Muda unakikimbia sana na nyakati mbalimbali kwenye maisha nazo zinapita, kuna wakati wa shida ambao wengi huwa mbali na wewe na wachache sana hubaki kuwa nawe na kukusaidia katika kufanikisha njia zako za upambanaji kwa kila hali kama ilivyokua kwa Robertinho na Kibu Denis.

Nyakati mbaya wengi wetu wale tuliowategemea kuwa msaada kwetu na kutupa faraja na wakutushika mkono huwa hatuwaoni wanakuwa mbali sana nasi na kubaki wenyewe tukitafuta msaada, lakini hao hao wakati wa raha na furaha huwa nasi karibu yetu na hata kutoa maneno ya fahari kwetu.

Lakini jua kati ya wale wachache ambao walikuwa nasi kipindi kigumu ndiyo utupatia nguvu na  hali ya kupambana zaidi, na hapa jina la mchezaji wa Simba SC Kibu Denis Prosper likanijia na kukumbuka nyakati zake bora akiwa na kikosi cha Lunyasi, msimu wake wa kwanza alikuwa mfalme na tegemezi fahari na faraja ya wanasimba wengi.

Msimu wake wa kwanza alimaliza akiwa na magoli 8 huku akitengeneza mengine manne nyakati zake bora tokea akiwa Mbeya City zilihamia Simba, ila ilichukua mechi chache wanasimba kuanza kumpigia kelele kuwa hana thamani ya kucheza kwenye kikosi na hiyo ni baada ya kupitia kipindi kibaya cha kutofanya vizuri kwa kufunga na kutengeneza pia wengi walimkimbia na kumuacha mwenyewe kwenye wakati wa shida ila mwamba aliendelea kupambana na kupiga kazi.

Safari hii ni mzaliwa wa bara la Amerika Kusini katika nchi ya vipaji duniani Brazil Roberto Oliviera Robertinho akawa mfariji wake na huyu ndiyo mwanzo wa Kibu Denis mpya Kibu wa sasa ambaye amekuwa Lulu kwa klabu yake na Taifa pia kwa sasa afunge au asifunge basi hakuna hata mmoja ataongea kitu.

Ilimchukua dakika chache sana akiwa kwenye jukwaa la uwanja wa Amani (Sasa New Amani Complex) kuona ubora wa Kibu Denis na aliposema huyu ndiyo Mchezaji bora kwenye kikosi wengi walikataa na kutoa maneno ya kejeli, ila huyu ndiyo alikuwa mfariji wake kwa wakati huu kumuonyesha kuwa yeye ni bora na ana nafasi ya kuonyesha ubora wake.

Hapo ikawa mwanzo wa kumuona Kibu Denis mpya ambaye ilifika muda akikosekana kwenye kikosi cha Simba SC basi mashabiki watapiga kelele kukosekana kwake, maisha yake kwenye soka akiwa na Simba yanatuonyesha kuwa hakuna kumkatia mtu tamaa Bali ni kuwa naye wakati wote hata ambao mambo ni magumu kwake.

Safari ya Kibu Denis ilikuwa ngumu kufikia hatua ya kila Mtanzania kumuhitaji kikosini, hatuna nafasi tena ya kumuona siyo bora na wale wote waliyokuwa wakimdharau na kumuhitaji aachwe kwenye kikosi cha Simba SC nao wanamuimba na kumshangilia wamegeuka na kuungana na wale wachache waliyoamini anahitaji mtu mmoja tu kumrudisha Kibu Denis yule na kumfanya kuwa bora zaidi ya yule wa zamani.

Kwa sasa Kibu Denis amekuwa mtulivu hodari wa kupiga chenga na kuwalambisha nyasi wapinzani anaokutana nao wakati ambao panga pangua ni sehemu ya Kikosi cha Simba SC, mabadiliko ya kiuchezaji wake ni makubwa sana na anatufundisha kuwa nyakati mbaya huwa hazidumu bali zinakuwa za muda tu.

SOMA ZAIDI: Wachezaji hatari wa kuchungwa ligi kuu.

1 Comment

  1. Pingback: Mzimu wa Mayele Uliomtesa Konkoni Na Sasa Uko Na Guede? - Kijiweni

Leave A Reply


Exit mobile version