Kocha wa Simba, Juma Mgunda amefafanua maneno yanayotembea mitandaoni kwamba si sehemu ya kikosi kipya cha Mnyama.

Kauli hiyo imekuja siku chache baada ya kujiridhisha kwamba Kocha Robertinho, amewaambia Simba wampe mkataba Mnyarwanda, Hategekimana Corneille wa Rayon kama Kocha wa viungo lakini awali akiwa nae Rwanda alikuwa akimtumia kama mshauri wake.

Kocha Mgunda ambaye ni mzoefu na miongoni mwa wazawa wasomi akiwa na leseni A ya CAF, ameeleza kuwa bado yupo sana Simba, akizikana tetesi za kutaka kurejea kwenye timu yake ya zamani Coastal Union ya Tanga.

Amefafanua kwamba kwanza Coastal licha ya kuwa washikaji zake lakini ana matatizo nayo binafsi ambayo hakutaka kuyaweka wazi.

Mgunda ambaye kwa sasa yupo mapumzikoni Tanga baada ya kumalizika msimu wa Ligi Kuu Bara amesema bado ataendelea kuwatumikia wana Msimbazi hadi mkataba wake utakapomalizika ndipo atakapojua kinachofuata na bosi wake, Robertinho hajamwambia kama kuna mabadiliko yoyote kwenye kibarua chake.

“Mmefanya vizuri kuniuliza, kwani majibu yangu yatawapa kujua bado ni mfanyakazi wa Simba. Kuhusu Coastal siwezi kukataa kwamba ni timu yangu ambayo nimetoka nayo mbali, tukirekebisha matatizo yetu tutaendelea salama,” alisema kocha huyo ambaye amejiwekea rekodi nzuri Simba.

“Nipo Tanga kwa mapumziko utakapofika muda wa kurejea kwenye majukumu Simba mashabiki wangu wataniona,”alisema na kuongeza kuwa msimu uliomalizika aliuona ushindani mkubwa ambao unawapa picha ya kufanya maandalizi makubwa zaidi kwa ajili ya ujao.

“Ligi ina ushindani mkali na soka linakuwa, hivyo kila timu itakuwa inajipanga kulingana na mahitaji yake ya msimu mwingine,”alisema.

Kocha Mgunda ana mchango mkubwa Simba, aliivusha kipindi anakaimu ukocha mkuu baada ya kuondoka Zoran Maki, aliitengeza timu licha ya kushinda mechi nyingi za Ligi Kuu pia alifanya vizuri kimataifa.

Kwa taarifa zaidi za michezo ulimwenguni tufuatilie hapa.

Leave A Reply


Exit mobile version