwenye maelezo yake Binafsi akafikiria kua huwenda Salma baada ya kumtuma Muuwaji alienda kuonana na huyo Mwanaume wake wa siri, naye akamgeuka Salma na Kumuuwa, lakini akajiuliza kama alimuuwa ili apate pesa kwanini aliziacha pesa nyingi kiasi kile? Hapa akawa anakuna kichwa chake chenye nywele nyingi za Singa Singa.

Mmoja wa Maaskari wake akafika eneo ambalo Daudi alikua akiikagua gari hiyo, akampatia Daudi simu iliyopigwa na Msamalia mwema kutokea Mwenge Vinyago akidai kua alimwona Mtu aliyeingia kwenye hiyo gari na kutoka. Msamalia huyo alimweleza Daudi kua, Mwanamke mmoja mwenye umri wa chini ya Miaka 30 aliingia ndani ya gari hiyo kisha alitoka baada ya dakika tano tu na kwa wakati wote aliokua ndani ya gari hiyo gari ilikua ikicheza cheza

Msamalia huyo alieleza kua yeye alikua pembeni akifanya kazi yake ya kushona viatu, alipotoka Mtu huyo alionekana kutokua na viashiria vyovyote kua ni Muuwaji, Daudi akamuuliza

“Alikua anaonekanaje?”

“Mfupi kiasi, Mweusi, alivalia baibui lakini siikumbuki rangi yake. Alinipita na kunisalimia kwa salamu ya Kiislam, ni mzuri mno Binti huyo” alisema Msamalia huyo, baada ya mazungumzo hayo Daudi akamwachia jukumu yule askari kumsikiliza zaidi Msamalia huyo.

Hadi kufikia hapo picha ya Muuwaji ilikua ni Msichana wa chini ya Miaka 30, mweusi, mzuri na aliyevaa Baibui, Daudi alizidi kupagawa, sasa swali alilojiuliza, Msichana huyo alikua anataka nini kwa Salma, akawaza zaidi kua inawezekana akawa ndiye aliyemuuwa Bilionea Mzee Yusuf? Inaendelea Usikose SEHEMU YA TANO 

KAMA ULIPITWA NA SEHEMU ZILIZOPITA Gusa Hapa  

27 Comments

  1. Temy Peter on

    Mtunzi apewe ulinzi maana Sophy simuamini kabisaa asije akapota na mtunzi wetu.. 😂😂😂
    I’m kidding 🤣🤣🤣

  2. Pingback: KOTI JEUSI ( Sehemu Ya Kwanza) KOTI JEUSI - 01 - Kijiweni

  3. Pingback: KOTI JEUSI (Sehemu Ya Kumi Na Tatu) KOTI JEUSI – 13 - Kijiweni

  4. Pingback: KOTI JEUSI (Sehemu Ya Kumi Na Tatu) KOTI JEUSI – 14 - Kijiweni

Leave A Reply


Exit mobile version