Taarifa mbalimbali zimekuwa zikisema kutakuwa na ugumu wa Yanga kumzuia Fiston Mayele kuondoka baada ya msimu huu kumalizika, huku gazeti kubwa la Far Post la Afrika Kusini likieleza mchezaji huyu mshahara wake anataka ni milioni 53.
ATAENDELEA KUSALIA JANGWANI? ndiyo unavyosema kusema baada ya taarifa kutoka Afrika Kusini kueleza kiwango cha mshahara ambacho mshambuliaji wa Yanga, Fiston Mayele anataka apewe ili atue Kaizer Chiefs.
Mayele amekuwa kwenye ubora wa hali ya juu msimu huu akiwa amemaliza kinara wa mabao Ligi Kuu Bara baada ya kufunga mara 16, huku akiwa pia kinara kwenye Kombe la Shirikisho Afrika ambalo timu yake ipo fainali akifunga mabao saba.
Gazeti hilo ambalo linafuatiliwa na wasomaji wengi Afrika Kusini, jana liliandika habari hiyo, huku likieleza ni kwa nini Kaizer Chiefs itakuwa rahisi kwao kumpata mshambuliaji wa Marumo Gallants, Ranga Chivaviro kuliko Manyele.
Kaizer Chiefs, wana mpango wa kuboresha kikosi chao kwa ajili ya msimu ujao na Mayele ni mmoja kati ya wachezaji inayowataka kwa kuwa staa wao Caleb Bimenyimana anatarajiwa kuondoka baada ya kushindwana na Kocha Arthur Zwane.
Baada ya timu hiyo kugundua mchezaji huyo anaondoka, gazeti hilo limesema Kizer ambayo ni timu maarufu kwenye ligi hiyo imeweka majina mawili mezani kwao Mayele na Chivaviro wa Marumo Gallants, lakini wao wanampa nafasi kubwa Chiva kutokana na mshahara wa Mayele kuwa mkubwa.
Wamesema endapo Kaizer watamchukua Mayele mwenye miaka 28, watatakiwa kutoa kitita cha randi 450,000, sawa na Sh53 milioni, huku wakisema mchezaji huyo kwa sasa akiwa na Yanga analipwa milioni 21 kila mwezi.
“Mshahara wake ni R450,000, kwa mwezi kwa kuwa ni mchezaji mwenye soko kubwa zaidi kwa sasa kutokana na uwezo ambao ameouonyesha kwenye michuano ya Afrika msimu huu, hii inaonekana ni fedha nyingi kwa mchezaji ambaye anakuja kuwa mpya kwenye DStv Premiership. Tumeona huko nyuma wachezaji waliofanya vizuri kwenye ligi nyingine, hawana uhakika wa kufanya vizuri hapa PSL,” liliandika gazeti hilo.