Nyakati zinaenda sana ni kama mshale wa saa uanzapo kuhesabu taratibu lakini ndiyo mwendo wake kama kinyonga na mitembeo yake ya kibingwa zaidi kama Kobe.
Mwendo wake ndiyo imekuwa silaha yake muda wote, utaratibu wake umeambatana na usahihi wake kiwanjani takwimu zake ni bora zaidi ya mwendo wa Chita mbugani usahihi wake ni jicho la windo la mfalme wa nyika, ndani ya Serengeti na mbuga zote watalii wanajua kuwa huyu ndiyo mfalme wa nyika kwa sasa na wasimamizi wamekumbana naye mara kadhaa.
Miguu yake ilianzia Ndola, Zambia na kusafiri hadi mji mkuu wa Lusaka huku akiacha kitovu chake kikiwa kimezikwa kwenye udongo, alizaliwa tarehe 18 June ya mwaka 1991 akisoma nchini Zambia na mwaka 2009 Mwamba huyu alimaliza elimu yake ya Sekondari.
Amezaliwa kwenye familia ya Soka na kaka yake Andrian Chama amecheza vilabu vikubwa nchini Zambia na ikiwemo ni Zesco United ambayo amehudumu kwa muda mrefu na kufikia hatua ya kupewa kitambaa cha Unahodha, maisha yake ya Soka yalianzia kwenye klabu ya Nchanga Rangers FC ya Zambia 2010 ambapo 2011 alijiunga na Rone Utd huku dhahabu ya miguu yake bado ikiwa haijaonyesha ung’aavu wake kwani ilimchukua msimu mmoja tu na kurudishwa kwenye kikosi cha Nchanga Rangers kwa mkopo 2013.
Ni kama muda wake wa kung’aa ulifika na thamani ya miguu yake ilionekana kwani mwaka mmoja mbele alijiunga na Zesco United ambayo alihudumu kwa misimu miwili hadi 2016 alipoamua kuvuka mipaka ya Zambia na kutua kwenye kikosi cha Al Ittihad ya Misri lakini ilikuwa ni kama siyo bahati kwake kucheza kwenye kikosi hicho kwani hakufanikiwa kucheza mchezo hata mmoja, haikumrudisha nyuma aliamua kugeuka nyuma ma kurudi nyumbani na mara hii alijiunga na Lusaka Dynamos ya nyumbani klabu ambayo iliwafanya viongozi wa Simba SC kumuona kiungo huyu ambaye safari ya kujiunga kwenye mbuga ya Msimbazi ipatikanayo Kariakoo, Dar es Salaam ilimvusha mipaka na mwaka 2018 aliingia kwenye mbuga hiyo na kilichobaki ni historia ya kurarua na uwindaji mzuri alionyesha kiungo huyo.
Mbuga ya Msimbazi ilimuimba na kutambua uhodari wake wa uwindaji pale alipowavusha kwa mara ya kwanza kuingia hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, kisigino kilichobebwa na kasi ya Hassan Dilunga uhodari na utulivu wake ilikuwa ni zaidi ya windo la Chui na hatimaye anaipeleka Simba SC makundi, hakuishia hapo kuonyesha ubora wake kile tuonacho sasa ni marudio ya kile alichofanya usiku wa March 6 2019 na utulivu mkubwa kwenye box anaivusha Simba SC hatua ya makundi kuingia Robo Fainali kwa goli la dakika ya 89.
Kama ni uwindaji ndani ya Ardhi hii ya Hayati Kambarage ndani ya mbuga ya Benjamini mkapa na viunga vyake vyote chini ya usimamizi wa Shirikisho la Soka Tanzani basi Clatous Chota Chama hana cha kuongeza tena zaidi ya kufanya marudio ya kile alichozoea kukifanya kila msimu. Amefanya mengi ndani ya nchi hii iliyoongizwa na Jakaya Kikwete ikipita tena kwenye mikono ya John Joseph Magufuli awamu ya kwanza kushuhudia movi ya kweli hadi awamu ya Sita sasa ikishuhudia marudio ya yale aliyofanya nyuma.
Mwamba huyu amelinganishwa na viungo wengi nchini kila usajili ulikuwa ukitaja jina lake, kila kiungo mpya alilinganishwa naye ila bado aliendelea kuonyesha utofauti wake wa uwindaji na wengine, ifike hatua sasa tukubali kuwa ndiyo mfalme wa mbuga yote ya viungo washambuliaji nchini wazawa na wageni kwa sasa, kila mbuga aliyopita ameacha alama siyo CCM Kirumba, Mkwakwani, Kambarage, Sokoine kote wanajua uhatari wake.
Miguu yake imefanikiwa kuipeleka Simba SC hatua ya makundi Ligi ya Mabingwa kwa mara nne, huku ikivusha robo fainali nne pia kwa ubora na uhodari ule ule ni wakati sasa wa kumuheshimisha na kukubali kutazama marudio ya ubora wake kufunga na kutengeneza magoli zaidi kuwalambisha nyasi wapinzani anaokutana nao.
SOMA ZAIDI: Hongereni Wawekezaji Soka Letu Limekua Kwa Kasi
2 Comments
Pingback: Usipompenda Karia Basi Uuchukie Na Mpira Wa Bongo - Kijiweni
Pingback: Ni Mwaka Wao Watachukua Tuzo Nyingi Sana Msimu Huu - Kijiweni