Muda wowote kuanzia sasa zinaweza kusikia habari za kushtua. Jonas Mkude yuko kwenye mazungumzo na Yanga na atasaini mkataba wa kazi.

Mkude ambaye aliichezea Simba kwa miaka 13 mfululizo alikula ‘Thank You’ wiki iliyopita, sababu kubwa ikielezwa kwamba ni kiwango kushuka.

Chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya Yanga  kimeeleza kuwa staa huyo aliyekulia Simba, Yanga watampa mkataba wa mwaka mmoja wenye masharti ya kuongeza kama kiwango kitamridhisha Kocha Miguel Gamondi.

Chanzo hicho kilisema mkataba wa kiungo huyo umeambatana na makubaliano ya staa huyo kuahidi kuwa mtiifu na kufanya kilichompeleka ndani ya timu hiyo na kutumika kwa asilimia zote na sio vingine.

Mwanaspoti lilimtafuta Mkude mwenyewe ambaye alisisitiza kuwa yeye ni mchezaji huru kwa sasa baada ya kumalizana na waajiri wake wa zamani Simba.

“Mimi ni mchezaji na sasa nipo huru sina timu ninayoitumikia lolote linaweza kutokea kuhusu Yanga hii taarifa ndio kwanza naisikia kutoka kwako siwezi kuizungumzia sana muda utaongea;

“Hiki ni kipindi cha usajili mengi yanazungumzwa lakini ukweli wa mimi kucheza wapi utajulikana muda sio mrefu kwasasa mimi nipo naendelea na mambo yangu mengine lakini msimu ujao nitacheza, kuhusu timu mtajua tu kwani mpira ni mchezo wa wazi.” alisema Mkude.

 

Swali kubwa kwa mashabiki baada ya kusikia tetesi za Mkude kusaini Yanga, ni nini kitatokea kikosini haswa kwenye eneo la kati anapokwenda kucheza.

Je, yule namba 6 ndiyo huyo? Je, kati ya Khalid Aucho na Yanick Bangala nani atakwenda benchi? Ni suala la muda, lakini habari za ndani zinasema kwamba Yanga huenda wakapumua kama Mkude ataweza kuwa kwenye ubora wake kwani Bangala tayari walishaanza kumtafutia mbadala kutokana na kiwango chake pamoja na mengine ya nje ya uwanja.

Kocha Gamondi, anaweza kuanza na Mkude na Aucho katikati mbele wakasimama Makabi Lilepo(Al Hilal) na Fiston Mayele.

Tutaendelea kukujuliza undani wa taarifa hii kadri itakavyotufikia kupitia ukurasa wetu huu. Ungana Nasi.

Leave A Reply


Exit mobile version